STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 21, 2013

Amissi Tambwe aizamisha Yanga Taifa

Kitu Simba wakiandika bao lao la kwanza dhidi ya Yanga
Sisi ndiyo Majembe ya Ukweli tusio na longolongo nyingi

MABAO mawili ya Mrundi Amissi Tambwe na jingine la Awadh Juma yametosha kuwanyamazisha Yanga licha ya Emmanuel Okwi kufunga bao la kufutia machozi wakati Simba ikipata ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe uliomaliza hivi punde uwanja wa Taifa.
Tambwe, anayeongoza kwa magoli katika Ligi Kuu Tanzania Bara alifunga bao la kwanza dakika ya 14 kabla ya kuongeza la pili kwa mkwaju wa penati dakika 43 baada ya David Luhende kumuangusha mshambuliaji aliyeichachafya Yanga kwa siku ya leo, Ramadhani Sindano 'Messi' na kuifanya Yanga kwenda mapumziki wakiwa nyumba kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilichokuwa na mshikemshike kilishuhudia timu zote zikipata bao moja moja , Simba wakitangulia dakika ya 62 kupitia kiungo aliyetua Simba akitokea Mtibwa Sugar,Awadh Juma  kabla ya Okwi kufunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Simon Msuva dakika ya 87.
Katika mechi hiyo iliyokuwa kali ilishuhudiwa beki kisiki, Kelvin Yondani akitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyesha kadi mbili za njano baada ya kumuangusha Ramadhani Singano 'Messi'.
Langoni mwa Yanga lidaka kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja ambaye kipigo hicho huenda kikamuweka katika wakati mgumu, licha ya kwamba soka ndivyo lilivyo, lakini mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiamini wangeshinda gemu hiyo wanaoenekana hawaamini kama wamefungwa na mtani wao licha ya klabu yao kuzoa poiinti nyingi za promosheni ya Nani Mtani Jembe na kuondoka na Sh. Milioni 98 wakati Simba ikitwaa ubingwa na Sh., Mi. 1.6 tu.

Liverpool yaiengua Arsenal kileleni, Suarez aendelea kuua EPL

Liverpool striker Luis Suarez (right) volleys in against Cardiff at Anfield
Suarez akitupia kambani moja ya mabo yake muda mfupi uliopita wakiizamisha Cardiff City

VIJOGOO vya Anfield, Liverpool imekalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu ya England baada ya kuinyuka Cardiff City kwa mabao 3-1 na kuiengua Arsenal ambayo yenyewe itashuka dimbani Jumatatu kuumana na Chelsea.
Mabao mawili ya Luis Suarez katika dakika ya 25 na 45 kwa pasi za Henderson na goli jingine ya Raheem Sterling zilitosha kuwapeleka Liver kileleni kwa kufikisha pointi 36, moja zaidi ya ilizonazo Arsenal.
Bao la kuftia machozi la wageni lilifungwa na Jordon Mutch katia dakika ya58 kipindi cha pili ambalo halikufanya Liverpool kutetereka.
Mabao mawili aliyofungwa Suarez ambaye mechi ya pili sasa anacheza kama nahodha baada ya Steven Gerrard na msaidizi wake kuwa majeruhi yamemfanya afikishe jumla ya mabao 19 katika orodha ya wafungaji wa ligi hiyo akiendelea kuongoza kileleni.
Jioni hii kuna mechi kadhaa zinachezwa ikiwamo ile ya Manchester City kuumana na Fulham ugenini na Machester United kuwakaribisha West Ham United.

AJALI TENA! Watu 7 wafa ajali ya gari la AllysROHO za watanzania wenzetu zimeendelea kuteketea kwenye ajali za barabarani mwishoni mwa mwaka baada ya watu 7 kufariki papo hapo na wengine kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Ally's na Hiace iliyokea jijini Mwanza.
Inadaiwa kuwa, basi hilo la Ally's linalofanya safari zake kati ya DSM na Mwanza liligongana  uso kwa uso na Hiace hiyo inayofanya mizunguko ya kubeba abiria (daladala) katika eneo la Buhongwa jijini Mwanza.

Usajili wa dirisha dogo huu hapa, Ashanti Utd nouma

Ashanti United inayoongoza kwa kuomba usajili wa wachezaji 15 katika dirisha dogo
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa Pingamizi la wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo mwisho wake utakuwa Desemba 23 mwaka huu.
Usajili huo uliohusisha klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ulifanyika kati ya Novemba 15 mpaka Desemba 15 mwaka huu.

Katika VPL, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Coastal Union ndiyo timu pekee kati ya 14 za ligi hiyo ambazo hazikuwasilisha maombi ya usajili katika dirisha dogo.

Ashanti United ndiyo inayoongoza kwa wachezaji 15 ambao ni Kassim Kilungo, Mohamed Banka, Bright Obinna, Victor Costa, Juma Mpongo, Juma Jabu, Ally Kondo, Shafii Rajab, Mohamed Faki, Abubakar Mtiro, Patrick Mhagama, Ally Kabunda, Hassan Kabuda, Idd Ally na Rahim Abdallah.

