STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, September 11, 2012

Omari Matuta: Wanchope wa Mtibwa aliyeamua kutundika daluga kwa muda

Omar Matuta 'Wanchope'Omar Matuta 'Wanchope' (kati) akishangilia bao lililoipa Mtibwa Ubingwa wa Kombe la Tusker lililofungwa na Rashid Gumbo (kulia), Kushoto yao ni Uhuru Seleman alipokuwa wakiichezea Mtibwa Sugar

UMAHIRI wake wa kuwasumbua mabeki na kuwatungua makipa hodari uwanjani, ilimfanya Omar Matuta abatizwe jina la 'Wanchope' akifananishwa na nyota wa zamani wa Costa Rica aliyetamba timu za West Ham na Manchester City, Paulo Wanchope.
Kwa wanaomkumbuka Wanchope aliyezichezea pia Derby County na Malaga alikuwa na kipaji kikubwa cha ufungaji kilichomfanya ashikilie nafasi ya pili ya wafungaji bora wa timu yake ya taifa akiifungia mabao 45 katika mechi 73 alizoichezea.
Kama ilivyokuwa kwa Wanchope, ndivyo ilivyokuwa kwa Matuta, ambaye katika timu zote alizozichezea kuanzia zile za Ligi daraja la nne mpaka za Ligi Kuu Tanzania  amekuwa akifungia mabao muhimu na kuwa tegemeo.
Nyota huyo aliyewahi kutamba na timu za Ndanda Republic, Vijana Ilala, AFC Arusha kabla ya kudakwa na Mtibwa Sugar tangu mwaka 2004 anakumbukwa na mashabiki nchini kwa mabao yake mawili yaliyoipa nafasi timu ya vijana 'Serengeti Boys' tiketi ya kucheza Fainali za Vijana Afrika za mwaka 2005.
Matuta alifunga katika ushindi wa 3-1 dhidi ya vijana wa Zimbabwe yaliyoifanya ifuzu kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kwenda kushinda 1-0 Harare kwa bao la Nizar Khalfan, hata hivyo waliondolewa fainali na kufungiwa na CAF kwa udanganyifu.
Bao lake la pili katika mechi hiyo, Matuta analitaja kama bao bora kwake kwa namna alivyolifunga, ingawa mechi isiyofutika kichwani mwake ilikuwa ni dhidi ya Ethiopia mwaka 2005 kwa namna walivyofanyiwa vimbwanga na kufungwa kwa hila.
Matuta, ameamua kupumzika soka msimu huu baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Mtibwa klabu anayoitaja kuwa bora kwake na anayeishabikia.
"Nimeamua kupumzika ili nifanye mambo yangu binafsi, ila  nikiwahi kumaliza huenda  nikarejea tena dimbani kwenye duru la pili la ligi kuu, ingawa sijui itakuwa timu ipi."
Mkali huyo anayefurahia soka kumpa mafanikio kimaisha ikiwamo kujenga nyumba Kigamboni na kumiliki miradi kadhaa ya biashara, anasema hajawahi kuona klabu iliyo makini na inayojali wachezaji wake kama Mtibwa Sugar.
Anasema kama mfumo wa klabu hiyo wa kujali na kuwathamini wachezaji wake ndio unaomfanya aiheshimu Mtibwa iliyomuuguza goti lake kwa miaka miwili kitu alichodai kwa klabu nyingine nchini ni vigumu kufanya jambo hilo hata kama umeisaidia vipi.

OWINO
Matuta asiyekumbuka idadi ya mabao aliyoyafunga kwa kutoweka kumbukumbu,  anasema licha ya umahiri wake dimbani, kwa beki wa kimataifa wa Azam, Mganda Joseph Owino ndiye ananayemnyima raha kwa uwezo wake mkubwa kisoka.
"Ni bonge la beki, anacheza kwa akili na ndiye anayenisumbua dimbani tangu nianze kukutana nae katika mechi za kimataifa na zile za Ligi Kuu Tanzania Bara."
Matuta anayependa kula ugali kwa samaki au nyama choma na kunywa vinywaji laini, anasema uwezo wake uwanjani na mwili na nguvu alizojaliwa huwa hapati shida kwa  mabeki wenye papara na wanaotumia nguvu, tofauti akutanapo na Owino.
Matuta, ambaye hajaoa ila ana mtoto mmoja aitwae Zuma, anayesoma darasa la tatu katika Shule ya msingi Bunge, anasema soka la Tanzania licha ya kusifiwa kukua ukweli  limedumaa kwa muda mrefu kutokana na sababu kadhaa.
Anadai moja ya sababu hizo ni u-Simba na u-Yanga uliowaathiri karibu wadau wote wa soka, kufutwa kwa mfumo wa ligi ya madaraja kama ilivyokuwa zamani na kupewa kisogo kwa michezo ya Yosso.
"Usimba na uyanga na kubadilishwa kwa mfumo wa ligi ya madaraja kama ilivyokuwa zamani ni sababu ya kukwama kwetu sawa na kupuuzwa kwa soka la vijana wenzetu wamekuwa wakilitegemea kupatia mafanikio yao," anasema.
Anasema ni muda wa wadau wa soka kubadilika japo anakiri huenda ikawa ngumu kwa namna ushabiki huo ulivyowathiri watu, pia akiwaomba viongozi wa FA na klabu kuwekeza nguvu kwa vijana sawia na kuwaruhusu kucheza soka nje ya nchi.

