STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 23, 2010

Al Madina yafuturisha wanawake Dar, wakizundua ofisi



TAASISI ya Huduma za Kijamii ya Al Madinah, 'Al Madinah Social Services Trust' jana jioni ilizindua ofisi yao mpya kwenye jengo la BinSlum Plaza sambamba na kuwafuturisha futari wanawake wa Kiislam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ally Hassani Mwinyi, Mama Sitti Mwinyi aliyeambana na Bi Khadija Mwinyi.
Shughuli hizo za uzinduzi na ufuturishwaji futari, iliandaliwa na Kamati ya Wanawake wa taasisi hiyo ya Al Madinah na kudhaminiwa na benki ya Stanbic na ilifanyika kwenye jengo hilo la Bin Slum lililopo mitaa ya Livingstone na Mkunguni, Kariakoo jijini Dar.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Wanawake wa Al Madinah, Hajat Mariam Dedesi, alisema hafla hiyo ya kuwafuturisha wanawake wa Kiislam ilikuwa na lengo kubwa la kujenga umoja na mshikamano pamoja na kutekeleza moja ya sunna iliyokokotezwa kwenye mfungo wa Mwezi wa Ramadhani ya watu kulishana kwa lengo la kupata dhawabu.
Mariam alisema mbali na hilo, lakini kubwa ni kutaka kutoa hamasa kwa wanawake wa Kiislam kuungana pamoja na kujitokeza kwa wajili ya kwenda Hijja kupitia taasisi yao ambayo inajishughulisha na huduma za kuwasafirisha mahujaji.
Alisema wanashukuru msaada mkubwa waliopewa na benki ya Stanbic, ambayo aliwahimiza wanawake nchini kote kujiunga nayo kwa lengo la kuweza kuhifadhia fedha zao bila ya riba na pia kupata mikopo itakayowawezesha kujianzishia na kuendesha miradi yao ya kimaendeleo kujikuza kiuchumi.
Naye mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Sheikh Ally Mbaraka, alitoa wito kwa waumini wote wanaotaka kwenda hija kujitokeza kujiandikisha na kulipia ada zao kupitia taasisi hiyo akidai ina huduma murua na gharama nafuu wakati wa kwenda na watakapokuwa hija.
Sheikh Mbaraka alisema huduma za malazi, usafiri kupitia Shirika la Ndege la Oman ni zenye kiwango cha hali juu na zitakazowawezesha mahujaji kutosafiri kwenda mbali na miji watakayofanyia hija zao.
Naye meneja wa Stanbic Bank, Bi Jennifer Hillal, alisema ni vema mahujaji na waumini wengine kuchangamkia kujiunga na benki yao kwa kuwa inazingatia miiko na sharia za kiislam kwa kutotoza riba ya aina yoyote.


Ukiondoa mgeni rasmi, Mama Sitti aliyeambatana na 'mkemwenza' Bi Khadija Mwinyi, wengine waliohudhuria ni Mwenyekiti wa

Waislam wahimizwa kujiunga na benki zisizotoza riba




WAUMINI wa dini ya Kiislam wamehimizwa kujiunga na mabenki kwa lengo la kuhifadhi fedha zao kwa salama pamoja na kuwawezesha kupata fursa ya kukopa fedha za kuendeshea shughuli zao za kimaendeleo na uchumi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kidini na Kijamii ya Al Madinah, Sheikh Ally Mbaraka, alipozungumza na Micharazo mara baada ya uzinduzi wa ofisi yao mpya eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Mbaraka alisema ni vema waumini wa Kiislam wakajiunga na mabenki na hasa yasiyotoa riba kwa lengo la kupata fursa ya kukopa fedha ili kuanzisha miradi ya kimaendeleo na kiuchumi kujikwamua kimaisha.
Alisema kutokana na kujitokeza kwa mabenki kadhaa yanayoendesha shughuli zao kwa kuzingatia Sharia za Kiislam ni wasaa nzuri kwa waumini kujiunga nazo kuzilinda fedha zao salama na pia kupata faida bila kumuasi Mola wao.
Aliongeza kuwa taasisi yao inayohusika na masuala ya huduma za kijamii na kuratibu safari za Mahujaji, inawaomba waumini wanaotarajia kwenda Hija kuchangamka kujitokeza mapema kujiandikisha kwenye ofisi zao.
"Safari za Hija zinakaribia kuanza hivyo tunawahimiza waumini watakaoenda kuhiji kujitokeza mapema kujiandikisha ili kuwahi nafasi chini ya taasisi yetu ambayo inaendesha shughuli zake kwa kushirikiana na benki ya Stanbic itakayowawezesha mahujaji kutoa na kutuma fedha wakiwa hija," alisema.
Naye Meneja wa Huduma wa Benki ya Stanbic, Jennifer Hillal, alisema benki yao imeweka huduma mbalimbali zinazozingatia sharia ya kiislam kwa lengo la kuwawezesha watu wa imani hiyo kujiunga nao ili wanufaike na mikopo isiyo na riba pamoja na kusaidia kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
Alisema benki yako yenye huduma ya ATM Visa Card ni muhimu kwa mahujaji kujiunga nayo kwa vile popote watakapokuwepo hata huko kwenye hija zao wataweza kupata huduma za kifedha kwa mfumo ule ule.
Pamoja na kuwahimiza kujiunga nao, pia aliwataka waumini hao na wananchi kwa ujumla kuingia kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31 wakihakikisha unakuwa wa amani na utulivu.
Jennifer, alisema bila ya kuwepo kwa amani na utulivu hata wao wenye mabenki na watanzania kwa ujumla hawawezi kuendesha shughuli zao za kimaendeleo na kiuchumi kama inavyoshuhudiwa na mataifa mengine.

Mwisho

Mama Sitti Mwinyi ataka uchaguzi wenye amani na salama



WAKATI kampeni za wagombea wanaowania kinyang'anyiro cha uchaguzi zikiendelea nchini kote, Mke wa Rais wa Pili Mstaafu, Ally Hassani Mwinyi, Sitti Mwinyi, ameibuka na kuuombea uchaguzi huo uwe wa salama na amani.
Pia aliwahimiza wanawake nchini kote kuchangamkia uchaguzi huo kwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuhakikisha wanawachagua viongozi watakaosaidia kudumisha umoja na mshikamano.
Mama Sitti alitoa wito huo alipozungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ofisi mpya ya Taasisi ya Kijamii ya Al Madinah, iliyoambatana na ufuturishwaji wa futari kwa wanawake wa Kiislam uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa, wananchi bila kujali itikadi ya kidini au siasa wahakikishe kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa amani na utulivu wakiwa na maelewano kwa lengo la kudumisha umoja na mshikamano kwa watanzania wote.
"Nawasihi wananchi wote wake kwa waume bila kujali dini, kabila au itikadi za kisiasa washiriki uchaguzi mkuu kwa amani na salama wakiwa na maelewano, ili kudumisha umoja wetu," alisema.
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na mke mkubwa wa Mwinyi, Bi Khadija, alihudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Wanawake wa Al Madinah inayoongozwa na Hajat Mariam Dedesi na kudhaminiwa na Benki ya Stanbic.
Bi Khadija, alisema kwa kuwa Tanzania ni moja na wananchi ni wamoja ni vema wakashirikiana kuona uchaguzi wao unafanyika kwa amani na utulivu ili kuendeleza hali hiyo iliyozoeleka nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Wanawake ya Al Madinah, Mariam Dedesi alisema lengo la kuandaa futari hiyo kwa wanawake wenzao ni kujenga umoja na mshikamano na pia kusaidia kuhamasisha wenzao kujiunga na benki kwa lengo la kujiwezesha na hasa benki zisizo na riba.
Alisema kamati yao inawahamasisha wanawake kujiunga na mabenki yasiyo na riba ili kuweza kukopa fedha za kujianzishia miradi ya kimaendeleo ambazo itawakwamua kiuchumi wao na familia zao.

Mwisho

Aisha Sururu ataka umoja jumuiya za Kiislam

MWENYEKITI wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania, BAKWATA, Aisha Sururu, ameziomba taasisi za Kiislam nchini kushikamana na kuombea uchaguzi mkuu uwe wa amani na utulivu.
Sururu, ambaye ni mgombea wa udiwani wa Viti Maalum CCM, alisema umoja na mshikamano ndio silaha pekee ya kuifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani na utulivu na kuzikumbusha jumuiya hizo Kiislama kuidumisha.
Mwenyekiti huyo aliyasema hayo alipozungumza na Micharazo jana jijini Dar es Salaam na kudai taasisi na jumuiya hizo zina wajibu mkubwa wa kuwa mfano kwa wengine kwa kuwa na umoja na mshikamano bila kubaguana.
Alisema kujumika pamoja kwa viongozi na wafuasi wa jumuiya mbalimbali za kiislam katika hafla ya ufuturishwaji futari uliofanywa na Taasisi ya Al Madinah ni moja ya dalili njema za umoja miongoni mwao aliotaka udumishwe milele.
Alisema umoja huo hautafaa kama hawatashirikiana kwa ajili ya kuiombea nchi kufanya uchaguzi mkuu Oktoba 31 kwa amani na utulivu ili kuendeleza hali ya utilivu iliyopo nchini kwa miaka mingi.
"Kama kiongozi wa jumuiya ya wanawake ya BAKWATA nilikuwa nahimiza umoja na mshikamano kwa jumuiya zingine kuiombea Tanzania ifanye uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu ili tuishi na raha mustarehe," alisema.
Sururu, alisema kwa kuwa lengo la kila Mtanzania ni kuona amani na utulivu unaendelea kudumu basi ni vema wananchi wakashikamana na kutokubali kuwaachia wachache wawavuruge kwani majuto yake ni makubwa baadae.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuhimiza umoja huo, pia anawaomba wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 31 kuchagua viongozi wanaowataka na kuwaamini kwa mustakabali wa nchi na maisha yao kwa ujumla.
Juu ya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo, Sururu aliwataka wafanye kampeni za kistaarabu kwa kumwaga sera zao ili kuwashawishi wananchi wawapigie kura siku ya kufanya hivyo.
Hafla hiyo ya kufuturishwa kwa wanawake wa Kiislam ilidhaminiwa na Benki ya Stanbic
Mwisho