STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 19, 2012

Paparazi asimulia magumu aliyopata akipiga picha mauaji ya Mwangosi

Mfumo wa picha uliotengenezwa na kurushwa na mitandao ya kijamii ukionyesha namna marehemu Daud Mwangosi aliyekuwa mwanadishi wa kituo cha Channel Ten alivyopoteza uhai wake hivi karibuni.
MPIGAPICHA mkongwe nchini wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga, ni kati ya walioshuhudia tukio la kuzingirwa, kuteswa hadi kuuawa kinyama na askari wa Jeshi la Polisi kwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi hapo Septemba 2, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Senga, kati ya wapiga picha maarufu na wakongwe nchini waliopita katika magazeti mbalimbali, anayefanya kazi hiyo kwa takribani miaka 28 sasa, anasimulia aliyoyashuhudia siku hiyo wakati akitimiza wajibu wake.
Kubwa zaidi, Senga anasema ameweza kupata picha nyingi za ukatili huo uliofanywa na askari polisi dhidi ya Mwangosi, kuanzia kukamatwa kwake, kupigwa na kuteswa kabla ya kuelekezewa bunduki ya mdomo mpana katika tumbo na kuukatisha uhai wake.
Katika mahojiano maalumu, Senga anasema tangu kutokee mauaji yale ya kinyama ambayo yangeweza kumtisha yeyote yule kutokana na kufanywa na askari polisi wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao, mengi yamezungumzwa.
Anasema kinachomsikitisha zaidi, ni kitendo cha baadhi ya waandishi kuibuka na kudai kuwa sio tu walikuwepo karibu ya tukio hilo, pia ndio waliopiga picha zikionesha mauaji hayo ikiwemo ile ya askari aliyeelekeza mtutu tumboni kwa Mwangosi.
Senga anasema kwake haoni fahari yoyote kujitwika jukumu hilo la kuueleza umma kuwa alikuwa hatua chache tu wakati Mwangosi anafanyiwa unyama ule na askari polisi, bali ameamua kuweka sawa ili kuepuka upotoshwaji wa tukio hilo la kikatili lililogharimu uhai wa Mwangosi.
Anasema ameamua kufanya hivyo baada ya kubaini kuwa kupitia tukio hilo lililogusa wengi, baadhi ya watu ambao hawakuwepo kwenye eneo alilosulubiwa Mwangosi hadi kuuawa, wamejitwisha ushuhuda wa tukio hilo na kusema ni hatari kuleta maigizo kwenye tukio nyeti kama hilo.
Senga anasisitiza kuwa amekuwa kimya kuhusu jambo hilo, lakini baada ya kushauriwa na watu wenye busara wakiwamo wakuu wake wa kazi, akaona aeleze kilichotokea kuweka mambo sawa, japo hakutaka kwani hakuona ni tukio la kujipatia sifa isipokuwa simanzi isiyofutika haraka machoni.
Anasema licha ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka yote hiyo na kuwahi kukumbana na kadhia nyingi, lakini mazingira ya kuuawa kwa Mwangosi, hatayasahau kamwe katika maisha yake yote atakayojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
“Jamani tukio la kuuawa kwa Mwangosi linatisha. Wakati anaburutwa, kupigwa, kuteswa na kundi la askari, usingeweza kusema ni mwandishi wa habari, pengine ungeweza kusema ni kibaka au jambazi, hakuwa na muda wa kujihami zaidi ya kusema ‘mnaniua mimi ni mwandishi’,” anasema Senga.
Anasema alishangazwa namna askari polisi walivyokuwa wamempania Mwangosi kwani alikumbana na mateso hayo akiwa na kamera mkononi na mkoba mdogo begani kwake, kuashiria hakuna kilichompeleka Nyololo, isipokuwa kutimiza wajibu wake.
Senga anasema cha kushangaza zaidi ni kuona askari wale walivyokuwa wamejawa na jazba iliyowafanya wampuuze hata bosi wao (aliyemkumbatia Mwangosi), ambaye licha ya kuwaeleza wamwache, wasiendelee kumtesa kwani anamjua, wakazidi kumshambulia wakati huo Mwangosi akijitetea na kuwasihi wamwache bila mafanikio.
Katika mazingira hayo, Mwangosi akiwa amezingirwa na askari kama nane hivi akiwemo mtetezi wa mwandishi huyo, na askari ambaye alikuja kujulikana jina lake baadaye kuwa ni Pacificus Cleophace Simon (G2372), akiwa karibu mno akaelekeza mdomo wa bunduki tumboni mwa mwandishi huyo na kumlipua.
Mbali ya kuusambaratisha mwili wa Mwangosi, alimjeruhi pia eneo la mapaja askari yule aliyekuwa akimtetea Mwangosi (OCS Mwampamba).
Kinachosikitisha zaidi, ni kwamba wakati wote huo askari wakimtesa Mwangosi, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Iringa, Michael Kamuhanda, alikuwepo mita chache tu kutoka kwenye tukio, akiwa kwenye gari yake (angalia picha namba 7).
Kabla ya Mwangosi kupigwa bomu, mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah Hamis alimfuata Kamuhanda aliyekuwa ndani ya gari yake iliyofungwa vioo (pengine kuogopa moshi wa mabomu) na kuhoji vipi askari wanamsulubu Mwangosi?
Alichofanya Kamuhanda, ni kumpuuza Abdallah na alipoona anazidi kusumbuliwa, akashusha kioo kumsikiliza, lakini hakujibu kitu zaidi ya kufunga kioo na kutoa picha kuwa, alichokuwa akifanyiwa Mwangosi ni agizo lake au ni malipo aliyostahili kwa siku ile.
Senga anasema kwa kulishuhudia kwa macho yake tukio hilo la kinyama lililokatisha uhai wa Mwangosi, kamwe hataweza kulisahau kutokana na kufanywa katika mazingira ya kutisha na kuogofya huku yeye akipiga picha za kuteswa hadi kuuawa kwa bomu kikatili.
Mwanahabari huyo mkongwe amebainisha kuwa, katika tukio hilo aliweza kupiga picha karibia zote zilizotumika kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje, yakiwemo magazeti na hata televisheni, kubwa zaidi zikipingana na hila za Jeshi la Polisi kutaka kupindisha ukweli wa mambo.
Ikumbukwe, jioni ya siku ya tukio, Kamanda Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, bila hata hofu ya Mungu ndani yake, akaanza kudai eti kabla ya kutokea mlipuko wa bomu, Mwangosi alitokea upande wa wafuasi wa CHADEMA. Ni aibu na hatari kubwa kwa taifa.
Mazingira kabla ya kifo
Senga anasema asubuhi ya siku ya tukio, waandishi wa habari walialikwa katika mkutano na Kamanda Kamuhanda ambao ulifanyika ofisini kwake, mjini Iringa, yeye akiwa mmoja wao.
Anasema ulikuwa ni mkutano wa kutoa tamko la kuzuia mikutano ya kisiasa, lakini hususan iliyokuwa imepangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kilikuwa kinaendelea na mikutano yake mkoani humo baada ya kutoka Morogoro.
Polisi walitaka kusitishwa kwa mikutano hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kuongezwa kwa muda wa zoezi la sensa kwa siku saba zaidi, baada ya zile siku saba za kwanza kumalizika huku lengo lililokuwa limekusudiwa kutotimia.
Senga anasema baada ya mkutano huo, waandishi walitaka kujua upande wa pili yaani CHADEMA, hivyo walielekea walikokuwa ambako nako kulifanyika mkutano na waandishi wa habari ukiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Baada ya zuio la mkutano
Senga anasema CHADEMA walitoa tamko wakilaumu utendaji wa Jeshi la Polisi kwa madai kuwa, lilikuwa likifanya kazi zake kwa kuongozwa na matakwa ya wanasiasa hususan wa chama tawala (CCM), lakini walisitisha mikutano yao japo kwa shingo upande.
“Katika mkutano wa waandishi wa habari na Kamanda Kamuhanda, yalijitokeza maswali mengi likiwemo la mikutano ya ndani iliyokuwa ikifanywa na CHADEMA, wakati wa zoezi la sensa likiendelea kabla ya kuongezwa zile siku saba, ambalo lilijibiwa na kamanda huyo, kwamba mikutano hiyo inaruhusiwa,” anasema Senga na kuongeza:
“Uongozi wa CHADEMA uliamua kuendelea na mikutano ya ndani ikiwa ni pamoja na kufungua matawi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa katika kila jimbo, wakati wakisuburi kumalizika kwa sensa ya awamu ya pili.”
Ufunguzi wa matawi
Senga anasema baada ya hapo ndipo Chadena wakajipanga kwenda kufanya zoezi hilo mchana wa siku hiyo kufungua matawi katika kijiji cha Nyololo kwa kuteua viongozi wawili kuongoza zoezi hilo bila kumshirikisha Katibu Mkuu, Dk. Slaa.
“Nakumbuka walipangwa viongozi wa kuendesha zoezi hilo akiwemo Naibu Katibu (Zanzibar), Hamad Yusuf na Kamanda wa Operesheni hiyo, Benson Kigaira. Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa hakushiriki kabisa siku hiyo, alibaki hotelini,” anaongeza Senga.
Mwangosi anasita kwenda katika ufunguzi
Wakati wa maandalizi ya kwenda katika ufunguzi wa matawi, Senga anasema Mwangosi alimwambia asingekwenda katika hafla hiyo kwa kuwa hakuona tena kama kungekuwa na habari kwani ilikuwa ni mikutano ya ndani tu.
Anasema kama ilivyo kawaida kwa wanahabari, kunusa na kutafuta habari zilipo, zilizagaa taarifa kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walikuwa wamemwagwa katika eneo ambalo CHADEMA wangefungua matawi katika kijiji hicho.
Kwa taarifa hizo, wanahabari wengi wakatamani kwenda kushuhudia ufunguaji huo wa matawi (akiwemo Mwangosi), pasipo kujua kuwa kumbe yeye ndiye anakwenda kuwa habari iliyotikisa nchi.
“Ni kweli ndivyo ilivyokuwa, baada ya kufika katika Kijiji cha Nyololo, tulikuta maandalizi yamekamilika, askari hao wakiwa na silaha za kila aina. Nilijua ni kazi yao pengine walipewa maelekezo ya kuwalinda viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wakati wakifungua matawi yao ili kuwahakikishia usalama wao,” anasema Senga.
Hata hivyo, anasema fikra zake hizo zilianza kupotea baada ya kuanza kutolewa amri na viongozi wa Jeshi la Polisi wa mkoa huo, wakiongozwa na RPC Kamuhanda na RCO ambao kwa nyakati tofauti walionekana kutofautiana, mwingine akikubali kufanyika kwa zoezi hilo kwa vile halikuwa na madhara na mwingine akitaka kusitishwa.
Kwa mujibu wa Senga, CHADEMA walifanikiwa kufungua tawi la kwanza wakiwa wamezingirwa na askari, lakini hali ilibadilika wakati wakifungua tawi la pili ambako polisi walianzisha mapambano dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho.
“Nasema leo hatutapiga mabomu, tutakamata viongozi, wakamateni viongozi wote wa CHADEMA,” anasimulia Senga alivyosikia amri kutoka kinywani mwa RPC alipokuwa akiwaamuru askari wake kutekeleza amri hiyo.
Senga anasema kabla amri hiyo haijatekelezwa, ghafla yakaanza kulipuliwa mabomu ya machozi kutoka kwa askari polisi kwa lengo la kuwatawanya wana-CHADEMA waliokuwa nje ya ofisi hizo.
Wakati mgumu kwa wanahabari
Anasema viongozi hao walitawanyika huku hata wasio viongozi wakakimbia kusikojulikana. Hapo ndipo wakati mgumu ulipoanzia kwa wanahabari, kwa kubwia moshi mzito wa mabomu yaliyolipuliwa katika kila kona ya eneo hilo.
Kama vile hapakuwa na tukio la kulipuliwa kwa mabomu, Senga anasema baadaye utulivu ulirejea, lakini wakati huo hakukuwa na mwananchi hata mmoja akipita katika maeneo hayo, isipokuwa askari tu na baadhi ya waandishi wa habari.
Senga anasema aliendelea kutekeleza majukumu yake akiamini kuwa kwake mbele ya askari wale ni hakikisho la usalama ingawa baadhi yao walishaanza kuondoka baada ya kukamilisha kazi yao, wakitembea na mbele yao kukiwa na magari matatu yakielekea barabara kuu ya Dar es Salaam - Mbeya.
Mwangosi anaanza kusulubiwa
Anasema wakiwa katika msafara huo, ghafla aliona mtu akishambuliwa kwa kipigo na askari hao waliokuwa mbele yake, akashtuka na kujiuliza ni nani na kwa sababu gani kwani hali ya mambo tayari ilikuwa tulivu.
“Mmoja wa askari hao aliingilia kati na kumkumbatia, akiwazuia askari wenzake wasiendele kumpiga akisema: “mwacheni namfahamu ni mwandishi, acheni jamani,” akijaribu kuokoa uhai wa mtu huyo ambaye wakati huo miguu yake ilikuwa katikati ya miguu ya askari yule msamaria. Wakati huo akionekana kuishiwa nguvu kwa kipigo kikali,” anasema Senga.
Anasema licha ya jitihada kubwa za askari yule msamaria mwenye nyota tatu mabegani mwake kuwazuia wenzake wasiendelee kumpiga, bado kundi la askari wale waliendelea kumpa kipigo. Baadaye alimtambua kwa ukaribu kuwa alikuwa ni Daudi Mwangosi.
Wakati hayo yakiendelea, Senga anaeleza kuwa, akili yake ilimkumbusha kuwa alikuwa kazini, hivyo pamoja na huruma ya kuguswa na unyama ule, pia akapaswa kuchukua picha za tukio hilo bila kujali kitu gani kingempata kutoka kwa askari wale wenye hasira iliyopitiliza.
Anaongeza kuwa, ghafla mmoja wa askari hao alimkaribia na kumshika mkono kabla ya wengine wawili kuongezeka, wakamzonga sana, wakati huo Mwangosi akiendelea kusulubiwa.
“Tukupeleke pale na wewe?” lilikuwa swali kutoka kwa askari hao kwa Senga, akimaanisha pale alipokuwa akisulubiwa Mwangosi. Senga anasema wakati huo hakuwa na jibu la haraka.
Mwangosi alipuliwa
Senga anasema wakati askari hao wakiwa bado wanamsulubu Mwangosi, ghalfa akasikia mlipuko mkubwa na kwa macho yake, akashuhudia wale askari waliokuwa wamemzingira wakatawanyika kwa taharuki.
Anasema baadhi yao walionekana wakielekea kwenye magari yaliyokuwa mbele, wakati huo Kamanda Kamuhanda akiwa umbali kama wa mita tano hivi ndani ya gari yake iliyokuwa imefungwa vioo vyote.
Senga anasema baada ya mlipuko ule alichoweza kushuhudia ni nyama zilizosambaa huku kando yake akiwepo askari (yule aliyekuwa akimtetea kabla ya kulipuliwa kwake), akiwa amejiinamia kando ya mabaki hayo ya mwili wa Mwangosi, naye akiwa amejeruhiwa sehemu ya paja la kushoto.
Anasema tukio hilo lilimfanya abaki ameduwaa kwa dakika chache asijue la kufanya, kwani ni mara yake ya kwanza kuona unyama na ukatili wa kiwango hicho, tena ukifanywa na askari polisi kwa mtu asiye na silaha yoyote zaidi ya begi na kamera mkononi mwake.
“Swali kubwa ambalo nilijiuliza moyoni mwangu, ni kama kweli nilichokuwa nikishuhudia mbele yangu ulikuwa mwili wa Mwangosi,” anasema Senga.
Katikati ya swali hilo, Senga anasema akakumbuka kuwa yu kazini, hivyo akaendelea kupiga picha za mabaki ya mwili wa Mwangosi, wakati huo kando yake akiwepo yule askari aliyekuwa akilia kwa uchungu akisema, “Afande wameniua.” Pengine akimweleza Kamuhanda aliyekuwepo karibu.
Anasema baadaye Kamuhanda akiwa ndani ya gari lake karibu na eneo la tukio, aliwaamuru askari warudi kumchukua askari yule majeruhi, hivyo wakarejea na kumbeba wakimweka kwenye gari.
Senga anasema dakika hizo chache kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwake, akibaki eneo hilo ameduwaa, akiangaza macho mbele na nyuma kwani wakati huo hakuona raia wa kawaida zaidi ya askari.
Anasema katikati ya butwaa hiyo, ufahamu ukaanza kumrejea kuwa kilichokatisha uhai wa Mwangosi kwa kuusambaratisha mwili wake, si risasi ya kawaida pengine ni mlipuko wa bomu kutokana na ukubwa wa kishindo chake.
Senga anasema baada ya tafakuri hiyo, hofu ya kibinadamu ikaanza kumpata, akijiona kuwa kumbe hata yeye hakuwa eneo salama kwake, akatamani kujificha kutokana na hofu kubwa aliyokuwa nayo.
Anasema alichofanikiwa kufanya baada ya kurudi katika hali ya kawaida, alirejea nyuma kama mita hamsini na kuuona ua uliojengwa kwa magome ya miti, akajibanza hapo huku machozi yakimtiririka akimlilia Mwangosi na kuongeza kuwa, hakuwa tena na hamu wala nguvu ya kushika kamera.
“Bado sikuamini na kuridhika na nilichokishudia kwa macho yangu mawili, niliendelea kuchungulia kujua nini kitaendelea. Ilichukua takribani dakika 15, askari hao wakikusanya mabaki ya mwili wa Mwangosi kwa kutumia ngao zao na kupakiza katika moja ya magari yao,” anaongeza.
Anasema baada ya zoezi hilo askari hao waliondoka, wakiwa ndani ya magari pamoja na baadhi ya viongozi, pia baadhi ya wafuasi waliokuwa wamewakamata kabla ya kuuawa kwa Mwangosi, wakielekea kusikojulikana.
“Mwenyezi Mungu ailaze pema roho ya marehemu Mwangosi. Amina,” anamaliza Senga.

Moja ya picha iliyopigwa na Senga ikionyesha askari Polisi (FFU) wakiwa kamili na zana zao
 CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA

Khaleed Abeid kuongoza Kamati ya Uchaguzi ya SPUTANZA

KIUNGO wa zamani wa kimataifa nchini aliyewahi kung'ara na timu za Simba na Taifa Stars, Khaleed Abeid, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Chama cha Umoja wa Wachezaji Soka Tanzania, SPUTANZA.
Khaleed ameteuliwa pamoja wajumbe wengine sita kuiongoza kamati hiyo kwa minajili ya kusimamia uchaguzi mkuu wa SPUTANZA unaotarajiwa kufanyika Oktoba 20.
Uteuzi huo ulitangazwa jana na Katibu Mkuu Msaidizi wa SPUTANZA, Abeid Kasabalala alipozungumza na MICHARAZO na kuwataja wengine waliopo katika kamati hiyo kuwa ni Hashim Memba ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Kasabalala aliwataja wengine wanaounda kamati hiyo ni  Sued Mwinyi anayekuwa Katibu wa Kamati pamoja na wajumbe wanne akiwamo nyota za zamani wa timu za Yanga na Pan Africans.
"Wajumbe wa kamati hiyo ni Is'haka Hassani 'Chukwu', Carlos Mwinyimkuu, Saad Mateo na Hamis Shaaban," alisema Kasabalala.
Kasabalala aliongeza mpaka sasa zoezi la uchukuaji na urudishaji wa fomu kwa ajili ya uchaguzi wao unaendelea na zoezi hilo litahitimishwa keshokutwa kabla ya kamati yao kupitia majina kwa ajili ya kuyachuja.

Mwisho

Kivumbi za Mabingwa Ulaya kuendelea tena leo

Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson

KOCHA wa Manchester United, Alex Ferguson amesema hapatakuwa na marudio ya kutolewa mapema kama mwaka jana katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakati wakijiandaa kucheza mechi yao ya ufunguzi wa Kundi H nyumbani dhidi ya Galatasaray leo.
Mabingwa hao mara tatu wa Ulaya walishindwa kusonga mbele kutoka katika hatua ya makundi msimu uliopita baada ya kipigo cha kustusha cha 2-1 kutokakwa klabu ya Uswisi ya FC Basel katika mechi yao ya mwisho.
"Tumefungwa katika fainali mbili dhidi ya Barcelona na tumeshinda fainali nyingine mbili katika miaka 10 iliyopita lakini tunataka kufanya vizuri zaidi," Ferguson aliiambia tovuti ya klabu hiyo (www.manutd.com). "Hakika tutafanya vyema kuliko msimu uliopita, hakuna maswali kuhusu hilo.
"Kombe la Ulaya ni bab'kubwa. Kuna hisia kali kuelekea katika fainali ya Ulaya.
"Pia, bila ya maswali, kombe linainua heshima yako mchezoni kama ilivyo kwa Real Madrid na AC Milan. Tunataka kufikia kule kwa idadi ya makombe katika soka la Ulaya."
Kuanzia kwenye kipigo kutoka kwa Barcelona katika fainali ya mwaka 2011, Man U imeshinda mechi tatu tu za Ulaya kati ya 11 na imefungwa nne kati ya tano zao za mwisho.
Kikosi cha Ferguson, kinachoshiriki michuano hiyo kwa mara ya 18, ambayo ni rekodi, kitakuwa bila ya majeruhi wa muda mrefu Wayne Rooney leo lakini timu inalo "jembe" Robin van Persie lililotayari kuanza kwa mara ya kwanza kuichezea timu yake mpya katika michuano hiyo ya Ulaya.
Van Persie amekuwa katika kiwango cha juu tangu alipowahama mahasimu Arsenal mwisho wa msimu na tayari anaongoza katika ufungaji wa Ligi Kuu ya England akiwa na magoli manne, sawa na Michu wa Swansea City.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliachwa nje ya kikosi kilichoanza Jumamosi kabla ya kuingia kipindi cha pili na kuisaidia Man U kuifunga Wigan Athletic 4-0 katika ligi.
Mtokea benchi mwenzake Nick Powell alicheza mechi yake ya kwanza Man U na kufunga goli kali la shuti la mbali dhidi ya Wigan na mchezaji huyo wa zamani wa Crewe Alexandra alisema alikuwa na presha kubwa wakati alipoingia mbele ya mashabiki 75,142 kwenye Uwanja wa Old Trafford.
"Nilipoingia kwa mara ya kwanza ilinitisha kidogo kwa sababu nilizoea kucheza mbele ya mashabiki 5,000 tu," alisema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 18. "Lakini ni mazingira mazuri na mashabiki walikuwa bab'kubwa.
"Najifunza kila siku kutoka kwa viungo Paul Scholes, Michael Carrick, Ryan Giggs. Wameshapitia hayo na kutwaa mataji na nataka kushinda mataji pia."
Galatasaray wanacheza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika miaka sita.
Klabu hiyo ya Uturuki haijashinda mechi yoyote kati ya saba walizocheza dhidi ya timu za England lakini ilipata sare za kukumbukwa dhidi ya Manchester United, Liverpool na Leeds United katika rekodi zao.
Umut Bulut, ambaye amefunga magoli matano katika mechi nne za ligi msimu huu, anajiandaa kuwa patna wa mshambuliaji wa zamani wa Bolton Wanderers, Johan Elmander katika mashambulizi. Beki wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Eboue, anatarajiwa kuanza katika ulinzi.

Ratiba ya mechi za leo Ligi ya Mabingwa Ulaya:

Kundi E
Shakhtar          v Nordsjaelland
Chelsea           v Juventus
  
Kundi F
Lille                  v BATE Borisov
Bayern Munich v Valencia
  
Kundi G
Barcelona        v Spartak Moscow
Celtic               v Benfica
  
Kundi H
Man U             v Galatasaray
Braga              v CFR Cluj

Arsenal, Real Madrid zaanza vema Ligi ya Mabingwa Ulaya


UEFA Champions League | RESULTS


18 September
 
Dinamo Zagreb0 - 2FC Porto
 
LO Gonzalez (40)
S Defour (90)
Maksimir StadiumAttendance (15000)
Teams
18 September
 
PSG4 - 1Dynamo Kiev
Z Ibrahimovic (pen 18)
E Thiago Silva (28)
Alex (31)
J Pastore (90)

MLP Veloso (85)
Parc des PrincesAttendance (48000)
Teams

18 September
 
Montpellier1 - 2Arsenal
Y Belhanda (pen 8)
L Podolski (15)
YK Gervinho (17)
La MossonAttendance (30000)
Teams | Report
18 September
 
Olympiacos1 - 2Schalke 04
D Abdoun (57)
B Howedes (40)
K Huntelaar (58)
Karaiskakis StadiumAttendance (28000)
Teams

18 September
 
Malaga3 - 0Zenit St Petersburg
AFR Isco (2)
J Saviola (12)
AFR Isco (75)

 
La RosaledaAttendance (28000)
Teams | Report
18 September
 
AC Milan0 - 0Anderlecht
San SiroAttendance (20000)
Teams | Report

18 September
 
Borussia Dortmund1 - 0Ajax
R Lewandowski (86)
 
Signal Iduna ParkAttendance (80500)
Teams | Report
18 September
 
Real Madrid3 - 2Man City
JVdS Marcelo (75)
K Benzema (86)
CdSA Ronaldo (89)

E Dzeko (68)
A Kolarov (84)
Santiago BernabeuAttendance (67000)
Teams | Report

SIMBA, YANGA MAJARIBUNI TENA LEO


KINYANG'ANYIRO Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa michezo ya raundi ya pili ambapo mabingwa watetezi, Simba na watani zao Yanga watakuwa kwenye viwanja viwili tofauti kujaribu tena bahati yao katika ligi hiyo.
Jumla ya mechi saba zinatarajiwa kuchezwa kwenye ambapo kwenye dimba la Taifa, jijini Dar 'Mnyama' Simba itaikaribisha JKT Ruvu ya Pwani, wakati Yanga iliyoanza ligi kwa suluhu na timu ilipoapanda daraja ya Prisons-Mbeya, itakuwa ugenini tena uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuumana na  Mtibwa Sugar.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuanza vyema katika ligi hiyo kwa ushindi wa magoli 3-0 iliopata dhidi ya African Lyon wakati mabingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Yanga wana pointi moja iliyotokana na suluhu dhidi ya Prisons mkoani Mbeya.
Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic amenukuliwa akisema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na anachotaka kuona wanapata pointi tatu.
Cirkovic alisema kurejea kwa mshambuliaji wake Mzambia Felix Sunzu kumekifanya kikosi hicho kuwa na ushindani zaidi wa namba katika eneo la ushambuliaji kutokana na kila mmoja kuonyesha kiwango cha juu mazoezini.
"Hakuna mechi nyepesi, ninachohitaji ni kuona tunashinda na kupata pointi tatu katika mechi hizi za kwanza ili kuondoa wasiwasi katika mechi za mwishoni mwa ligi, kikosi changu kimekamilika," alisema kocha huyo raia wa Serbia.
Charles Kilinda, kocha wa JKT Ruvu, aliliambia gazeti hili kuwa timu yake imejiandaa vyema na mechi zote za ligi na si kwa ajili ya kuikabili Simba tu.
Kilinda alisema kwamba anafahamu mchezo huo utakuwa na ushindani huku akisikitika kumkosa mshambuliaji wake mpya, Mussa Hassan 'Mgosi' ambaye hajapata kibali chake cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka katika timu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ameichezea msimu mmoja uliopita.
Akiondoka bila ya mshambuliaji, Jerry Tegete na Rashid Gumbo, kocha wa Yanga, Tom Saintfiet, alisema kwamba mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utakuwa na upinzani mkubwa.
Hata hivyo, Saintfiet aliahidi kupata matokeo mazuri katika mchezo huo na kurejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga.
Kocha huyo amemjumuisha kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima licha ya kuwa mgonjwa.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime aliliambia gazeti hili kwamba wachezaji wake wamejiandaa vyema kushinda na hatimaye kutorudia makosa yaliyojitokea wakati wanaivaa Polisi Morogoro katika mechi ya kwanza ya ligi iliyoisha kwa sare ya 0-0 pia.
Michezo mingine ya leo ni pamoja na pambano la African Lyon dhidi ya Polisi Moro utakaochezwa  kwenye Uwanja wa Chamazi jijini, Ruvu Shooting itashuka kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi kuikabili Mgambo Shooting ya Tanga na  Prisons itaikaribisha Coastal Union ya Tanga kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya.
JKT Oljoro ya Arusha baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Toto Afrika katika mechi yake ya awali itakuwa Kaitaba, Kagera kuumana na wenyeji wao Kagera Sugar, huku Azam iliyochanua katika pambano la fungua dimba mbele ya Kagera itaalikwa na Toto Afrika katika uwanja wa CCM Kirumba.
Kocha wa Toto, John Tegete ameapa kupata ushindi leo ili kujiongezea hazina ya pointi katika ligi hiyo aliyokiri ni ngumu kwa namna timu zilizvyojiandaa.

MSHINDI UCHAGUZI MGODO WA BUBUBU, VISIWANI ZANZIBAR

 DEREVA wa treni ya mizingo ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) Ali Kilumanga (57), amefariki dunia huku askari 10 wa jeshi la Polisi nchini wakinusurika kifo kwenye ajali ya treni

Na AFISA HABARI WA TAZARA
DEREVA wa treni ya mizingo ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) Ali Kilumanga (57), amefariki dunia huku  askari 10 wa jeshi la Polisi nchini wakinusurika kifo  kwenye ajali ya treni  iliyotokea karibu na stesheni ya Makambako mkoani Iringa.
 Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Akashambatwa Mbikusita-Lewanika aliwaambia waandIshi wa habari  jijini Dar es Salaam jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 11:40 jioni na kuhusisha Treni No 0755 ya shirika hilo, iliyokuwa ikiokea Dar es salaam kwenda Kapilimposhi  Zambia.
Alitaja chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu iliyojitokeza kwenye mfumo wa breki na hivyo kushindwa kufunga breki na baadae kuacha njia na kisha kupunduka, ambapo  dereva wa akiba wa treni hiyo, Mashaka Bujilima alilipata majeraha na kupelekwa Hospitali ya Ilembula iliyopo wilayani Njombe na baadae kuruhusiwa baada ya kupata matibabu.
" Tumepokea kifo cha mpedwa wetu  Kalumanga kwa masikitiko na hazuni kubwa kwa kuwa amekuwa nasi kwa muda mrefu,lakinisasa kametutoka jina la bwana lihimidiwe,’’ alisema Akashambatwa.
Alisema Treni hiyo ilikuwa imebeba shehena ya mizigo mbalimbali ikiwa ni pamoja na injini za teni mbili, magari 16 ya mbolea, magari tisa ya mafuta ya treni na mengine ni magari ya vifaa mbalimbali,ambapo tathimini ya hasara ya mali, inaendelea  kufanyiwa uchunguzi.

"Timu ya wataalamu mbalimbali  na waandamizi, mara moja imenzisha uchunguzi kwa kina sababu ya ajali hii ya  kutisha , lakini ripoti ya awali imewasilishwa kwa serikali  mbili za Tanzania na Zambia," alisema Akashambatwa.

Aidha Akashambatwa, alisema kuwa kwa  huzuni kubwa wametuma  rambirambi zao kwa familia  ya marehemu na  kuwapa  pole kwa niaba ya familia nzima ya TAZARA.
Mwisho

PICHA INAONYESHA JINSI YA MABEHEWA YALIVYOSAMBARATIKA

MABOGI YA BEHWA

BAADHI YA MIZIGO ILIYOSAMBARATIKA

Jengo la shule ya sekondari ya kata ya kiwalani liko katika hali mbaya

Jengo la shule ya sekondari ya kata ya kiwalani liko katika hali mbaya jengo hilo ambalo lina muda wa miaka ipatayo minane toka lijengwe halijaingiwa wanafunzi picha inapnyesha jinsi lilivyo milango imeibiwa silbodi imebomoka kama picha inavyonyesha hivi sasa ndio geto wanafunzi wanaonekana ni wa shule za msingi zilizopo karibu na jengo hilo wakati wanafunzi wanafanya mitihani ya darasa la saba  jee watapelekwa wapi kaama hali ni hii wanafunzi wa darasa la saba shule zilizopo katika kata hiyo ya kiwalani awanafanya mtihani jee wale ambao watakao faulu watakwenda katika shule gani  wanafuzi wanaofaulu katika shule za msingi za kiwalani hupelekwa katika shule za sekondari sehemu za chanika ,mbondole pugu ,kibada shule wananchi wa eneo hilo wanaiomba serikali kufanya kila jitihada wamalize miaka minane toka ijengwe ni mingi.

Mawaziri watatu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wanatarajiwa kutumika kama mashahidi katika kesi ya kupinga matokeo

