STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, August 1, 2012

Bondia Mbongo kuwania taji la IBF Afrika

BONDIA Ramadhani Shauri wa Tanzania anatarajiwa kupanda ulingoni siku ya Idd Pili kuzipiga na Mganda Sunday Kizito katika pambano la kimnataifa la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika. Pambano hilo limepangwa klufanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee na litaratibiwa na Promota Lucas Rutainurwa. Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini, TPBC ambaye pia ni Rais wa IBF Afrika/USBA, Onesmo Ngowi, aliiambia NIPASHE jana kuwa maandalizi ya pambano hilo yameanza na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi. Ngowi, alisema pambano hilo la Shauri na Kizito litakuwa ni la uzito wa Feather (kilo 58) kuwataja mabondia hao wana rekodi zinasisimua hivyo kutabiri pambano la aina yake siku husika. Rais huyo alisema Shauri anayetoka kambi ya kocha Christopher Mzazi ana rekodi ya mapambano 12 akishinda 11 na kupoteza moja, huku mpinzani wake akiwa na rkodi ya kucheza pia michezo12 akishinda saba ba kupoteza 9. Ngowi alisema siku ya pambano hilo Mtanzania mwingine Nassib Ramadhan atavaana na Mkenya, Twalibu Mubiru kuwania ubingwa wa IBF Afrika Mashariki na Kati. Naye promota wa pambano hilo lililopewa jina la 'The Rumble of the City' alisema ameamua kuwekeza katika Utalii wa Michezo ili kusaidia ajira kwa vijana sambamba na kukuza uchumi wa Tanzania. Rutainurwa alisema kuwa ana ratiba ya mapambano ya ubingwa wa Afrika kila baada ya miezi miwili mwaka huu na mwaka kesho ambayo itaipa Tanzania nafasi ya kunyanyua mataji na kuwawezesha vijana kujiajiri. Promota huyo aliyaomba makampuni na wadhamini mbalimbali kujitokeza kufanikisha michezo hiyo inayosimamiwa na kampuni yake ya Kitwe General Traders. Mwisho

Ngassa adaiwa kumfukisha kazi Azam kocha Stewart Hall

WINGA nyota wa timu ya Azam, Mrisho Ngassa anatajwa kuwa ndiye chanzo cha 'kutimuliwa' kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Stewart John Hall. Azam imedaiwa kumsitishia mkataba kocha huyo kutoka Uingereza ikiwa ni siku chache tu tangu aiwezeshe timu hiyo kucheza fainali za Kombe la Kagame, michuano iliyoishiriki kwa mara ya kwanza katika historia yao. Hata hivyo uongozi wa Azam umekuwa wagumu kuweka bayana ukweli juu ya taarifa hizo za kumtimua Stewart na sababu zilizowafanya waachane nae kutokana na baadhi ya viongozi wake kutupiana mpira kila walipokuwa wakitafutwa kuthibitisha ukweli. Afisa Habari wa klabu hiyo, Jafer Idd alisema asingeweza kusema lolote na kulitaka MICHARAZO iliwasiliane na Katibu Mkuu, Idrisa Nassor 'Father' ambaye naye alikwepa kijanja kuthibitisha suala hilo akidai angelitumia namba la mtu wa kulizungumzia hilo. "Aisee juu ya ukweli au la, ngoja nikutumie namba ya mtu ambaye atakuambia kila kitu," Nassor aliiahidi MICHARAZOP licha ya kutotekeleza ahadi hiyo. Hata hivyo habari zilizopatikana jana jijini zinasema kuwa, Stewart ni kweli ametemwa na Azam na sababu kuu ikiwa ni kitendo chake cha kukaidi agizo la uongozi huo juu ya kumtomchezesha winga Mrisho Ngassa. Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ni kwamba uongozi wa Azam ulimtaka kocha huyo asijaribu kumuingiza uwanjani Ngassa katika mechi yao ya fainali dhidi ya Yanga kwa kukerwa na kitendo cha winga huyo kuibusu jezi ya Yanga mara baada ya pambano la nusu fainali dhidi ya As Vita ya Kongo. Inadaiwa, uongozi ulihisi winga huyo asingeitendea haki Azam kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa klabu yake ya zamani ya Yanga ambayo imetajwa kuchuana na Simba ili kumrejesha kikosini kwa msimu ujao.

UNAMKUMBUKA MWANA ZANZIBAR?

MPULIZA Saksafone wa zamani wa bendi ya Msondo Ngoma, Ally Rashid 'Mwana Zanzibar' yu hoi nyumbani kwake Keko Machungwa jijini Dar
kutokana na kupatwa na maradhi ya Kiharusi. Mmoja wa watoto wake, Mwanahawa Ally 'Chipolopolo' alisema baba yake alipatwa na maradhi hayo wakati akienda katika mazoezi ya bendi hiyo na kwa sasa hawezi kuzungumza wala kutembea. Kinachomliza Mwanahawa ni kitendo cha baba yake kutelekezwa na uongozi wa bendi hiyo. MICHARAZO ilijaribu uusaka uongozi wa bendi hiyo, lakini baadhi ya viongozi simu zao zilikuwa hazipatikani na nyingine zikilia bila kupokelewa bila kufahamika sababu yake.