MIKWAJU
Matuta, mwenye ndoto za kufika mbali kisoka na kuwa mfanyabiashara mkubwa hapo baadae, anasema wakati akiibukia kwenye soka alipata wakati mgumu kwa baba yake ambaye ni marehemu kwa sasa aliyekuwa hapendi acheze soka badala yake asome.
Anadai baba'ke alilazimika wakati mwingine kumcharaza bakora ili kumzuia kucheza soka na kukazinia masomo, lakini haikusaidia kitu kwani alijikuta akikacha hata masomo ya sekondari ili ajikite kwenye soka.
"Nilikacha masomo ya sekondari pale JItegemee kwa ajili ya soka, wakati mwingine huwa najuta, lakini nafarijika kwa mafanikio niliyonayo," anasema.
Matuta aliyemudu pia nafasi za kiungo, anawashukuru makocha Mussa Stopper, Mzee Panju na Abdallah Kibadeni waliogundua na kukikiendeleza kipaji chake, pia akiwataja wazazi wake na uongozi mzima wa Mtibwa kumsaidia kufika hapo alipo.
Mkali huyo, aliyezaliwa mwaka 1988, akiwa mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Othman Matuta, anadai alivutiwa kisoka na nyota wa zamani wa RTC Kagera, Msabah Salum, licha ya kukiri kukunwa na soka la Ronaldo de Lima na Romario wa Brazil.
Matuta alianza safari yake kisoka tangu akisoma Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, akiichezea timu ya yosso ya Vijana Ilala na baadae kupandishwa timu B na baadae kutua Ndanda kuichezea Ligi Daraja la Nne wilayani Ilala kabla ya kurudishwa Vijana Ilala alioisaidia kuipandisha Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2002.
Bao pekee aliloifungia Vijana dhidi ya Pallsons ya Arusha ndilo lililoipandisha daraja timu hiyo jambo ambalo anadai anajivunia mpaka sasa kabla ya kuichezea AFC Arusha katika michuano ya Nane Bora ya Ligi Kuu na mwaka 2004 kutua Mtibwa aliyoichezea mpaka msimu uliopita akiisaidia kuiwezesha kushika nafasi ya nne katika Ligi Kuu.
Akiwa Mtibwa, Matuta anayechizishwa na rangi zote isipokuwa zenye mng'ao mkali,

alitwaa nao ubingwa wa Kombe la Tusker- 2008, akiwa mmoja wa walioifungia mabao akishirikiana na Uhuru Seleman, Monja Liseki na Rashid Gumbo.
Kuhusu timu ya taifa aliyoichezea kuanzia timu za vijana tangu mwaka 2004, anasema inaweza kufuzu fainali za kimataifa iwapo TFF na wadau wote wataipa maandalizi ya kutosha.
Anasema chini ya kocha Kim Poulsen anamatumaini makubwa licha ya kutaka wadau kumpa nafasi kocha huyo na kuepukwa kubadilishwa kila mara kwa kikosi cha timu hiyo ili kuwafanya wachezaji wazoeane.
Pia anataka timu za taifa za vijana zipewe kipaumbele zikitafutiwa wadhamini wake ili kuwa na maandalizi mazuri, huku akiitaka TFF irejeshe mfumo wa ligi ya madaraja na kuwa wakali kwa wavunjaji wa kanuni za sheria za soka.

