STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 26, 2013

Mfanyabiashara mwingine wa madini auwawa kwa risasi Arusha

MFANYABIASHARA wa madini ya Tanzanite, Bw. Steven Alex, amepigwa risasi jana jioni na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi eneo la Pangani, jijini Arusha na kuporwa zaidi ya sh. milioni 60.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema mfanyabiashara huyo alikuwa ndani ya gari lake akiwa amepaki eneo la Pangani ili aweze kulipa madeni kwa watu waliokuwa wamemuuzia madini.
Walisema ndani ya gari hilo ambalo lilifungwa vioo, alikuwa na wenzake wawili ambapo ghafla walitokea vijana watatu waliokuwa na pikipiki aina ya Toyo ambazo namba zake hazikufahamika wakiwa wameifunika na mifuko ya nailoni.
“Walimgongea dirishani wakitaka afungue mlango, huyu mfanyabiashara hakufungua ndipo vijana hao walichomoa bastola na kuanza kugonga tena kwenye dirisha la gari. 
 
Emmanuel Shilatu

CCM yamaliza vikao vyake Dodoma, UVCCM yamtosa Shigella

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiongoza kikao
cha NEC, mjini Dodoma leo mchana. Kushoto ni Katibu Mkuu
wa CCM Abdulrahman Kinana.
BASHIR NKOROMO, Dodoma

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo imemamliza kikao chake cha siku tatu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ikiwa imeridhia mapendekezo kadhaa ya Kamati Kuu ya CCM, ikiwemo kumfuta uongozi Mbunge wa jimbo la Mjini Magharibi, Zanzibar,  Mansor Yusuf Himid.

Kikao hicho pia kimeridhia, uteuzi wa Makatibu wateule wapya wa Jumuia za CCM, za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Jumuia ya Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Katika uteuzi huo mapendekezo hayo yaliyofanywa na Kamati Kuu ya CCM, na kuridhiwa na NEC, kwa upande wa Umoja wa Vijana wa CCM ameteuliwa aliyekuwa Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda na kwa upande wa Jumuia ya Wazazi ni Mjumbe wa NEC kutoka Pemba, Seif Shabani Mohamed, huku kwa upande wa UWT akiachwa Katibu Mkuu wa sasa, Amina Makilagi.

Mapunda atachukua nafasi iliyokuwa imneshikiwa na Martine Shigela ambaye ameongoza UVCCM kwa miaka mitano sasa, na Seif Shabani Mohammed kutoka Pemba akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Hamis Suleiman Dadi ambaye pia amekuwa katika wadhifa kwa miaka mitano sasa.

Pia, NEC imeridhia mapendekezo  ya Kamati Kuu kwa ajili ya kuziba nafasi Makatibu wa CCM wa mikoa mitatu ya Morogoro,  Kaskazini Pemba na Geita ambayo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa imekuwa wazi kwa muda mrefu sasa kutrokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Kufuatia mapendekezo hayo ya Kamati Kuu, ambayo yameridhiwa na NEC, walioteuliwa na mikoa yao ikiwa kwenye mabano ni Msaidizi Kitengo cha  Uchaguzi, CCM Ofdisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Romuli Rojas John (Morogoro), aliyekuwa Katibu Katibu wa wilaya ya Mkinga, Kassim Mabrouk Mbarak (Kaskazini Pemba) na aliyekuwa Katibu wa CCM Igunga, Mary Maziku (Geita).

Kuhusu sakata la madiwani wa Bukoba mjini, CCM imesema suala hilo, linaendelea kushughulikiwa ambapo baada ya kikao hicho cha NEC, Kamati kuu iliendelea kukutana na viongozi wa wilaya ya Bukoba, Mwenyekiti wa CCM na Katibu wa wilaya hiyo.

Mapema kabla ya kikao cha NEC, Kamati Kuu ilikutana na Mbunge wa Bukoba mjini Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba mjini na kuwahoji, wakati jana Kamati Kuu ilikutana na  Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wa Kagera.
 Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiongoza kikao cha NEC, leo Agosti 26, 2013 mjini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akitoa utangulizi kabla ya Mwenyekiti wa CCm Rais Jakaya Kikwete (kushoto) kufungua kikao cha NEC, Agosti 26, 2013
 Baadhi ya wajumbe wa NEC, ukumbini. Kulia mstari wa mbele ni Mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya Viongozi wastaafu wa CCM, John Malecela ambaye ni mwalikwa kwenye kikao hicho.
 Mjumbe wa NEC, Mama Salma Kikwete akiteta jambo na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Zakiah Meghji kabla ya kikao cha NEC kuanza, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma.
 Mjumbe wa NEC, Dk. Fenela Mkangala na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro wakijadili jambo kabla ya kikao cha NEC kuanza leo Agosti 26, 2013, Makamo Makuu ya CCM mjini Dodoma.
Wajumbe wa NEC kutoka Pemba wakiwa nje ya ukumbi kabla ya kikao kuanza. Kutoka Kushoto ni Hamadi Bakari Ali, Mwinyi Fakih Hassan, Ali Issa Ali,  Masoud Mohammed Abdallah, Seif Shaaban Mohammed na Mussa Fumu Mussa.

Jaji Francis Mutungi aapishwa kuongoza ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi vitendea kazi Msajili mpya wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi Ikulu jijini Dar es salaam leo.
 Jaji Mutungi akila kiapo
 Picha ya pamoja.

Mabao 19 yafungwa pazia la Ligi, Tegete, Mkude, Kondo nouma, wawili wajifunga wenyewewaan


Jerry Tegete (kulia) akiwa na baba yake
JUMLA ya magoli 19 yamepachikwa katika siku ya ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013-2014, huku wachezaji watatu, Jerry Tegete wa Yanga, Jonas Mkude wa Simba na  Bakar Kondo wa JKT Ruvu wakiongoza msimamo wa wafungaji kwa sasa.
Tegete aliyafunga mabao hayo wakati Yanga wakiiua Ashanti Uniteda kwa mabao 5-1, wakati Mkude aliwatungua Rhino Rangers na Kondo alifanya hivyo wakati JKT wakiizamisha Mgambo JKT kwao jijini Tanga.
Mechi sita kati ya saba zilizochezwa kwenye ufunguzi wa ligi hiyo zilikuwa na mabao, wakati pambano la jijini Mbeya kati ya wenyeji Mbeya City na Kagera Sugar ndilo pekee lililoisha bila kutikiswa nyavu.
Kadhalika mechi mbili kati ya hizo saba zilishuhudiwa wachezaji wakijifunga magoli, ambapo Laurian Mpalile alijifungwa na kuisaidia Ruvu Shooting kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons anayoichezea hali iliyomkuta pia beki wa Oljoro JKT, Yusuf Machonge akliyeunganisha wavuni mwake mpira uliopigwa na Mkenya Crispian Odulla wa Coastal Union wakati Wagosi wa Kaya wakishinda mabao 2-0 jijini Arusha.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Jumatano wiki hii kwa timu zote 14 kushuka dimbani viwanja saba tofauti ambapo jijini Dar vinara na watetezi wa ligi hiyo, Yanga itawalika Coastal Union, huku Simba itakuwa jijini Arusha kuvaana na Oljoro, wakati JKT Ruvu itarudi nyumbani Pwani kuumana nna Prisons Mbeya.
Mechi nyingine itazikutanisha Kagera Sugar itakayokuwa dhidi ya ndugu zao wa Mtibwa kwenye uwanja wa Manungu,Turiani
Ratiba ya mechi hizo zijazo za Jumatano ni kama ifuatavyo;
Mtibwa Sugar vs Kagera Sugar
Rhino Rangers vs Azam
JKT Ruvu  vs Prisons
Mbeya City vs Ruvu Shooting
Mgambo  vs Ashanti United
JKT Oljoro vs Simba
Young  vs Coastal Union

Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014                                    P  W  D  L  F  A  GD  PTS
Yanga                     1   1   0   0   5  1    4    3
Ruvu Shooting        1   1   0   0   3   0   3    3
Coastal Union         1   1   0   0   2   0   2    3
JKT Ruvu               1   1   0   0   2   0   2    3
Rhino Rangers        1    0   1   0   2   2   0    1
Simba                     1   0   1   0   2   2   0    1
Azam                     1    0   1   0   1   1   0    1
Mtibwa Sugar         1   0   1   0   1    1   0   1
Kagera Sugar         1    0   1   0   0   0   0   1
Mbeya City            1    0   1   0   0   0   0   1
Mgambo                1   0   0   1   0   2   -2   0
Oljoro                    1   0   0   1   0   2   -2   0
Prisons                   1   0   0   1   0   3   -3   0
Ashanti                   1   0   0   1   1   5   -4   0

Wafungaji:
2- Jerry Tegete (Yanga), Jonas Mkude (Simba), Bakar Kondo (JKT Ruvu)
1- Abdul Banda (Coastal), Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Simon Msuva (Yanga), Saad Kipanga, Iman Joel (Rhino Rangers), Aggrey Morris (Azam), Laurian Mpalile (Prisons-OG), Elias Maguli, Jerome Lembeli (Ruvu Shooting),  Yusuph machonge (Oljoro-OG), Juma Liziu (Mtibwa Sugar), Shaaban Juma (Ashanti Utd)

Jina la Rais Kikwete lahusishwa kutaka kupora ardhi ya wanakijiji Bagamoyo

Katibu wa wamiliki wa mashamba na makazi wa kijiji cha Buma, Gumbo Majibwa akisoma taarifa kwa wananakijiji wenzake, huku pembeni yake Mwenyekiti Hassani Tenela akimsikiliza kwa makini katika mkutano wao wa kupinga kutaka kuchukuliwa kwa maeneo yao ili kumpish mradi wa hospitali ya kimataifa inayodaiwa itamilikiwa JWTZ
Mmoja wa wamiliki wa mashamba na makazi wa kijiji cha Buma akiandikisha jina katika karatasi ya mahudhurio

Sehemu ya wahudhuriaji wakisikiliza kwa makini taarifa juu ya sakata la kutaka kuporwa kwa maeneo yao


Wamikili wa mashamba na makazi kijiji cha Buma, wilaya ya Bagamoyo wakiwa kwenye mkutano wao uliofanyika juzi Jumamiosi
Mpaka kieleweke hapa....Ardhi yetu anaitaka Rais au Jeshi? wanaulizana wamamiliki wa ardhi ya kijiji cha Buma

Najiorodhesha ili wasiseme sikuwepo!
Khadija Omary mmoja wa wanaomiliki ardhi katika kijiji cha Buma akitoa hoja na kuuliza maswali katika mkutano wao wa Jumamosi.

Viongozi wa Kamati waliosimama kando ya gari wakisoma taarifa kwa wamiliki wenzao kuhusu sakata la kutaka kuporwa kwa ardhi yao,.

Na sisi tumo mpaka kieleweke!

Hata iwe vipi ardhi yetu haiwezi kuchukuliwa kienyeji


Husna Mohammed naye hakuwa nyuma kutoa maoni yake. Mwanamama huyo ni mmoja wa watu sita walioteuliwa katika kamati maalum ya kwenda kumuona Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa ili kujua ardhi yao inachukuliwa na mwekezaji aliyetafutwa na Rais au ni JWTZ

"Tujiadharini isije kuna matapeli wanalitumia jeshi na jina la Rais kutaka kupora eneo leo. Hospitali gani inayojengwa katika eneo la ekari 1500? Dk Ally Ponza alihoji katika makutano huo
Tupo nanyi mwanzo mwisho mpaka kieleweke, hatukubali kirahisi kuachia ardhi yetu.

Frank Lyimo naye alitaka upatikane uthibitisho juu ya nani anayetaka kuchukua ardhi yao ili wasije wakambebesha lawama Rais Kikwete bure wakati kumbe hajui chochote kinachoendelea katika kijiji cha Buma.

Tupo pamoja

Katibu Gumbo Majubwa akitoa ufafanuzi baada ya kuulizwa na wanakijiji wenzake

Umoja ni nguvu! Hapa mwanzio mwisho mpaka tujue ukweli

Mwenyekiti wa kamati Hassan Tenela akifafanua jambo kwa wamiliki wenzake kuhusu ufuatuiliaji wao juu ya sakata la kutaka kuporwa ardhi yao.

"Jamani, tumeelezwa jeshi limetumwa tu kusaka ardhi, lakini mwekezaji ametafutwa na Rais alipokuwa nje ya nchi, lakini cha ajabu Mbunge wetu hajui na wala bajeti ya kulipwa fidia kwa kuporwa ardhi haipo kwenye Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya 2013-2014' Mwenyekiti Hassan Tenela akiwafafanulia wenzake mahali alipofikia.
JINA la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete linadaiwa kutumika kuwatisha wamiliki wa mashamba na makazi wa Kijiji cha Buma, kilichopo Kata ya Kiromo wilaya ya Bagamoyo-Pwani ili waachie maeneo yao yanayodaiwa kutaka kuporwa kwa kisingizio cha kupisha mradi wa hospitali kubwa ya kimataifa inayodaiwa itamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wamiliki hao walitoa tuhuma hizo katika mkutano wa pamoja na  viongozi wa kamati yao, uliofanyika siku ya jumamosi kijiji hapo, ambapo uongozi wa kamati yao ulisema kuwa baada ya awali kuelezwa kwamba mradi huo ni wa JWTZ sasa wanaambiwa unahusu Rais Kikwete.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hassani Tenela alisema katika kufuatilia kinachoendelea juu ya mgogoro wa kuporwa maeneo yao, alielezwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chambezi, Abdallah Mchayungu kuwa, mradi huo siyo wa jeshi bali ni mradi uliopelekwa kwao na Rais Kikwete baada ya kupata mwekezaji nje ya nchi, hivyo ni lazima waachie eneo lao.
Hata hivyo alisema taarifa hiyo imewapa shaka na kuhisi kama jina la Rais linatumika ili kuwatisha kwa sababu awali walijulishwa ni jeshi linalotaka eneo lao ambapo bila kupata ridhaa yao waliweka alama (beacons) wakitaka eneo kwao na katika kijiji cha jirani cha Mataya.
"Kama mradi huo una mikono ya Rais, vipi mwenyewe kutowahi kuzungumzia kokote na kama ni jeshi mbona katika bajeti ya wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya 2013-2014 hakuna fungu la fidia kwa vijiji vya Buma na Mataya? Katibu wa wamiliki hao, Gumbo Majubwa alihoji.
Majubwa alisema pia suala kwamba fidia ya kila ekari kutofautiana kati ya vijiji hivyo viwili inawapa shaka na kusema wanaendelea kushikilia msimamo wao wa kugoma kutoa maeneo yao hadi wahakikishwe mwekezaji halali anayetaka eneo hilo na wakae wakubaliane naye.
Katibu huyo alisema taarifa walizonazo ni kwamba kwa wenzao wa Mataya waliolazimishwa na kuridhia kuachia maeneo yao watalipwa kila ekari Sh Mil. 3, wao wa Buma wakidaiwa watalipwa  Sh Mil 7-10 kwa kila ekari kitu kinachomshangaza kwa vile ardhi inayochukuliwa ni moja.
Mara baada ya uongozi wa wamiliki hao kutoa taarifa hiyo, baadhi ya wamiliki walisema licha ya kwamba tangu awali walikuwa na shaka na mradi ulioelezwa utafanyika katika vijiji hivyo vya Buma na Mataya ukihusisha eneo la ekari 1500, kutajwa kwa Rais Kikwete linawatia shaka zaidi.
"Tunaomba uongozi wa kamati ufuatilie ukweli kama mradi huu unamhusisha Rais au jina lake linatumika kama njia ya kututisha, kwani pia zipo taarifa kwamba hata Mbunge wetu Dk Shukuru Kawambwa hajui lolote kuhusu mradi huu," alisema Dk Ally Ponza.
Dk Ponza, pia alisema kwa ufahamu wake ekari 1500 kwa mradi wa hospitali tu ni kubwa mno na kuhoji isije  ikawa ni matapeli wanaotaka kulitumia jeshi au jina la rais kuwapora ardhi yao ambayo wanamiliki kwa miaka mingi iliyopita.
Wamiliki wengine pamoja na uongozi wa kamati yao ulimtuhumu diwani wao, Hassan Usinga, wakidai wanahisi anawazunguka na kushiriki katika kutaka kuporwa kwa ardhi yao hasa kutokana na usaliti wanaodai amekuwa akiuonyesha tangu saka hilo lilipoanza.
"Katika mkutano tuliofanya Agosti 17 alitamka mwenyewe akidai yu tayari kumpa mwanakijiji wa Mataya viwanja vitatu vilivyopimwa na vyenye hati vilivyo barabarani ili atoe eneo lake kupisha mradi huu, tujiulize iweje awe tayari kutoa eneo lake kwa mradi usiomhusu?" Alihoji Samuel Lema.
Naye Husna Mohammed, alisema wanahisi viongozi wa kitongoji na kijiji chao pamoja na diwani lao moja na wanafanya mipango kuporwa ardhi yao kwa kuwalazimisha kama wenzao wa Mataya na kutaka kuugomea mkutano waliouitisha viongozi utakaofanyika Septemba 7.
Baada ya majadiliano marefu hatimaye wamiliki hao na uongozi wao uliazimia mambo matatu kuunda kamati ya watu sita kufuatilia ukweli wa mtu anayetaka kuchukua eneo lao kama ni Mwekezaji wa Rais Kikwete au jeshi, kuonana na Mbunge wao Dk Kawambwa ili awape ufafanuzi juu ya kuwepo kwa mradi huo au la.
Pia kuuzuia mahakamani mkutano ulioitishwa na uongozi wa kijiji utakaohudhuriwa na wanaodaiwa wawakilishi wa jeshi wanaoitaka ardhi yao, mpaka kwanza wapate uthibitisho wa kuwepo kwa mradi huo wa hospitali.
Katika kutaka kupata ufafanuzi wa sakata hilo na tuhuma zilizoelekezwa kwake, MICHARAZO lilimsaka Diwani Hassan 'Wembe' Usinga' kwa njia ya simu ambapo kwanza alikanusha suala la kuwasaliti wapiga kura wake akidai mradi huo ulipitishwa na wanakijiji wenyewe mwaka 2010.
Hata hivyo alikiri juu ya ahadi yake ya kumpa mwanakijiji wa Mataya aliyemtaja kwa jina la Mzee Nyanza viwanja vitatu ili atoe ardhi yao kama njia ya kumsaidia kutoka porini na kukaa barabarani na kudai  siyo kama kuna mkono wake katika mradi huo.
"Wamiliki hao wanashindwa kunielewa tu, mimi nipo hapa kusimamia haki zao ndiyo maana umeitishwa mkutano Septemba 7 ili wazungumze na wanaotaka ardhi yao, kudai mimi nawasaliti ni kutaka kunionea kwani mradi ulitambulishwa tangu 2010, wakati sijawa diwani," alisema diwani huyo.
Aliongeza kilichotokea ni kweli haya yeye hakuwa anaujua mradi huu na kuufuatilia na kugundua waliokuwepo wakati mradi ukipitishwa waliouza maeneo yao kwa watu wengine ambao ndiyo wanaoibua hoja za kuugomea, huku akikana mradi huo kumhusu Rais Kikwete na kusisitiza ni mradi wa Jeshi, ingawa alishindwa kufafanua iweje lichukuliwe eneo kubwa la ekari 1500 huku bajeti la kulipia fidia haikutajwa katika bajeti ya 2013-2014 ya wizara yao.
"Aaah wanataka eneo hilo, lakini walisema wataanza kulipa eneo la eka 250 au 300 kwa vile bajeti waliyonayo kwa sasa inahusu eneo hilo, japo mpaka sasa bado utathimini wa kiwango cha malipo hakijaanza na siyo kweli kama fidia zinatofautiana katika vijiji hivyo," alisema diwani huyo.
Alifafanua kuwa ni kweli wanajeshi hao waliweka alama bila kuwashirikisha wamiliki halali wa maeneo hayo, akidai walifanya hivyo kuweka alama ya eneo wanalolihitaji kwanza na sasa ndiyo wameanza tararibu za kutaka kulimiki kihalali eneo hilo na kutaka wanakijiji kuelewa.
"Huu mradi utakuwa mkubwa kwa mujibu wa wawakilishi wa Jeshi waliokuja kujitambulisha kwa uongozi wa kijiji cha Buma Agosti 20, hivyo wananchi waupokee kwa moyo mmoja kwani una manufaa kwao, ingawa wana hiari ya kutoa eneo lao baada ya kujiridhisha," alisema.
Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa ambaye ni Waziri wa Elimu na Ufundi, alipoulizwa mradi huo, alisema ofisi yake haina taarifa rasmi ya kina na kudai ataanza kuufuatilia ili ajue ukweli wa mradi huo kisha atatoa taarifa kwa vyombo vya habari.
"Ofisi yangu ina taarifa za juu juu tu, tumeanza kufuatilia kujua ukweli ila nitahadharishe wananchi wawe makini na miradi inayoibuliwa hivi sasa ili wasiingwe mkenge," alisema Dk Kawambwa.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi alipotafutwa na MICHARAZO alisema asingekuwa tayari kuzungumza suala hilo kwa vile suala hilo lipo chini ya Afisa Ardhi, ingawa alisema wilaya yake suala la migogoro ya ardhi imekuwa kama fasheni na kuikuta tangu aingie madarakani.
"Kwa kweli siwezi kufafanua lolote kuhusu suala la kijiji hicho cha Buma au kwingineko kwa sababu wanaohusika kutoa majibu kamili ni afya ardhi, ila ukweli migogoro ya ardhi hapa Bagamoyo ni ya kawaida, ni vyema kama ukija kupata ufafanuzi zaidi," alisema DC huyo.

Dillish wa Namibia ndiye mshindi wa BBA The Chase 2013







MSHIRIKI kutoka nchini Namibia, Dillish; ndiye aliyeibuka mshindi wa Shindano la Big Brother Africa-The Chase 2013 na kuondoka na kitita cha Dola za Kimarekani 300,000 katika fainali zilizofanyika usiku huu (Agosti 25)
Dillish mwenye miaka 24, hajawahi kuwa head of the house hata siku moja katika siku zote 91 alizokuwa ndani ya jumba, alishawahi kuwa nominated mara 5 na mara zote alibaki kwa kura za Africa, na hajawahi kuwa na mahusiano na mshiriki yoyote.


Dillish amekuwa ni mwanamke wa pili kushinda BBA tangu ilivyoanzishwa, baada ya Cherise kutoka Zambia kushinda kwenye BBA season  7 zilizopita


Katika top 5 waliobaki, alianza kutoka Beverly (Nigeria), akafuatia Melvin (Nigeria) na watatu kutoka ni Elikem (Ghana) wa nne ni Cleo (Zambia) na hatimaye Dillish kuwa mshindi wa BBA The Chase 2013.
Katika shindano hilo Tanzania iliwakilishwa na Nando na Feza ambao walitolewa mapema, Nando kwa utovu wa nidhamu na mwenzake kwa kup[ata kura chache wiki mbili zilizopita.

Barca bila Messi, Neymar akianzia benchi yashinda 1-0

Messi na Neymar

IKICHEZA bila ya nyota wake Lionel Messi na ikimuanzisha benchi Mbrazil Neymar, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Hispania, Barcelona wameibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Malaga.
Messi alishindwa kuwekwa kikosini kutokana na kuwa majeruhi, lakini hiyo haikuifanya Barca washindwe kufurukuta baada ya kujipatia bao la dakika za lala salama kabla ya kwenda mapumziko lililofungwa na beki Adriano Correia na kujipatia pointi tatu muhimu.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa mabingwa hao katika ligi hiyo baada ya wiki iliyopita kuanza kwa kishindo kwa kuicharaza Levante kwa mabao 7-0 walipoumana nao uwanja wa Nou Camp.
Katika mechi nyingine ziliuzochezwa leo, Atletico Madrid walipata ushindi mnono wa mabao 5-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Rayo Vallecano, nazo timu za Levante na Sevilla zikitoshana nguvu kwa kutoka sare ya bila kufungana. 
Pambano linaloendelea kwa sasa ni kati ya Real Betis dhidi ya Celta Vigo ambapo mpaka sasa matokeo ni 0-0 ikiwa ni dakika ya 13.