Ruvu Shooting; Ally Khan na Jumanne Khamis, Rhino Rangers; David Siame, John Kauzeni, Salum Mamlo, Jingo Seleman, Darlington Enyinna, Rajab Twaha, Godfrey Mobi na Mussa Digubike. Mbeya City; Saad Kipanga. Tanzania Prisons; Dennis Liwanda, Godfrey Pastory, Henry Mwalugala, Jamal Salum na Brayton Mponzi.

Oljoro JKT; Jacob Masawe, Mansour Ali, Juma Mohamed, Amour Mohamed, Mohamed Ali, Mussa Nahoda, Benedict Ngasa, Seleman Makame, Shija Mkina, Ali Omar na Shaweji Yusuf. Simba; Uhuru Selemani, Ivo Mapunda, Ali Badru, Awadh Juma, Donald Mosoti na Yaw Berko. Azam; Mouhamed Kone.

Yanga; Hassan Dilunga, Juma Kaseja na Emmanuel Okwi. Mgambo Shooting; Suleiman Khatib, Bolly Ajali, Amri Sambinga na Issa Ali. JKT Ruvu; Chacha Marwa, Sino Augustino, Idd Mbaga na Cecil Luambano.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jamal Malinzi.

Kikao hicho kitakachofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitapitia ajenda mbalimbali ikiwemo uundwaji wa vyombo vya haki (Kamati ya Nidhamu, Kamati ya Maadili na Kamati ya Uchaguzi).

Tiketi za Electroniki kwa Azam na Ruvu Shooting

Azam
Ruvu Shooting
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa mechi mbili za majaribio ya matumizi ya tiketi za elektroniki zitakazochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi ya kwanza itakuwa Desemba 26 mwaka huu saa 10 jioni ambapo itazikutanisha timu za Azam na Ruvu Shooting. Mechi nyingine itachezwa Januari Mosi mwakani kwa kuzikutanisha Ashanti United na JKT Ruvu.
TFF tunatoa mwito kwa washabiki kujitokeza katika mechi hizo ambapo mbali ya kushuhudia burudani pia watajionea jinsi mfumo huo wa tiketi za elektroniki unavyofanya kazi.
Kwa kushirikiana na benki ya CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo ya tiketi za elektroniki, TFF imepanga vilevile kuandaa mechi nyingine majaribio mikoani kabla ya mfumo huanza kutumika rasmi Januari  25 mwakani katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

SIMBA, YANGA NANI MTANI JEMBE TAIFA LEO?

