STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, January 13, 2014

Ghana waanza vyema CHAN wainyuka Congo kimoja

CHAN 2014 : Group C Ghana and Congo collide
GHANA imeanza vyema michuano ya CHAN inayofanyika nchini Afrika Kusini baada ya jioni hii kuilaza Jamhuri ya Kongo kwa bao 1-0 katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Free State.
Bao pekee lililoihakikishia 'vigogo' hao kukusanya pointi tatu muhimu, lilitupiwa kambani na Theophilus Anobaah katika dakika ya 34 ya pambano hilo.
Muda mfupi ujao kundi hilo la C litashuhudia pambano jingine kali kati ya DR Congoi itakayoumana na Ethiopia kwenye uwanja huo huo katika mfululizo wa michuano hiyo.

Simba yashindwa kutamba kwa Waganda taji hilooo!


FUPA lililowashinda watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam jioni ya leo umewashinda pia Simba, baada ya 'Mnyama' kuchezea kichapo cha bao 1-0 toka kwa vijana wa KCC ya Uganda ambao wamenyakua taji hilo na kuondoka nalo ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa timu ya nje ya Tanzania kutwaa kombe hilo.
Simba ambayo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kuficha aibu ya Tanzania kushuhusia timu zake zote zikikongotwa na wageni, ilishindwa kuhimili vishindo vya Waganda licha ya kucheza jihad hasa dakika za lala salama.
Bao pekee lililowanyong'onyesha Simba na watanzania kwa ujumla lilitumbukiwa na Herman Wasswa katika kipindi cha kwanza.
Kwa ushindi huo KCC imekuwa klabu ya kwanza nje ya Tanzania kunyakua taji hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 2006, ikiwa haijapoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa michuano hiyo Januari Mosi.
Timu hizo zote zilikuwa kundi B mpaka kufika fainali zilikuwa hazijapoteza mechi zao na katika mechi baina yao zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu.
Michuano hiyo ilishirikisha timu 12 nne kutoka nje na nyingine za Tanzania Bara na Zanzibar. klabu za nje ni URA na KCC za Uganda, Tusker na AFC Leopards za Kenya.
Kutwaa kwa taji hilo KCC imefuata nyayo za dada zao wa netiboli waliotwaa ubingwa wa mchezo huo kwa kuifunga Tanzania katika fainali siku mbili zilizopita.
Simba iliifunga URA ya Uganda katika mechi ya nusu fainali na KCC ikailamba Azam kwa mabao 3-2 na kuitemesha taji ililotwaa mwaka jana kwa kuichapa Tusker ya Kenya.

Yanga wampa kazi Mholanzi kuing'oa Al Ahly


Tayari Yanga imekubaliana na kuingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Mholanzi, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm.

Kazi hiyo ilipangwa kumalizika leo asubuhi na kocha huyo ana mambo mengi sana ya kuburudisha.

Pamoja na kuwa na miaka 64, lakini ni mchapakazi na amekuwa gumzo alipokuwa na kikosi cha Berekum Chelsea ya Ghana.

Akiwa na timu hiyo msimu wa 2012-13, alizitoa jasho na kuzipa wakati mgumu pia timu vigogo kama Al Ahly, TP Mazembe na Zamalek.

Sasa ndiyo wakati wake na Yanga wamempa kazi ya kuhakikisha kikosi chao kinafanya kazi ya uhakika katika Ligi ya Mabingwa na mtihani mkubwa ni watakapokutana na Al Ahly kama watavuka kizingiti laini cha Wacomoro.

Gazeti la Championi lilikuwa chombo cha kwanza nchini cha habari kuandika kuhusu uamuzi wa Yanga kujitupia kwa van der Pluijm.

Sasa tayari yuko na leo alikuwa apelekwe Zanzibar, lakini huenda akapumzika kujiandaa na safari ya Uturuki.

Pamoja na mambo mengi lakini kocha huyo ana mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake.

Utulivu:
Yanga imeamua kufanya kwa utulivu suala la kocha, awali lilikuwa likipelekwa mbio na kambi ya Uturuki, ikitaka kocha awahi kambi hiyo.
Lakini sasa uongozi wake umekubali hata kama kocha mpya hatakwenda Uturuki, lakini inataka ipate ‘mtu’ wa uhakika wa kuziba nafasi ya Brandts na ambaye atakuwa na uwezo kweli.

