STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 1, 2013

MWANDI WAANZISHA MICHUANO YA VIJANA AFRIKA

 http://www.tanzaniamwandi.co.tz/images/Tanzania%20Mwandi.png
KAMPUNI ya Tanzania Mwandi kwa kutambua kuwa Tanzania na Afrika nzima kuna vijana wengi ambao wana vipaji vya mpira wa miguu na hivyo wanachohitaji ni kuonyeshwa tu jinsi ya kuufikia ‘Ulimwengu Halisi’ wa Mpira duniani Tanzania Mwandi imeamua kuanzisha michuano ya African Youth Football Tournament ambayo itawashirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 21.

Michuano hiyo itaambatana na mafunzo kwa siku tano ambapo vijana hao watapata mafunzo ya mpira wa Miguu (elimu, ujuzi na hata mbinu za uwanjani) kutoka kwa makocha wawili wa hapa nchini na watatu wa kimataifa kutoka nje ya nchi, kuanzia tarehe 10/06/2013 hadi tarehe 14/06/2013 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Aidha, mafunzo yatafanyika nyakati za asubuhi na jioni wachezaji hao watashiriki Mashindano ya kucheza wao kwa wao ili kupata vijana 11 bora miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki.

Wachezaji Bora 11 watakaopatikana watakuwa mabalozi wa Mdhamini Mkuu wa Michuano ya African Youth Football Tournament na watapata fursa ya kutangazwa zaidi kimataifa na kutafutiwa vilabu vya kucheza soka Barani Ulaya katika nchi nane (Ufaransa, Ureno, Uswis, Ubelgiji, Uholanzi, Norway, Sweden na Denmark pamoja na barani Afrika na Asia.

Ili kupanua wigo wa kuwatangaza kimataifa wachezaji wengi zaidi, Michuano hii pia itaalika skauti na mawakala wa soka wa kimataifa ili kufuatilia uwezo wa wachezaji hao asubuhi katika mazoezi na jioni kwenye michuano, kuwapata vijana bora ambao watapendelea kuwatafutia timu nje ya nchi kukipiga huko kwa makubaliano ambayo pande hizo mbili (mchezaji na wakala) zitaafikiana.

Miongoni mwa Mawakala ambao watakuwepo ni wakala wa Kimataifa wa Tanzania, Dk. Damas Ndumbaro, Phillip Mwakikosa (Sweden) na wengine wengi.

Hata hivyo kutokana na gharama kubwa za uandaaji wa Michuano hii, na ndio kwanza ikiwa inaanzishwa, Kampuni ya Tanzania Mwandi kwa kujali mahitaji ya Kitanzania tumeweka kiingilio kwa mchezaji wa Tanzania kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300, 000) na mchezaji wa nje ya Tanzania Dola 500 za Kimarekani (USD 500).

Fedha hizo zitagharamia malazi, chakula na mahitaji mengine yote kwa mchezaji pindi atakapokuwa kambini.
 
Hii ni fursa adimu kwa vijana wa Kitanzania kuonyesha uwezo wao ili kutimiza ndoto za kucheza soka barani Ulaya, Asia na barani Afrika katika vilabu vikubwa huku ikikumbukwa kuwa mnamo Mwaka 2012 ni wachezaji wachache sana wa Kitanzania waliopata fursa ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kutokana na uchache wa mawakala na gharama hivyo kuletwa mawakala hao nyumbani Tanzania ni fursa pekee ya kufikia malengo.

Mpaka sasa tayari Kampuni ina majina takribani ya vijana 10 wa Nje ya nchi (Uganda, Nigeria na Ghana) ambao wameomba kushiriki hivyo tunatoa wito kwa Watanzania kutoipoteza fursa ya kuletewa njia ya kuelekea kusakata soka Barani Ulaya mlangoni mwao.

Lakini tunafahamu hali halisi ya maisha yetu kwahiyo nitoe wito kwa Wadhamini mbalimbali ambao tumewaomba kutusaidia kufanikisha Mashindano haya ambayo naamini yatalitangaza taifa letu na kulitangaza zaidi soka letu kimataifa. Pia udhamini wao utatuwezesha kupunguza hizi gharama kwa washiriki kutoka Tanzania na hivyo kuwachukua vijana wengi zaidi.

Kampuni ya Tanzania Mwandi ni Kampuni binafsi ambayo imejikita katika kuendeleza sekta za utalii, michezo na burudani ndani na nje ya nchi na hivyo kuiongezea kipato nchi moja kwa moja ama kupitia kuwawezesha wananchi kama vile kuwatengenezea fursa za ajira vijana kupitia michezo.