Yanga


Simba

KUANZIA Mitaani, vijiweni mpaka maofisini na kwenye daladala gumzo na tambo ni pambano litakalochezwa jioni ya leo kati ya Simba na Yanga.
Nguo na bendera zenye rangi zinazovaliwa na klabu za timu hizo ndizo zilizotapakaa mitaani huku kila mtu akisema leo ndiyo leo, akitambia timu yake.
Hata hivyo ukweli na jibu kamili la nani mbabe au Nani Mtani Jembe kama pambano hilo la kirafiki maalum lilivypewa jina litafahamika baada ya dakika 90.
Klabu hizo mbili wapinzani wa jadi wa soka nchini zitashuka dimba la uwanja wa Taifa kuumana ikiwa ni miezi miwili tu tangu zilipotoshana nguvu kwa kutoka sare ya mabao 3-3 kwenye uwanja huo huo.
Tofauti na mechi ya leo, katika mechi yao iliyochezwa Oktoba 20, Simba na Yanga zilizokuwa zikipimana ubavu kwenye pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga walitangulia kupata mabao matatu yaliyofungw ana Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza 'Diego' kabla ya Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kazze kurejesha mabao hayo kipindi cha pili.
Hivyo mashabiki na wanachama wa timu hizo kila mmoja pamoja na kutamba mtaani, lakini presha zao zitakuwa juu kabla na baada ya dakika 90 za pambano hilo kutokana na aina na vikosi vyao.
Yanga ikiwa na kocha yule yule, Ernie Brandts itaikabili Simba ikiwa na silaha mpya tatu, kipa Juma Kaseja, kiungo Hassan Dilunga na mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyekuwa gumzo kwa wiki nzima juu nchini.
Ujio wa Okwi umekuwa gumzo na kufunika kila kitu katika soka la Tanzania kutokana na ukweli ni kati ya wachezaji waliokuwa wakiinyima Raha wakati akiichezea Simba.
Ndiye aliyekuwa mwiba mkali wakati Yanga ikilowa mabao 5-0 toka kwa Mnyama akifunga mawili na kusaidia mengine yaliyowafanya Jangwani wawe na deni jingine kubwa toka kwa watani zao.
Deni hilo ni mbali na lile waliloshindwa kulilipa kwa zaidi ya miaka 30 waliponyolewa 6-0 mwaka 1977.
Hata hivyo Simba ikiwa imebadilisha benchi la ufundi kwa aliyekuwa kocha mkuu, Kibadeni Abdallah King na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelu 'Julio' kutimuliwa Msimbazi na nafasi zao kuchukuliwa na Mcroatia.
Mbali na kocha huyo, pia Simba ina wachezaji kadhaa wapya akiwamo makipa Ivo Mapunda na Yew Berko waliowahi kuichezea Yanga, beki toka Kenya, Donaldo Musoti na viungo, Badru Ally na Awadh Juma na huku Uhuru Suleimana akirejea kikosini toka Coastal Union.
Tusubiri tuone nani atakayemtambia mwenzake baada ya dakika hizo 90 au mikwaju ya penati kama watashindwa kuonyeshana ubabe, lakini TFF kupitia Kaimu Katibu Mkuu na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema maandalizi ya mechi hiyo ya aina yake yamekamilika.
Wambura alisema vikosi vya ulinzi na usalama katika mechi ya leo vimekamilika kila idara na kwamba Barabara ya Taifa inayoanzia Keko-Maghorofani hadi Barabara ya Mandela, itafungwa kuanzia saa 12 asubuhi kupisha hekaheka za mtifuano huo.
Alisema magari hayataruhusiwa kuegeshwa kuanzia eneo la Baa ya Minazini hadi msikiti unaotazamana na Uwanja wa Uhuru, hivyo magari yote yataegeshwa nje ya Uwanja wa Ndani wa Taifa – kando ya Barabara ya Mandela.
“Magari yatakayoruhusiwa kuingia maeneo hayo na hata ndani ya Uwanja wa Taifa ni yatakayokuwa na stika zilizotolewa na TFF. Tunawaomba wadau na mashabiki wa soka kuheshimu na kutii maagizo ya vikosi vya ulinzi,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa milango ya kuingilia uwanjani itakuwa wazi kuanzia saa sita mchana ambapo baada ya mauzo ya tiketi ya jana, zoezi hilo litaendelea leo nje ya uwanja huo kabla ya mechi ili kuwapa mashabiki fursa ya kukata na kuingia moja kwa moja.
Viingilio vya leo  cha chini ni sh 5,000 kwa viti vya kijani, huku upande wa viti vya rangi ya bluu, kiingilio ni sh 7,000; viti vya rangi ya chungwa sh 10,000; VIP C ni sh 15,000; VIP B sh 20,000 huku VIP A sh 40,000.
Kwa upande wa waamuzi, kati atasimama Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles wa Dodoma huku Israel Nkongo wa Dar es Salaam akiwa mezani. Kazi ya kutathimini utendaji wa waamuzi wote itakuwa chini ya Soud Abdi wa Arusha.

MECHI TANGU 2010
Rekodi ya watani hawa inaonyesha kuwa mechi ya leo ni ya tisa tangu 2010 na katika mechi nane, Yanga imeshinda tatu, Simba mbili na wamekwenda sare tatu.
Aprili 18, 2010: Simba 4, Yanga 3
Oktoba 16, 2010: Yanga 1, Simba 0
Machi 5, 2011: Yanga 1, Simba 1
Oktoba 29, 2011: Yanga 1, Simba 0
Mei 6, 2012:  Simba 5, Yanga 0
Oktoba 3, 2012: Yanga 1, Simba 1
Mei 18, 2013: Yanga 2, Simba 0
Oktoba 20, 2013: Simba 3, Yanga 3

Kila la heri Tanzanite kwa Madiba

WAKATI macho na masikio ya mashabiki wa soka leo wanaelekezwa kwenye pambano la soka la Simba na Yanga, wawakilishi wa Tanzania katika kuwania tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake U20 Tanzanite wapo Afrika Kusini kujaribu kuutafuna mfupa uliowashinda wiki mbili zilizopita.
Tanzanite watawakabilia wenyeji wao, katika pambano la marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kuchezea kichapo cha mabao 4-1 nyumbani.
Kocha wa timu hiyo Rogatian Kaijage amewapa matumaini Watanzania kwamba watapigana kiume dhidi ya wenyeji wao, ingawa hatarajii miujiza yoyote katika pambano hilo.
Tanzanite iliyowang'oa Msumbiji kwa kipigo cha mabao 15-1 katika mechi zilizopita kama itafanikiwa kuitoa Afrika kusini itaumana na mshindi kati ya Nigeria au Tunisia katika hatua ya mwisho ya kuwania nafasi mbili za kwenda Canada kwenye fainali za dunia mwakani.
Kila la heri kwa wawakilishi wetu hao, hatya kama akili zetu zitakuwa kwenye pambano ma Nani Mtani Jembe linalochezwa jioni hii uwanja wa Taifa, kati ya Simba na Yanga.