Mvuto:
Mvuto wa van der Pluijm kwa Yanga umetokana na mafanikio yake kwa Berekum Chelsea ambayo ilifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.
Ilikuwa Kundi B na timu za Al Ahly, TP Mazembe na Zamalek ambao ni vigogo waliowahi kuchukua ubingwa Afrika zaidi ya mara moja, lakini Berekum Chelsea ikaonyesha inaweza.
Hicho ndiyo kitu cha kwanza kilichoivutia Yanga kwa kuwa inahitaji kocha wa kuifikisha mbali kwenye Ligi ya Mabingwa ikizingatiwa katika mechi ya pili tu (kama itawang’oa Wacomoro), itakutana na Al Ahly ambao ndiyo mabingwa.
Kingine kinachoonyesha kuwavuta Yanga ni umri wa kocha huyo, miaka 64 ni sawa na mzazi hasa, lakini makocha wengi wenye umri huo wamekuwa wakali, wanajali zaidi kazi na wasiokuwa na mzaha hata kidogo.

Mazingira:
Kwa mazingira ya nchi za Kiafrika, van Pluijm hawezi kuwa na hofu hata kidogo kwa kuwa ameishi katika bara hili kwa zaidi ya miaka 10.
Miaka yote hiyo ameishi nchini Ghana ambako ameoa mrembo wa Kiafrika wa nchi hiyo.

Uwanja:
Mholanzi huyo ni mtu wa misimamo sana, amewahi kususia mazoezi kutokana na ubovu wa uwanja. Kama Yanga itaingia mkataba naye, basi ina wakati mgumu kuhakikisha inamaliza tatizo hilo.
Kabla ya kuondoka kwa Brandts, kilio chake kilikuwa uwanja usiokuwa na kiwango na magoli madogo, maana yake van Pluijm lazima atalizungumzia, kama halitatekelezwa kama ilivyokuwa kwa Brandts, basi kuna tatizo linaweza kutokea.

Misimamo:
Van der Pluijm ni mtu mwenye misimamo kweli, kama akikubaliana na Yanga na kuanza kazi, maana yake wachezaji wajiandae.
Anatoa ushirikiano mkubwa kwa wachezaji, lakini ni mkali na asiyehofia jina la staa yeyote.
Vyombo vya habari vya Ghana vilimbandika jina la Kiboko ya Vigogo kwa sababu mbili, kwanza kuzipa wakati mgumu timu kongwe za Ghana kama Asante Kotoko lakini kuwaweka benchi wachezaji nyota walioonekana kuvimba vichwa na timu ya Berekum Chelsea ikaendelea ‘kukamua’.

Wachezaji wageni:
Amekuwa na msimamo wa kutaka wachezaji wa kigeni wanaoonyesha uwezo mkubwa kuthibitisha tofauti yao na wenyeji.
Hivyo, Emmanuel Okwi, Mbuyu Twite, Hamisi Kiiza na Didier Kavumbagu wanalazimika kufanya kazi kweli na si kubahatisha, la sivyo kibarua kitakuwa kigumu ikizingatiwa msimu ujao ni wachezaji watatu tu.

Mfumo:
Uchezaji wa timu anazozifundisha ni kasi sana, anataka washambulie pamoja na kurudi pamoja, lakini amekuwa akisisitiza kikosi chenye walinzi warefu au wenye uwezo mkubwa wa kupiga vichwa.
Mchezaji akiwa mvivu, huenda akawa na wakati mgumu wa kupata namba katika kikosi chake.
Ndiyo maana mazoezi yake ya mwanzo wa msimu kama timu ataanza nayo, yanakuwa makali sana kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa fiti kweli.