Omar Matuta 'Wanchope' akiwa ameshikilia kombe la Tusker la mwaka 2008 alilotwaa na Mtibwa Sugar

Vazi la taifa miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika

Waziri wa Habari Utamaduni Vijana na Michezo Dk Fenella Mukangara

VAZI rasmi la Taifa linatarajia kuanza kuvaliwa siku ya kilele cha sherehe za miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania zitakazofanyika Desemba 9, mwaka huu imeelezwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema vazi hilo litavaliwa baada ya mchakato mzima wa kulipata vazi hilo utakapokamilika ambapo umepitia hatua mbalimbali.
Waziri Fenella alisema wizara yake inatarajia kuchukua michoro minne kati ya tisa iliyopitishwa na Kamati ya Vazi la Taifa iliyoundwa ambapo pia mchakato huo unahusisha kupata aina ya kitambaa kitakachotumika kutengenezea vazi hilo.
Waziri huyo alisema kuwa michoro hiyo minne (miwili ya vazi la kitenge na mingine ya khanga) itachukuliwa na kuwasilisha kwa sekretariati ya Baraza la Mawaziri ambalo litatakiwa kufanya maamuzi kabla ya Oktoba 31 mwaka huu.
"Baada ya kupata vazi hilo,kila mtu atakuwa na uhuru wa kuvaa mtandio, kushona gauni, shati au kuvaa kitambaa cha kichwani ambacho kitakuwa kinaonyesha vazi la taifa," alisema Fenella.
Katibu wa Kamati ya Vazi la Taifa, Angella Ngowi alisema kuwa kamati yake ilipokea maoni kutoka katika sehemu mbalimbali nchini na kuongeza kwamba mchakato wa kupata vazi hilo ulianza mwaka 2003.
Alisema kuwa michoro yote iliyopo katika mchakato huo ina rangi za bendera ya taifa na alama mbalimbali kama picha ya mlima Kilimanjaro, mwenge wa Uhuru, ala za muziki na picha za wanyama (Twiga na Pundamilia).


