STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 10, 2013

Super Nyamwela: Dansa aliyeamua kuwakomboa wenzake Bongo

Super Nyamwela katika pozi
UZOEFU alionao katika fani ya uenguaji akiwa mmoja wa madansa wakongwe, Hassan Mussa Mohammed 'Super Nyamwela' umemfanya kutambua tamu na chungu za fani hiyo nchini.
Kufahamu kwake faraja na madhira katika fani hiyo ndiko kulikomfanya Nyamwela kuamua kushirikiana na wasanii wenzake kuasisi Chama cha Madansa ambacho yeye ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mnenguaji kiongozi huyo wa bendi ya Extra Bongo anasema udhalilishaji na dhuluma ambazo wamekuwa wakifanyiwa madansa ndio kilichomfanya hata aamue kutafuta namna ya kuasisi chama hicho ili kutafuta ukombozi.
"Licha ya mchango mkubwa wa madansa katika mabendi, matangazo ya biashara na mambo mengine, lakini hawathaminiki na hata wanapopatwa na matatizo hutelekezwa, kitu ambacho kinasikitisha sana," anasema.
Nyamwela ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya SN Stars Entertainment, anasema hata wanapofikwa na maradhi au vifo, baadhi ya madansa huzikwa tofauti na wasanii wengine wanaopewa heshima na hadhi ndani ya jamii.
"Tumeamua kuunda umoja na chama hiki ambacho mpaka sasa kwa jijini Dar tuna wanachama zaidi ya 400, na tunaamini muda ukizidi kusonga mbele idadi itaongezeka kwani uitikiaji umekuwa mkubwa mno," anasema.
Chama hicho kinachokaribia kufikisha muda wamiezi sita, licha ya kufanana na baadhi ya vyama vya nyuma kama TDMA na TDDA kilichokuwa chini ya dansa Mc Cool, Nyamwela anasema chao kipo tofauti kiutendaji na malengo.
Anasema kwa waliohudhuria mazishi ya mmenguaji wa zamani wa Twanga Pepeta na Extra Bongo, Mwantumu Athuman wanaweza kuona utofauti huo kwa namna madansa walivyoshirikiana mwanzo mwisho kumzika mwenzao.
"Ilikuwa inaumiza watu wa Bongo Movie au Bongofleva na wasanii wengine wanazikana na kusaidiana kwa shida na raha, madansa haikuwa hivyo kiasi kwamba wapo madansa wengine waliozikwa bila kujulikana," anasema.
Nyamwela anasema chama chao ni kama vyama vya kuzika na kuzikana na kubwa kuhakikisha kinatetea haki na masilahi ya wanenguaji bila kujali yupo kundi gani na jinsia ipi, cha muhimu awe mwanachama wao ili wamtambue.

Mkali
Nyamwela anayetajwa kama Mwalimu wa Madansa kutokana na asilimia kubwa ya wanenguaji wanaotamba nchini wamepitia mikononi mwake au kuiga uchezaji, licha ya umri kumtupa mkono bado anaonekana moto.
Mwenyewe anafichua siri ya kuendelea kutisha nchini wakati madansa alioanza nao fani hiyo baadhi kutoweka inatokana na kupenda kwake kufanya  mazoezi na kujituma bila kuchoka akiendelea kukimbiza na 'damu changa'.
Pia kutambua sanaa ndiyo iliyomfikisha hapo alipo akiwa na mjengo wake wa kisasa, kumiliki usafiri na maduka kadhaa pamoja na kundi lake la madansa, ndiko kunakomfanya azidi kukomaa na kuiheshimu fani hiyo daima.
Jina la msanii huyu lilianza kufahamika miaka ya mwanzoni ya 1990 wakati mchezo wa Disko ulipokuwa juu kwa kushiriki mashindano mbalimbali na kunyakua mataji kadhaa hasa katika miondoko ya Bolingo.
Moja ya mataji aliyonyakua mkali huyo mwenye mke na watoto kadhaa kwa sasa ni lile na Bingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyotwaa mwaka 1998 kabla ya kuungana na madansa wengine kuunda kundi la Top Family.
Kundi hilo lililotamba kwenye ukumbi wa 'Kwa Macheni' kisha kuwenda kuasisi kundi la Billbums na baadaye mwaka 2000 kutua African Stars 'Twanga Pepeta' aliokaa nao kwa miaka 10 mfululizo akijijengea jina kubwa.
Hata hivyo mapema mwaka juzi mnenguaji huyo aliamua kulitema kundi hilo la Twanga Pepeta na kutua Extra Bongo sambamba na wasanii wengine na kuendeleza libeneke lake kama kawaida akiwa hana mpinzani.
Anaimba vilevile
Mafanikio
Nyamwela anayependa kula chukula na kinywaji halali vinavyolinda siha na afya yake anakiri sanaa imemsaidia kwa mengi ukiacha ya kiuchumi na kumpa jina kubwa, lakini pia amekuwa akisafiri sehemu mbalimbali duniani.
"Kama siyo sanaa pengine nisingefika katika nchi ambazo sikuwahi hata kuziota kwenda kama Namibia, Botswana, Afrika Kusini, Liberia, Finland na kwingineko. Ila unenguaji umenifikisha huko kwa nini nisiheshimu fani hii?"
Mkali huyo anayesikitishwa na tukio la kuunguliwa kwa nyumba yake iliyopo Mbezi Beach pamoja na kumpoteza aliyekuwa mama wa watoto wake, Halima White, anasema amejipanga anapanua miradi yake ya biashara na kundi lake.
Anasema anataka kundi lake la SN linakuwa la kimataifa kwa kutoa mafunzo kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuhakikisha linajikita katika kuandaa matamsha mbalimbali ya sanaa.
Nyamwela ambaye kwa sasa pia ni muimbaji na mpiga tumba, anasema angetamani kuona disko likirejesha hadhi yake kama zamani ambapo kuliko na mashindano karibu kila mara na kukomesha madansa kucheza uchochoroni.
Akionyesha manjonjo yake barani Ulaya
Albamu
Nyamwela anayemshukuru Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka kwa namna alivyoweza kumsaidia kufika hapo alipo tangu alipokuwa chini ya bendi yake ya Twanga Pepeta, kwa sasa yu mbioni kufyatua albamu yake ya tatu.
Kabla ya kuanza maandalizi ya albamu hiyo ambayo imeshatambulishwa na nyimbo kadhaa kama 'Tumechete' na 'Duveleduvele', mkali huyo alishatoa albamu nyingine mbili za 'Master of the Tample' na 'Afrika Kilomondo'.
Katika albamu zote hizo Nyamwela alifyatua nyimbo zake kwa kushirikiana na wasanii wenye majina makubwa kama akina Ally Choki, Richard Maalifa, Sir Juma Nature na Amin na sasa anajiandaa kutoa wimbo na Prince Dully Sykes.
Nyamwela anayemwagia sifa Ally Choki kwa msaada mkubwa aliomfanyia tangu aanze kufahamiana naye mpaka kuwa katika bendi moja, alizaliwa zaidi ya miaka 30 iliyopita mjini Ruvuma kabla yua kuhamia Zanzibar kusoma.
Akiwa visiwani humo akisoma Shule ya Msingi Mji Mkongwe ndiko alikoanza fani ya muziki akinengua na kujitosa jumla mwaka 1997 na tangu wakati huo mpaka sasa anaendelea kunengua huku akishughulika na kazi zake binafsi.

Tanzanite. Wasauzi wavuna Mil 5 Taifa

PAMBANO la soka kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) lililochezwa jana (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 5,353,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 816,559.32, gharama za kuchapa tiketi sh. 1,649,754, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 577,573) wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 433,003.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,732,012.01.

Mechi iliyopita ya Tanzanite dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na timu hiyo kushinda mabao 10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na kuingiza sh. 6,190,000.