Van Nistelrooy:
Alimuibua mshambuliaji nyota wa Uholanzi, Ruud van Nistelrooy akiwa na umri wa miaka 17 tu na kumpa nafasi ya kucheza katika kikosi cha FC Den Bosch cha nchini kwao Uholanzi.
Van Pluijm aliitumikia FC Den Bosch kwa miaka 28 akiwa mchezaji na baadaye kocha. Akiwa kipa alicheza mechi 338 kwa misimu 18 kabla ya maumivu ya goti kumlazimisha kupumzika soka.
Aprili 1995, aliingia mkataba wa miaka miwili kuinoa SBV Excelsior hadi Desemba kabla ya kumuachia nafasi hiyo msaidizi wake John Metgod.
Mwaka 1999 alitua nchini Ghana na kujiunga na Ashanti Gold SC na kusaini mkataba wa mwaka, baadaye alitua nchini Ethiopia na kuanza kuinoa Saint George.
Sasa amekuwa akifanya kazi ya kuinoa timu ya vijana ya Feyenoord Ghana inayopata msaada kutoka katika klabu ya Feyenoord ya Rotterdam nchini Uholanzi.

Ngumi mkononi:
Oktoba, mwaka jana, akiwa na kikosi cha mabingwa wa Ghana wakati huo cha Medeama Sporting Club, van Der Pluijm alisaini mkataba wa miaka miwili, lakini hakudumu hata robo ya mkataba huo.

Kwani siku chache baada ya Makamu wa Rais wa Madeama, Albert Commey, kumtangaza kuwa kocha mkuu, akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi saba tu, van Der Pluijm alitangaza kuachia ngazi.
Uongozi wa Madeama ulikubali na kuficha, lakini ukweli baadaye uligundulika kuwa kocha huyo Mholanzi alizozana na msaidizi wake akavurumisha ngumi.
Katika mahojiano yake na mtandao wa Caf na vyombo vingine vya habari, Mholanzi huyo amekuwa akisisitiza kutotaka kulizungumzia suala hilo kwa madai ni sawa na kuongeza maadui bila sababu za msingi.
Kutokana na hali hiyo, alionyesha kuchukizwa na mwenendo wa mambo kwa kuwa kila alichokuwa akieleza kibadilishwe hakikufanyika, pia msaidizi wake pamoja na kwamba alipendekeza kuchukuliwa kwa Mholanzi huyo kama bosi wake, alikuwa mbeya sana.
Pamoja na hivyo, kikosi chake cha Madeama hakikufanya vizuri kabisa, kwani alianza na mechi ya Kombe la Super Cup dhidi ya Asante Kotoko na kuchapwa  bao 3-0. Aliiongoza timu kwa jumla ya mechi saba, badala ya kubeba jumla ya pointi 21, timu yake ilipata pointi nane tu!
Katika mechi hizo saba, kikosi chake kilishinda mechi moja tu, sare tano na kupoteza mechi moja.
Wakati anaondoka alikiacha kikiwa katika nafasi ya tisa kwenye ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara wakati huo, Asante Kotoko.
 
Credit:SALEH ALLY BLOG

TFF yatoa ubani msiba wa Njohole, kuzikwa kesho Mngeta


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Boniface Njohole kilichotokea jana (Januari 12 mwaka huu) mkoani Morogoro.
Njohole ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Ufundi na Mashindano ya Chama cha Soka Morogoro (MRFA) hadi umauti unamkuta anatarajia kuzikwa kesho (Januari 14 mwaka huu) kijijini kwao Mngeta wilayani Ifakara.
TFF imesema msiba huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira wa miguu kwani alitoa mchango akiwa mchezaji, kocha na kiongozi kwa nyakati tofauti, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF imetoa pole kwa familia ya marehemu Njohole, klabu ya Reli na MRFA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. 
Aidha, TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
Wakati huo huo: Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB) ya TFF, Hamad Yahya atakuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa semina ya waamuzi na makamisha.
Semina hiyo ya siku mbili itafungwa kesho (Januari 14 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi zaidi ya 100 na makamishna 50 wanashiriki katika semina hiyo. Makamishna hao ni baadhi ya wale wanaosimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Kwa upande wa waamuzi ni wale wa daraja la kwanza (class one) ambao ndiyo wanaochezesha mechi za VPL na FDL. TFF inatarajia kuandaa semina nyingine baadaye mwaka huu kwa makamishna wapya wanaotaka kusimamia mechi za VPL na zile za FDL.