Fomu za ushiriki Michuano hii zinapatikana kupitia www.tanzaniamwandi.co.tz na www.blog.tanzaniamwandi.co.tz

“African Youth Football Tournament; Live your Dream.”

YANGA, KAGERA SUGAR WAINGIZA MILIONI 77

ZANa Boniface Wambura
JUMLA  ya Watazamaji 13,398 wameshuhudia pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Kagera Sugar lililochezwa juzi (Februari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuingiza sh. 77,117,000.
Mechi hiyo namba 130 iliyochezeshwa na Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani ilimalizika kwa Yanga ambao wanaongoza VPL wakiwa na pointi 42 kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 45 na Haruna Niyonzima.
Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 18,291,297.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 11,763,610.17.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 11,908 na kuingiza sh. 59,540,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 80 na kuingiza sh. 1,600,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 9,300,659.97, tiketi sh. 3,348,990, gharama za mechi sh. 5,580,395.98, Kamati ya Ligi sh. 5,580,395.98, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,790,197.99 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,170,153.99.

POLISI MORO KUVUNA NINI KESHO KWA JKT OLJORO?


Na Boniface Wambura
TIMU ya Polisi Morogoro inaikaribisha Oljoro JKT ya Arusha kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mechi pekee ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itakayochezwa kesho (Machi 2 mwaka huu).
Hata hivyo, timu hizo haziko katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa ambapo Yanga ndiyo inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 42 wakati Oljoro JKT inayofunzwa na Alex Mwamgaya ikiwa nazo 21 na Polisi Morogoro pointi 15.
Oljoro JKT iko katika nafasi ya tisa. Polisi Morogoro ambayo katika mzunguko wa pili imebadilika ikiwa chini ya Kocha Adolf Rishard inashika nafasi ya 12 ikiziacha mkiani Toto Africans yenye pointi 14 na African Lyon ambayo ina pointi 13.
Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Machi 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Oljoro JKT vs Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid), African Lyon vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Chamazi) na Mgambo Shooting vs Mtibwa Sugar (Mkwakwani) wakati Machi 7 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Kagera Sugar (Azam Complex, Chamazi).
Machi 9 mwaka huu kutakuwa na mechi mbili; Yanga vs Toto Africans 9Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).

VILLA SQUAD KUIVAA ASHANTI UNITED FDL


Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Boniface Wambura
MICHUANO ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Machi 2 mwaka huu) katika makundi yote matatu. Villa Squad itaivaa Ashanti United kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B.
Kundi A ni mechi kati ya Kurugenzi ya Mafinga dhidi ya Mbeya City wakati Polisi Iringa vs JKT Mlale, na Majimaji vs Mkamba Rangers zilizokuwa zicheze kesho (Machi 2 mwaka huu), sasa zitaumana Machi 3 mwaka huu mjini Iringa na mjini Songea.
Pia kundi B kesho (Machi 2 mwaka huu) ni Green Warriors vs Transit Camp (Mlandizi) wakati keshokutwa (Machi 3 mwaka huu) Polisi Dar vs Tessema (Karume) na Ndanda vs Moro United katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi za kundi C kesho ni JKT Kanembwa vs Polisi Tabora (Lake Tanganyika), Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Karume, Musoma), Morani vs Pamba (Kiteto) na Mwadui vs Rhino Rangers (Kambarage, Shinyanga).


FIFA yawasilisha marekebisho 10 ya katiba kwa TFF


Na Boniface Wambura
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limetuma mapendekezo 10 ya marekebisho ya Katiba yake kwa wanachama wake kwa njia ya waraka.

Mapendekezo hayo yametumwa kwa kila nchi mwanachama kupitia waraka namba 1320, ambapo wanachama kwa kupitia kwa mashirikisho yao ya mabara watapiga kura ya ndiyo au hapa. Kwa upande wa Afrika, wanachama wa FIFA wanatakiwa kuwasilisha kura zao kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Baadhi ya mapendekezo hayo ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa FIFA (FIFA Congress). Makamu wa Rais wa FIFA na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaochaguliwa katika mabara ambapo itabidi wathibitishwe na FIFA Congress.

Muundo wa Kamati ya Utendaji; nafasi moja ya vyama vya mpira wa miguu vya Uingereza (British FAs) sasa inahamishiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA). Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya FIFA anatakiwa kushiriki vikao vya Kamati ya Utendaji bila kuwa na haki ya kupiga kura.

