STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 1, 2012

Azam Marine yaleta meli ya kisasa, abiria kusafiri na magari yao

Kampuni za meli za Azam Marine, imeamua kufanya kweli ambapo hivi karibuni inatarajia kuzindua meli kubwa ya kisasa ambayo itawawezesha abiria wake kwenda na magari yao visiwani Zanzibar. Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Hussein Mohammed Said, amesema Julai 15 mwaka huu meli hiyo yenye urefu wa mita 100 itazinduliwa. Mohamedi alisema shida ya usafiri itapungua kwa asilimia kubwa kutokana na meli hiyo kuwa na uwezo wa kubeba abiria 1500, Mizigo tani 500 na magari 200 ambapo abiria atakae jisikia kwenda na gari lake Zanzibar, Pemba au Dar es Salaam ataweza kufanya hivyo. Waziri Mwenye dhamana ya Mawasiliano na Miundombinu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hamadi Masoud, alithibitisha kwamba ana taaarifa za ujio wa meli hiyo ambayo alisema kwa kiasi kikubwa itakuwa ni ya kutoa huduma tu na siyakutengeneza faida. Meli hiyo inauwezo wa kwenda kasi ya notkomail 20.
MELI HIYO INAVYOONEKANA NDANI NA NJE

Lamata: Muongozaji anayeota kuwafunika 'madume' kimataifa

HUENDA akawa ndiye muongozaji pekee wa kike anayewapeleka puta waongozaji wengine wa kiume waliojaza nchini kwa namna anavyoifanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu. Wengi wanamfahamu kwa jina la 'Lamata', ingawa majina yake halisi ni Leah Richard Mwendamseke, mmoja wa waandishi wa miswada na waongozaji mahiri wa filamu nchini. Lamata, alisema aliipenda kazi hiyo tangu akiwa mtotoni na ndio maana alitumia muda mfupi kama muigizaji akiwa na kundi la Amka Sanaa lililorusha michezo yake katika kituo cha ITV kabla ya kugeukia uongozaji wa filamu. Mwanadada huyo alisema, mara alipoosha 'nyota' kwa kushiriki igizo la 'Ndoano' alijiunga na kampuni ya RJ chini ya Vincent Kigosi 'Ray' na Blandina Chagula 'Johari' kuandaa filamu huku akijifunza uongozaji kabla ya kuianza rasmi kazi hiyo mwaka 2010. Lamata, anayemiliki kampuni yake binafsi iitwayo 'Lamata Enterteinment, alisema kupenda kwake kuangalia filamu na kusoma vitabu vimechangia kuwa 'malkia' wa uandishi miswada na kuongoza filamu kazi aliyodai imemsaidia kwa mengi kimaisha. Alisema mbali na Ray, pia hawezi kuwasahau Salles Mapunda na Adam Kuambiana waliomnoa sambamba na kujifunza uongozaji wa filamu kupitia njia ya mtandao kiasi cha kuwa muongozaji pekee wa kike anayeifanya kazi hiyo kama ajira rasmi. Baadhi ya kazi alizoziandika na kuziongoza ni pamoja na Candy, All about Love, My Angel, Rude, My Princess, Tears Forever, Time After Time, Dunia Nyingine, Mke Mwema, Mr President, Chocolate, Life to Life, The Avenger, Family War na kazi zilizopo njiani kutoka za House Maid na Injinia. Lamata anayependa kula pilau na chips kwa kuku na kunywa vinywaji laini, alisema kati ya kazi zote alizoziandika na kuziongoza zilizo bomba kwake na kujivunia ni Candy na Rude. Mwanadada huyo anayechizishwa na nguo za rangi ya zambarau na pinki, alisema kabla ya kuingia kwenye filamu aliwazimia mno Desire Washington, Mel Gibson na James Canon, Juu ya filamu Bongo, Lamata ambaye hajaolewa wala kuwa na mtoto ingawa anatamani kuja kuzaa watoto watatu atakapoolewa, alisema imepiga hatua kubwa kulinganisha na miaka ya nyuma ila alisema wapo watu wachache wanaoikwamisha kuvuka mipaka ya kimataifa. Alisema ni watayarishaji wabishi wasiokubali kukosolewa na kugawa majukumu ya kazi kwa wengine na wasanii wasiotambua wapo katika fani hiyo kwa ajili ya kitu gani. Pia alisema wizi na uharamia uliokithiri katika fani hiyo na kukosekana kwa wasambazaji wengi wa kutosha ni tatizo ambalo aliiomba serikali kujaribu kuwasaidia ili wasanii wainuke kimaisha. Lamata mwenye ndoto za kuja kuwa muongozaji wa kimataifa na kujikita kwenye biashara, alimtaja msanii Jacklyne Wolper kama msanii anayemkubali na kumuona yupo makini katika fani hiyo nchini na anayefurahia kufanya nae kazi kama ilivyo kwa Jennifer Kyaka 'Odama'. Muongozaji huyo aliyewaasa wasanii na wadau wote wa filamu kupendana na kushikiana, alisema ukimuondoa Mungu na Yesu Kristo wengine anawashukuru kumfikisha alipo ni Ray, Wolper na Daniel Basila. Leah Richards Mwendamseke 'Lamata' alizaliwa miaka kadhaa iliyopita mjini Mbeya akiwa mtoto wa mwisho wa familia ya watoto sita na alisoma Shule za Msingi Ikuti na Karobe kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari za Arage Mbeya aliyosoma hadi kidato cha pili. Alimalizia masomo yake ya sekondari katika shule ya Wanging'ombe ya mjini Iringa na kisha kuendelea na masomo ya juu ya Sekondari Shule ya Perfect Vision kabla ya mwaka 2008 kujitosa kwenye sanaa akianzia kundi la Amka Sanaa lililotamba katika kituo cha ITV.