Hosea Mgohachi: Mpiga besi wa Extra afurahie muziki kumwezesha kimaisha

Hosea Mgohachi akiwa kwenye pozi kwenye ukumbi wa White House, Kimara

Moja ya nyumba za mwanamuziki Hosea Mgohachi
Hosea Mgohachi akicharaza gitaa kwenye mazoezi ya bendi yake ya Extra Bongo
Hosea akionyesha manjonjo yake kwenye moja ya maonyesho ya Extra Bongo nchini Finland hivi karibuni ilipoenda kwa ziara maalum nchi za Scandinavia
WAKATI wasanii na wanamuziki wengine wakilia kwamba fani zao zimekuwa zikishindwa kuwanufaisha kimaisha kwa sababu hizi na zile, kwa mkung'uta gitaa la besi wa Extra Bongo, Hosea Mgohachi 'Fukuafuku' kwake ni tofauti. Mgohachi, anasema anashukuru Mungu muziki aliouanza tangu akiwa kinda akiimba na kupiga ala shuleni na kanisa la Anglican-Kurasini, umemsaidia kwa mengi kiasi hajutii kujitosa kwke kuifanya fani hiyo. "Sio siri muziki umenisaidia mengi kiasi najivunia fani hii kwani, imeniwesha kumiliki nyumba mbili zilizopo Mbagala Kilungule na Mbagala Kuu, pia nina mradi wa 'Bodaboda' wenye pikipiki kadhaa," anasema. Mbali na hayo, Mgohachi anasema muziki umemwezesha pia kutembea nchi kadhaa duniani, kupata rafiki na kuitunza familia yake kwa pato la fani hiyo. Mgohachi, mwenye ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa, anasema siri ya mafanikio yake imetokana na nidhamu yake katika matumizi ya fedha na kiu kubwa aliyonayo ya kuwa mfanyabiashara atakapostaafu muziki. "Mtu hupata mafanikiokwa kujituma kwa bidii, ila kubwa ni suala la nidhamu hasa kwa matumizi ya fedha, kitu ambacho nimekuwa nikizingatia kwa muda mrefu hadi kufika hapa nilipo," anasema. Anasema hata kwa wasanii na wanamuziki wenzake ni vema wakazingatia hilo iwapo wanataka kufika mbali licha ya ukweli pato litokanalo na sanaa kukiri kuwa dogo kulinganisha na ukubwa wa kazi. MDUDU Mpiga gitaa huyo aliyesoma darasa moja na nyota wa muziki wa kizazi kipya anayetamba kundi la Wanaume Halisi, Sir Juma Nature, anasema wakati akichipukia kwenye muziki alivutiwa na kwaya za St James na Kristo Mfalme. Ila kwa sasa anadai anakunwa na wapiga gitaa Minicha na Kapaya waliopo pamoja na nyota wa DR Congo, Werrason Ngiama Makanda na mpiga solo nyota wa Extra Bongo, aliyewahi kutamba na bendi kadhaa nchini Ephrem Joshua 'Kanyaga Twende'. "Hawa jamaa nawazimia sana kwa ucharazaji wao wa magitaa, hasa Joshua, yaani tukiwa kundi moja utashangaa vitu tunavyotoa," anasema. Mkali huyo, anayeitaja Extra Bongo kama bendi bomba kwake kwa namna inavyomtunza na kumlipa dau kubwa kuliko bendi zote alizowahi kuifanyia kazi, anasema hakuna chakula anachopenda kula nyama ya nguruwe maarufu kama 'Kitimoto' au 'Mdudu'. "Aisee katika vyakula ninavyopenda kula hakuna kama 'mdudu' yaani ukitaka kunifurahisha we nipe nyama hii kwa ndizi za kuchoma ," anasema. Mgohachi, ambaye hajaoa kwa sasa ingawa yu mbioni kufanya hivyo kwa mwanamke anayeishi naye, anasema pia anapenda kunywa soda na siku moja moja kusuuza roho yake kwa kugida bia. OKWI Akiwa na watoto watatu, Wilson, 7 anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Mwananyamala, Mery, 7, anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Mtoni na Junior, 3, Mgohachi anasema japo soka halicheza sana utotoni mwake, lakini ni shabiki mkubwa wa mchezo huo. Anasema yeye ni shabiki mkubwa wa Simba na Manchester United akimtaja Emmanuel Okwi anayichezea Simba kama anayemkuna kwa umahiri wake wa kufumania nyavu uwanjani. "Kati ya nyota wanaonipa raha katika soka Emmanuel Okwi ndiye kinara wao, huyu jamaa ana akili ya kufunga, mjanja na ana kipaji cha kipekee hata Yanga wanamjua," anasema kwa utani huku akicheka. Mgohachi anayepiga magitaa yote na kupapasa kinanda, anasema hakuna tukio la furaha maishani mwake kama alipomaliza kujenga nyumba yake ya Mbagala Kuu na kusitikishwa na kifo cha dada yake kilichotokea mwaka 1999. Juu ya muziki wa Tanzania, Mgohachi anayeiomba serikali iitupie macho fani ya sanaa ili kuwainua wasanii, anasema umepiga hatua kubwa tofauti na miaka ya nyuma, ingawa anataka wanamuziki kubadilika na kuwa wabunifu zaidi./ Anasema ubunifu utaweza kuutangaza muziki huo kimataifa kama ilivyokuwa ikifanywa na makundi kama Tatu Nane, InAfrica Band na wengine. "Lazima tuwe wabunifu tuweze kutamba kimataifa, tuachane na kasumba na kupenda kuwaiga wakongo tunawatangaza zaidi wao badala ya muziki wetu," anasema. ALIPOTOKA Hosea Simon Mgohachi, alizaliwa Aprili 14, 1978 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa nne kati ya watano wa familia yao, alisoma Shule ya Msingi Kurasini alipoanza kuonyesha kipaji chake cha sanaa akiimba kwaya na kupiga ala. Mbali na shuleni, Mgohachi pia alikuwa akiimbia kwaya ya kanisa lao la Anglican chini ya walimu Charles na Yaredi Disanura kabla ya kupitia makundi ya Chikoike Sound na Mwenge Jazz. Bendi yake ya kwanza kuifanyia kazi kama mwanamuziki kamili ni African Beat mnamo mwaka 1998 kabla ya kutua Mchinga Sound 'Wana Kipepeo' akiwa na rafikie Ibrahim Kandaya 'Profesa' aliyepo Msondo Band kwa sasa. Bendi nyingine alizofanyia kazi mwanamuziki huyo anayewaasa wasanii wenzake na watanzania kwa ujumla kujiepusha na Ukimwi kwa kujenga utamaduni wa kuwa waaminifu na kupima afya zao sawia na kutumia kondomu inaposhikana ni Double M Sound, Double Extra, Chipolopolo na African Vibration. Pia amewahi kufanya kazi za muziki Umangani kwa zaidi ya mara mbili wakati akiipigia bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kabla ya mwaka jana kuhamia Extra Bongo alionao mpaka sasa akiwa amerejea nao kutokea nchi za Skandinavia. Mgohachi anayependa kutumia muda wake kuangalia vipindi vya runinga na kusikiliza muziki wa Bongofleva akimzimia Sir Juma Nature anasema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatawashukuru wazazi wake, Mama Shuu, Mudhihir Mudhihir na Ally Choki kwa namna walivyomfikisha hapo alipo.

Hosea Mgohachi akiwa katika pozi
Hosea Mgohachi akiwa na mwanae Junior