STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 5, 2013

Mwaisabula hatimaye akumbukwa na TFF, ateuliwa jopo la makocha

Kocha wa zamani wa Yanga na Bandari Mtwara, Kennedy Mwaisabula (kushoto) akiwa na viongozi wenzake wa Tukuyu Stars Family
HATIMAYE kocha maarufu nchini Kennedy Mwaisabula 'Mzazi' ameula na kukumbukwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kumteua miongoni mwa makocha wanaounda jopo maaluim la kutafuta mbinu za kuiwezesha Tanzania kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) 2015.
Mwaisabula, alitangazwa jana na TFF baada ya Rais wake Jamal Malinzi kutangaza kamati mbalimbali ikiwemo kumteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa mshauri wake kwa upande wa masuala ya ufundi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika hafla maalum iliyoandaliwa na wadhamini wakuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, Malinzi alisema jopo hilo litakutana kwa siku tatu Desemba 6-8, mwaka huu visiwani Zanzibar kupanga mkakati wa kuonyesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki michuano ya Afcon itakayofanyika 2015 nchini Morocco.
Malinzi alisema jopo hilo litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Kipingu, huku wengine wanaounda jopo hilo linalohusisha pia makocha wakiwa ni Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah 'King' Kibaden, Rutahyuga (Katibu wa Jopo), Kidao Wilfred, Salum Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay, Boniface Mkwasa na Dan Korosso.
"Wajumbe wengine watatu wa jopo hili wanatoka Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).  Ni memteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa mshauri wa rais (ufundi). Mshauri wa rais (utawala) nitamteua baadaye," alisema Malinzi.
Aidha, Malinzi alisema Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana Desemba 22, mwaka huu kujadili masuala mbalimbali yakiwamo ya uteuzi wa wajumbe wa kamati za kisheria na mgogoro wa uongozi wa Klabu ya Simba.

TBL WAMPONGEZA
Katika hatua nyingine, uongozi wa TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro, umempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema jana katika hafla hiyo, uongozi wa kampuni yao utaendelea kushirikiana na TFF kuendeleza soka la Tanzania.

Mtoto wa Kigogo CCM matatani kwa tuhuma za kuua kwa risasi




Jeshi la polisi mkoani Arusha limemshikilia na kisha kumwachia “chapchap” mtoto wa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na mfanyabiashara maarufu nchini,Oscar Themi kwa kosa la kumpiga risasi ya kichwa mhudumu wa bar ya Empire iliyopo eneo la Shoprite jijini Arusha.
Mtuhumiwa huyo ,Dereck Themi alishikiliwa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya kutofautiana na mhudumu huyo wakati alipompatia bili ya vinywaji aliyokuwa akitumia ndani ya bar hiyo kabla ya kumtandika risasi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa mnamo novemba 29 mwaka huu majira ya saa 7.30 usiku mtoto huyo wa kigogo alimfyatulia risasi mhudumu huyo aliyetambulika kwa jina la Witness Erasto wakati alipompatia bili ya vinywaji.

Mashuhuda walidai kuwa kulitokea na hali ya tofauti kati yao ambapo Themi alikubali kulipa bili hiyo ambapo alichukua fedha na kisha kumwekea katika matiti yake na ghafla kuchomoa bastola yake na kisha kumtandika eneo la kichwa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa mara baada ya tukio hilo ndipo mtuhumiwa alijaribu kukimbia nje ya bar hiyo kuelekea usawa wa eneo la maegesho la magari lakini kabla hajafika alifyatua risasi nyingine zaidi ya tano hali iliyopelekea tafrani katika eneo la Shoprite.