LEO NDIO LEO FAINALI ZA UERO 2012

MABINGWA watetezi wa Kombe la nchi za Ulaya, Hispania leo inatarajiwa kushuka dimbani kujaribu kuendeleza rekodi yake katika michuano ya kimataifa kwa kuvaana na Waitalia. Timu hizo mbili zilizofuzu fainali za mwaka huu za barani humo, zitaavanaa kila moja ikitaka kudhihirisha ubabe wake baada ya mechi yao ya awali ya makundi kuisha 1-1. Baina ya nchi hizo Hispania na Italia zimetoa mabingwa 25 wa Ulaya katika ngazi ya klabu lakini hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu zao za taifa kukutana katika fainali ya kombe la Mataifa ya Ulaya. Ni wachache watahoji uhalali wa timu hizo kufika fainali. "Mshindi atakuwa bingwa anayestahili," alisema kiungo wa Hispania Cesc Fabregas. "Nadhani timu hizi mbili ndiyo zimekuwa na matokeo mazuri mfululizo katika michuano hii." Italia ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia, mara ya mwisho 2006, wakati Hispania inajaribu kufanya kitu cha kipekee kwa kuwa timu ya kwanza kutwaa mfululizo vikombe vitatu vikubwa baada ya Euro 2008 na Kombe la Dunia miaka miwili iliyopita. Wakati mafanikio ya Vicente Del Bosque na Hispania yamejengwa katika safu imara ya ulinzi na kukaa muda mrefu na mpira, Italia imefika fainali kutokana na kufanya mashambulizi mfululizo yakiongozwa na mtukutu Mario Balotelli ambayo yaliiwezesha kuitoa Ujerumani katika nusufainali. Mfumo wa Hispania, wa pasi fupi-fupi 'Tiki Taka' umewapa mafanikio ya kujivunia - hakuna timu ya Ulaya tangu Ujerumani Magharibi mwanzoni mwa miaka ya 1970 imefanikiwa kucheza fainali tatu mfululizo za michuano mikubwa. Lakini 'enzi ya Hispania' kwa namna nyingi itaelezewa na jinsi itakavyokabiliana na timu iliyoshangaza kwa kucheza soka la kuvutia ya Italia leo. Kuweka historia ya kutwaa taji la tatu mfululizo, huku vigogo Ujerumani na Uholanzi vikiwa vilishafunga virago kwenye fainali hizi, kutaiweka Hispania kama moja ya timu kabambe zaidi zilizowahi kutokea. Lakini kipigo, mwishoni mwa fainali ambazo wameshindwa kuchengua mashabiki, kutaendelea kuitambulisha 'La Roja' kama moja ya timu za kawaida miongoni mwa vigogo vya soka. Hispania imefika hatua hiyo ya fainali kwa kuiondosha kwa mikwaju ya penati 4-2 wareno wakiongozwa na nahodha wao Cristiano Ronaldo, huku Waitalia maarufu kama 'Azzurri' waliwanyamazisha waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa wa mwaka huu, Ujerumani kwa mabao 2-1, magoli yaliyofungwa na 'mtukutu' Mario 'Super Mario' Balotelli ambaye ana asili ya Afrika hususani nchini Ghana.