Jamal Malizni kuzuru kituo cha soka Alliance cha Mwanza


Rais wa TFF, Jamal Malinzi
Na Boniface Wambura RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atafanya ziara ya siku moja kutembelea kituo cha mpira wa miguu wa vijana cha Alliance cha jijini Mwanza. Lengo la ziara hiyo ni kuangalia jinsi Alliance inayoendesha shughuli zake ili Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liweze kushirikiana na kituo hicho kwa karibu. Rais Malinzi katika ziara hiyo atakayoifanya keshokutwa (Januari 15 mwaka huu) atafuatana na Mwenyekiti wa Kamati ya ya Vijana ya TFF, Ayoub Nyenzi na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ramadhani Nassib.
Alliance inatarajia kufanya mashindano yatakayoshirikisha vituo vyote vya kuendeleza soka kwa vijana (academy) wiki ya tatu ya Februari mwaka huu jijini Mwanza.
Mashindano hayo yatashirikisha timu za umri wa miaka 13, 15 na 17 ambapo Alliance itagharamia malazi, chakula na usafiri wakati timu hizo zikiwa jijini Mwanza.

AC Milan yazidi kudoda Seria A

Berrard Demonico
Sassuolo - AC milan
'Muuaji' Demonico Berardi (25) akishangilia bao na wachezaji wenzake walipoiangamiza AC MIlan

KLABU ya AC Milan imeendelea kuteseka kwenye Ligi Kuu ya Italia Seria A baada ya usiku wa jana kunyukwa mabao 4-3 na 'vibonde' Sassuolo iliyokuwa uwanja wake wa nyumbani.
Shujaa wa wenyeji alikuwa ni Domenico Berardi aliyefunga mabao yote manne ya Sassuola katika dakika za 15, 28, 41 na 47 na kinda huyo mwenye miaka 19 kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo kufunga idadi hiyo ya mabao manne katika Seria A ikiwa ni baada ya zaidi ya miaka 80 na kumweka pabaya kocha wa AC Massimiliano Allegri.
Wageni walianza kuwaduwaza wenyeji kwa kupata mabao mawili ya chapchap kupitia nyota wake, Robinho na Mario Balotelli waliofunga dakika ya 9 na 13 kabla ya Berardi kuyarejesha na kuongeza jingine na kufanya timu ziende mapumziko zikiwa 3-2.
Kipindi cha pili Berardi aliendelea kuinyanyasa ngome ya AC Milan kwa kuongeza bao jingine kabla ya wageni kujipatia bao jingine la kujifutia machozi lililofungwa na Montolivo dakika nne kabla ya kumalizika kwa mchezo huo na kuicha Milan ikisaliwa na pointi zake 22 ikiwa nafasi ya 11.
Kwa ushindi huo Sassuolo iliyokuwa nafasi ya 18 imepanda hadi kwenye nafasi ya 16 ikifikisha pointi 17.Uganda The Cranes waanza vyema CHAN 2014


Man of the match Yunus Ssentamu celebrates his second goal against Burkina Faso
Sentamu akishangilia bao lake la pili

VINARA wa kandanda Kanda ya Afrika Mashariki, Uganda The Cranes imeanza vyema kampeni zake za kuwania ubingwa wa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) baada ya kuisambaratisha Burkina Faso kwa mabao 2-1 katika pambano la kundi B lililochezwa usiku wa jana.
Mabao mawili kutoka kwa aliyekuwa nyota wa mchezo huo, Yunus Sentamu moja kila kipindi yalitosha kuiweka Uganda kileleni mwa kundi hilo ikifikisha pointi tatu na mabao mawili, huku Burkina Faso wakienda mpaka mkiani ikiwa haina pointi yoyote.
Sentamu alifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 15 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 73 na wapinzani wao kupata bao la kufutia machozi dakika mbili kabla ya kumalizika kwa pambano hilo kupitia kwa Cyrille Bayala.
Michuano hiyo itaendelea tena jioni ya leo kwa mechi za kundi C, Ghana kuvaana na Jamhuri ya Congo na Libya kukabiliana na wawakilishi wengine wa ukanda wa CECAFA, Ethiopia.