STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 18, 2011

Mabondia 10 kuwasindikiza Nassib vs Kariuki


BINGWA wa zamani wa Dunia wa World Boxing Forum, Juma Fundi na Rashid Ally ni miongoni mwa mabondia watakaolisindikiza pambano la kimataifa kati ya Nassib Ramadhan 'Manny Pacquiao wa Tz' dhidi ya Anthony Kariuki kutoka Kenya.
Nassib anayeshikilia kwa sasa taji la dunia la World Boxing Forum baada ya kumvua Juma Fundi Mei mwaka huu, atapigana na Karikuki katika pambano litaklofanyika siku ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, Desemba 9 kwenye ukumbi wa DDC Keko, jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa pambano hilo, Pius Agathon, aliiambia MICHARAZO kwamba Fundi na Ally ni kati ya mabondia 10 watakaopanda ulingoni kusikindikiza pambano hilo la raundi 10 lisilo la ubingwa kati ya Nassib na Kariuki.
Agathon, alisema Fundi atapigana siku hiyo na Juma Seleman katika pambano la raundi sita la uzani wa kilo 51, Fred Sayuni dhidi ya Bakar Dunda na Ramadhani Kumbele ataonyeshana kazi na Shabaan Madilu.
"Mipambano mingine siku hiyo itakuwa ni kati ya Rashid Ally atakayepigana na Daud Mhunzi katika uzito wa kilo 57 na Faraji Sayuni ataumizana na Alfa George ndipo Nassib atakapopanda ulingoni kupigana na Kariuki katika uzani wa Fly," alisema.
Mratibu huyo alisema maandalizi ya jumla ya mapambano hayo yanaendelea vema ikiwemo kumalizana na mabondia wote ambao kwa sasa wanaendelea kujifua kwa mazoezi tayari kuonyeshana ubabe siku hiyo kwenye ukumbi huo wa DDC Keko.
Aliongeza lengo la michezo hiyo mbali na kuwaweka fiti mabondia hususani Nassib ambaye mwakani atalitetea taji lake la World Boxing Forum, pia ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru.
"Tumeandaa michezo hii ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru sambamba na kumuandaa vema Nassib kabla ya kulitetea taji lake mwakani," alisema.

Mwisho

Niyonzima aikana Simba, awatroa hofu Jangwani



KIUNGO nyota wa kimataifa wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima 'Fabregas' amewatoa hofu wanayanga kwa kuweka wazi kwamba hana mpango wa kujiunga na mahasimu wao Simba kwa kile alichodai anaridhika na maisha yake Jangwani.
Pia, kiungo huyo alisema kama ni kuondoka Yanga, basi sio kwa kujiunga na klabu nyingine ya Tanzania, bali ni kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, ikiwa ni kati ya ndoto anazoota kila siku maishani mwake.
Akizungumza moja na kipindi cha michezo cha Radio One 'Spoti Leo', Niyonzima, amedai kushangazwa na taarifa kwamba Simba inamnyemelea wakati hajawahi kufanya mazungumzo yoyote na uongozi wa klabu hiyo au mtu yeyote.
Kiungo huyo aliyetua Jangwani akitokea klabu ya APR ya Rwanda, alisema mbali na kutowahi kuzungumza na mtu yeyote ili kujiunga Simba, lakini yeye binafsi hana mpango huo kwa vile anaridhika na maisha yake ndani ya klabu yake ya sasa.
"Aisee sina mpango wa kuihama Yanga na hivyo nawataka wanayanga wasiwe na hofu nadhani yanayosemwa yanatokana na kuvutiwa na soka langu, lakini sijawahi kuzungumza na mtu yeyote kujiunga Simba," alisema.
"Pia kwa namna mambo yangu yanayotekelezwa ndani ya Yanga na mie kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio, sioni sababu ya kutaka kuhama na kama ikitokea hivyo basi ni kwenda zaidi ya Tanzania, lakini sio kujiunga Simba," alinukuliwa Niyonzima.
Nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya nchi yake ya Rwanda 'Amavubi' alisema ingawa yeye ni mchezaji na lolote linaweza kutokea, lakini hadi wakati akizungumza hakuwa amewaza lolote juu ya kuiacha Yanga aliyosaini nayo mkataba wa miaka miwili.
Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kwamba Simba imekuwa ikimwinda kiungo huyo ambaye soka lake limewakuna wengi tangu atue Jangwani, ikiwa kama jibu la watani zao, Yanga kudaiwa kumnyatia mshambuliaji wao, Felix Sunzu.
Tetesi hizo za Yanga na Simba kubadilishana wachezaji zimekuja wakati mbio za usajili wa dirisha dogo nchini likizidi kupambana moto.

