STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 28, 2013

Hatma ya ubingwa Simba mikononi mwa Toto na Yanga J'mosi

 
Yanga


Simba

HATMA ya Simba kuendelea kulifukuzia taji lake la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inalolishikilia inatarajiwa kufahamika Jumamosi wakati itakapovaana na Toto African jijini Mwanza katikia mfululizo wa ligi hiyo iliyobakisha mechi tano kabla ya kufunga msimu.
Simba iliyojeruhiwa jana kwa kulambwa bao 1-0 na wenyeji wao Kagera Sugar, mjikni Bukoba itaikabilia Toto kwenye uwanja wa CCM Kirumba na matokeo yoyote mabaya kwao yatawafanya waliteme rasmi taji lao na kuliacha bila mwenyewe.
Kwa sasa mabingwa hao wana pointi 34, pointi 14 nyuma ya vinara wanaoongoza ligi hiyo Yanga ambayo nayo itakuwa dimbani wikiendi hii mjini Morogoro kuvaana na maafande wa Polisi Moro na ushindi wowote utamaanisha utawavua Simba ubingwa.
Hata hivyo Simba itavuliwa rasmi ubingwa Jumamosi iwapo Yanga itashinda kisha wao wapate sare au kipigo toka kwa Toto kwani haiataweza kufikisha pointi ambazo itakuwa imezikusanya Yanga yaani 51. Kwa sasa Yanga ina pointi 48.
Tayari Simba kupitia kocha wake msaidizi Jamhuri Kihwelu 'Julio' wameapa kupigana kiume CCM Kirumba ili kuhakikisha wanazoa pointi tatu toka Kanda ya Ziwa.
Wakati Simba ikiwa katika kitimtim hicho jini Mwanza, Yanga timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote ndani ya mwaka huu wa 2013, itakabiliana na timu isiyotabirika ya Polisi ambayo tangu ifanye mabadiliko ya benchi la ufundi imekuwa tishio.
Kocha wa Yanga Ernst Brands amenukuliwa akisema kuwa vijana wake tayari kuendeleza rekodi ya ushindi ili kutangaza ubingwa mapema, licha ya kukiri Polisi sio timu ya kubeza.
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo mbali na mechi hizo za watani wa jadi zinazochezwa viwanja tofauti, michezo mingine ya wikiendi hii inatarajiwa kuzikutanisha timu ndugu za Kagera Sugar itakayoialika Mtibwa Sugar mjini Bukoba, huku Azam wenyewe watakuwa Mlandizi kuvaana na Ruvu Shooting iliyotamba kuwashikisha adamu Jumamosi.
Mechi nyingine kwa wikiendi hii itazikutanisha timu zaJKT Oljoro watakaovaana na maafande wenzao JKT Ruvu mjini Arusha ambayo haitakuwa na nyota wake, Zahoro Pazi aliye majeruhi wa goti, huku African Lyon itaikaribisha Coastal Union uwanja wa Chamazi ikiwa inapigana kujinasua mkiani ilipokung'ang'ania kwa muda sasa.

Bunge lamlilia Mbunge wa CUF aliyefariki mchana

TANZIA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGE LA TANZANIA 


Spika wa Bunge, Mhe. Anne Makinda, (Mb) anasikitika kutangaza kifo cha Mbunge wa Chambani, Pemba, Mhe. Salim Hemed Khamis (CUF) kilichotokea leo mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Marehemu Khamis, alilazwa jana katika Hospitali hiyo baada ya kuanguka ghafla akishiriki vikao vya kamati za Bunge vinavyoendelea katika Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam.
Marehemu ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alikimbizwa Hospitalini na kulazwa katika chumba cha wagonjwa Mahututi Muhimbili baada ya kubainika kuwa alikuwa amepata kiharusi kufutia shinikizo la damu lililopelekea kuanguka kwake ghafla akiwa katika majukumu yake katika Kamati za Bunge. Kutokana na Msiba huu, Shughuli zote za Kamati za Bunge zimearishwa hadi jumanne tarehe 2 Aprili, 2013.
Marehemu ataangwa kesho tarehe 29 Machi, 2013 saa mbili na Nusu Asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na kusafirishwa kwa ndege kwenda Pemba Saa Nne Asubuhi ambapo Mazishi yatafanyika nyumbani kwake Chambani, Pemba Mchana. Mhe. Spika anatoa Pole kwa Familia ya Marehemu, wananchi wa Chambani, Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Wabunge wote na Watanzania wote kwa ujumla.
Mungu alilaze Roho ya Marehemu, Mahali Pema Peponi, Amina!
Imetolewa na
Idara ya Habari, Elimu Kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
28 Machi, 2013

Mechi ya Azam yahamisha Bonanza la Wanahabari TCC

BONANZA la vyombo mbalimbali vya habari lililopangwa kufanyika Aprili 6 mwaka huu viwanja vya Leaders Klabu likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), sasa litafanyika viwanja vya Sigara (TCC), Chang’ombe pia Dar es Salaam.

Uamuzi wa kuhamisha bonanza hilo umechukuliwa na sekretarieti ya TASWA kutokana na maombi ya waandishi wengi wa michezo kwa vile siku hiyo kuna mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika kati ya timu ya soka ya Azam na Barrack Young Controllers ya Liberia  itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku hiyo.

Azam ni timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye michuano ya Afrika kwa ngazi ya klabu baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kutolewa katika raundi ya awali.
Tunaamini kwa bonanza kufanyika Sigara itakuwa rahisi kwa wadau wetu kushiriki kwenye bonanza na wale wengine watakaohitaji kwenda uwanjani wafanye hivyo wakitokea Sigara kwa hakuna umbali mrefu na kisha warejee kujumuika na wenzao mpaka mwisho.
Tunawaomba radhi kwa mabadiliko hayo, lakini yakiwa na lengo la kujenga na kuwa pamoja na wenzetu wa Azam kuhakikisha tunashirikiana nao kwa namna mbalimbali siku hiyo.
Bonanza hili linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Bonanza hilo ambalo litahusisha wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka katika moja ya bendi kubwa za muziki wa dansi hapa nchini, ambayo itatangazwa siku zijazo.
Nawasilisha
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA