STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 4, 2011

Mwanza yaenguliwa Tamasha la Pasaka

MKOA wa Mwanza uliokuwa kwenye ratiba ya Tamasha la Pasaka, umeenguliwa na kufanya kwa sasa isalie mikoa mitatu tu itakayoshuhudia maonyesho hayo ya muziki wa Injili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama, alisema mikoa iliyosalia katika maonyesho hayo ni Dar es Salaam, Dodoma na Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Msama Promotions, alisema onyesho la kwanza la tamasha hilo litafanyika jijini Dar es Salaam siku ya April 24 kisha siku inayofuata litafanyikia mjini Dodoma kisha kumalizika Shinyanga Aprili 26.
Msama alisema onyesho la jiji la Mwanza limefutwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao na kuwaomba radhi mashabiki wa muziki wa Injili kwa jambo lililotokea.
"Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tumefuta onyesho la jijini Mwanza na tunatanguliza kuomba radhi kwa lililotokea ambalo lilikuwa nje ya uwezo wetu, ila tunawahidi wale wa mikoa mingine watarajie burudani kabambe," alisema Msama.
Msama alisema onyesho la jijini litakalofanyika siku ya Sikukuu ya Pasaka litafanyikia kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo waimbaji nhyota wa muziki huo akiwemo Upendo Nkone na waimbaji toka mataifa mbalimbali ya Kiafrika watakuwepo ukumbini kutumbuiza.
"Onyesho la Dar na mengineyo yatapambwa na waimbaji nyota wa Tanzania na nchi jirani kama za Kenya, Uganda, Rwanda, DR Congo, Afrika Kusini na Zambia, lengo likiwa ni kukusanya fedha za kuwasaidia yatima na wajane," alisema Msama.
Aliongeza mbali na fedha hizo kuwanufaisha yatima na wajane kwa nia ya kujikumu na kupata mitaji ya kujiendeshea shughuli za biashara, pia sehemu ya mapato ya maonyesho hayo yatatolewa kwa waathirika wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya jeshi Gongo la Mboto.
"Sehemu ya fedha zitakazopatikana kwenye maoanyesho hayo itatolewa kama pole kwa waathirika wa Mabomu ya Gongo la Mboto kama nilivyoahidi awali," alisema Msama.
Tamasha la Pasaka limekuwa likifanyika kila mwaka zaidi ya mwaka wa tatu sasa, ambapo waimbaji na makundi mbalimbali ya muziki wa Injili wa ndani ya nje hujumuika pamoja kutumbuiza sambamba na kuhamasisha upatikanaji wa fedha za kuwasaidia wenye matatizo nchini.

Jokha Kassim akwama kushebeduka

MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab, Jokha Kassim, amesema bado anaendelea kuhangaikia uzinduzi wa albamu yake binafsi ya 'Wacha Nijishebedue' iliyokwamba kuzinduliwa mwaka jana.
Uzinduzi wa albamu hiyo ulikwama katikati ya mwaka jana kutokana na sababu mbalimbali kubwa kukosa wafadhili na wadhamini wa kumpiga tafu.
Jokha, alisema bado hajakata tamaa kwa vile anaendelea kuwasiliana na wafadhili ili kufanikisha uzinduzi huo ndani ya mwaka huu.
"Najipanga kufanikisha uzinduzi wangu ndani ya mwaka huu, naamini Mungu atanisaidia nipata wadhamini wa kunipiga tafu," alisema.
Mwimbaji huyo alizitaja nyimbo zinazounda albamu yake hiyo 'Yamekushinda', 'Meseji za Nini', 'Kinyang'anyiro Hukiwezi', 'Kelele za Mlango' na Wacha Nijishebedue' uliobeba jina la albamu.
"Niliporekodi na kushuti video ya nyimbo zangu nilipata mfadhili na sasa anatafuta wengine watakaonisaidia kwenye uzinduzi wa albamu yangu, hivyo mashabiki wangu wajue kuwa bado ninahangaikia fedha," alisema.
Alisema, baadhi ya nyimbo zake ukiwemo uliobeba jina la albamu zimekuwa zikisikika kwenye vitu mbalimbali vya redio na televisheni na kumpa matumaini kwamba huenda akapata soko atapozindua.

Mtenda Akitendewa videoni

WIMBO mpya wa bendi ya Extra Bongo unatarajiwa kutambulishwa rasmi leo kwa mashabiki sambamba na vibao vingine na wanamuziki wapya uitwao, Mtenda Akitendewa umefyatuliwa video yake.
Video ya kibao hicho ambacho awali lilipangwa kufahamika kama 'Under 18' kimefyatuliwa na wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa kambini kupitia kampuni ya Sophia Records ya jijini Dar es Salaam na utaanza kuonekana hewani wakati wowote kuanzia sasa.
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki 'Kamarade' aliiambia micharazo kuwa, waliamua kurekodi video ya wimbo huo wakiwa kambini kama njia ya kuwapa burudani mashabiki wao kuwaonyesha hawakuwa bure kambini bali walikuwa wakiwaandalia mambo mapya.
"Pamoja na kuandaa kazi mpya, lakini pia tumefyatua video ya moja ya vibao hivyo kiitwacho Mtenda Akitendewa ambacho kitaanza kuonekana wakati wowote,tumeshasambaza, kibao hicho na vingine pamoja na wanamuziki wapya tutawatambulisha rasmi Ijumaa (leo)," alisema.
Choki alisema onyesho la utambulisho kwa bendi yao utafanyika kwenye ukumbi wa New Msasani Club, ambapo kesho litafuatiwa na onyesho jingine TCC-Chang'ombe na kabla ya Jumapili kutambulishwa Mango Garden na kwenda kuvunja kambi yao ili kujiandaa kwenda Zanzibar.
Mtunzi na muimbaji huyo alizitaja nyimbo nyingine zitakazotambulishwa sambana na wanamuziki sita waliowanyakua wakienda kambini kutoka Twanga Pepeta ni Neema, Nguvu na Akili na Fisadi wa Mapenzi vinavyoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya na ya pili.
Wanamuziki watakaotambulishwa kwenye maonyesho hayo ya mwishoni mwa wiki ni mtunzi na muimbaji nyota nchini, Rogert Hegga 'Caterpillar', Rapa Saulo John 'Ferguson', mpiga besi, Hoseah Mgohachi na wanenguaji Hassani Mohammed 'Super Nyamwela', Isaac Burhan 'Super Danger' na Otilia Boniface waliotoka African Stars 'Twanga Pepeta'.