STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 12, 2016

Hakuna ujanja FDL yafikia mwisho nani kupanda Daraja?

Lyon na Ashanti katika mechi yao
PATAMU! Ligi Daraja la Kwanza Bara (FDL), imefikia patamu kwani wikiendi hii, lazima kieleweke wakati mechi za kufungia msimu zitakapopigwa.
Licha ya kufungia msimu, lakini mechi hizo zitakazochezwa katika muda mmoja bila kujali tofauti mazingira ya hali ya hewa, pia zitatoa timu mbili za mwisho za kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2016-2017.
Kwa mujibu wa agizo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mechi zote zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni, huku makundi ya A na C yakimulikwa kwani ndio yanayoshikilia hatma ya timu mbili za mwisho za kuungana na Ruvu Shooting kucheza Ligi Kuu ijayo.
Kundi C keshoJumamosi itashuhudia michezo minne, ila miwili ndiyo mikali ikizihusisha JKT Kanembwa dhidi ya Geita Gold mjini Kigoma na ule wa Polisi Tabora itakayoialika Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Geita na Polisi zote zina nafasi sawa ya kupanda daraja zikiwa na pointi 27 kileleni, huku zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, japo pia viwanja vingine zitapigwamechi za Mbao dhidi ya Polisi Mara na Panone itakayomalizana na Rhino Rangers .
Katika kundi A African Lyon, Friends Rangers na Ashanti Utd zote zina nafasi ya kufuzu VPL na zote zitashuka uwanjani keshokutwa Jumapili.
Friends itaivaa Kiluvya United pale Chamazi, jijini Dar, Ashanti na Lyon zitamalizana Karume, Dar es Salaam, huku Polisi Dar na Polisi Dodoma zitacheza Uwanja wa Mabatini, Mlandizi na CDA itamalizana na KMC.
Lyon ina pointi 26 ikihitaji sare kurudi Ligi Kuu, wakati Friends na Ashanti kila moja ina pointi 23 zikihitaji kushinda na kuiombea Lyon iteleze ili mojawapo ipande daraja.
Mechi za kukamilishia ratiba ya kundi B zipo hivi; Kimondo itacheza na Kurugenzi, Njombe Mji dhidi ya Lipuli, Ruvu itaikaribisha Polisi Moro na Burkina Faso itavaana na JKT Mlale mjini Morogoro.
Timu mbili za kushuka daraja kuungana na Kanembwa zinatarajiwa kufahamika katika mechi hizo za kesho na keshokutwa.

Msimamo Kundi A
                                   P   W  D  L    F   A  Pts
Africans Lyon                13  8   2  2   17  9  26
Friends Rangers            13  6   5  2   21  10  23
Ashanti Utd                   13  6   5  2   18  11  23
KMC FC                         13  6   4  3   12  10 22
Kiluvya United               13  5   5  3   12   8   20 
Polisi Dar                       13  3   5  5    9  13  14
Polisi Dom                     13  2   1  10  10 23  7
CDA                              13  1   3   9   6   21  6

Msimamo Kundi B
                               P  W  D  L  F  A  Pts
Ruvu Shooting          13  10  2  1  26 7  32
Njombe Mji               13   7   1   5  14  12 22
JKT Mlale                  13   5   6  2  17 10 21
Kurugenzi                 13   6   3  4  16 13 21
Polisi Moro                13  5   2  6   12 17  17
Lipuli Fc                    13   3  5   5   12  15 14
Kimondo                   13   2   3  8   8  22 9
Burkina Faso             13   1   4   8  10 18 7

Msimamo Kundi C
                              P W  D  L  F   A  Pts
Polisi Tabora            13  8  3  2  20  5   27
Geita Gold               13  8  3  2  20  6   27
Oljoro JKT               13  6  4  3  12  14  22
Mbao FC                  13  5  4  4  14  18  19
Panone                    13   4  4  5  16 13  16
Polisi Mara               13   2  7  4  11  15  13
Rhino Rangers          13   2  6  5  8   13  12
JKT Kanembwa         13  0  3  10  7  24  3

Ratiba kamili ya wikiendi hii:
Kesho Jumamosi:
Kimondo FC      vs     Kurugenzi FC    
Njombe Mji       vs     Lipuli FC                      
Ruvu Shooting   vs     Polisi Morogoro    
Burkinafaso FC  vs     JKT Mlale    
Mbao FC            vs     Polisi Mara    
Polisi Tabora       vs     JKT Oljoro    
JKT Kanembwa   vs     Geita Gold FC    
Rhino Rangers    vs     Panone FC    

Jumapili:
Polisi Dar            vs     Polisi Dodoma    
Mji Mkuu             vs     KMC FC                      
African Lyon        vs     Ashanti United    
Friends Rangers   vs     Kiluvya United   
 

BASATA YAUPIGA STOP 'SHIKA ADABU YAKO'YAMETIMIA. Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) hatimaye limeufungia rasmi wimbo mpya wa nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nay wa Mitego uitwao 'Shika Adabu Yako'.
Basata ilitangaza hatua hiyo leo Ijumaa kupitia taarifa yake iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wake, Godfrey Mngareza, ikiwa saa chache tangu kuzagaa kwa taarifa hizo baada ya wimbo huo kuwa gumzo kupitia mitandao ya kijamii.
Katika wimbo huo ulioachiwa mapema wiki hii, rapa huyo aliichana Basata katika moja ya mistari yake na taarifa hiyo ya Basata imesema imeufungia wimbo huo kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo. Ikitumia kifungu cha 4 (1) (i) ya sheria  namba 23 ya mwaka 1984 na kifungu cha 4 (2) baraza hilo limetangaza kuupiga marufuku wimbo huo na kumpa onyo kali msanii huyo.
"Tunafahamu kuna wsanii wamekuwa wakifanya hivyo makusudi kutafuta umaarufu uchwara ambao wanadhani utakuja kutokana na kuzungumzwa sana. Tunapenda kusema wazi kuwa umaarufu hauji kwa upuuzi wa namna hiyo..."
Sehemu ya taarifa hiyo ya Basata ilisomeka hivyo, ikifafanua pia imechukua hatua hiyo dhidi ya wimbo huo kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili, kashfa, uchochezi, kudhalilisha watu na kuhatarisha amani na utengani miongoni wa wasanii na jamii.
na kuzima tetesi zilizotapakaa tangu juzi kuwa wimbo huo uliorekodiwa na Mr T Touch umefungiwa kutokana na kuwa na mistari inayowananga wasanii mbalimbali akiwamo Wema, Ray, Ommy Dimpoz, Shetta, DJ Choka na hata Basata lenyewe.
"Ujumbe huu uwafikie Basata.....kazi kufungia nyimbo za wasanii, hivi mnajua tabu tunazopata, mmeshindwa kazi kama mngekuwa watoto tungeshawachapa..." 
Ni moja ya mstari uliopo kwenye wimbo huo ambao umelalamikiwa na wasanii waliombwa na kuwagawa mashabiki wengine wakiuponda na kuufagilia.
Basata imesisitiza pia kwa kumuonya msanii huyo kuwa makini katika kazi zake vinginevyo atachukuliwa hatua zaidi. Wa Mitego hakupatikana kusema lolote, lakini juzi alikakariwa kuwa hata kama wimbo utafungiwa basi wakubwa watakuwa wamechelewa kwa sababu kama ujumbe umeshafika kwa jamii na akitetea alichokiimba ni ukweli mtupu.

Hatimaye Yanga wapaa usiku huu kwenda Mauritius

Picha haihusiani na habari hii. Wachezaji wa Yanga wakiwa katika moja ya safari zao
KIKOSI cha Yanga kilichokwama kuondoka alfajiri ya leo kwenda Mauritius hatimaye kimepaa muda huu kuelekea nchini humo kwa ajili ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim utakaochezwa kesho jioni.
Yanga ilikwama kuondoka na ndege ya ATCL kutokana na kuharibika kwa kifaa kilicholazimika kwenda kununuliwa Afrika Kusini na kufungwa, huku marubani wa ndege hiyo wakitishwa na hali ya hewa ya huko waendako.
Mpaka saa 12 jioni kulikuwa bado kuna hatihati ya safari hiyo baada ya rubani wa ndege kutaka kupimwa kwa watu wote wa msafara ili kuona kama uzito wao utaendana na safari yao wakiwa angani.
Hata hivyo mwishowe saa 1 msafara huo ulipaa kuelekea huko, licha ya kwamba Yanga kuonekana ilishavunja Kanuni ya 8 ya michuano ya CAf juu ya timu wageni kutakiwa kuwa nchi wanayoenda kucheza ndani ya saa 48. Kitu kizuri ni kwamba Mkuu wa msafara wa Yanga, Ayoub Nyenzi aliwasiliana mapema na CAF na wenyeji wao pamoja na kamisaa kuwajulisha juu ya tatizo lao.
Kwa taarifa hiyo, kikao cha mchezo huo (pre-match meeting) ambacho hufanywa siku moja kabla ya mchezo husika kimesogezwa mbele hadi kesho asubuhi na jioni mchezo utapigwa kama kawa, licha ya kwamba Yanga itaingia Mauritius usiku wa manane.
Mwendo wa kutoka jijini Dar es Salaam mpaka Curepipe mji utakaochezwa mchezo huo kwenye Uwanja wa George V ni kama saa nane, hivyo ni wazi Yanga huenda ikafika kati ya saa 9 alfajiri na jioni watashuka dimbani bila hata ya kupasha.
Kosa hilo la kuchelewa kwa Yanga ambayo awali ilikuwa ipae tangu Jumatano kabla ya kubadilishwa kwa ratiba yao, inaweza kuwa faida kwa wenyeji ambao kwa msimu wa pili sasa ndio mabingwa wa taifa hilo la kisiwani katika Bahati ya Hindi.

