STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 15, 2011

Twiga Stars kuanza na Ghana All African Games

SHIRIKISHO la Soka Afrika, CAF, imetangaza ratiba ya michuano ya soka kwa timu za wanawake zinazoshiriki michuano ya Afrika (All African Games) ambapo timu ya taifa ya Tanzania, Twiga Stars itaanza kibarua chake kwa kuumana na Ghana.
Michuano hiyo ya Afrika inatarajiwa kuanza kufanyika Septemba 3-18 kwenye mji wa Maputo, Msuimbiji, ambapo kwa mujibu wa ratiba hiyo ya CAF ni kwamba Twiga iliyopo kundi B itafungua dimba kwa kuumana na Ghana siku ya Septemba 5.
Timu zingine zilizopo katika kundi hilo ni Afrika Kusini na mabingwa wapya wa Kombe la COSAFA, Zimbabwe.
Ratiba hiyo ya CAF inaonyesha kuwa Twiga itashuka dimbani tena Septemba 8 kucheza na Afrika Kusini kabla ya kumaliza mechi zake, Septemba 11 kwa kucheza na Zimbabwe.
Twiga imejikuta kundi moja na timu hizo mbili ambazo ziliichachafya katika michuano ya Kombe la COSAFA, ambapo Afrika Kusini waliokuwa nao kundi moja waliwalaza bao 1-0 kabla ya Zimbabwe kuifunga kwenye mechi ya nusu fainali kwa mikwaju ya penati 4-2.
Timu zingine zitakazoshiriki michuano hiyo na zilizopangwa kundi A ni wenyeji Msumbiji, Cameroon, Algeria na Guinea, ambapo washindi wawili wa kwanza wa kila kundi ndizo zitakazosonga mbele kwa hatua ya nusu fainali.
Nigeria ndiyo waliokuwa mabingwa wa mwaka 2007, lakini hawakufanikiwa kufuzu
kwa michuano hiyo mwaka huu ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne.
Wakati huo huo mikoa mitatu ya Dodoma, Mwanza na Ruvuma imeteuliwa kuwa vituo vya kuendeshea semina na mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa waamuzi wa daraja la pili na tatu inayotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kupitia Afisa Habari wake, Boniface Wambura, ni kwamba semina na mitihani hiyo itafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Agosti 2-5 katika vituo hivyo.
Taarifa hiyo inasema washiriki wa semina na mitihani hiyo watajitegemea kila kitu kuanzia gharama za usafiri, chakula na malazi, huku vyama vya soka vya mikoa ya Tanzania Bara vikihimizwa kuwakumbusha washiriki kuhudhuria semina na mafunzo hayo kwa faida yao.
Iliongeza kuwa semina na mitihani hiyo itatumika kuwapandisha daraja washiriki hao.
Hiyo ni semina ya pili kuandaliwa na TFF ndani ya kipindi kifupi ikiwa ni maandalizi na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani karibu wiki moja sasa ilikuwa ikiendesha semina kama hiyo inayowahusisha waamuzi wa daraja la IA na IB iliyokuwa ikifanyika katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Semina na mitihani hiyo ilianza Julai 13 na inatarajiwa kufungwa leo Julai 16.