Tanzanite na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba 20 na 22 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Timu zipi kutinga 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Juve inayohitaji ushindi ili kutinga 16 Bora
MECHI za hatua ya mwisho za makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zinatarajiwa kuanza kuchezwa leo na kumalizika kesho ili kujua timu za mwisho za kuingia hatua ya 16 Bora ya ligi hiyo maarufu duniani.
Mpaka sasa ni timu nane tu kati ya 16 zilizojihakikishia hatua hiyo ya mtoano kuwania Robo Fainali, huku nane nyingine zikitarajiwa kujulikana leo na kesho baada ya mechi zao za kufungia makundi yao.
Mabingwa watetezi, Bayern Munich, Chelsea, Manchester City, Manchester United, Real Madrid, Paris St-Germain, Barcelona, na Atletico Madrid.zenyewe tayari zimeshatangulia mapema katika hatua hiyo, huku
Arsenal ikiwa inaonekana kutinga japo bado inatishwa na wapinzani wake, Napoli anaocheza nao na Borussia Dotmund zenye pointi 9, tatu pungu na ilizonazo wao wenyewe 12.
Vigogo vinavyohitajika kutoka jasho ili kutinga hatua hiyo ya mtoano ni pamoja na Juventus na AC Milan, japo zinaonekana zina nafasi kubwa ya kufuzu hatua hiyo inayofuata.


Robin van Persie anatarajia kucheza mechi hii wakati United watakapominyana na Shakhtar Donetsk

RATIBA ILIVYO
LEO Jumanne Des 10, 2013
Manchester United FC v FC Shakhtar Donetsk
Real Sociedad de Fútbol v Bayer 04 Leverkusen
Galatasaray v A.Ş. Juventus
FC København v Real Madrid CF
SL Benfica v Paris Saint-Germain
Olympiacos v FC RSC Anderlecht
FC Bayern München v Manchester City FC

Viktoria Plzeň v PFC CSKA Moskva

KESHO Jumatano Des 11, 2013
FC Schalke 04 v FC Basel 1893
Chelsea FC v FC Steaua Bucureşti
Olympique de Marseille v Borussia Dortmund
Napoli v Arsenal FC
FK Austria Wien v Football Club Zenit
Club Atlético de Madrid v FC Porto
AC Milan v AFC Ajax
FC Barcelona v Celtic Fc

Rais Kikwete awasili Afrika Kusini kumuaga Mandela

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amewasili nchini Afrika Kusini usiku wa kuamkia leo  Desemba 10, 2013 tayari kuhudhuria maziko ya Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mzee Nelson R. Mandela.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya serilai, Ibada Kuu ya kumwombea Marehemu itafanyika leo Desemba 10, 2013 katika Uwanja wa FNB Johannesburg, ambapo viongozi na watu mashuhuri mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia wataungana na wananchi wa Afrika Kusini katika shughuli hiyo ya kihistoria. 
Kesho Novemba 11 hadi Novemba 13, 2013 mwili wa marehemu utakuwepo katika jengo la Union Building ambapo viongozi na watu mashuhuri watatoa heshima zao za mwisho. Jengo hilo ni kama Ikulu ya nchi hiyo.
Maziko yatafanyika Desemba 15, 2013 katika kijiji cha Qunu, Mthatha, Easter Cape
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa katika uwanja wa ndege wa Waterkloof Airforce Base ulioko Kusini mwa jiji la Pretoria alikowasili usiku wa kuamkia leo tayari kuhudhuria mazishi ya Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mzee Nelson R. Mandela.
Rais Kikwete akisalimiana na Mwambata wa Kijeshi katika Ubalozi wa Tanzania Afrika kusini katika uwanja wa ndege wa Waterkloof Airforce Base ulioko Kusini mwa jiji la Pretoria
Rais Kikwete akisindikizwa kuelekea kwenye gari baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Waterkloof Airforce Base ulioko Kusini mwa jiji la Pretoria . Nyuma yake mwenye ushungi kichwani ni Mama Salma Kikwete
Rais Kikwete akisindikizwa kuelekea kwenye gari baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Waterkloof Airforce Base ulioko Kusini mwa jiji la Pretoria . Nyuma yake kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM Ndg Abdurahman Kinana. 
PICHA NA IKULU

Allain Kamote ampiga Deo Samuel; kwa Pointi

Bondia Alan Kamote (kulia) akimshambulia Deo Samweli wakati wa mpambano wao uliofanyika Manzese Dar es salaam kamote alishinda kwa pointi


Bondia Alan Kamote kulia akipambana na Deo Samweli wakati wa mpambano wao uliofanyika Manzese Dar es salaam kamote alishinda kwa pointi.

Ribery, Messi, Ronaldo uso kwa uso 3 Bora ya Ballon d'Or

Ribery anayejaribu bahati yake mwaka huu

'Mfalme' anayeshikilia tuzo hiyo mara nne

Ronaldo akiwa na tuzo ya FIFA ya 2008

Bern, Uswisi
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limewatangaza rasmi Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Franck Ribery kuwa nyota watatu waliobaki kati ya 10 watakaowania Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia (Ballon d'Or 2013) jana.
Mshambuliaji wa Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Messi ameibuka kidedea katika tuzo hiyo, ambayo awali ilikuwa ikiitwa Tuzo ya Fifa ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia, kwa miaka minne mfululizo, wakati mshambuliaji wa Real Madrid, Ronaldo aliitwaa kwa mara ya mwisho katika kura za mwaka 2008.
Licha ya kutotwaa taji lolote kubwa msimu uliopita, Mreno Ronaldo anapewa nafasi kubwa ya kuhitimisha rasmi utawala wa Messi wa kuwa mwanasoka bora wa dunia wakati matokeo yatakapotangazwa Januari 13, mwakani.
Nyota huyo mwenye miaka 28 ameifungia Real Madrid mabao 25 msimu huu na pia alifunga 'hat-trick' ya kusisimua wakati Ureno ikiifunga Sweden katika mechi yao ya mtoano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Messi aliifungia Barcelona mabao 56 msimu uliopita, akiisaidia Barca kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania wakati Ribery akiisaidia Bayern Munich kutwaa taji la Bundesliga (Ligi Kuu ya Ujerumani), Kombe la Ligi na taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson, Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynkes na Kocha wa Borussia Dortmund, Juergen Klopp wameingia katika nafasi tatu bora 'top 3' ya vinara wanaowania Tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka wa Dunia.
Mshambuliaji wa Paris St Germain na timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic alishindwa kuingia katika 'top 3' ya wanaowania Ballon d'Or ingawa anafukuzia tuzo ya Puskas inayotolewa kwa mfungaji wa "bao zuri zaidi la mwaka" kutokana na bao la mbali la 'tik-taka' alilofunga dhidi ya England.
Wote waliongia katika fainali ya kuwania tuzo mbalimbali walithibitishwa baada ya kura kupigwa na manahodha na makocha wa timu za taifa kutoka nchi zote wanachama wa Fifa na wawakilishi wa vyombo vya habari wanaoteuliwa pia na Fifa na jarida la soka la Ufaransa.

Kili Stars kufa ama kupona leo kwa Wakenya


Kili Stars inayotegemewa kuwatoa kimasomaso watanzania
Na Somoe Ng'itu, Nairobi
WKATI timu ya soka ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), ikitarajia kushuka dimbani leo kuikabili Kenya (Harambaee Stars) katika mechi ya hatua ya nusu fainali, Watanzania wanachotaka kukiona ni ikiwachakaza wenyeji hao na kusonga mbele hatua ya fainali.
Mchezo huo utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Kenyata uliopo mjini Machakos.
Kilimanjaro Stars imefika hatua hiyo baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa penalti 3-2 katika mechi ya hatua ya robo fainali wakati wenyeji Harambee Stars waliiondoa Rwanda (Amavubi) kwa ushindi wa bao 1-0.
Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen, alisema mjini hapa jana, mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu kuliko zilizopita kwa sababu anacheza na mwenyeji wa mashindano haya ya Kombe la Chalenji.
Poulsen alisema amewaandaa wachezaji wake kuikabili Harambee Stars na kuwa makini na mwamuzi ili kuepuka wenyeji kubebwa.
Alisema mechi hiyo pia huenda ikawa nyepesi kiufundi kutokana na wenyeji kuingiwa na presha ya kutaka kushinda ili wasonge mbele.
"Ni mechi nyingine ngumu ambayo tutaingia uwanjani kucheza, naamini kama wataendeleza kasi yao waliyoionyesha katika mechi dhidi ya Uganda, tunatarajia matokeo mazuri, kikubwa ni kuwa makini na kujiandaa kukutana na changamoto za aina yoyote uwanjani, " alisema Kim.
Kocha huyo aliongeza kuwa, licha ya kumkosa kiungo, Salum Aboubakar 'Sure Boy' katika mechi ya leo, anaamini mchezaji atakayempanga ataitendea haki nafasi hiyo ya kiungo kwenye timu.
"Siwezi kukwambia nani ataziba pengo la Sure Boy, kila mchezaji yuko tayari kupambana, tuna safari ngumu mwakani ya mechi za AFCON," Kim alisema.
Naye Kocha Mkuu wa Harambee Stars, Mbelgiji, Adel Amrouche, alisema anakutana na Tanzania kwa mara ya kwanza na ameiona inaundwa na wachezaji wenye vipaji.
Amrouche alisema mechi zote za hatua ya mtoano huwa na ushindani wa hali ya juu kwa sababu ni lazima mshindi apatikane ili asonge mbele.
"Ni timu nzuri na inayoonyesha imejipanga, napenda wanavyocheza na najua mechi yetu itakuwa na ushindani, si mechi rahisi," aliongeza kocha huyo.
Kilimanjaro Stars na Harambee zilisafiri kwa ndege tangu juzi jioni kutoka mjini Mombasa na kurejea Nairobi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.
Mechi nyingine ya hatua ya nusu fainali inayotarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Manispaa ya mjini Mombasa ni kati ya Zambia dhidi ya Sudan.
Timu zitakazoshinda leo zitafuzu kucheza fainali ya mashindano ya mwaka huu yatakayofanyika keshokutwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Nyayo na wale watakaopoteza watawania nafasi ya tatu.

Ngasa aleta matumaini
Winga wa Tanzania Bara, Mrisho Ngasa, amesema wachezaji wote leo wamejipanga kucheza kufa au kupona ili kusaka ushindi na kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la Chalenji, hata hivyo Ngasa ambaye aliumia enka na kutolewa nje katika mechi ya robo fainali dakika 10 kabla ya mechi haijamalizika anaendelea vizuri.
Alisema maumivu ya enka yamebaki kwa mbali na anamuomba Mungu leo aamke vyema.
Ngasa aliifungia Kilimanjaro Stars mabao mawili katika mchezo dhidi ya Uganda (The Cranes) katika dakika ya 90 za awali huku Kelvin Yondani, Athumani Iddi 'Chuji' na Amri Kiemba wakiipa ushindi baada ya kuingia hatua ya matuta.
Ngasa alisema kuwa kazi ya kwanza ilikuwa ni kuiondoa Uganda na sasa wamejipanga kuendeleza kasi waliyoionyesha.
"Tunajua nao Kenya watashuka dimbani wakiamini wanaweza, sisi tutashuka uwanjani tukisema tunaenda kupambana," alisema.

NIPASHE

Mashetani yapo kwa Easy Man

Easy Man

MFALME wa miondoko ya mchiriku nchini, Is'haka Saleh ' Easy Man', amefyatua wimbo mpya uitwao Mashetani anaotarajia kuachia hewani wiki  ijayo.
Akizungumza na MICHARZO, Easy Man aliyefunika kupitia wimbo wake wa 'Kasoro Wewe', alisema wimbo huo ni wa tatu kwake kuurekodi, mwingine ukiwa ni 'Nimpende Nani' aliouachia kwenye mitandao ya kijamii tu.
Easy Man alisema wimbo huo ameurekodia katika studio za Natal na ....... amepanga kuutoa mapema kabla ya sikukuu ya Krismasi kuwapa ladha mashabiki wa muziki wa kizazi kipya ambao wamekosa burudani toka kwake.
"Baada ya kuwaonjesha kupitia mitandao ya kijamii kwa wimbo wa 'Nimpende Nani' nimekamilisha kibao kipya kiitwacho 'Mashetani' ambacho nitakitambulisha katika vituo vya redio kama 'Kasoro Wewe'," alisema.
Msanii huyo anayefanya kazi chini ya lebo la Mkubwa na Wanae, alisema wimbo huo kama nyimbo zake nyingine zote ameujimba pekee yake bila kumshirikisha mtu na upo katika miondoko ya mchiriku.