TASWA YALAANI UHUNI WA KAZIMOTO KUMPIGA MWANDISHI


Kazimoto anayetuhumiwa kumpiga mwanahabari, Mwanahiba Richard mjini Shinyanga

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) kimelaani vikali kitendo cha kiungo wa Simba, mwinyi Kazimoto kumpiga mwandishi wa gazeti la Mwanaspoti, Mwanahiba Richard akitekeleza majukumu yake mjini Shinyanga. taarifa rasmi ya Taswa inasomeka hivi:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama Cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), kimestushwa na kitendo cha mchezaji wa Simba kudaiwa kumpiga mwandishi  kwa masikitiko makubwa kitendo cha wa  habari za michezo la gazeti la Mwananchi, Mwanahiba Richard.
Tumeongea na Mwandishi mwenyewe kujua ukweli, tumemtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange naye kutaka kufahamu hali ya upelelezi ilipofikia lakini kufanyika haraka kwa uchunguzi ili  haki ya kila mtu ipatikane.
Lakini tumeweza kuzungumza na upande wa pili, kwa viongozi wa Simba kujua kama nao wao wamebaini kosa la mchezaji huyo.Mwenyekiti wa Simba,Evans Aveva ameahidi kutoa ushirikiano na kuomba tusubiri uchunguzi wa Polisi ndipo upatikane ukweli wa jambo ili.
Sisi kama TASWA tunalaani tukio ili na tumekuwa tukikemea sana vitendo hivi kwa kupiga waandishi, lakini kumekuwa hakuna jitihada zozotew ambazo polisi inalichukua kwa wahusika na badala yake madai kama haya yanapotea.
Kwa kuwa jeshi la polisi limeahidi kutoa ufafanuzi wa upelelezi wa tukio ili haraka iwezekanavyo, naomba waandishi wenzangu pamoja na muathirika wa tukio ili, tuvute subira ili haki ichukue mkondo wake ili sheria ifanye kazi yake.
Taswa itaendelea kulinda heshma ya mwandishi wa habari za michezo na isingepeda kuona mwandishi anaonewa na kudhalilishwa wakati akifanya majukumu yake.
Kwa upande wetu napenda kutoa shukrani kwa nahodha wa Simba, Mussa Hassan Mgosi na kocha wa timu hiyo Jackson Mayanja kwa ushirikiano walioonesha katika tukio hilo na wamedhihilisha uwezo wa kuwaongoza wenzao.
TASWA itakuwa inafuatilia suala ili kwa karibu zaidi.Tupo katika kuhakikisha waandishi anafuata taratibu, sheria za taaluma ya habari.Jambo ambalo Mwanahiba amelifanya kwa kumlinda source wake hadi kupata kipigo .
Juma Pinto
Mwenyekiti TASWA
12.02.2016