Stars kukipiga ughaibuni na Palestina, Jordan

KATIKA kujiweka fiti kabla ya kumaliza viporo vya michezo yake miwili iliyosalia ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika za mwaka 2012, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kwenda Mashariki na Kati kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuopitia Afisa Habari wake, Boniface Wambura inasema, Stars itaumana na timu za mataifa ya Palestina na Jordan mapema mwezi ujao.
Wambura alisema mechi ya kwanza ya timu hiyo inayoshikilia nafasi ya tatu katika kundi D lenye timu za Morocco, Afrika ya Kati na Algeria, itachezwa siku ya Agosti 10 katika mji wa Ramallah dhidi ya wenyeji wao Palestina.
Mechi ya Tanzania na Palestina itakuwa ni kama marudiano, kwani mapema mwaka huu timu hizo zilipepetana hapa nchini katika pambano jingine la kirafiki la kimataifa.
Katika mechi hiyo ilichezwa Februari 9 kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Stars iliitambia Palestina kwa kuilaza bao 1-0, bado lililofungwa na winga mahiri, Mrisho Ngassa ambaye kwa sasa yupo Marekani kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Seattle Sounders inayoshiriki ligi ya Marekani, MLS.
Wambura aliongeza Stars itashuka tena dimbani Agosti 13 kupepetana na Jordan katika pambano litakalochezwa kwenye mji mkuu wa nchi hiyo ya Jordan, Amani.
Wambura alisema Stars itaondoka nchini Agosti 7 na kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kutajwa mara baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen kurejea kutoka mapumziko nchini Denmark, mapema mwezi ujao.
Stars inahitaji ushindi katika mechi zake zilizosalia dhidi ya Algeria itakayochezwa nyumbani na ile ya mwisho dhidi ya Morocco, iwapo inataka kufuzu fainali hizo za Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

Hatimaye Sunzu atua Bongo


MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa timu ya Al Hilal ya Sudan, Felex Sunzu ametua nchini mapema leo tayari kufanya mazungumzo na klabu ya Simba ili kuichezea tyimu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2011-2012.
Sunzu alitua leo asubuhi akiambatana na mkewe na hadi wakati huu alikuwa akiendelea kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba ili kuweza kumwaga wino wa kuichezea klabu hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu aliyempokea mshambuliaji huyo aliyeng'ara kwenye mihuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana akiichezea Zambia, iliyoalikwa amesema wakati wowote wataweka taarifa juu ya kumnasa rasmi mkali huyo.
Kwenye uwanja wa ndege, Sunzu ambaye alikuwa akitokea mapumzikoni nchini Nigeria, alisema amekuja nchini na kama atapata fursa ya kumalizana na Simba basi mashabiki wa timu hiyo watarajie makubwa kutoka kwake muhimu apewe ushirikiano.
Nyota huyo ambaye ameshindwa kuitumikia Al Hilal kwa kiwango stahiki kiasi cha klabu yake kutaka kumtoa kwa mkopo, alisema anazifahamu Simba na Yanga na anaimani atang'ara nchini kama ilivyo kwa mzambia mwenzake Davis Mwape aliyepo Yanga.
Simba inahaha kusaka mshambuliaji wa kuziba nafasi ya Mbwana Samatta aliyenunuliwa na TP Mazembe, ambayo Sunzu anaonekana kama 'muarubaini'wa tatizo la safu butu ya ushambuliaji ya timu hiyo iliyoshindwa kutwaa taji la Kagame kwa kulazwa na Yanga bao 1-0 katika mechi ya fainali baina yao iliyochezwa Jumapili iliyopita.

Rostam Aziz alipobwaga manyanga IgungaUTANGULIZI

WAZEE wangu, kwanza kabisa kabla ya kueleza kile ambacho kimenisukuma kuzungumza nanyi leo, napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kufikia siku hii ambayo inatukutanisha waja wake.

Wazee wangu wa Igunga, baada ya kufanya hivyo napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru ninyi nyote mmoja mmoja na katika umoja wenu kwa kuitikia wito wangu, kijana wenu, niliyewaomba nije nizungumze nanyi siku hii ya leo.

Nafanya hivyo nikitambua vyema kwamba, kama si nyinyi wazee wangu na wengine wengi ambao hatuko nao hapa leo kwa sababu mbalimbali, ambao mmekuwa na imani kubwa nami nisingeweza kufikia hapa nilipofika sasa.