Uchaguzi wa Rais; mgombea anatakiwa kuungwa mkono na idadi ya kutosha ya vyama wanachama kutoka katika mabara mawili tofauti. Ukomo wa uongozi; kuanzisha vipindi vya uongozi. Ukomo wa umri; ukomo wa umri usiozidi miaka 72 wakati wa kugombea utekelezwe.

Uwakilishi wa kutosha kwa makundi yenye maslahi katika FIFA; makundi yenye maslahi katika mpira wa miguu kama wachezaji wapate uwakilishi katika Kamati ya Mpira wa Miguu. Uteuzi wa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia; uteuzi sasa ufanywe na Mkutano Mkuu wa TFF.

BFT kuutangaza uchaguzi wake mkuu wiki ijayo


Katibu wa BFT, Makore Mashaga
SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BTF) wiki ijayo linatarajiwa kutangaza mchakato mzima wa uchaguzi wao mkuu unaopaswa kufanyika mwaka huu kutokana muda wa uongozi wa sasa kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, alisema kwa mujibu wa Katiba iliyowaingiza madarakani miaka minne iliyopita, muda wao wa kuongoza unakoma Machi 29, hivyo wanapaswa kuitisha mchaguzi ili kupatikana kwa viongozi wapya.
Mashaga, alisema kutokana na kutambua kukaribia kumalizika kwa muda wao wa uongozi wanafanya mipango ya kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi huo ambao watautangaza kwa wanahabari wiki ijayo.
"Ni kweli muda wetu wa kuwepo madarakani unakaribia kumalizika na tunapaswa kujipanga kuwapisha viongozi wapya, lakini hatuwezi kukurupuka hivyo mipango yote itatangazwa ndani ya wiki mbili zijazo," alisema Mashaga.
Katibu huyo alisema uongozi wao unaheshimu katiba na hivyo watahakikisha kila kitu kinaenda sawa kuhakikisha BFT inapata viongozi wengine wa kuiongoza kwa miaka mingine baada ya uongozi wao kufanya waliyoyafanya katika mchezo huo wa ngumi.
Uongozi wa sasa wa BFT uliokuwa chini ya Rais wao, Joan Minja uliingia madarakani katika uchaguzi uliofanyika Machi 14, 2009 baada ya uliokuwa uongozi wa Alhaj Shaaban Mintanga kujiuzulu kufuatia kashfa ya usafirishaji wa dawa za kulevya.

Bondia Pascal Ndomba amtaka mshindi wa Kaseba v Maneno apigane naye

Bondia Pascal Ndomba (kushoto) akiwa na meneja wake, Hamoud Salim
Bondia Pascal Ndomba
 
WAKATI mabondia Japhet Kaseba na Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' wakitarajiwa kupigana kesho  kuwania ubingwa wa Taifa, bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Pascal Ndomba ameibuka na kuomba mshindi wa pambano hilo avaane naye.
Pambano hilo la Kaseba na Maneno litafanyika kwenye ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, Dar es Salaam kuwania ubingwa huo wa taifa unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini (PST) ambapo Kaseba atakuwa anatetea taji.
Kaseba alitwaa taji hilo Oktoba mwaka jana kwa kumpiga Mtambo wa Gongo, hivyo pambano hilo  lililoandaliwa na bingwa wa kick boxing nchini, Pendo Njau ni kama marudiano baina yao.
Waratibu wa pambano hilo wamesema kila kitu kimekaa vema ikiwamo mabondia wote watakaopanda ulingoni kesho kupimwa afya na uzito wao asubuhi ya leo.
Katika hatua nyingine Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati aliyekuwa nchini Marekani, Pascal Ndomba ameibuka na kusema angependa kucheza na mshindi yeyote atakayepatikana katika pambano hilo la kesho dhidi ya Kaseba na Osward.
Ndomba, alisema yu tayari hata kucheza bure dhidi ya mshindi wa mchezo huo wa kesho ambao ni wa kumaliza ubishi baada ya Osward kulalamikia ushindi wa Kaseba walipovaana mwaka jana.
"Nilikuwa naomba mshindi atakayepatikana katika pambano kati ya Kaseba na Maneno nipambane naye, hata kama bila ya malipo yoyote mradi tu nipigane nao, kwa sababu imekuwa ni desturi mabondia kupigana kwa mazoea na kuchaguana," alisema Ndomba.
Naye meneja wa bondia huyo, Hamoud Salim, alisema wao wapo tayari kuandaa pambano la mshindi wa pambano la Kaseba na Osward dhidi ya Ndomba ambaye amedai amekuwa akikimbiwa tangu aliponyakua taji la Afrika Mashariki mwaka juzi.

