STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 16, 2010

Amer Lugunga Mwenyekiti Mpya Halmashauri ya Kilosa

DIWANI wa Kata ya Kimamba, wilayani Kilosa, Amer Lugunga, amefanikiwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kuwaangusha wagombea wenzake wenzake wawili.
Wagombea walioangushwa na Lugunga, ni pamoja na Leonard Mapunda na mtu mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mbiza.
Katika mchuano huo uliofanyika kwenye ofisi za CCM wilaya ya Kilosa, Lugunga aliibuka mshindi kwa kuzoa jumla ya kura 40 kati ya 60 zilizopigwa kwenye kinyang'anyiro hicho kilichokuwa na ushindani mkali.
Mbiza alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 17 na Mapunda aliambulia tatu tu.
Akizungumza na MICHARAZO mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Lugunga alisema atafanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kuhakikisha Kilosa inaondokana na aibu iliyoighubika kwa sasa.
"Nawashukuru walionichagua, na ahadi yangu ni kwamba nitafanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, ili kuirejeshea heshima wilaya yetu iliyopewa hati chafu hivi karibuni kutokana na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo," alisema Lugunga.
Alipoulizwa juu ya 'zengwe' alilokuwa akiwekewa na baadhi ya wapinzani wake, Lugunga, alisema mambo yote yameisha na hana kinyongo na mtu.

Mwisho

Extra Bongo yawanyatia akina Chokoraa

BAADA ya bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kuwatimua kundini, wanamuziki wao nyota wawili, Khalid Chokoraa na Kalala Junior, uongozi wa bendi ya Extra Bongo, umeanza mipango ya kuwachukua wanamuziki hao kuimarisha kikosi chao.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki, aliiambia MICHARAZO kuwa, tayari wameshaanza mazungumzo ya awali na wanamuziki hao ambao pia wanaunda kundi la Mapacha Watatu wakishirikiana na Jose Mara wa FM Academia.
Choki alisema walikuwa na mipango ya kuwachukua waimbaji hao kitambo kirefu,ila walikuwa wakisita kuhofia kutifuana na uongozi wa Twanga Pepeta, lakini kutimuliwea kwao kwa utovu wa nidhamu ni kama kumewarahisishia kazi.
"Kutimuliwa kwao Twanga Pepeta kumeturahisishia kazi ya kuwapata waimbaji hawa wenye vipaji vya aina yake na tumeshaanza mazungumzo ya awali, nadhani ndani ya wiki hii mambo yatakuwa shwari na wataanza kazi Extra Bongo," alisema Choki.
Choki aliongeza katika kuonyesha kuwa wapo karibu na wanamuziki hao na kuwakubali kwa kazi zao kupitia kundi lao la Mapacha watatu wanatarajia kufanya nazo onyesho la pamoja wakati wa Mkesha wa Mwaka Mpya na siku ya Mwaka Mpya wenyewe jijini Dar es Salaam.
Alisema onyesho la kwanza baina yao na Mapacha Watatu linalotamba na albamu ya 'Jasho la Mtu' litafanyika mkesha wa Mwaka Mpya, Vatican Hotel, Sinza na kisha siku ya Mwaka Mpya watakuwa wote pale TCC Chang'ombe.
"huwezi jua kwenye maonyesho hayo mawili yanaweza kutumiwa kama utambulisho wao ndani ya Extra Bongo," Choki alitania.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, lengo la bendi yao ni kutaka kuona wanatamba kwenye muziki wa dansi nchini baada ya kurejea kwa mara ya pili baada ya kufariki enzi ikitumia miondoko ya 3x3.
Choki aliongeza wakati wakiwa, katika harakati hizo za kuwanyakua akina Chokoraa, aliyekuwa mmoja wa waasisi wa Extra Bongo ya awali, pia bendi yao inajiandaa kufanya uzinduzi wa albamu ya 'Mjini Mipango'.
Alisema uzinduzi uliofanyika Mei 25 mwaka huu ulikuwa ni wa bendi yao iliyofufuliwa upya na sio wa albamu kama baadhi ya watu walivyokuwa wanadhani na hivyo wanajipanga kuifanyia uzinduzi wake.
Choki alisema watazindua albamu hiyo yenye nyimbo sita ambazo baadhi zinaendelea kutamba kwenye vituo vya redio na runinga, huku wakiendelea kuandaa ya pili ambayo tayari baadhi ya nyimbo zake zimeshakamilika.

Dk Remmy kuzikwa leo

SAFARI ya mwisho ya hapa duniani kwa mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi na ule wa Injili, Ramadhan Mtoro Ongalla 'Dk Remmy' aliyefariki mapema wiki hii, inatarajiwa kuhitimishwa rasmi leo atakapozikwa kwenye makaburi ya Sinza, jirani na nyumbani kwake.
Remmy, aliyezaliwa nchini Zaire (sasa DR Congo) miaka 63 iliyopita alifariki Jumatatu baada ya kuugua kwa muda mrefu atazikwa jioni ya leo kwenye makaburi hayo baada ya kuagwa kwa tamasha la muziki wa Injili kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, jijini.
Mjomba wa marehemu, Mzee Makassy, alisema mwili wa marehemu utazikwa kwenye makuburi hayo jirani kabisa na mahali alipokuwa akiishi, Sinza kwa Remmy.
Marehemu Remmy aliingia nchini mwaka 1977 na kujiunga na bendi ya mjomba wake, Makassy Band na kutamba na kibao cha Siku ya Kufa kabla ya baadae kuhamis Super Matimila ambayo ilimpa umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake wa kutunga, kuimba na kupiga gita la solo ambapo alishiriki matamasha makubwa barani Ulaya mara kwa mara.
Hata hivyo miaka michache iliyopita alipata kiharusi na kupooza, ambapo aliamua kuokoka na kuanza kutumikia muziki wa Injili hadi mauti yalipompata akiwa ameacha mke na watoto kadhaa akiwemo mshambuliaji wa timu ya Azam, Kalimangonga 'Kally' Ongalla.
Bwana Alitoa Naye Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe. Micharazo tunamtakia safari njema aendako nasi tu nyuma yake kwa kuwa kila nafsi ni lazima ionje mauti.