STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 10, 2013

Kili Stars kufa ama kupona leo kwa Wakenya


Kili Stars inayotegemewa kuwatoa kimasomaso watanzania
Na Somoe Ng'itu, Nairobi
WKATI timu ya soka ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), ikitarajia kushuka dimbani leo kuikabili Kenya (Harambaee Stars) katika mechi ya hatua ya nusu fainali, Watanzania wanachotaka kukiona ni ikiwachakaza wenyeji hao na kusonga mbele hatua ya fainali.
Mchezo huo utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Kenyata uliopo mjini Machakos.
Kilimanjaro Stars imefika hatua hiyo baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa penalti 3-2 katika mechi ya hatua ya robo fainali wakati wenyeji Harambee Stars waliiondoa Rwanda (Amavubi) kwa ushindi wa bao 1-0.
Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen, alisema mjini hapa jana, mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu kuliko zilizopita kwa sababu anacheza na mwenyeji wa mashindano haya ya Kombe la Chalenji.
Poulsen alisema amewaandaa wachezaji wake kuikabili Harambee Stars na kuwa makini na mwamuzi ili kuepuka wenyeji kubebwa.
Alisema mechi hiyo pia huenda ikawa nyepesi kiufundi kutokana na wenyeji kuingiwa na presha ya kutaka kushinda ili wasonge mbele.
"Ni mechi nyingine ngumu ambayo tutaingia uwanjani kucheza, naamini kama wataendeleza kasi yao waliyoionyesha katika mechi dhidi ya Uganda, tunatarajia matokeo mazuri, kikubwa ni kuwa makini na kujiandaa kukutana na changamoto za aina yoyote uwanjani, " alisema Kim.
Kocha huyo aliongeza kuwa, licha ya kumkosa kiungo, Salum Aboubakar 'Sure Boy' katika mechi ya leo, anaamini mchezaji atakayempanga ataitendea haki nafasi hiyo ya kiungo kwenye timu.
"Siwezi kukwambia nani ataziba pengo la Sure Boy, kila mchezaji yuko tayari kupambana, tuna safari ngumu mwakani ya mechi za AFCON," Kim alisema.
Naye Kocha Mkuu wa Harambee Stars, Mbelgiji, Adel Amrouche, alisema anakutana na Tanzania kwa mara ya kwanza na ameiona inaundwa na wachezaji wenye vipaji.
Amrouche alisema mechi zote za hatua ya mtoano huwa na ushindani wa hali ya juu kwa sababu ni lazima mshindi apatikane ili asonge mbele.
"Ni timu nzuri na inayoonyesha imejipanga, napenda wanavyocheza na najua mechi yetu itakuwa na ushindani, si mechi rahisi," aliongeza kocha huyo.
Kilimanjaro Stars na Harambee zilisafiri kwa ndege tangu juzi jioni kutoka mjini Mombasa na kurejea Nairobi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.
Mechi nyingine ya hatua ya nusu fainali inayotarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Manispaa ya mjini Mombasa ni kati ya Zambia dhidi ya Sudan.
Timu zitakazoshinda leo zitafuzu kucheza fainali ya mashindano ya mwaka huu yatakayofanyika keshokutwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Nyayo na wale watakaopoteza watawania nafasi ya tatu.

Ngasa aleta matumaini
Winga wa Tanzania Bara, Mrisho Ngasa, amesema wachezaji wote leo wamejipanga kucheza kufa au kupona ili kusaka ushindi na kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la Chalenji, hata hivyo Ngasa ambaye aliumia enka na kutolewa nje katika mechi ya robo fainali dakika 10 kabla ya mechi haijamalizika anaendelea vizuri.
Alisema maumivu ya enka yamebaki kwa mbali na anamuomba Mungu leo aamke vyema.
Ngasa aliifungia Kilimanjaro Stars mabao mawili katika mchezo dhidi ya Uganda (The Cranes) katika dakika ya 90 za awali huku Kelvin Yondani, Athumani Iddi 'Chuji' na Amri Kiemba wakiipa ushindi baada ya kuingia hatua ya matuta.
Ngasa alisema kuwa kazi ya kwanza ilikuwa ni kuiondoa Uganda na sasa wamejipanga kuendeleza kasi waliyoionyesha.
"Tunajua nao Kenya watashuka dimbani wakiamini wanaweza, sisi tutashuka uwanjani tukisema tunaenda kupambana," alisema.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment