STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 10, 2013

Super Nyamwela: Dansa aliyeamua kuwakomboa wenzake Bongo

Super Nyamwela katika pozi
UZOEFU alionao katika fani ya uenguaji akiwa mmoja wa madansa wakongwe, Hassan Mussa Mohammed 'Super Nyamwela' umemfanya kutambua tamu na chungu za fani hiyo nchini.
Kufahamu kwake faraja na madhira katika fani hiyo ndiko kulikomfanya Nyamwela kuamua kushirikiana na wasanii wenzake kuasisi Chama cha Madansa ambacho yeye ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mnenguaji kiongozi huyo wa bendi ya Extra Bongo anasema udhalilishaji na dhuluma ambazo wamekuwa wakifanyiwa madansa ndio kilichomfanya hata aamue kutafuta namna ya kuasisi chama hicho ili kutafuta ukombozi.
"Licha ya mchango mkubwa wa madansa katika mabendi, matangazo ya biashara na mambo mengine, lakini hawathaminiki na hata wanapopatwa na matatizo hutelekezwa, kitu ambacho kinasikitisha sana," anasema.
Nyamwela ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya SN Stars Entertainment, anasema hata wanapofikwa na maradhi au vifo, baadhi ya madansa huzikwa tofauti na wasanii wengine wanaopewa heshima na hadhi ndani ya jamii.
"Tumeamua kuunda umoja na chama hiki ambacho mpaka sasa kwa jijini Dar tuna wanachama zaidi ya 400, na tunaamini muda ukizidi kusonga mbele idadi itaongezeka kwani uitikiaji umekuwa mkubwa mno," anasema.
Chama hicho kinachokaribia kufikisha muda wamiezi sita, licha ya kufanana na baadhi ya vyama vya nyuma kama TDMA na TDDA kilichokuwa chini ya dansa Mc Cool, Nyamwela anasema chao kipo tofauti kiutendaji na malengo.
Anasema kwa waliohudhuria mazishi ya mmenguaji wa zamani wa Twanga Pepeta na Extra Bongo, Mwantumu Athuman wanaweza kuona utofauti huo kwa namna madansa walivyoshirikiana mwanzo mwisho kumzika mwenzao.
"Ilikuwa inaumiza watu wa Bongo Movie au Bongofleva na wasanii wengine wanazikana na kusaidiana kwa shida na raha, madansa haikuwa hivyo kiasi kwamba wapo madansa wengine waliozikwa bila kujulikana," anasema.
Nyamwela anasema chama chao ni kama vyama vya kuzika na kuzikana na kubwa kuhakikisha kinatetea haki na masilahi ya wanenguaji bila kujali yupo kundi gani na jinsia ipi, cha muhimu awe mwanachama wao ili wamtambue.

Mkali
Nyamwela anayetajwa kama Mwalimu wa Madansa kutokana na asilimia kubwa ya wanenguaji wanaotamba nchini wamepitia mikononi mwake au kuiga uchezaji, licha ya umri kumtupa mkono bado anaonekana moto.
Mwenyewe anafichua siri ya kuendelea kutisha nchini wakati madansa alioanza nao fani hiyo baadhi kutoweka inatokana na kupenda kwake kufanya  mazoezi na kujituma bila kuchoka akiendelea kukimbiza na 'damu changa'.
Pia kutambua sanaa ndiyo iliyomfikisha hapo alipo akiwa na mjengo wake wa kisasa, kumiliki usafiri na maduka kadhaa pamoja na kundi lake la madansa, ndiko kunakomfanya azidi kukomaa na kuiheshimu fani hiyo daima.
Jina la msanii huyu lilianza kufahamika miaka ya mwanzoni ya 1990 wakati mchezo wa Disko ulipokuwa juu kwa kushiriki mashindano mbalimbali na kunyakua mataji kadhaa hasa katika miondoko ya Bolingo.
Moja ya mataji aliyonyakua mkali huyo mwenye mke na watoto kadhaa kwa sasa ni lile na Bingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyotwaa mwaka 1998 kabla ya kuungana na madansa wengine kuunda kundi la Top Family.
Kundi hilo lililotamba kwenye ukumbi wa 'Kwa Macheni' kisha kuwenda kuasisi kundi la Billbums na baadaye mwaka 2000 kutua African Stars 'Twanga Pepeta' aliokaa nao kwa miaka 10 mfululizo akijijengea jina kubwa.
Hata hivyo mapema mwaka juzi mnenguaji huyo aliamua kulitema kundi hilo la Twanga Pepeta na kutua Extra Bongo sambamba na wasanii wengine na kuendeleza libeneke lake kama kawaida akiwa hana mpinzani.
Anaimba vilevile
Mafanikio
Nyamwela anayependa kula chukula na kinywaji halali vinavyolinda siha na afya yake anakiri sanaa imemsaidia kwa mengi ukiacha ya kiuchumi na kumpa jina kubwa, lakini pia amekuwa akisafiri sehemu mbalimbali duniani.
"Kama siyo sanaa pengine nisingefika katika nchi ambazo sikuwahi hata kuziota kwenda kama Namibia, Botswana, Afrika Kusini, Liberia, Finland na kwingineko. Ila unenguaji umenifikisha huko kwa nini nisiheshimu fani hii?"
Mkali huyo anayesikitishwa na tukio la kuunguliwa kwa nyumba yake iliyopo Mbezi Beach pamoja na kumpoteza aliyekuwa mama wa watoto wake, Halima White, anasema amejipanga anapanua miradi yake ya biashara na kundi lake.
Anasema anataka kundi lake la SN linakuwa la kimataifa kwa kutoa mafunzo kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuhakikisha linajikita katika kuandaa matamsha mbalimbali ya sanaa.
Nyamwela ambaye kwa sasa pia ni muimbaji na mpiga tumba, anasema angetamani kuona disko likirejesha hadhi yake kama zamani ambapo kuliko na mashindano karibu kila mara na kukomesha madansa kucheza uchochoroni.
Akionyesha manjonjo yake barani Ulaya
Albamu
Nyamwela anayemshukuru Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka kwa namna alivyoweza kumsaidia kufika hapo alipo tangu alipokuwa chini ya bendi yake ya Twanga Pepeta, kwa sasa yu mbioni kufyatua albamu yake ya tatu.
Kabla ya kuanza maandalizi ya albamu hiyo ambayo imeshatambulishwa na nyimbo kadhaa kama 'Tumechete' na 'Duveleduvele', mkali huyo alishatoa albamu nyingine mbili za 'Master of the Tample' na 'Afrika Kilomondo'.
Katika albamu zote hizo Nyamwela alifyatua nyimbo zake kwa kushirikiana na wasanii wenye majina makubwa kama akina Ally Choki, Richard Maalifa, Sir Juma Nature na Amin na sasa anajiandaa kutoa wimbo na Prince Dully Sykes.
Nyamwela anayemwagia sifa Ally Choki kwa msaada mkubwa aliomfanyia tangu aanze kufahamiana naye mpaka kuwa katika bendi moja, alizaliwa zaidi ya miaka 30 iliyopita mjini Ruvuma kabla yua kuhamia Zanzibar kusoma.
Akiwa visiwani humo akisoma Shule ya Msingi Mji Mkongwe ndiko alikoanza fani ya muziki akinengua na kujitosa jumla mwaka 1997 na tangu wakati huo mpaka sasa anaendelea kunengua huku akishughulika na kazi zake binafsi.

No comments:

Post a Comment