Gaucho, Uhuru waachwa msafara wa Azam


Abdulhalim Humoud 'Gaucho'

Uhuru Seleman

VIUNGO mahiri wa timu ya Azam, Abdulhalim Humoud 'Gaucho' na Uhuru Seleman ni baadhi ya nyota walioachwa kwenye msafara wa kikosi cha timu hiyo kinachotarajiwa kuondoka kesho alfajiri kwenda Sudan Kusini kurudiana na Al Nasir Juba.
Azam inatarajiwa kuvaana na Al Nasir katika mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Jumapili, huku wawakilishi hao wa Tanzania wakiwa na faida ya ushindi wa mabao 3-1 iliyopata nyumbani.
Kwa mujibu wa Katibu Msaidizi wa Azam, Twalib 'Chuma' Suleiman kikosi cha wachezaji 20 na viongozi watano na benchi zima la ufundi likiongozwa na kocha mkuu Stewart Hall watambatana pamoja katika msafara huo.Chuma aliwataja wachezaji walioambatana na timu hiyo kwa safari hiyo ya Sudan Kusini kuwa ni pamoja na makipa; Mwadini Ally na Aishi Manula, mabeki; Joackins Atudo, David Mwantika, Himid Mao, Malika Ndeule, Waziri Salum na Luckson Kakolaki.
Aliongeza wachezaji wengine ni viungo ni Kipre Balou, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar, Humphrey Mieno, Abdi Kassim 'Babbi' na Khamis Mcha 'Vialli', huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco 'Adebayor', Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Brian Umony na Gaudence Mwaikimba 'Caroll'.
Baadhi ya wakali walioachwa kwenye msafara huo ni pamoja na viungo, Abdulhalim Humoud, Uhuru Suleiman Omar Mtaki, Jackson Wandiwi na Samih Haji Nuhu.
Chuma alisema kikosi chao kinaenda Sudan Kusini wakiwa na dhamira moja tu ya kuhakikisha wanapata ushindi ugenini na kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya michuano hiyo wanayoishiriki kwa mara ya kwanza.
Viongozi watakaoambatana na timu hiyo ni Katibu Mkuu, Nassor Idrissa, Meneja Msaidizi, Mameneja, Patrick Kahemela, Jemedari Said, Ibrahim Shikanda na Abubakar Mapwisa, huku benchi la ufundi mbali na Stewart pia wamo Kally Ongalla, Idd Abubakar Dardenne Paul na Yusuf Nzawila.

Golden Bush Veterani kuvaana na watoto wao kesho Kinesi

Kikosi cha Golden Bush kinachojiandaa na Ligi ya TFF-Kinondoni
Kikosi cha Golden Bush Veterani

BAADA ya kuikung'uta Clouds The Dream Team kwa mabao 4-1, kikosi cha Golden Bush Veterani kesho asubuhi kwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo wanatarajia kupimana ubavu na vijana wao, Golden Bush Fc inayojiandaa na michuano ya Ligi Daraja la Nne Wilayani Kinondoni.
Golden Bush itaishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kufanikiwa kupata usajili na uongozi wake umetamba kwamba wanataka kuwa klabu ya mfano nchini kwa kupanda ngazi kutoka ligi ya TFF wilaya hadi Ligi Kuu msimu michache ijayo.
Mlezi wa timu hizo, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema kuwa wameandaa mechi hiyo kupima makali ya vijana wao na pambano hilo litaanza kuchezwa saa 2 asubuhi.
Ticotico alisema lengo la mechi hiyo kutoa nafasi kwa makocha wa timu ya vijana kubaini makosa ya kuyarekebisha kabla ya kuanza mbio za ligi ambayo imepangwa kuanza rasmi kesho kwa michezo kadhaa huku wao wakila shushu kwanza.
Alisema pamoja na kwamba wanacheza na vijana wao, bado watashuka dimbani kama wanacheza mechi ya fainali kwa nia ya kuhakikisha wanawapata ushindi kama walivyofanya wiki iliyopita kwa Clouds waliokuwa wakitamba kabla ya mechi yao iliyochezwa kwenye uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe.