STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 1, 2013

Bondia Pascal Ndomba amtaka mshindi wa Kaseba v Maneno apigane naye

Bondia Pascal Ndomba (kushoto) akiwa na meneja wake, Hamoud Salim
Bondia Pascal Ndomba
 
WAKATI mabondia Japhet Kaseba na Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' wakitarajiwa kupigana kesho  kuwania ubingwa wa Taifa, bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Pascal Ndomba ameibuka na kuomba mshindi wa pambano hilo avaane naye.
Pambano hilo la Kaseba na Maneno litafanyika kwenye ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, Dar es Salaam kuwania ubingwa huo wa taifa unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini (PST) ambapo Kaseba atakuwa anatetea taji.
Kaseba alitwaa taji hilo Oktoba mwaka jana kwa kumpiga Mtambo wa Gongo, hivyo pambano hilo  lililoandaliwa na bingwa wa kick boxing nchini, Pendo Njau ni kama marudiano baina yao.
Waratibu wa pambano hilo wamesema kila kitu kimekaa vema ikiwamo mabondia wote watakaopanda ulingoni kesho kupimwa afya na uzito wao asubuhi ya leo.
Katika hatua nyingine Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati aliyekuwa nchini Marekani, Pascal Ndomba ameibuka na kusema angependa kucheza na mshindi yeyote atakayepatikana katika pambano hilo la kesho dhidi ya Kaseba na Osward.
Ndomba, alisema yu tayari hata kucheza bure dhidi ya mshindi wa mchezo huo wa kesho ambao ni wa kumaliza ubishi baada ya Osward kulalamikia ushindi wa Kaseba walipovaana mwaka jana.
"Nilikuwa naomba mshindi atakayepatikana katika pambano kati ya Kaseba na Maneno nipambane naye, hata kama bila ya malipo yoyote mradi tu nipigane nao, kwa sababu imekuwa ni desturi mabondia kupigana kwa mazoea na kuchaguana," alisema Ndomba.
Naye meneja wa bondia huyo, Hamoud Salim, alisema wao wapo tayari kuandaa pambano la mshindi wa pambano la Kaseba na Osward dhidi ya Ndomba ambaye amedai amekuwa akikimbiwa tangu aliponyakua taji la Afrika Mashariki mwaka juzi.

No comments:

Post a Comment