Ratiba ya Kagame Cup 2012 hadharani

Release No. 102 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Juni 29, 2012 YANGA KUANZIA KWA ATLETICO KOMBE LA KAGAME Mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wataanza kutetea ubingwa wao Julai 14 mwaka huu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye ametangaza ratiba ya michuano hiyo leo (Juni 29 mwaka huu) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Timu 11 zitashiriki katika michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 mwaka huu ambapo kwa siku zitachezwa mechi mbili (saa 8 mchana na saa 10 jioni) huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na Yanga, Simba na Azam. Mechi ya kwanza siku ya ufunguzi (saa 8 mchana) itakuwa kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini. Kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti. Azam, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya ziko kundi B. Yanga inaunda kundi C lenye timu za APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi. Timu nane zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati B litatoa timu mbili. El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambayo yanafanyika Tanzania Bara kwa mwaka wa tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali. Coffee haitashiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14 mwaka huu wakati El Merreikh wikiend ya Julai 13-15 mwaka huu itakuwa na mechi ya michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Bingwa wa michuano hiyo atapata dola 30,000, makamu bingwa dola 20,000 na mshindi wa tatu dola 10,000. Michuano hiyo itaoneshwa moja kwa moja (live) na Televisheni ya SuperSport. KAGAME CUP 2012 FIXTURE Sat. 14th July 1 APR vs WAU SALAAM Uwanja wa Taifa 2pm 2 YANGA vs ATLETICO Uwanja wa Taifa 4pm Sun. 15th July 3 AZAM vs MAFUNZO Chamazi 4pm Mon. 16th July 4 VITA CLUB vs PORTS Uwanja wa Taifa 2pm 5 SIMBA vs URA Uwanja wa Taifa 4pm Tue. 17th July 6 ATLETICO vs APR Uwanja wa Taifa 2pm 7 WAU SALAAM vs YANGA Uwanja wa Taifa 4pm Wed. 18th July 8 VITA CLUB vs URA Uwanja wa Taifa 2pm 9 PORTS vs SIMBA Uwanja wa Taifa 4pm Thu. 19th July 10 ATLETICO vs WAU SALAAM Uwanja wa Taifa 2pm 11 MAFUNZO vs TUSKER Uwanja wa Taifa 4pm Fri. 20th July 12 PORTS vs URA Uwanja wa Taifa 2pm 13 YANGA vs APR Uwanja wa Taifa 4pm Sat. 21st July 14 AZAM vs TUSKER Uwanja wa Taifa 2pm 15 SIMBA vs VITA CLUB Uwanja wa Taifa 4pm Sun. 22nd July REST DAY QUARTER FINALS Mon. 23rd July 16 B2 vs C2 17 A1 vs C3 Tue. 24th July 18 C1 vs A2 19 B1 vs A3 Wed. 25th July REST DAY SEMI FINALS Thu. 26th July 20 Winner 16 vs Winner 17 21 Winner 18 vs Winner 19 Fri. 27th July REST DAY FINALS AND 3rd PLACE PLAY OFFS Sat. 28th July 22 Loser 20 vs Loser 21 23 Winner 20 vs Winner 21 Boniface Wambura Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Licha ya mafanikio, Diamond hajamsahau Mungu wake

NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amesema licha ya mafanikio makubwa aliyonayo katika sanaa hiyo, bado haachi kufanya ibada kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kumfikisha hapo alipo. Akizungumza na MICHARAZO, Diamond anayetamba na nyimbo kama 'Moyo Wangu', Lala Salama' na Nimepende Nani, alisema ni vigumu kumsahau Mungu kwani anaamini ndiye aliyemnyanyua hapo alipo kisanii. Diamond, alisema jambo la kumkumbuka Mungu na kufanya ibada ni kitu kinachopaswa kufanywa na kila mtu hususani wasanii ambao hutumia muda wao mwingine katika kufanya shughuli zao kiasi cha kubanwa kufanya ibada. "Kaka huwezi amini sijamsahau Mungu, naendelea kufanya ibada kama kawaida kwa sababu najua bila ya uwezo na mapenzi yake Mungu, nisingefika kokote," alisema. Mkali huyo alisema, kumtanguliza Mungu katika kila analofanya pamoja na kujibidiisha kufanya mazoezi na kuumiza kichwa kuandaa kazi makini, zimemfanya awe mmoja wa wasanii wenye majina makubwa kwa sasa nchini na ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Aliongeza kwa sasa anajiandaa kupakua kazi mpya ambazo zitazidi kumweka katika matawi ya juu nchini. "Nipo katika maandalizi ya kupakua kazi mpya, hivyo mashabiki wangu wakae mkao wa kula," alisema.

Watayarishaji wengi wa filamu wabishi- Lamata

MMOJA wa waongozaji wa filamu wa kike nchini, Leah Richard Mwendamseke 'Lamata' amesema baadhi ya watayarishaji wa filamu hawataki kukosolewa katika kazi zao na kufanya filamu nyingi kukosa ubora wa kimataifa. Pia, alisema kama watayarishaji hao hawatawadharau waongozaji na kuwathamini wasanii wanaozicheza filamu zao, huenda soko la filamu katika anga la kimataifa likapanuka na kuchuana na zile za nchi za Nigeria, Ghana na kwingineko. Lamata, aliyasema hayo alipozungumza na MICHARAZO na kusema, licha ya kwamba waongozaji ndio wenye nafasi kubwa ya kubebeshwa lawama kazi ikiwa mbaya, ila ukweli wengi wao wanaangushwa na ubishi walionao watayarishaji wa filamu wasiopenda kuelekezwa. Muongozaji na mwandishi huyo wa filamu, alisema wapo watayarishaji hata wakielekezwa kufanya mabadiliko katika kazi zao ili kuziboresha hukataa na kuamini wapo sahihi na kusababisha kazi nyingi kulipuliwa na kushindwa kutamba sokoni. "Pia wamekuwa wakiwadharau waongozaji na kuwathamini zaidi wasanii bila kujua injini ya filamu kuwa nzuri ni muongozaji makini anayeweza kupangilia kazi kulingana na hadithi ilivyo na namna ya kuiboresha ili iendane na uhalisi unaosisimua," alisema. Alisema kama watayarishaji na baadhi ya wasanii wataamua kubadilika na kufanya kazi kwa lengo la kuiinua sanaa hiyo ni wazi filamu za Tanzania zinaweza kutamba kimataifa na kuchuana na kazi za mataifa mengine ambayo wamekuwa vinara kwa miaka mingi iliyopita. Mwanadada huyo aliyeziongoza filamu kadhaa kama 'My Princess', 'Candy', 'Mr President', 'Rude' na sasa akimalizia kazi mpya ya 'Injinia', alisema wapo baadhi ya wasanii hawajui wapo katika sanaa hiyo kwa sababu ipi kwa mambo wanayoyafanya.

Okwi kupaa kwenda Parma ya Italia

MSHAMBULIAJI wa kutumaini wa kimataifa wa timu ya soka ya Simba, Emmanuel Okwi anatarajiwa kutua nchini Italia kwa ajili ya kufanyiwa majaribio katika klabu ya Parma inayoshiriki Ligi ya Seria A, baada ya kuzitosa ofa za timu za Afika Kusini. Mganda huyo ambaye amekuwa chachu kubwa ya Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, anatarajiwa kwenda nchini humo, keshokutwa. Habari za kuaminika toka ndani ya Simba na kuthibitishwa na mmoja wa wajumbe wa kamati ya Utendaji aliyekataa kutajwa jina lake, zinasema kuwa Okwi anaenda huko kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Parma. "Ni kweli Okwi anatarajiwa kutua Italia Julai 4 kwa ajili ya kufanya mazungumzo na klabu ya Seria A ya Parma kwa ajili ya kujiunga nao kwa msimu ujao baada ya kuachana na ofa za klabu za Orlando Pirates, Mamelodi Sundowns na Super Sports zilizokuwa zikimtaka," chanzo hicho kilidokeza. Chanzo hicho kilidokeza kuwa, iwapo Mganda huyo atafanikuwa kunyakuliwa na Parma huenda Simba ikavuna mamilioni ya fedha kwa usajili huo. Hata hivyo Simba italazimika kugawana mgao huo unaokadiriwa kufikia Sh Bilioni 2 na klabu ya Sc Villa ya Uganda iliyowauzia nyota huyo ambaye aliidhalilisha Yanga kwenye mechi ya kufungia msimu kwa kufunga mabao mawili na kusaidia jingine moja. Hiyo haitakuwa mara ya kwanza Simba kuuza wachezaji wake na kuvuna fedha, kwani mwaka jana iliwauza Mbwana Samatta na Patr
ick Ochan kwa TP Mazembe na kuvuna fedha za kutosha hiyo ni mbali na zile za akina Danny Mrwanda, Henry Joseph na wengineo.

Yanga yatamba 'MTATUKOMA' safari hii

UONGOZI wa
klabu ya soka ya Yanga umetamka neno moja tu 'Mtatukoma' wakitambia kikosi chao katika ushiriki wao wa michuano ya Kombe la Kagame. Yanga watashiriki michuano hiyo itakayoanza Julai 14 na kumalizika mwishoni mwa mwezi huu kama mabingwa watetezi, michuano itakayofanyika kwenye ardhi ya Tanzania Bara. Afisa habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kwa namna kikosi chao kilivyoimarishwa na kujifua wana hakika ya kutetea taji hilo, na pia kufanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao. Sendeu, alisema kwa halili yoyote wapinzani wao watakaopambana kwenye michuano hiyo ya Kagame na Ligi Kuu wanapaswa kujipanga kwani vinginevyo watakiona cha moto. "Kwa kweli Watatukona kwa namna tunavyoendelea vema na maandalizi yetu ya michuano ya Kagame na kujipanga kwa Ligi Kuu msimu ujao kama unavyojua tumeshaanza kujifua na tumeimarisha kikosi kwa kunasa wachezaji kadhaa," alisema. Sendeu alisema, anaamini wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya michuano hiyo na ligi ijayo wataisaidia Yanga kurejesha makali yake baada ya kumaliza msimu wakiambulia patupu wakipoteza ubingwa na kukosa hata nafasi ya kuiwakilisha nchini katika michuano ya kimataifa. Yanga ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu, ikiziacha Simba iliyotwaa ubingwa na Azam walioshika nafasi ya pili wakiwatambia na kupata fursa ya uwakilishi wa nchini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Kikosi hicho cha Yanga kinaendelea kunolewa kwa sasa na Kocha Msaidizi ambaye ndiye Kaimu Kocha Mkuu, Fred Felix Minziro baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Kostadin Papic kutimika kwao baada ya kutoongezewa mkataba mwingine na klabu hiyo. Tayari uongozi wa juu ya Yanga umesema wakati wowote utalitangaza jina la kocha mkuu wa timu hiyo baada ya kupitia maombi ya makocha bora watano waliopita katika orodha ndefu ingawa majina ya makocha hao haijawekwa bayana zaidi ya tetesi wapo wa ndani ya Afrika na Ulaya. Timu hiyo jana ilikitambulisha kikosi chake kwa mashabiki wa soka jijini Dar kwa kuumanana na Express ya Uganda na kuikandamiza mabao 2-1, mabao yote ya Yanga yakitupiwa nyavuni Jerry Tegete kwa pasi murua za kinda la Stars, Simon Msuvah na Bahanuzi.