Wazee wangu, waasisi wa taifa letu walitufundisha kutambua na kuheshimu ukweli kwamba; ‘Uongozi ni Dhamana’ dhana ambayo kila ninapokaa na kutafakari huwa inanirejesha nyuma na kukumbuka jinsi nyinyi mlivyokaa katika umoja wenu na kuniteua mimi, miongoni mwa vijana wenu wengi, kuwa mwakilishi wa Jimbo la Igunga tangu mwaka 1994.

Katika kipindi hicho chote cha utumishi wangu, nyinyi wazee wangu mmekuwa mhimili muhimu ambao umeniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu nikitambua namna ambavyo mmekuwa na imani kubwa juu yangu.

Ari na moyo wa imani, ushirikiano na mshikamano ambao wazee wangu mmekuwa nao kwangu ndiyo ambao kwa kiwango kikubwa umetuwezesha kufanya kazi kwa pamoja, tukishinda changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilikabili jimbo letu katika kipindi chote ambacho mmeendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.

Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

Miongoni mwa mafanikio makubwa tuliyoyafikia kupitia ushirikiano wetu na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora lakini leo ndiyo ya kwanza, taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.

Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi chote ambacho mmendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.

Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi hicho chote hayajaweza kumaliza changamoto zote za maendeleo ambazo zinatukabili.

Wazee wangu, ingawa nimekuwa na kawaida ya kukutana na kuzungumza nanyi mara kwa mara, mmoja mmoja na wakati mwingine katika umoja wenu, wito wangu wa leo una makusudi ambayo kwa kiwango kikubwa ni tofauti na yale ambayo tumeyazoea.

Japokuwa ujumbe ninaotaka kuzungumza nanyi wazee wangu, si mgeni sana masikioni mwenu, tofauti ya leo na mikutano yetu mingine iliyopita ni uamuzi ambao nimekusudia kuufanya na ambao nitayatangaza muda mfupi ujao.

YATOKANAYO

Wazee wangu, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini na hususani afya ya kisiasa na matukio mengine ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho mimi ni mwanachama wake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) nikiuwakilisha Mkoa wetu wa Tabora.

Naamini kwamba katika kufuatilia kwenu mtakuwa mmebaini kuwapo kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakitokea huku yakiligusa jina langu na wakati fulani nafasi yangu kama kiongozi wa chama hicho.

Wazee wangu, nayasema hayo kwa sababu mara kwa mara ninapokutana nanyi nikiwa katika ziara zangu jimboni na wakati mwingine mnapowasiliana nami kwa njia mbalimbali mmekuwa mkionesha kuguswa kushitushwa na kutaka kujua kulikoni kuhusu mambo hayo yanayotokea.

Mimi, kama mnavyonijua nyote, ni mtu muwazi na mkweli. Siku zote nimekuwa mwepesi sana wa kuwaeleza kuhusu kila kinachotokea ili kuwaondoa hofu na wakati huo huo kuwahakikishia kwamba masuala yasiyo na msingi hususani yale yanayogusa siasa za kitaifa hayawezi kutuondoa katika mstari sahihi wa kuwahudumia wananchi wa Igunga, mkiwamo nyinyi wazee wangu ambao mmeniamini na kunituma kuwawakilisha.

Nyinyi wenyewe ni mashahidi wazuri kwamba tangu matukio yanayogusa jina langu yaanze kutokea miezi michache tu baada ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikweti kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, tumekuwa tukiyapuuza na tukaendelea kufanya kazi pamoja kwa bidii.

Bado naamini na nitaendelea kuamini kwamba tulifanya uamuzi sahihi wa kuyapuuza matukio hayo kwani mbali ya kuendelea kutimiza malengo mbalimbali yaliyokuwamo katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM, pia mliendelea kuniamini kwa nafasi yangu ya kuwa mwakilishi wenu bungeni na hata mkaniruhusu nibebe jukumu jingine kubwa la kuwa Mjumbe wa NEC ninayewakilisha mkoa wetu wa kihistoria wa Tabora.