Hatahivyo,taarifa hizo zimedai kuwa askari mmoja aliyekuwa akilinda benki ya Exim iliyopo ndani ya eneo hilo la Shoprite alimvizia kimafia na kisha kumnyang”anya bastola hiyo mtuhumiwa kabla ya kuwataarifu polisi waliofika eneo hilo na kisha kumfikisha katika kituo kikuu cha polisi cha kati.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa katika kituo hicho na kisha kukabidhi bastoa hiyo pamoja na maganda matano ya risasi ambapo baada ya muda aliwasili mdogo wake aliyetambulika kwa jina la Bernad Themi aliyechukua mali zake na fedha.

Akihojiwa na gazeti hili majeruhi wa tukio hilo Erasto alisema kuwa hawezi kuongea chochote kwa kuwa hali yake ni sio nzuri lakini alipotafutwa mmiliki wa bar hiyo,Tumaini Ulomi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tayari wameshafungua mashtaka mbalimbali ikiwemo hasara aliyoipata siku ya tukio.
Mmiliki huyo alisema kuwa mara baada ya milio ya risasi kuanza kurindima ndani ya bar yake wateja mbalimbali wakiwemo watalii walitokomea kusikojulikana bila kulipa hali ambayo imemtia hasara kubwa.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa kifupi kwamba bado wanafanya uchunguzi wa kina kabla ya kulifikisha suala hilo mahakamani. 
Credit :libeneke la kaskazini

Tanzanite ikiitoa Afrika Kusini kuwavaa Nigeria au Tunisia


WAKATI kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Afrika Kusini U20 kikitua leo kwa ajili ya pambano la awali dhidi ya wenyeji wa Tanzanite, timu hiyo ya Tanzania kama itafanikiwa kuiondosha wapinzani wao itakuwa na kibarua kingine kigumu dhidi ya mshindi kati ya Nigeria au Tunisia kukata tiketi ya Fainali za Dunia za 2014.
Fainali hizo za Kombe la Dunia kwa timu za U20 wanawake zitafanyika nchini Canada, na mechi za kupata wawakilishi wawili wa Afrika zinatarajiwa kufanyika kati ya Januari 10-24 mwakani.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo timu nyiungine zilizopo katika hatua ya 8 Bora mpaka sasa ukiziondoa Tanzania na Afrika Kusini ni Nigeria, Tunisia, Ghana, Uganda, Zambia na Equatorial Guinea.
Tanzania imefika hatua hiyo baada ya kuiondosha patupu Msumbiji katika mechi za raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 15-1 baada ya awali kuitandika mabao 10-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kuisulubu nyumbani kwao kwa mabao 5-1.
Jumamosi itashuka dimbani kuikaribisha Afrika Kusini iliyoing'oa Botswana kwa mabao 7-2, mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kiingilio cha chini siku hiyo ni Sh. Elfu Moja (1,000) tu.
Tanzanite itaifuata Afrika Kusini wiki mbili baadaye na iwapo itafanikiwa kushinda mechi hizo na kuitoa Afrika Kusini, itasubiri kujua hatma yake dhidi ya mshindi kati ya Nigeria na Tunisia ambazo wikiendi ijayo nazo zitapepetana nchini Nigeria.
Kikosi hicho cha U20 kinanolewa na kocha Rogasian Kaijage kwa sasa kinaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Karume na ule wa Taifa kujiandaa kwa mechi hiyo na kambi yake ipo  Msimbazi Hotel baada ya kutoka Ruvu mkoani Pwani.
Watanzania wamekuwa na imani kubwa na Tanzanite kutokana na kuonekena kuelekea kuziba nafasi ya Twiga Stars na bila shaka Jumamosi itaendelea kuwapa RAHA watanzania katika pambano hilo dhidi ya Afrika Kusini ambalo litachezeshwa na refa Nabikko Ssemambo kutoka Uganda.
Waamuzi wasaidizi katika mchezo huo ni  Gebreyohanis Trhas kutoka Ethiopia ,Nakitto Nkumbi na Irene Namubiru wote kutoka Uganda na kamishna atakuwa John Muinjo kutoka Namibia.
Muinjo pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Namibia (NFA) na mjumbe wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)..