Mwisho

Mkwasa, Julio wambeep Poulsen kwa Boban



MAKOCHA wapya wa timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu 'Julio' wamembeep, kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen bada ya kumuita kikosi kiungo wa wa Simba, Haruna Moshi 'Boban'.
Boban na mshambuliaji mpya wa Azam, Gaudence Mwaikimba, wameitwa katika kikosi cha Kilimanjaro Stars kitakachotetea ubingwa wake katika mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayoanza Novemba 25 jijini Dar es Salaam.
Baada ya Boban kusajiliwa na Simba na kuanza kuitumikia kwenye fainali zilizopita na Kombe la Kagame mwaka huu, kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen, alimuita katika kikosi cha vijana wa umri chini ya miaka 23 kilichokuwa na mechi mbili za kirafiki na Shelisheli jijini Arusha lakini kiungo huyo alikacha wito huo na hivyo kuendelea kuwa nje ya timu hiyo kwa muda mrefu.
Akitangaza kikosi cha nyota 28 jana, kocha msaidizi wa Kili Stars, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema kuwa kikosi chake kitaanza mazoezi leo kwenye Uwanja wa Karume na lengo la kuita wachezaji hao ni kuwapima zaidi na baadaye watachujwa na kubaki 20 kama kanuni za usajili wa mashindano hayo zinavyoeleza.
Julio alisema kuwa ameita wachezaji wengi chipukizi ili kuwapa nafasi zaidi ya kujifunza na kuitumikia nchi yao kwa bidii huku pia akiwaita wazoefu ili waweze kupambana na changamoto kutoka kwa timu pinzani kwenye michuano hiyo.
"Tunawaomba Watanzania wajue kuwa hii ni timu yao, watupe ushirikiano, waipende na kuishangilia ili sisi wazawa tuweze kulitetea kombe, tunaahidi kupambana na kukibakisha kikombe," alisema kocha huyo.
Alisema kuwa wanaahidi kupambana na wachezaji wasio na nidhamu ili wajirekebishe na hatimaye kuitumikia vyema nchi yao kutokana na uwezo wa kucheza soka walionao.
"Hii ni timu ya wote na kwa kuwa mpira hauchezwi chumbani, hata Saidi Maulidi (SMG) kama anaweza kuja aje katika mazoezi apambane na akionyesha anaweza tutamchukua katika kikosi cha watu 20," aliongeza Julio kuhusiana na uteuzi wa wachezaji wanaocheza nje ya nchi.
Kikosi kamili cha timu hiyo kilichoitwa jana ambacho nahodha wake atakuwa ni kipa Juma Kaseja kutoka Simba ni pamoja na Deo Munishi 'Dida' kutoka Mtibwa Sugar, Shabani Kado (Yanga), huku mabeki wa pembini wakiwa ni Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati walioitwa ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United) huku viungo wakiwa ni Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Boban, Ramadhan Chombo (Azam), Rashid Yusuf (Coastal Union), Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars) na Mohamed Soud (Toto Africans).
Washambuliaji walioitwa ni Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe ), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Daniel Reuben (Coastal Union) na Nizar Khalfan wa Vancouver Whitecaps ya Canada.
Kilimanjaro Stars itaanza kampeni ya kutetea ubingwa wake siku moja baada ya kwanza ya michuano hiyo kwa kuumana na Rwanda 'Amavubi' kwenye Uwanja wa Taifa.

Jailan, Matimbwa kuonyeshana kazi Morogoro

BONDIA mahiri wa ngumi za kulipwa wa mkoa wa Morogoro, Mohamed Jeilani anatarajiwa kupanda ulingoni kuonyeshana ubabe na Mohammed Matimbwa wa Dar katika pambano lisilo la mkanda litakalofanyika siku ya Desemba 3, mjini Morogoro.
Pambano hilo la raundi nane litafanyika kwenye ukumbi wa Urafiki na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Mkurugenzi wa kampuni ya BS Promotion, waandaaji wa pambano hilo, Daudi Julian aliiambia MICHARAZO kwamba mchezo huo ni wa uzani wa kilo 60 na lengo lake ni kuhamamisha mchezo wa ngumi mkoani humo.
Julian, alisema maandalizi ya pambano hilo na michezo yote ya utangulizi yanaendelea vema na tayari mabondia wote watakaopigana siku hiyo wanaendelea kujifua kujiweka tayari kuonyeshana kazi ulingoni.
Aliwataja mabondia watakaowasindikiza Jailan na Matimbwa siku ya pambano lao ni pamoja na Maneno William ‘Chipolopolo’, Nassib Msafiri ‘Ngumi Nondo’ na Said Idd ‘Simple Boy’ watachapana na mabondia kutoka Dar es Salaam na Tanga.
"Kampuni yetu imeandaa pambano la ngumi la kirafiki kati ya Mohammed Jailan dhidi ya Mohammed Matimbwa litakalofanyika Desemba 3 mwaka huu na kusindikizwa na michezo mingine kati ya mabondia wa Moro dhidi ya wale wa Dar na Tanga," alisema.
Alisema mbali ya pambano hilo, kampuni hiyo pia inatarajia kuandaa mapambano mengine ya ngumi , siku ya kusherehekea sikukuu ya X-mass ambapo mabondia wa mkoa wa Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma na Tanga wataonyeshana kazi.
Julian ametoa wito kwa wafadhili wa michezo kujitokeza na kudhamini mapambano mbalimbali yatakayoandaliwa na kampuni yake kwa lengo la kuhamasisha mchezo huo mkoani humo.

Mwisho

Banka afichua kilichompeleka JKT Ruvu



KIUNGO mahiri wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Mohammed Banka ametua JKT Ruvu akisema ni klabu aliyokuwa akiiota kwa muda mrefu kutokana na na kuwa na soka la kuvutia na lenye ushindani uwanjani.
Aidha amekanusha kuwahi kufanya mazungumzo na viongozi wa timu za Coastal Union na Moro United ili ajiunge navyo kama ilivyokuwa ikiripotiwa.
Akizungumza na MICHARAZO Banka, alisema tayari ameshamwaga wino wa kuichezea JKT kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara na amefurahi mno.
Banka, alisema soka la JKT ndilo lililomsukuma kujiunga akiamini namna ya uchezaji wa klabu hiyo na aina ya wachezaji anaoungana nao itamsaidia kurejea upya katika soka la Tanzania baada ya nusu msimu kuwa nje ya dimba kutokana na mzozo wake na Simba.
"Nimemwaga wino wa kuichezea JKT Ruvu, kikubwa kilichonivutia kujiunga na timu hii ni aina ya soka inalocheza na wachezaji iliyonayo, ni kati ya klabu nilizokuwa naota kuzichezea kwa vile ni timu yenye malengo na ushindani wa kweli dimbani," alisema Banka.
Alipoulizwa imekuwaje amezitosa Coastal Union na Moro United ambazo zimekuwa
zikijinasibu kumnyemelea, Banka, alisema zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari
hakuwahi kufuatwa na kiongozi yeyote wa timu hizo kuzungumza nao.
"Ndugu yangu sijawahi kufuatwa wala kuwasiliana japo kwa simu kuzungumza kuhusu
kujiunga na klabu hizo, zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba natakiwa nazo, ila JKT Ruvu kabla ya kujiunga nilishafanya nao mazoezi weakati duru la kwanza likielekea ukingoni," alisema Banka.
Banka, aliyewahi kuichezea Moro United na aliyekuwa mchezaji wa Simba kabla ya kuigomea klabu hiyo kumtoa kwa mkopo kwa klabu ya Villa Squad ni miongoni mwa wachezaji watano wapya waliongezwa katika klabu hiyo ya JKT Ruvu.
Wengine waliotua JKT Ruvu ni George Mketo na Paul Ngahyoma toka Kagera, Said Hamis toka Polisi Morogoro na Bakar Kondo aliyerejeshwa kikosini.

Mwisho

Bondia Moro amtaka Miyeyusho

BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa mkoani Morogoro, Maneno William 'Chipolopolo' ameibuka na kudai anamtaka bingwa wa UBO-Mabara, Francis Miyeyusho wa Dar es Salaam, ili apigane nae.
Chipolopolo aliyejipatia umaarufu mkubwa mkoani humo, kutokana na uwezo wake wa kurusha makonde makali ulingoni, hivi sasa yuko katika mazoezi makali chini ya mwalimu Boma Kilangi.
Akizungumza na blog hii kutoka Morogoro, bondia huyo alisema amejipanga vizuri kufanya maajabu katika mchezo wa ngumi huku kiu yake kubwa ikiwa ni kuchapana na Miyeyusho maarufu kama 'Chichi Mawe'.
Chipolpolo, alisema anamuona Miyeyusho ni bondia wa kawaida na kwamba atapigika kirahisi licha ya kufanya vizuri katika mchezo huo katika siku za hivi karibuni.
Alisema, ili kutimiza dhamira yake yupo tayari kupanda ulingoni wakati wowote kuzipiga na Miyeyusho kama atatokea promota wa kuwaandalia pambano hilo.
Bondia huyo wa Morogoro alisema licha ya Miyeyusho kumchapa Mbwana Matumla hivi karibuni katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam, ni lakini kwake lazima apate kipigo.
"Nipo fiti, najiamini na nafikiri sasa ni wakati wa kuchapana na Miyeyusho na kizuri zaidi ni bondia wa uzito wangu," alisema.
Chipolopolo alisema hachagui mahali pa kupambana na bondia huyo na kwamba yupo tayari kuvaana naye hata jijini Dar es Salaam.
MIcharazo lilijaribu kumsaka Miyeyusho kwa njia ya simu kupata maoni yake juu ya tambo za bondia huyo wa Morogoro, lakini hakuweza kupatikana.

Mwisho