Wazee wangu, nyinyi ndiyo watu mnaolifahamu vyema jimbo letu la Igunga na hakika nyinyi ni sehemu muhimu ya watu wanaojua historia ya kisiasa ya Mkoa wa Tabora kwa miaka mingi hata kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Hakuna shaka hata kidogo kwamba, Tabora ni kitovu hasa cha uasisi wa siasa za vyama vingi hapa nchini. Ni wazi kwamba huwezi ukazungumzia chimbuko la vyama vya upinzani tunavyoviona hapa nchini leo pasipo kugusa mkoa huu ambao umekuwa chimbuko la wanasiasa wenye mizizi hapa na nchini kwa ujumla.

Majina ya wanasiasa wa aina ya wazee wetu, hayati Chifu Said Abdallah Fundikira na Christopher Kassanga Tumbo, Kasela Bantu (Mungu awalaze mahala pema peponi), James Mapalala, Profesa Ibrahim Lipumba na mengi mengine yana mizizi yao katika Mkoa wetu wa Tabora.

Kutokana na ukweli huo basi ni wazi kwamba, nikiwa Mbunge wa Igunga kwa vipindi vinne mfululizo na wakati huo huo nikiwa Mjumbe wa NEC kwa vipindi vitatu mfululizo, moja ya kazi ambazo nimezifanya kwa uaminifu na kwa bidii kubwa huku nikiungwa mkono na kushirikiana nanyi ni ile ya kuhakikisha kwamba mkoa huu pamoja na kuwa kitovu cha upinzani unaendelea kubakia kuwa ngome muhimu ya kisiasa ya CCM.

Si vibaya tukakumbushana kwamba, wakati nachaguliwa kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa mwaka 1997, jimbo moja katika mkoa wetu lilikuwa likishikiliwa na upinzani. Leo hii Tabora ni mkoa pekee miongoni mwa mikoa iliyotuzunguka ambao haukupoteza jimbo hata moja kwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2010. Mafanikio haya tuliyafikia kwa pamoja kutokana na ushirikiano wenu wazee wangu.

Wazee wangu, Waswahili wanasema usione vyaelea, vimeundwa. Kazi ya kuijenga CCM katika mazingira yenye mizizi hasa ya upinzani nikiwa mbunge na hususani M-NEC kutoka Mkoa wa Tabora haijapata kuwa rahisi na itaendelea kuwa ngumu na ambayo mapambano yake ni makali sana.

Wazee wangu, kwa namna ya pekee kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyinyi wazee wangu wa Igunga na wananchi wenzangu wote wa Mkoa wa Tabora kwa kushikamana na kuifanya kazi hiyo kwa bidii, uaminifu na mafanikio makubwa.

Matunda ya kazi hiyo kubwa yanaonekana. Pamoja na kuwa kitovu cha kihistoria cha siasa za upinzani, Tabora ndiyo mkoa pekee katika eneo hili ambao unaongozwa na wabunge wote kutoka CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na hata kabla ya hapo.Kwa sababu hiyo basi, wazee wangu, sote katika umoja wetu ukiacha mafanikio makubwa tuliyopata katika jimbo na Wilaya yetu ya Igunga, tunayo mambo mengine ya msingi ya kujivunia. Kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa napenda kuwapongeza kwa namna mlivyojitoa kukipigania na kukitetea chama chetu kwa ari na nguvu ya kipekee.KUJIVUA GAMBAWazee wangu, chama chetu chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kimeamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya chama chetu ilitangazwa rasmi na Mwenyekiti wetu Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma.Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘Kujivua Gamba’.Wazee wangu hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho mimi nilikuwa mjumbe wake.Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya chama chetu wa wakati huo kwa kauli moja tulikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa Mwenyekiti wetu fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa Chama.Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana.Niliseme kwa maneno machache tu hili. Ingawa ni kweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha madarakani chama chetu kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi tulichopata kimeonyesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwetu kuilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia aislimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule.Tungekuwa ni chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo tungekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.Matokeo hayo ya uchaguzi ambayo hapana shaka yamekitikisa chama chetu yalitukumbusha wasia ambao tuliachiwa na Baba wa Taifa aliyesema; ‘Bila ya CCM Madhubuti Nchi Yetu Itayumba’.Wazee wangu, kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu kama nilivyosema awali, mimi na wenzangu tuliokuwa katika Kamati Kuu tuliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kututaka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama chetu.KUJIVUA GAMBA KWAPOTOSHWAWazee wangu, kilichotokea baada ya kujiuzulu kwetu kila aliye ndani na nje ya chama chetu amekisikia na anakifahamu. Chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wetu mpya, Mhe. Wilson Mukama, na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti wetu aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mhe. John Chiligati, na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Mhe. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo.

Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.Niliseme hili mapema. Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa yaliyo ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.Wazee wangu, nyinyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.Wazee wangu, ni wazi kwamba kama chama chenye siasa chenye dhamana ya kuwaoongoza Watanzania kutoka katika lindi la ufukara, maradhi, matatizo ya makaazi na mengineyo siku zote tunapaswa kuwa makini katika kuhakikisha kwamba changamoto za kuwaongoza na kuwakomboa wananchi waliotupa dhamana hazitikiswi na mawimbi ya matakwa ya nyakati ama ya vyombo vya habari au wapinzani wetu wa kisiasa walio nje ya CCM.Ni kwa sababu ya kulitambua hilo na hasa kuyatambua madhara yanayoweza kukipata chama chetu na nchi yetu iwapo tutaendekeza siasa za kupakana matope pasipo na sababu za msingi, kuchafuana kusikokoma na kulipizana kisasi ndiyo maana nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi wazee wangu ili kuweka kumbukumbu sahihi.MAAMUZI YANGUWazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara. Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi kwa sababu tofauti na wengine wengi hapa nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa.

Katika ulimwengu wa kibiashara wa leo, vita hivi ambavyo vinaweza kuonekana kuwa ni vidogo tu vyenye malengo ya kuchafuana kisiasa, vinakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa kibiashara kuliko hata wale wasioelewa wanavyoweza kukadiria. Ndiyo maana nimeona ni afadhali sasa niwape nafasi wale wanaoendesha siasa hizi uchwara na zisizo na tija waendelee na siasa zao hizo ambazo kwa bahati mbaya kwao, mimi sina muda nazo na siwezi kuwa sehemu yake. Na mimi kwa upande wangu niendelee na maisha yangu.Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.Aidha, nimefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wangu ambao naamini baada ya mimi kujitoa watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizo nazo za kukiongoza chama chetu na nchi yetu kupitia Serikali yake.Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kwa upande mwingine, uamuzi wangu huu naona ni fursa kwa viongozi wa Chama changu cha CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama chetu na ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.Sambamba na hilo, ninayo imani thabiti kwamba, uamuzi wangu wa kubakia kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM utakuwa chachu kwa chama changu na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.Mwisho kabisa, nikimalizia naomba nitumie fursa hii kutoa heshima za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa aliyoifanyia na anayoendelea kuifanyia nchi yetu. Amefanya mengi na makubwa kuiendeleza nchi yetu na watu wake kuliko inavyothaminiwa na kufahamika. Kazi yake kubwa inashindwa kuthaminiwa na kufahamika kutokana na siasa chafu tunazoziendesha Tanzania. Wasia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa ujumla ni kuwa tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndiyo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo.