Kikapu sasa kuchaguana Desemba 29 Dodoma

Baadhi ya viongozi wa sasa wa TBF katika mikutano yao na wanahabari
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) uliotangazwa awali kuahirishwa kufanyika Desemba 10 jijini Mbeya, sasa unatarajiwa kufanyika Desemba 29, mwaka huu mkoani Dodoma.
Uchaguzi huo utakwenda sambamba na mkutano mkuu wa shirikisho hilo ambao utafanyika siku moja kabla huku ukihudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa TBF, Mussa Mziya, ilieleza tarehe hiyo imetangazwa baada ya wajumbe kuridhia na kukubaliana.
Aliema kutokana na ukata unaolikabili shirikisho hilo, wamewaomba wajumbe wote wa mikutano  wajigharamie kwa nauli, malazi na chakula kwa kipindi chote cha mkutano na uchaguzi.
Rais huyo aliwataka wadau na makampuni mbalimbali kujitokeza ili kuwadhamini na kwamba fedha zinazohitajika kwa ajili ya gharama za uchaguzi huo ni Sh. milioni 17.
Alisema ada za fomu kwa wanaotaka kugombe nafasi ya urais na makamu wa rais ni Sh. 150,000, nafasi ya katibu mkuu, katibu mkuu msaidizi na mweka hazina ni Sh. 100,000. Kwa upande wa wajumbe wa kamisheni zote ni alisema ni Sh. 50,000 huku mwisho wa kuchukua na kurudisha  fomu za ikiwa ni Desemba 13, 2013 saa tisa mchana.
Awali uchaguzi huo uilitangazwa kufanyika Mbeya Desemba 10 siku moja baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Taifa kwa mchezo huo ambao kwa sasa limeota mbawa kufanyika kwake.

Hatari! Askari wa KMKM anaswa na kete za unga Zanzibar




Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa

JESHI la Polisi Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya limemtia mbaroni askari wa Kikosi cha KMKM, Hussein Soud Hussein (30) baada ya kukamatwa na dawa za kulevya jumla ya kete 270 katika eneo la Darajabovu mjini Zanzibar.

Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Upelelezi na Makosa ya Jinai Yussuf Ilembo alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo na kusema inasikitisha sana kuona askari ambaye ndio tegemeo la kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya anajishughulisha na biashara hiyo haramu.

“Ni kweli tumemkamata kijana mmoja Hussein Soud Hussein ambaye baada ya kumfanyia usaili alikiri na kuthibitisha kwamba yeye ni askari wa Kikosi cha KMKM na tuliona kitambulisho chake,” alisema Ilembo.

Ilembo alisema askari huyo alikamatwa ikiwa sehemu ya msako unaoendelea wa Jeshi la Polisi pamoja na Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kuwatafuta wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo.

Kukamatwa kwa askari huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambao walichukizwa na tabia yake ya kufanya biashara ya dawa za kulevya wakati akiwa askari wa ulinzi.

Alisema kwa sasa Polisi wapo katika doria endelevu ya kuwatafuta vijana wanaofanya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo ya mjini na vijijini.

Taarifa zaidi ziliopo sasa kwa mujibu wa Jeshi la Polisi ni kwamba biashara ya dawa za kulevya hufanywa zaidi vijijini kutokana na msako wa Polisi Jamii ulioshamiri mjini ambao hautoi nafasi kwa wafanyabiashara hao kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa

Addyng'ari awakumbuka wa nyumbani Mbeya

Addyng'ari katika pozi
MSANII anayekuja kwa kasi katika muziki wa kizazi kipya Addy Michael 'Addy Ng'ari' kutoka jijini Mbeya ameachia wimbo mpya uitwao 'Nawakumbuka Nyumbani' ambao  tayari umeanza kurushwa hewani katika vituo vya redio vya jijini humo na anafanya mchakato ili kuusambaza katika vituo vya redio jijini Dar es Salaam ili nako usikike.
Msanii huyo alisema wimbo huo ni maalum kwa wale wanaokuwa mbali na kwao na jinsi wanavyokuwa wakikumbuka nyumbani kwao kiasi kwamba hupata wakati mgumu kufanya kazi zao kwa ufanisi.
"Ni moja ya wimbo unaoelezea namna watu wanavyopata tabu wawapo mbali na nyumbani kwao  na zipo nyingine ambazo nimeshatunga na kuzifanyia mazoezi, lakini nasubiri nitoe video ya kibao hiki kabla ya kuingia tena studio," alisema Ng'ari.
Aliongeza kuwa wakati akianza mipango ya kuusambaza vituo vya redio vya jijini Dar es Salaam, pia tayari ameanza mchakato wa kuanza video yake huku akiendelea kufanyia mazoezi nyimbo nyingine mpya ili kuzirekodi.

Man Utd hoi, Liverpool ikiua 5-1, Arsenal burudaniiii kama Chelsea

Fellaine dhidi ya timu yake ya zamani Everton na kushindwa kuitetea baada ya kulala 1-0

Natupia tu! Luis Suarez akifunga moja ya mabao yake manne usiku wa jana

Nipe tano mwanangu! Arsenal wakishangilia mabao yao walipoizamisha Hull City

Lampard akitupia kambani bao lake wakati Chelsea ikishinda mabao 4-3 ugenini
LONDON, England
WAKATI mashabiki wa Manchester United wakiendelea kupata 'vidonda vya tumbo' kutokana na timu yao kufanya vibaya, wenzao wa Arsenal wanachekaa baada ya usiku wa jana timu hiyo kuendeleza wimbi lake la ushindi.
Vijana hao wa Arsene Wenger, waliishindilia Hull City kwa mabao 2-0 na kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Mabao ya Nicklas Bendtner la dakika ya pili ya mchezo na jingine la kipinbdi cha pili kupitia Mesut Ozil, lililtosha kuwafanya vijana hao wa London Kaskazini kuendelea kukenua wakati wapinzani wa Manchester United ikiendelea kununa.
Hii ni kwa sababu mabingwa watetezi hao usiku wa kuamkia leo walidunguliwa nyumbani na Everton kwa bao 1-0 lililofungwa na Bryan Oviedo baada ya mwishoni mwa wiki kulazimishwa sare ya 2-2 na Tottenham Hotspur.
Hali ikiwa hivyo, Liverpool ilitoka kufungwa mabao 3-1 ilizinduka jana kwa kuilaza Norwich City kwa mabao 5-1, huku mabao manne yakitupiwa kambani na mkali Luis Suarez na jingine likifungwa na Raheem Sterling.
Bao la kufutia machozi la Norwich liliwekwa kimiani na Johnson.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa usiku wa jana, Chelsea ilipata ushindi wa kindondokela baada ya kuzima Sunderland nyumbani kwao kwa mabao 4-3, huku wenyeji wakijifunga moja ya mabao hayo.
Chelsea ilipata ushindi huo kwa mabao ya Frank Lampard, Eden Hazard aliyefunga mawili kabla ya Bardsley kuwazadia bao wakati katika harakati za kuokoa mpira. Wenyeji walipata mabao yao ya kufutia machozi kupitia kwa  Altidore na Bardsley.
Naye Mwanasoka Bora wa Afrika wa BBC, Yaya Toure alifunga magoli mawili wakati timu yake ya Manchester City ikipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya West Brom.
Sergio Kun Aguero aliifungia City bao jingine na kuwasogeza hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, huku wapinzani wao wakipata mabao yake kupitia kwa Pantilimon na Anichebe.
Tottenham nayo ilizinduka kwa kupata ushindi wa jioni wa mabao 2-1 dhidi ya wenyejki wao Fulham waliotangulia kupata bao kupitia kwa Dejagah katika kipindi cha pili.
Spurs walipata mabao yake yaliyowafanya wajongee kwenye msimamo hadi nafasi ya sita kupitia kwa Chiriches aliyesawazishia na Holtby aliyefunga bao la ushindi.
Nayo Newcastle United baada ya kupata ushindi mfululizo jana ilijikuta ikikwama ugenini baada ya kufungwa mabao 3-0 na Swansea City, huku Aston Villa ikiwa ugenini ikipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Southampton na Stoke City ikibanwa nyumbani na Cardiff City kwa kutoka sare ya kutofungana.

Wasanii kiubao kupamba Uhuru Marathoni jijini Dar


Katibu wa kamati ya maandalizi ya mbio za uhurumarathon, Innocent Melleck, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam juu ya maandalizi na wasanii watakaoshiriki kwenye mkesha wa Uhuru utakaofanyika viwanja vya Leaders Club baada ya kukamilika kwa mbio za uhuru. Kushoto ni katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Selemani Nyambui.
*********************************

ZIKIWA zimebaki siku chache kwa ajili ya shindano la mbio ndefu za Uhuru, 'Uhuru Marathon', kufanyika, wasanii watakaotoa burudani siku ya mkesha wa uhuru wapania kufanya kweli.
Wasanii wanaotarajiwa kutoa burudani ni Roma Mkatoliki, Joh Makini, G Nako, Nick wa Pili, Mrisho Mpoto, Mrisho Mpoto, TMK Wanaume, Mfalme Siboka na kundi la Twanga Pepeta.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasanii hao walisema wanashukuru kupewa heshima kubwa kutumbuiza siku hiyo na hasa ukichukulia umuhimu wa amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
“Nitafanya makamuzi ya kweli siku hiyo na watu wategemee mistari iliyokwenda shule,” alisema Roma Mkatoliki, huku Mrisho Mpoto akidai ana vitu vikali zaidi atakavyoweka hadharani siku hiyo.
Naye Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, homa ya mbio hizo imepanda, hasa baada ya kujitokeza kwa wanariadha wengi wa mataifa, kutoka nchi mbalimbali.
Melleck alisema, mbali na wengi kujitokeza bado anaamini wengi wataendelea kujiandikisha ili kufanikisha lengo la mbio hizo.
Aidha alisema kuwa usajili bado unaendelea kwa wale wanaotaka kushiriki ambapo fomu zitakazotolewa kwa mshiriki wa kilomita 3 atalipa Sh 100,000 yule wa kilomita 5 Sh 2,000 na washiriki wa kilomita 21 na 42 watalipia Sh 6,000.

Yaya Toure ashukuru kunjyakua tuzo ya BBC

Yaya Toure akiwajibika uwanjani
LONDON, England
KIUNGO wa kimataifa wa Ivory Coast na klabu ya Manchester City ya England, Yaya Toure amewashukuru mashabiki kwa kumchagua kuwa mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika ya BBC.

Toure (30), ambaye aliteuliwa kuwania tuzo hiyo kwa miaka minne mfululizo, alitangazwa kuwa mshindi juzi baada ya kuwabwaga wanasoka wenzake wanne waliofuzu kuingia fainali.

Wanasoka wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni Pierre-Emerick Aubameyang, Victor Moses, John Mikel Obi na Jonathan Pitroipa.

"Asanteni mashabiki wote duniani, mnaoendelea kuniunga mkono. Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani mashabiki wanakupenda na kuikubali kazi yako,"amesema kiungo huyo.

"Hiki ni kitu fulani maalumu kwa sababu si kura ya kocha, klabu au nahodha wa timu ya taifa. Ni kura za mashabiki,"aliongeza nyota huyo wa zamani, aliyewahi kuchezea klabu ya Barcelona ya Hispania.

"Siku zote, ni jambo linalofurahisha unapokuwa na mashabiki wengi nyuma yako. Nimefurahi kwa sababu tuzo hiyo nimepewa na mashabiki, nawashukuru sana,"anasema.

