STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 4, 2013

Azam sasa kuvaana na Waliberia, kurejea leo kishujaa

Wakali wa Tanzania, Azam Fc
USHINDI wa mabao 5-0 iliyopata Azam jana na kuiwesha kuing'oa Al Nasir Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1 imeifanya klabu hiyo kuweka historia na sasa inatarajiwa kuvaana na tiu ya Barrack Young Controllers Fc ya Liberia  katika mechi yao ya raundi wa kwanza katikati ya mwezi huu.
Azam iliyoshinda mchezo huo wa Sudan Kusini kwa mabao ya Mcha Khamis 'Vialli', aliyefunga mabao matatu na mengine kupitia kwa John Bocco 'Adebayor' na Salum Abubakar 'Sure Boy' itakutana na wapinzani wao klabu iliyoanzisha mwaka 1997.
Wapinzani wao walipata nafasi hiyo baada ya kuing'oa timu ya Johansens ya Sierra Leone kwa jumla ya bao 1-0  baada ya juzi kutoshana nguvu kwa kutofungana wiki tangu BYC II kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
Kwa kufuka hatua hiyo Azam imezidi kuweka rekodi katika michuano mikubwa ya kimataifa inayoishiriki kwa mara ya kwanza, kwani ni hivi karibuni tu iliweka rekodi ya kufika fainali za Kombe la Kagame na kutwaa ubingwa wa michuano ya Hisani ya nchini DR Congo.
Klabu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2008-2009, ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia kwenye michuano ya Afrika baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kung'olewa jana kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa vichapo vya aibu.
Simba wenyewe walinyukwa mabao 4-0 na Recreativo do Libolo ya Angola na hivyo kung'oka kwa mabao 5-0 wakati wenzao walinyukwa mabao 5-0 jana mjini Addis Ababa, Ethiopia na wenyeji wao Kedus Giorgi.
Katika mechi ya awali iliyochezwa visiwani Zanzibar, Jamhuri ilinyukwa mabao 3-0 na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 8-0.
AAzam inatarajiwa kuwasili leo nchini kishujaa kusubiri kujiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu ikiufukuzia ubingwa kwa mara ya kwanza, na pia kwa pambano la kwanza la raundi ya kwanza dhidi ya Barrack Y. C. II ya Liberia mechi itakayochezwa kati ya Machi 15-17.

Ndomba: Mkali wa ngumi anayeota makubwa kimataifa

Bondia Pascal Ndomba



Bondia Pascal Ndomba akiwa Marekani
WAKATI mabondia wengi nchini, wakiwamo wenye majina makubwa, wakilia juu ya mchezo wa ngumi kutowapa mafanikio ya kujivunia, kwa Pascal Ndomba hali kwake ni tofauti.
Bondia huyo anayefahamika zaidi kama 'Kimondo', anasema ngumi zimempa mafanikio ya kujivunia kiasi kwamba hajutii kuucheza mchezo huo.
Ndomba anasema mbali na ngumi kumwezesha kuzitembelea nchi mbalimbali duniani, lakini pia zimemfanya ajenge nyumba Kimara Suka, akimiliki kiwanja eneo la Mbezi Beach pamoja na kuitunza vema familia yake.
Bingwa huyo wa zamani wa Taifa wa TPBC na Afrika Mashariki na Kati, anasema na hivi karibuni ameingia mkataba nchini Marekani ambao unamfanya azidi kuuheshimu mchezo huo.
Anasema mkataba huo wa muda wa miaka minne aliingia mwishoni mwa mwaka jana na kampuni ya Nelson Boxing Promotion na umeanza kutumika mwaka 2013 hadi 2017.
"Ingawa ni kweli ngumi kwa hapa nchini na hata kanda ya Afrika Mashariki zimekuwa hazina tija kutokana na ubabaishaji uliopo, nashukuru Mungu zimenisaidia kwa mengi," anasema.
Anasema siri ya kufanikiwa kupitia mchezo huo ni kujitambua kwake na kuwa na nidhamu kwa kila senti anayoipata, huku akimwagia sifa 'bosi' wake Humoud M. Sumry, anayemfadhili.
"Bosi wangu Humoud Sumry, ndiye kila kitu kwangu kwa msaada anaonipa chini ya kampuni yake ya mabasi ya Sumry," anasema.


SIRI
Bondia huyo anafichua siri kwa kusema kuwa chanzo cha mabondia wengi nchini na hata Afrika kushindwa kufanikiwa kimaisha na kimichezo kupitia ngumi inatokana na ubabaishaji uliopo katika sekta hiyo.
Anasema mapromota na viongozi wa ngumi wamekuwa wakiwanyonya mabondia kwa kutumia udhaifu wao wa kuwa na elimu ndogo ama kushindwa kujitambua wapo katika mchezo huo kwa ajili ya nini.
Pia anasema kumekuwa na hila zikifanywa kati ya viongozi wa vyama na mapromota wa nje wa kutaka mabondia dhaifu ndiyo wapelekwe nje kuicheza na hata kama ni wakali basi hulazimishwa wacheze chini ya kiwango.

Pascal Ndomba akiwa nje ya nchi
"Hufanya hivyo kwa lengo la kutaka mabondia wao kuendeleza rekodi zao na ikitokea bondia anayepelekwa huko akashinda kama alivyofanya Karama Nyilawila basi huzua tafrani baina ya pande mbili zilizokubaliana," anasema.
Akaongeza hiyo ndiyo sababu inayofanya mabondia wengi wa Tanzania au barani Afrika kupigwa kila wanapoenda nje.
"Ni 'dili' tu zinazofanywa na baadhi ya watu wachache kwa tamaa za fedha," anasema.
Ndomba anayependa kula ugali au ndizi kwa nyama na kunywa Fanta, pia anasema mabondia wamekuwa wakidhulumiwa haki zao na baadhi ya viongozi wa ngumi kwa kuwapunja fedha za malipo tofauti na makubaliano.

Pascal Ndomba akiwa na 'bosi' wake, Humoud Salim
Anasema inawezekana bondia ameitwa kwenda kucheza nje kwa dola 5,000, lakini huishia kulipwa 3,000 au nusu ya hapo kwa kisingizio hiki na kile, wakati mwingine asipewe kabisa.
Bondia huyo aliyeingia kwenye ngumi kwa kuvutiwa na bingwa wa zamani wa dunia, Mike 'Iron' Tyson, anasema ni vema kungekuwa na utaratibu chini ya serikali kuhakiki mikataba na kujua kinachompeleka bondia nje ya nchi.
"Japo hizi ni ngumi za kulipwa, ni vyema kungekuwa na chombo cha namna hiyo kusimamia safari za mabondia nje kuepusha kudhulumiwa na kuichafua nchi nje kwa vile hupeperusha bendera ya taifa," anasema.

MATAJI
Ndomba, mume wa Ikupa aliyezaa naye watoto wawili, Michael (8) na Abel (5) wanaosoma Shule ya Msingi Makuburi, anasema alianza rasmi ngumi mwaka 1996 katika klabu ya Kiwira iliyopo Kyela Mbeya.
Kocha aliyemnoa anaitwa Said Tambwe na alishiriki michuano kadhaa ya ngumi za ridhaa na alipoona hazina tija yoyote, mwaka 2000 aliamua kuhamia ngumi za kulipwa.
Anasema akizcheza ngumi hizo aliweza kunyakua ubingwa wa mkoa wa Mbeya na kupata fursa ya kupigania ubingwa wa Taifa wa TPBC mwaka 2005 kwa kumpiga Fike Wilson.
Aliendelea kutoa vipondo kwa wapinzani wake kabla ya mwaka 2009 kutwaa taji la Afrika Mashariki na Kati kwa kumchapa kwa KO Mkenya Joseph Odhiambo.
Pia amewahi kuwania mikanda ya kimataifa inayotambuliwa na WBC, WBO na IBF, uzito wa Cruiser mara ya mwisho ikiwa Desemba, 2012 alipoenda Ghana kupigana na Mghana asiyepigika Braimah Kamoko na kunyukwa.

Pascal Ndomba (Kushoto) akichapana na Mghana Braimah Bamoko
Ndoto zake kubwa ni kuja kutwaa ubingwa wa dunia akiamini ana uwezo wa kufanya hivyo, pia akitamani kuja kumiliki gym na klabu ya kufunzia vijana mchezo huo.
"Napenda nije kuwafunza na kuwarithisha vijana kipaji changu, najua siwezi kusalia kuwa bondia milele," anasema.
Licha ya kucheza mapambano mengi, Ndomba analitaja pambano la kuwania ubingwa wa vijana wa IBF uzani wa 'cruiser' dhidi ya Mswisi, Agron Dzila, kuwa ndilo gumu kwake na asiloweza kusahau kwa 'kisago' alichoikipata.

CHIMBUKO
Pascal Ndomba alizaliwa mwaka 1983, Kyela Mbeya akiwa ni mtoto wa nne kati ya watano wa familia yao na alisoam  Shule ya Msingi Lema ya Kyela kabla ya kujiunga Tabora Boys kwa masomo ya Sekondari.
Tangu shuleni alipenda michezo, ila alivutiwa na ngumi na kujifunza kabla ya kuanza kuzipiga ulingoni na mabondia kama akina Bagaza Mwambene, George Sabuni, Hassani Matumla, Karama Nyilawila na Maneno Osward.
Ndomba anasema hana furaha mpaka atakapopanda ulingoni kupigana na Japhet Kaseba aliyenukuliwa hivi karibuni akidai amekuwa akikwepa na baadhi ya mabodnia kwa umahiri wake.
"Kwa kweli kiu yangu ni kuzichapa na Kaseba, dai lake kwamba amekuwa akikimbiwa na mabondia siyo kweli kwa vile nimekuwa nikiomba kucheza naye bila mafanikio," anasema.
Ndomba anayeiomba serikali itupie macho mchezo wa ngumi kwa madai umekuwa ukiiletea sifa Tanzania nje ya nchi kwa mabondia waliowahi kutwaa mataji ya kimataifa.

Pascal Ndomba (kushoto) akiwa kwenye kazi yake ya uwakala wa mabasi kituo cha mabasi cha Ubungo
Bondia huyo anayependa kusikiliza muziki na kuangalia runinga mbali na kucheza ngumi pia ni wakala wa kampuni ya mabasi ya Sumry, akiishabikia Simba na Manchester United, na anawazimia Shomari Kapombe na Patrick Evra.
Tukio la furaha kwa Ndomba, ambaye anamkubali sana bondia mkongwe Mbwana Matumla, ni siku mkewe alipojifungua mtoto wake wa kwanza mwaka 2005. "Tukio la huzuni nisilolisahau ni kifo cha baba yangu kilichotokea mwaka 2002," anasema.

Pascal Ndoma (kushoto) akiwa na wakala mwenzake wa mabasi ya Sumry

TOTTENHAM  YAINYUKA ARSENAL, MANCHSTER CITY DIMBANI LEO

Garreth Bale akifunga bao la kwanza la Tottenham katika mechi ya jana


KIKOSI cha vijana wa Andre Villas Boas, Tottenham Hotspur, jana waliendeleza  makali na ubabe kwa klabu za London ya Kaskazini baada ya kuwanyuka wapinzani wa Arsenal kwa mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England.
Katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa White Hart Lane nyumbani kwa Spur, Arsenal ilishtukizwa kwa bao la mapema lililofungwa na Garreth Bale kabla ya Aaron Lennon kuongeza bao la pili dakika mbili kabla ya mapumziko.
Arsenal waliocheza kichovu kipindi cha kwanza na kurejea toka mapumziko walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na beki wake 'ngongoti' Mertesacker.
Ushindi huo umeifanya Spur kurejea kwenye nafasi yake ya tatu iliyokuwa inaishikilia kabla ya kuenguliwa Jumamosi na Chelsea waliopata ushindi dhidi ya West Brom kwa bao 1-0.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena usiku wa leo kwa pambano moja la timu za Aston Villa itakayoikaribisha mabingwa watetezi wa Li litakalowakutanisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Manchester City waliopo nafssi ya pili.