Wazee wangu, baada ya maelezo hayo, nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kunielewa.Ahsanteni sana.
Mwisho…

Ndolo, Fabriges wagonganisha vichwa Yanga


PANGA pangua ya nani abaki na yupo atoke kati ya Tonny Ndolo na Haruna Niyonzima 'Iniesta' ndani ya usajili mpya wa mabingwa wapya wa Kombe la Kagame, Yanga, imeibua mzozo ndani ya klabu hiyo.
Ndolo, Mganda aliyesajiliwa toka Kagara Sugar na Iniesta aliyetoka APR ya Rwanda, mmoja kati yao anapaswa kuachwa kwenye usajili ili kutekelezwa kwa kanuni ya idadi ya wachezaji wa kigeni wanaopaswa kusajiliwa na klabu za soka nchini.
Yanga tayari imetimiza idadi ya wachezaji sita wa kigeni, mmoja zaidi ya idadi inayotakiwa na TFF na kwa maana hiyo kuilazimisha klabu hiyo kupunguza jina moja na mzozo unakuja juu ya nani aachwe kati ya wachezaji hao wawili kutokana umuhimu wao katika kikosi hicho.
Awali ilikuwa ikitajwa kwamba mshambuliaji Hamis Kiza 'Diego' ndiye aliyekuwa katika hatihati ya kubakishwa Yanga, lakini kwa kiwango alichokionyesha kwenye michuano ya Kagame akiifungia mabao muhimu akishirikiana na 'mapro' wengine wawili, Davis Mwape wa Zambia na Kenneth Asamoah aliyewapa ubingwa mbele ya Simba, hali imekuwa kizungumkuti.
Mchezaji mwingine wa kigeni aliyepo Yanga ni kipa Yew Berko kutoka Ghana ambaye msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara alichaguliwa kuwa Kipa Bora akimfunika Juma Kaseja.
Habari za ndani za klabu hiyo zinasema mapendekezo ya kocha Sam Timbe tangu awali ni kuachana na Iniesta, lakini kamati ya usajili imekuwa ikimkumbatia kiungo huyo, ikitaka wa kuachwa awe Ndolo, kitu ambacho kocha hataki kusikia kutokana na kumhitaji nyota huyo.
Hali hiyo imefanya hata Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu kushindwa kujua ukweli yupi kati ya wachezaji hao wawili ndiye atakayeachwa wakati dirisha la uhamisho wa wachezaji likifungwa Alhamisi iliyopita.
"Kwa kweli mie sijui nani ataachwa, ila hatma yao itafahamika wakati wowote kwa vile tunajua tunatakiwa kupunguza jina la mchezaji mmoja kutokana na kuzidisha idadi ya wachezaji wa kigeni inayotakiwa na kanuni za usajili nchini," alisema Sendeu.

Msiwaite wafanyakazi wenu wa ndani majina mabaya


WAAJIRI wa wafanyakazi wa majumbani nchini, wameombwa kuachwa kuwaita majina
mabaya watumishi wao, kwa madai kufanya hivyo ni kushusha hadhi na utu wa wafanyakazi hao ambao ni watu muhimu kwao na familia zao kwa ujumla.
Kadhalika wametahadhariwa kuepuka tabia ya kuwaajiri wafanyakazi wenye umri chini ya
miaka 17 kutokana na ukweli umri huo ni mdogo kwa ajira na pia ni kosa kulingana na sheria za kimataifa kuhusu ajira za watoto.
Hayo yalisemwa na wawezeshaji wa semina ya siku moja ya 'Waajiri Makini' iliyoandaliwa na Shirika la kuhudumia Afya na Maendeleo ya Wanawake na Watoto ya Kiota, (KIWOHEDE), walipokuwa wakitoa mafunzo ya kujenga mauhusiano bora kati ya waajiri na wafanyakazi wa majumbani, iliyofanyika katikati ya wiki iliyopita.
Edda Kawala na Stella Mwambenja wote kutoka KIWOHEDE, walisema tabia ya waajiri
kuwaita majina mabaya watumishi wao na kuwanyanyasa au kuwabagua ni jambo baya kwani
linashusha hadhi na utu wa wafanyakazi hao kinyume na sheria na mikataba wa kazi kimataifa.
Wawezeshaji hao walisema ni wajibu waajiri kuishi kwa wema na watumishi wao kwa
kuwafanya kama sehemu ya familia zao badala ya kuwabagua na kunyanyapaa, kitu ambacho sio ubinadamu na kinachochangia uhasama usio na maana baina ya wawili hao.
Pia waliwataka waajiri kuchungua kuajiri wafanyakazi wenye umri mdogo ili wasiweze kunasa kwenye mikono ya sheria inayokataza ajira kwa watoto.
"Mbali na kuchunga umri, pia msiwe mnawabagua wafanyakazi wenu wakati wamekuwa
msaada mkubwa katika majumba yenu kwa kazi wanazowafanyia, muwalipe vema na kwa
wakati kwa vile nao ni wanastahili mahitaji kama watu wengine," alisema Stella.

Wafanyakazi wa Majumbani sasa wapata 'Rungu'

KUPITISHWA kwa Mkataba wa Kimataifa wa 189 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO,
kumeelezwa kuwa kama ni 'rungu' kwa wafanyakazi wa majumbani kuwashughulikia waajiri
wao watakaokiuka sheria na mikataba ya kazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine nchini.
Mkataba huo wa kuwatambua wafanyakazi hao wa majumbani ulipitishwa Juni 16 mwaka huu
katika mkutano wa 100 wa ILO uliofanyika nchini Uswisi, ambapo siku moja kabla ya
kupitishwa kwake, Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alihutubia mkutano huo kuuridhia,
Akizungumza na MICHARAZO, Mratibu wa Shirika la Wafanyakazi wa Majumbani Kanda ya
Afrika, IUF, Bi Vick Kanyoka, alisema kuridhiwa kwa mkataba huo kumetoa fursa na nafuu kwa watumishi hao wa majumbani ambao kwa miaka mingi walikuwa hawathaminiwi nchini.
Bi Kanyoka, alisema kulingana na mkataba huo ni kwamba wafanyakazi wa majumbani kwa
sasa wanatambuliwa kama wafanyakazi wengine wakihitajiwa kulindwa na kupewa haki zao
ikiwemo kusainishwa mikataba na makubaliano kabla ya kuanza kazi kwa muajiriwa.
Mratibu huyo alisema kitu cha muhimu baada ya kupitishwa kwa mkataba huo ni serikali ya Tanzania na wananchi wake kuutekeleza kwa vitendo mkataba huo ili kuhakikisha wafanyakazi wanajivunia kazi yao tofauti na siku za nyuma walipokuwa wakijificha.
"Kwa hakika kupitishwa kwa mkataba huo wa 189 ni kama rungu kwa wafanyakazi wa
majumbani kuweza kuwabana waajiri wao, ambao kwa miaka mingi walikuwa wakiwabagua,
kuwanyanyasa na kuwadharau wakiwachukulia kama 'vijakazi'," alisema.
Aliongeza kwa kuwataka watumishi hao kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa mkataba huo kwa kutokubali kuajiriwa kabla ya kuingia mkataba na kuridhia haki zake stahiki katika ajira yake, ili inapotokea tatizo mbele ya safari iwe rahisi kusaidiwa.
Bi Kanyoka, aliwasihi pia waajiri kuridhia na kuutekeleza mkataba huo kwa kuamini watumishi hao ni kama sehemu za familia zao na hivyo kuwapa huduma na stahiki zote ikiwemo kuwalipa fedha kulingana na kima wanachokubaliana na kwa muda muafaka.
"Pia wawajali na kuwathamini kwa sababu wao ni watu tegemeo kwao na familia zao, hivyo kukaa nao kwa ubaya ni kusababisha matatizo ambayo tumekuwa tukishuhudia katika jamii yetu," alisema.
Mratibu huyo alisema mkataba huo ulipitishwa kwa kupigiwa kura 396 za ndio huku kura 16 zikiukataa miongoni mwa nchi zilizougomea ikiwa ni taifa la Uingereza, huku mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania na yale ya Amerika Kusini na Kaskazini yakiongoza kwa kuupitisha.