Toure anasema, alikuwa na kila sababu ya kushinda tuzo hiyo baada ya kuteuliwa kuiwania kwa miaka minne mfululizo.

Anasema kushinda tuzo hiyo kwake ni mafanikio makubwa, hasa ikizingatiwa kuwa, wanasoka alioshindana nao, wapo kwenye kiwango cha juu na wanacheza soka ya kimataifa.

"Nadhani pia kuwa, soka ya Afrika imekuwa ikipiga hatua kubwa kimaendeleo na hii ina maana kubwa kwetu. Nikiwa mwafrika, ninayo furaha kubwa," anasema Toure.

Uteuzi wa wanasoka walioteuliwa kuwania tuzo hiyo, ulifanywa na wataalamu 44 wa soka kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Vigezo vilivyozingatiwa katika uteuzi huo ni
akili, ufundi, ushirikiano na wachezaji wengine na nidhamu.

Mshindi wa tuzo hiyo, alipatikana kutokana na kura zilizopigwa na mashabiki kupitia mtandao wa BBC, aidha kwa njia ya simu au ujumbe wa maandishi.

Mashabiki wamempa Toure tuzo hiyo kutokana na kuiletea mafanikio makubwa Ivory Coast mwaka uliopita na pia kuonyesha uwezo mkubwa katika kucheza soka na kufunga mabao.

Mwaka 2013 haukuwa wa mafanikio makubwa kwa Toure kutokana na kutoshinda tuzo yoyote katika klabu ya Manchester City na Ivory Coast, lakini alionyesha kiwango cha juu katika kusakata kabumbu.

Baada ya kukatishwa tamaa kutokana na Manchester City kushindwa kutetea taji lake msimu uliopita, Toure amerejea uwanjani msimu huu kivingine, akiwa ameongeza kitu kipya katika uchezaji wake, kutokana na kuwa mahiri kwa ufungaji wa mabao ya mipira ya adhabu.

Toure alionyesha uwezo huo katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu ya England dhidi ya Newcastle kabla ya kufunga tena bao kwa staili hiyo katika mechi dhidi ya Hull. Ameshafunga mabao manne kwa staili hiyo, kati ya mabao saba aliyoifungia Manchester City.

Kwa mujibu wa rekodi, Toure amefunga mabao 13 hadi sasa kwa klabu yake hiyo pamoja na timu ya taifa ya Ivory Coast, ambayo ni ya kujivunia kwa mchezaji wa kiungo.

Uwezo huo wa Toure pamoja na uongozi wake, umeiwezesha Manchester City kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo hadi sasa.

Toure pia alikuwa msaada kubwa katika kikosi cha Ivory Coast, kilichofuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014, zitakazofanyika nchini Brazil.

Ushindi huo ulikuwa faraja kubwa kwa Ivory Coast baada ya kuvurunda katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na Nigeria.

Nje ya uwanja, Toure amekuwa akiongoza mapambano ya kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi katika soka, baada ya kukumbwa na hali hiyo wakati wa mechi ya michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya CSKA Moscow ya Russia.

Wafuatao ni washindi wa tuzo zilizopita za mwanasoka bora wa Afrika wa BBC:

•2012 - Christopher Katongo (Zambia & Henan Construction)
•2011 - Andre 'Dede' Ayew (Marseille & Ghana)
•2010 - Asamoah Gyan (Sunderland & Ghana)
•2009 - Didier Drogba (Chelsea & Ivory Coast)
•2008 - Mohamed Aboutrika (Al Ahly & Egypt)
•2007 - Emmanuel Adebayor (Arsenal & Togo)
•2006 - Michael Essien (Chelsea & Ghana)
•2005 - Mohamed Barakat (Al Ahly & Egypt)
•2004 - Jay Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
•2003 - Jay Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
•2002 - El Hadji Diouf (Liverpool & Senegal)
•2001 - Sammy Kuffour (Bayern Munich & Ghana)
•2000 - Patrick Mboma (Parma & Cameroon)