Kocha Michelsen aita 22 Copa Coca Cola

Kocha wa timu za Taifa za vijana za Tanzania, Jakob Michelsen ameita wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Coca-Cola itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini. Baadaye watachujwa na kubaki 16 ambao ndiyo watakaokwenda kwenye michuano ya Afrika Kusini. Wachezaji waliochaguliwa wametokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani kuanzia Juni 24- Julai 2 mwaka huu. Wachezaji walioitwa ni Abdulrahman Mandawanga (Dodoma), Abraham Mohamed (Mjini Magharibi), Ayoub Alfan (Dodoma), Bakari Masoud (Tanga), Daniel Justin (Dodoma), Denis Dionis (Ilala), Edward Songo (Ruvuma), Fikiri Bakari (Tanga), Hassan Kabunda (Temeke), Joseph Chidyalo (Dodoma), Mutalemwa Katunzi (Morogoro) na Mwarami Maundu (Lindi). Wengine ni Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Omari Saleh (Singida), Rajab Rajab (Mwanza), Said Said (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma), Tumaini Baraka (Kilimanjaro) na William John (Ruvuma). Pia Michelsen ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi cha Serengeti Boys ambacho Septemba mwaka huu kitacheza na Kenya kuwania tiketi ya fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Wachezaji walioongezwa kwenye kikosi hicho ambao pia wametoka kwenye Copa Coca-Cola ni Abdallah Baker (Mjini Magharibi), Abdallah Kheri (Mjini Magharibi), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Hassan Mganga (Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni) na Mzamiru Said (Morogoro).

TFF yaridhia Ligi Kuu Tanzania kuendeshwa na kampuni

KWA mara ya kwanza Ligi Kuu Bara itaandika historia msimu ujao, ambapo sasa itasimamiwa na kuendeshwa na kampuni, 'Tanzania Premium League' (TPL). Hatua ya kupitisha mabadiliko hayo, ilifikiwa katika kikao cha siku mbili cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Akizungumza jana, mwenyekiti wa kamati ya kuendesha mchakato wa kampuni, Wallace Karia alisema TFF imepitisha kampuni kuwa chombo huru cha kuendesha ligi hiyo itakayoanza rasmi Septemba Mosi mwaka huu. "Tulichokuwa tunatofautiana na TFF juu ya ligi kuendeshwa na chombo huru, lakini sasa kamati ya utendaji imetoa baraka," alisema Karia."Kuna mambo madogo ya kufanyiwa mabadiliko, hata hivyo hali hiyo siyo kikwazo cha ligi kusimamiwa na chombo huru," aliongeza Kiria. Karia alisema baadhi ya maeneo ya kufanyiwa marekebisho ni suala la muundo wa kisheria wa uendeshaji ligi na kasoro ndogo walizozibaini awali. Kimuundo kutakuwa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa TPL, kiongozi wa juu wa klabu iliyoshinda Ligi Kuu msimu uliotangulia. Pia kutakuwa na Makamu Wenyeviti wa Bodi watatu, ambao ni viongozi wa juu wa timu mbili zilizoshika nafasi ya pili na tatu na Makamu wa pili wa Rais wa TFF anayewakilisha klabu. "Pia bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Ligi Kuu inahusisha wenyeviti au wakurugenzi au kiongozi wa juu wa klabu zote 14 (16) zinazocheza Ligi Kuu, ambapo kila klabu itatoa mjumbe mmoja na TFF pia itakuwa na hisa kwenye kampuni. Wajumbe wengine wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya ligi ambao hawatapiga kura ni mjumbe mmoja kutoka Chama cha Wanasoka wa Kulipwa, Chama cha Waamuzi (FRAT), Chama cha Makocha (TAFCA0 na Wadhamini wa Ligi Kuu. "Kutakuwa na kamati huru ya nidhamu na rufaa ambayo itateuliwa na Bodi ya wakurugenzi ya TPL kila mwaka. Maamuzi ya kamati hii yatapaswa kutekelezwa na klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu lakini yanaweza kupigwa kwenye Kamati ya Nidhamu na Rufaa ya TFF," aliongeza Kiria. Uhusiano kati ya TPL na TFF utaruhusu Makamu wa pili wa Rais TFF kuwa makamu wenyeviti wa bodi ya wakurugenzi wa TPL. Aidha, uchaguzi wa makamu wa rais wa TFF utafanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa TPL au UTAFOC na kiongozi huyo atapaswa kuwa ama kiongozi wa juu wa klabu ya Ligi Kuu au Ligi Daraja la Kwanza au mmoja wa wanahisa wa Klabu inayoshiriki Ligi Kuu au Daraja la Kwanza. Kuhusiana na mapato ya milango ambayo kwa sasa TFF inachukua asilimia 10, TPL itapaswa kutoa asilimia ya hisa za TFF kutoka pato lake na klabu zitapaswa kutoa asilimia tano (5%) pato la milangoni. Kuhusu kumiliki hisa za kampuni, klabu zote zinazocheza Ligi Kuu zitakuwa na hisa sawa kwenye kampuni, ambazo zitapatikana kutokana na klabu kuwa mwananchama, na iwapo iwapo itashuka daraja, hisa zake zitahamia kwa klabu iliyopanda daraja. Wakati huohuo, klabu zote 14 zinazoshiriki Ligi Kuu zinatarajia kufanya kikao leo kwenye ukumbi wa JB Delmont, ambapo moja ya ajenda ni kujadili kwa kina suala la kampuni hiyo.Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine alikiri kuwapo kwa mkutano huo leo. Msemaji wa Shirikisho la soka nchini, TFF, Boniface Wambura hakukataa wala kukubali taarifa hizo zaidi ya kusema wakati kikao cha Kamati ya Utendaji kinakutana, yeye hakuwepo ofisini. Source: Mwananchi