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar.
Mawaziri watatu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wanatarajiwa kutumika kama mashahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa Bububu, itakayofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chama hicho Issa Khamis Issa, katika Mahakama kuu ya Zanzibar.
Mawaziri hao watakaotoa ushahidi katika kesi hiyo, ni Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui na Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, ambao walikuwa waangalizi wa uchaguzi kupitia Chama cha Wananchi CUF.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar, Mkurugenzi wa habari, uenezi, haki za binadamu na mawasiliano na umma wa CUF, Salim Bimani alisema kwamba Mawaziri hao walishuhudia vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na sheria za uchaguzi.
Bimani alisema hivi sasa jopo la wanasheria wanaendelea kukusanya vielelezo muhimu, kabla ya kufungua kesi wiki hii katika mahakama Kuu ya Zanzibar, na kuiomba kutengua ushindi wa mgombea wa CCM, Hussein Ibrahim Makungu, kwa madai kuwa ushindi wake haukutokana na maamuzi ya wananchi wa jimbo la Bububu.
"Katika kesi tutakayofungua, tutawatumia Mawaziri watatu kama mashahidi, kwa vile wameshuhudia kwa macho yao, vitendo vya udanganyifu, kuruhusiwa watu wasiohusika kupiga kura, na askari wa vikosi vya SMZ kutumia nguvu na kuwatisha wananchi katika zoezi hilo la uchaguzi mdogo wa Bububu.
Aidha, Bimani aliongeza kuwa kuna watu wawili wamejeruhiwa akiwemo Abdallah Haji Mmanga, anayedaiwa kupigwa risasi katika sehemu ya paja la mguu wake wa kulia, na Shah Haji Shah ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa na vigae vya chupa, ambao walitibiwa katika hospitali ya Al Rahma.
"Safari hii tumeamua kupambana kuanzia Mahakama kuu, na kama haki haitotendeka, tutafika katika Mahakam ya Rufaa, hatuwezi kuachia misingi ya demokrasia na utawala bora ikiendelea kuvunjwa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa" alisema Bimani.
Alisema kwamba katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kuna viongozi bado wana dukuduku la maridhiano yaliyozaa Serikali hiyo, lakini kinyongo chao hakitofanikiwa kuzorotesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa au kuisambaratisha.
"Kuna viongozi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hawaungi mkono maridhiano, lakini Wazanzibari hatutaki kurejea katika malumbano ya kisiasa, hatua iliyofikiwa imeleta amani na utulivu katika nchi" alisema bimani
Hata hivyo, alisema kwamba uchaguzi wa Bububu hautopelekea Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuvunjika, kwa vile imekuja kutokana na maamuzi ya wananchi, ambao asilimia 66 waliunga mkono kuanzishwa kwa mfumo huo kupitia kura ya maoni iliypigwa 2010.
Alisema kwamba uchaguzi wa Bububu, Jeshi la Polisi lilishindwa kusimamia vyema majukumu yake na badala yake lilikasimu madaraka kwa vikosi vya SMZ ambavyo vilitumia vibaya majukumu yao na kushiriki katika vitendo vya kuwatisha wananchi kuweza kujitokeza na kupiga kura katika uchaguzi huo.
Bimani alisema CUF inalaani kitendo cha kupigwa kwa Mwandishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Munir Zakaria, kwa vile kimeingilia uhuru wake wa kikatiba wa kutekeleza majukumu yake ya kukusanya taarifa kwa ajili ya kuwahabarisha wananchi.
Alisema bahati mbaya tukio hilo limetokea siku chache tangu kuuwawa kwa Mwandishi wa Channel Ten mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, ambapo hakuna kiongozi dhamana wa Jeshi la polisi aliyewajibika kutokana na mauaji hayo ya kikatili.
Aidha aliongeza kuwa CUF imesikitishwa na kitendo cha kupewa masharti magumu ya dhamana kwa watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na vurugu za uchaguzi huo, ambapo kila mmoja alitakiwa kuweka dhamana ya shilingi laki tano kama fedha taslimu na dhamana ya maandishi 500,000 kwa kila mmoja kwa watuhumiwa 10 waliofikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Mwanakwerekwe.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa jimbo la Mtoni ambaye ni mmoja kati ya watu waliopigwa katika vurugu hizo, Faki Haji Makame, alisema kwamba alipigwa mtama na kuanguka chini, wakati akiokota kiatu baada ya kumvuka alipokuwa akiwakimbia vijana waliomvamia na kumjeruhi.
"Mimi sijapigana hadharani, nimevamiwa na vijana wawili baadae akatokea mwengine, mnamhoji wa nini, wakati tumeagizwa apigwe, ndipo nilipoamua kukimbia na wakaanza kunifukuza na kunipiga" alisema Mbunge huyo wa jimbo la Mtoni.
Akielezea mukhtasari wa tukio lake, alisema kabla ya kushambuliwa wakati akitokea eneo la Kijichi, kukagua ujenzi wa nyumba yake, alipofika karibu na tawi la CCM eneo la Bububu, alimuona Naibu Katibu Mkuu wa CCm Zanzibar, Vuai Ali Vuai na kuamua kwenda kumsalimia, lakini alikataa kupokea salamu yake na kumshutumu kuwa CUF inazuia wafuasi wa CCM kwenda kupiga kura katika vituo.
"Alitahadharisha kuwa CCM haitokubali watu wake kunyimwa haki ya kupiga kura, na baada ya maneno yake, mimi nilianza safari ya kwenda kuwasalimia wakwe zangu katika eneo la Bububu, ndipo nilipokutwa na maswahiba ya kupigwa na kujeruhiwa kwa mwili wangu, kwa kunipiga kwa mipira ya mabomba ya maji na mateke na ngumi" alisema Mbunge huyo.
Alisema anakanusha taarifa ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa kuwa alikamatwa kwa madai ya kupigana hadharani, wakati Polisi ndio waliomuokoa alipokuwa akipigwa na kupelekwa katika kituo cha Bububu pamoja na watu waliokuwa wakimpiga.
Hata hivyo alisema jambo la kushangaza Polisi mpaka jana wameshindwa kumpa majina ya watu waliompiga, licha ya kuwa wamehojiwa, na vile vile wameshindwa kuwafikisha Mahakamani kutokana na makosa ya kumpiga na kumshambulia mwilini.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa CUF, Issa Khamis Issa, alisema kwamba ameshindwa kufungua kesi yake jana kama ilivyopangwa awali, kwa vile wanasheria wake wanaendelea kukamilisha vielelezo vitalkavyotumika kama ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo.
Alisema sheria ya tume ya uchaguzi inaeleza kuwa ndani ya siku 14, mgombea yeyote ana haki ya kupinga matokeo mahakamani endapo atakuwa hajaridhika na anatarajia kufungua kesi hiyo mapema wiki hii.
Wakati huo huo Mwandishi wa Channel Ten, Munir Zakaria ambaye alipigwa katika vurugu hizo za uchaguzi, ameendelea kupata matibabu, na afya yake inaendelea vizuri, baada ya kupigwa ngumi sehemu ya mdomoni na mabegani, lakini pochi iliyopotea ikiwa na vitu muhimu bado haijapatikana.
Alisema kwamba, tayari amekamilisha taratibu za matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja, na anaamini watu waliomfanyia shambulia hilo watachukuliwa hatua za kisheria kwa vile tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha Polisi cha Mwembe Madema mjini Zanzibar.
uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu ulifanyika Septemba 16 mwaka huu, ambapo ulitawaliwa na vurugu, uharibifu wa mali za umma, na matumizi mabaya ya silaha, hatua ambayo wadadisi wa mambo wameitafsri kuwa ni mwanzo mbaya wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.