STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 18, 2015

Wenyeji AFCON waanza na sare, Gabon yaua 2-0

Nahodha wa Guinea ya Ikweta, Emilio Nsue akiifungia timu yake bao katika mechi dhidi ya Kongo
Pierre-Emerick  Aubameyang akishangilia bao la kuongoza na Gabon wakati akiiongoza timu yake kushinda mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso (Picha:SuperSport)
Mashabiki wa soka nchini Guinea ya Ikweta wakimimika uwanjani kushuhudia ufunguzi wa michuano hiyo mjini Bata
BATA, Guinea ya Ikweta
FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zimeanza kwa kishindo kwa kushuhudiwa wenyeji, Guinea ya Ikweta ikilazimishwa sare ya 1-1 huku Gabon wakiifumua wanafainali zilizopita, Burkina Faso kwa mabao 2-0 katika mechi za ufunguzi zilizochezwa mjini Bata.
Wenyeji wakiwaanikizwa na washangiliaji wao, walitangulia kupata bao katika mechi ya mapema kupitia kwa Nsue aliyefunga katika dakika ya 16 kabla ya Kongo kuchomoa zikiwa zimesalia dakika tatu kupitia kwa Thievy Bifouma na kuwanusuru wakali kuambulia pointi moja katika kundi lao la A.
Katika mechi iliyofuata, Gabon ikiongoza na mshambuliaji nyota anayeichezea Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang wakipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Aubameyang alianza kwa kufunga bao la kuomngoza katika dakika ya 19 kabla ya Malick Evouna kuongeza bao la pili lililowakatisha tamaa 'Farasi Weupe' wa Burkinabe baada ya kufunga bao katika dakika ya 72.
Katika mfululizo wa michuano hiyo leo timu za Kundi B zitashika dimba la Ebebiyin kwa  mabingwa mara tatu wa fainali hizo, Tunisia watavaana na Cape Verde huku  Zambia wakitarajiwa kuumana na DR Congo.
Zambia na DR Congo ndiyo watakaoanza kuumizana saa 1 usiku kabla ya Tunisia na Cape Verde kukutana katika mechi ya kisasi baada ya timu hizo kufanyiana mtimanyongo kwenye mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia kwa Tunisia kuichongea Cape Verde waliokuwa wamefuzu hatua ya mwisho kwa madai ya kumtumia mchezaji asiyestahili na Cape Verde kuzikosa fainali hizo, ingawa Tunisia walikwama licha ya kupeta katika rufaa yao baada ya kung'oka kwa Algeria walioenda kufanya maajabu kwa kufika raundi ya 16 Bora.
Jumla ya timu za mataifa 16 zinachuana kwenye fainali hizo ambazo zinachezwa Guinea ya Ikweta baada ya Morocco kugoma kuiandaa kwa madai ya kuhofia maambukizo ya Ugonjwa wa Ebola.
Kitu cha kustaajabisha ni kwamba waliokuwa mabingwa watetezi NIgeria wameshindwa kwenda kwenye fainali hizo zinazochezwa kuanzia jana na kutarajiwa kumalizika Februari 8 ambapo bingwa mpya atafahamika.

Hapatoshi leo England, Man City vs Arsenal

KIVUMBI cha Ligi Kuu ya England kinatarajiwa kuendelea leo kwa mechi mbili likiwamo linalovuta hisia za wengi litakalochezwa kwenye uwanja wa Etihad mjini Manchester kati ya wenyeji Manchester City dhidi ya Arsenal.
Pambano jingine la leo litazikutanisha timu za West Ham Utd watakaokuwa nyumbani kuwakaribisha Hull City katika uwanja wa Boleyn.
Mabingwa watetezi Manchester City wataikaribisha Arsenal wakitoka kulazimishwa sare katika mechi yao ya mwisho, ilihali Arsenal wakitoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Stoke City.
Ingawa Arsenal itakosa huduma za beki wake Mathieu Debuchy aliyeumia bega katika mechi yao iliyopita sambamba na kuwakosa wakali wengine ambao ni majeruhi kama ambavyo watetezi Man City watakavyokosa huduma za wakali wake akiwamo Yaya Toure na Wlifried Bony waliopo Afrika kwa sasa..
City itakuwa ikisaka ushindi nyumbani kuweza kuendelea kuwabana Chelsea wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo wakati wao wakiwa wapo nafasi ya pili.
Watetezi hao wana pointi 47 wakati wapinzani wao Arsenal wakiwa na pointi 36 wakishika nafasi ya tano.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa pambano moja tu litakalozikutanisha timu za Everton dhidi ya West Bromwich Albion mechi itakayochezwa kwenye uwanja wa Goodson Park.

MTIBWA, JKT RUVU NANI KUIENGUA AZAM?

JKT Ruvu
Mtubwa Sugar
BAADA ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam kukalia kiti cha uongozi kwa kuiengua Mtibwa Sugar iliyokuwa imeking'ang'ania tangu ligi ianze kufuatia ushindi wake wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Stand Utd, Wakata Miwa wa Manungu watajiuliza mbele ya maafande wa JKT Ruvu.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kuumana jioni ya leo kwenye moja ya mechi mbili zinazochezwa leo kwenye mfululizo wa ligi hiyo, pambano litakalochezwa uwanja wa Chamazi, huku pambano jingine likiwa ni kati ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union dhidi ya Polisi Moro mchezo utakaopigwa uwanja wa Mkwakwani-Tanga.
Mtibwa walifungwa na Simba kwa mikwaju ya penati 5-4 katika pambano la fainali ya Kombe la Mapinduzi na kuwa kipigo cha kwanza katika mechi za mashindano kwa msimu huu, na mchezo wa leo utakuwa na jasho na damu ili kurejea kileleni au kuwapisha maafande hao kukwea kileleni kwani wanalingana nao pointi.
JKT wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wakilingana pointi na Mtibwa sote zikiwa na pointi 16 na timu yoyote itakayoibuka na ushindi itaipiku Azam wenye pointi 17 baada ya ushindi wake wa jana.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime ametamba kuwa michuano ya Mapinduzi imewaivisha vema, licha ya kwamba hakufanikiwa kuitwaa ubingwa kama dhamira yao ilivyokuwa.
"Tunarejea kwenye ligi tukiwa tumekamilika, tuna hasira na dhamira ya kuendelea kulinda rekodi yetu ya kutopoteza mchezo wowote katika ligi hiyo," alisema Mexime.
Naye kocha wa timu ya JKT, Fred Felix Minziro alisema kuwa ameandaa vijana wake kuhakikisha wanaendelea vipigo kwa wapinzani wake ndani ya Ligi Kuu ili kutimiza lengo la kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri zaidi.
"Vijana wangu wapo tayari kwa vita, tunachotaka ni kupata ushindi bila kujali tunacheza na timu ipi," alisema Minziro.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Simba ikilata ushindi wa mabao 2-0 dhidi Ndanda mjini Mtwara, Yanga iling'anga'niwa na Ruvu Shooting kwa kutofungana kama ilivyokuwa kwa Mgambo JKT dhidi ya Prisons Mbeya na Kagera Sugar ililala nyumbani kwa bao 1-0 toka kwa Mbeya City.