STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 20, 2012

Shija Mkina achekelea kuitungua Yanga


MFUNGAJI wa bao pekee lililoizamisha na kuitemesha Yanga ubingwa wa Ligi Kuu
Tanzania Bara, Shija Mkina wa Kagera Sugar, amedai kufarijika mno kuitungua timu hiyo.
Mshambuliaji huyo za zamani wa Bandari Mtwara na Simba, alisema ingawa ni kawaida
yake kufumania nyavu, lakini kuifunga Yanga ni faraja kubwa kwake kwa vile imeisaidia timu yake kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye ligi kuu msimu ujao.
Mkina, aliyejiondoa Simba kwa lazima baada ya kushindwa kupewa nafasi na aliyekuwa
kocha wa timu hiyo, Mganda Moses Basena ambaye hayupo kwa sasa katika klabu hiyo,
alisema bao hilo dhidi ya Yanga lilikuwa muhimu kwa timu yake ya Kagera.
"Nashukuru kwa kuweza kufungia timu yao bao muhimu lililotuhakikishia pointi tatu
zinazotufanya tusiwe na hofu ya kushuka daraja," alisema.
Mchezaji huyo, aliyewahi kuwa mfungaji bora alipokuwa na Bandari Mtwara, alisema ligi ya msimu huu ilikuwa ngumu kuliko misimu ya nyuma na ndio maana hadi sasa ni vigumu kujua timu inayoshuka daraja au itakayonyakua ubingwa licha ya Simba kupewa nafasi.
"Naamini ligi zote zingekuwa hivi, basi soka letu lingekuwa lipo juu na klabu zetu kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa," alisema Mkina.
Kwa ushindi iliyopata ya Yanga, imeifanya Kagera Sugar kufikisha jumla 26 na ikisaliwa na mechi tatu dhidi ya Toto Afrika inayotarajiwa kucheza kesho mjini Bukoba, Coastal Union watakaoumana nao Aprili 30 mjini Tanga kisha kufunga msimu kwa kuvaana na Azam.

Mwisho

Polisi Moro yaifuata Mgambo Ligi Kuu, vita yabakia kwa Prisons Mbeya, Polisi Dar

WAKATI timu za soka za Mgambo ya Tanga na Polisi Moro zikiwa zimeshajihakikishia
kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, vita vya kuwania nafasi hiyo imesalia kwa
timu za Polisi Dar na Prisons ya Mbeya ambazo zitafunga dimba Jumatatu.
Polisi Moro jana ilijihakikishia nafasi ya kupanda daraja baada ya kuilaza Mbeya City mabao 2-0 na kufikisha pointi 17 na kuongoza msimamo wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza zinazochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
Mgambo ilikuwa timu ya pili kupata nafasi hiyo katikati ya wiki baada ya kuilaza Transit Camp mabao 3-0 na kufikisha pointi 15 zinazowaweka nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.
Nafasi ya tatu ya kupanda daraja imesaliwa kwa timu za Polisi Dar ambayo jana ilipata ushindi wa mabao 3-0 mbele ya JKt Mlale ya Songea na kufikisha pointi 10 ikishika nafasi ya nne nyuma ya Prisons ambayo yenye ina pointi 11.
Hata hivyo Prisons Mbeya ambayo ilitarajiwa kushuka dimbani leo jioni ndiyo yenye
nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo kutokana na pointi ilizonazo pia kuwa na kiporo
cha mechi moja ya ziada itakayochezwa Jumatatu dhidi ya Polisi Dar.
Iwapo timu hiyo itateleza kwa Rhino au kutoka sare itamaanisha kwamba mechi yao ya Jumatatu dhidi ya 'Vijana wa Kova' itakuwa ni kama fainali katika kuwania
nafasi hiyo moja ya kucheza ligi kuu msimu ujao.
Uongozi wa Polisi Dar kupitia kocha wake, Ngello Nyanjaba, alisema hawajakata tamaa
kupanda ligi kuu, licha ya kuwa na nafasi finyu nyuma ya Prisons ya Mbeya.
"Tunasubiri kuona inakuwaje hadi dakika za mwisho," alisema Nyanjaba.

Msimamo wa Fainali za 9 Bora kabla ya mechi za leo:

TIMU P W D L F A Pts
1. Mgambo Shooting 7 4 3 - 12 3 15
2. Polisi-Moro 7 5 2 - 14 4 17
3. Prisons-Mbeya 6 3 2 1 8 5 11
4. Polisi Dar 7 2 4 1 9 4 10
5. Mbeya City 7 2 2 3 7 8 8
6. Rhino Rangers 7 2 2 3 4 6 8
7. Mlale JKT 7 1 2 4 5 13 5
8. Polisi-Tabora 6 1 2 3 5 11 5
9. Transit Camp 6 - 1 5 2 12 1

Mwisho

Kocha Julio kuweka historia ya aina yake nchini


KOCHA maarufu nchini, Jamhuri Kihwelu 'Julio' anatarajiwa kuweka rekodi ya aina yake
nchini leo atakapokalia benchi za timu mbili tofauti katika pambano moja kati ya Coastal Union ya Tanga anayoifundisha na CDA-Dodoma anayojiunga nayo.
Mchezo huo maalum wa kirafiki kwa timu hizo utachezwa kwenye uwanja wa Jamhuri
mjini Dodoma, ambapo Coastal watautumia kumuaga na CDA kumkarisha kocha huyo
kwa ajili ya kuinoa kwa michuano ya Ligi ya TFF-Taifa inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Julio aliyeisaidia Coastal kusalia Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya awali kuchechemea, ameodai ameombwa na uongozi wa CDA, timu aliyowahi kuichezea miaka ya nyuma, jambo alilodai ameliafiki kwa moyo mmoja.
Akizungumza kutoka mjini Dodoma, Julio alisema amekubali kuachana na Coastal Union
ili aifundishe CDA klabu iliyomuibua katika maisha yake ya soka na katika mechi ya leo atakaa kwenye benchi za timu zote kwa dakika 45 za kila kipindi.
Kocha huyo mwenye maneno mengi, alisema dakika 45 za awali atakalia benchi la timu
yake ya sasa ya Coastal Union na katika kipindi cha pili atahamia katika benchi la CDA.
"Najiandaa kuachana na Coastal Union na kutua CDA baada ya kufuatwa na viongozi na
Jumamosi timu hizo mbili zitacheza mechi maalum ya kirafiki Coastal ikiniaga na CDA
kunikaribisha na kitakaa kwenye mabechi ya timu zote mbili kwa kila kipindi," alisema.
Julio alisema japokuwa imekuwa ngumu kwa makocha wenye majina kama yeye kukubali
kuzinoa timu za madaraja ya chini, lakini yeye anataka kuisaidia timu hiyo hadi ipande Ligi Kuu Tanzania Bara kuwahamasisha wengine kujitolea kusaidia timu za chini.
Kitendo cha kocha huyo kukaa katika benchi za timu mbili tofauti katika mchezo huo
itamfanya Julio aweke historia ya aina yake nchini, ingawa marehemu Syllersaid Mziray aliwahi kuzifundisha Simba na Yanga kwa wakati tofauti katika michuano ya Kombe la AICC mwishoni mwa miaka ya 1980, iliyokuwa ikifanyika mjini Arusha.

Mwisho