Maskini Yondani, TFF yamfungia mechi tatu alimwa faini kwa ubabe

KELVIN Yondani ndio basi tena, kwani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya Kusimamia na Kuendesha ligi iliyokutana kwa saa 72 jana Jumatano kupitia taarifa na ripoti mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu (VPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendeea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini imemkuta na hatia.
Taarifa rasmi ya TFF inasomeka hivi:
Ligi Kuu ya Vodacom
Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumpiga usoni kwa box la dawa Dk. Mganga Kitambi wa Coastal Union wakati akitoa huduma kwa kipa wake katika mechi namba 121 kati ya timu hizo iliyofanyika Januari 30, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Yondani alitenda kosa hilo baada ya kumuomba maji Daktari huyo, lakini akamnyima. Adhabu huyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 ambapo baada ya kutumia adhabu ya mechi hizo, hataruhusiwa kucheza hadi atakapokuwa amelipa faini hiyo.
Naye Dk. Kitambi anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kitendo chake cha kumrudishia Yondani kwa kumpiga ngumi. Kitendo cha Daktari huyo ni kinyume cha Kanuni ya 41(2), na pia Kanuni ya 36 kuhusu mchezo wa kiungwana.
Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa Coastal Union walipokuwa wakishangilia bao la pili.
Nayo klabu ya Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa washabiki wake kuvamia uwanja baada ya filimbi ya mwisho, kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni ya 14(11) inayohusu taratibu za mchezo.
Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia chumba cha waandishi wa habari badala ya kile cha timu wakati wa mechi kati yao na Simba iliyochezwa Februari 3, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Kocha Ally Jangalu wa Coastal Union ameripotiwa kutoa matamashi ya kuidhalilisha TFF kwenye vyombo vya habari kuwa Refa wa mechi kati yao na Ndanda SC iliyochezwa mjini Tanga alikwenda na maelekezo ya kuhakikisha wapinzani wao wanashinda. Coastal Union ilifungwa bao 1-0 katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 4, 2016. Suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.
Mchezaji Daud Jumanne amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumkanyaga vidole kwa makusudi mchezaji wa Simba aliyekuwa akisubiri kupatiwa matibabu kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Februari 7, 2016 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015. Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 37(20), hauruhusiwi kucheza mechi inayofuata ya timu yake mpaka faini hiyo iwe imelipwa. Iwapo atacheza kabla ya kulipa faini hiyo, timu yake itapoteza mchezo husika.
Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya African Sports iliyochezwa Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) kuhusu taratibu za mchezo.
Kamishna wa mechi hiyo namba 140, Idelfonce Magali amepewa karipio kwa kutoripoti vizuri tukio hilo, wakati Refa Elly Sasii amepewa karipio kali kwa kutoripoti kabisa tukio hilo.
Ligi ya StarTimes
Wachezaji Ismail Nkulo, Said Juma, Idd Seleman na Edward Amos wa Polisi Dodoma wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kumzonga, kumtolea lugha ya matusi ya nguoni na kutaka kumpiga Refa katika mechi ya Ligi ya StarTimes kati ya timu yao na African Lyon iliyofanyika Januari 30, 2016.
Kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ni kinyume cha Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa wachezaji.
Kiongozi wa Friends Rangers, Heri Mzozo anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kutoa lugha chafu kwa viongozi na waamuzi muda wote wa mchezo dhidi ya Ashanti United uliofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Vitendo vyake ni kiyume na Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa viongozi.
Mwamuzi Msaidizi namba 2 kwenye mechi kati ya Kimondo na Ruvu Shooting, Idd Mikongoti wa Dar es Salaam ameripotiwa na Kamishna kuondoka na timu ya Ruvu Shooting kwa kupanda basi lao mara baada ya mchezo, kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya uamuzi. Suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Waamuzi kwa ajili ya hatua stahiki dhidi yake.
Klabu ya Geita Gold imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) na onyo kali kwa kukataa kuingia kwenye chumba cha wachezaj, na badala yake kutumia chumba kingine ambacho pia walijisadia haja ndogo wakati wa mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo cha mshabiki wake kupita pembezoni ya uwanja (running track) kwa kasi wakati mechi hiyo dhidi ya Geita Gold ikiendelea.
Pia klabu ya Polisi Tabora imepewa onyo kali kutokana kipa wa timu yake kuvaa jezi ambayo haikuwa na nembo (logo) ya Mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza wakati wa mechi hiyo.
Geita Gold imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya JKT Oljoro kugomea mchezo kati ya timu hizo uliofanyika Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Nyankumbu Girls mkoani Geita. Timu hiyo iligomea mechi hiyo dakika 70 baada ya kufungwa bao la pili. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 29(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia JKT Oljoro imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na kitendo hicho kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4), wakati wachezaji wake Kapteni Shaibu Nayopa na Sunday Paul waliomvamia na kumpiga Refa wanapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki.
Naye Kocha Msaidizi wa JKT Oljoro, Bunu Abdallah  ambaye alitolewa kwenye benchi la timu yake kwa kosa la kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba 1 anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua stahiki.