STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 12, 2014

Simba, KCC hapatoshi kesho Fainali Kombe la Mapinduzi

kikosi cha Simba
KCC ya Uganda
 KIVUMBI cha michuano ya Kombe la Mapinduzi kinatarajiwa kumalizika kesho kwa pambano la Fainali kati ya Simba dhidi ya KCC ya Uganda litakalochezwa jioni kwenye uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
Simba inaivaa KCC baada ya kuitoa nishai URA pia ya Uganda kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mganda Joseph Owino, aliyekuwa akiichezea timu hiyo kabla ya kurejea Msimbazi na lile la Amri Kiemba.
KCC wenyewe waliwavua ubingwa Azam kwa kuwakandika mabao 3-2, licha ya kutanguliwa kufungwa 2-1 hadi wakati wa mapumziko.
Simba iliyowahi kunyakua taji hilo miaka miwili iliyopita, itakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha Kombe hilo halichukuliwi na wageni kwani tangu ilipoanzishwa michuano hiyo taji hilo halijawahi kutoka nje ya Tanzania.
Ikiwa chini ya kocha Zdrakov Lugarosic, Simba itaendelea kuwategemea wachezaji wake nyota Ramadhani Singano, Harun Chanongo, Amri Kiemba na golini atakuwa Ivo Mapunda kuhakikisha KCC hawafuruki katika mchezo huo wa fainali unaotarajiwa kuhudhuriw ana viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wale wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikizingatiwa kesho ni mapumziko kitaifa.
KCC ambayo haikuwa ikipewa nafasi kubwa, kabla ya kuja kuongoza kundi A walilokuwa na Simba katika mechi za awali siyo timu ya kubeza kwani imetoa upinzani mkubwa ikiwa haijafungwa mchezo wowote kama wapinzani wao ambao wana nyongeza ya rekodi ya kutoruhusu bao lolote langoni mwao mpaka sasa.
Timu huyo ya Jiji la Kampala inawategemea wachezaji wake kadaa nyota kama Ibrahim Kiiza na wengine ambao waliisimamisha Azam na kuwavua taji katika mechi ya Nusu Fainali ya kwanza juzi.
Uongozi wa Simba umenukuliwa jioni hii toka Zanzibar wakisema kikosi chao kipo imara tayari kuwapa raha Wazanzibar wanaosherehekea miaka 50 ya Mapinduzi na watanzania kwa ujumla ili kulibakisha taji hilo katika ardhi ya Tanzania kwa kuwazuia KCC wasiondoke nalo kama walivyofanya dada zao wa netiboli walioifunga timu ya taifa ya Tanzania kwenye fainali pia juzi.

Liverpool yatakata, Suarez nouma!

Liverpool's Steve Gerrard scores from the spot
Gerrard akitupia kambani bao la penati la Liverpool

LUIS Suarez ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kunyakua kiatu cha dhahabu cha Ufungaji Bora wa Ligi Kuu ya England baada ya muda mfupi uliopita kufunga mabao mawili na kufikisha mabao 22 wakati akisaidia Liverpool kupata ushindi mnono ugenini wa mabao 5-3 dhidi ya Stoke City.
Suarez alifunga mabao hayo katika dakika za 32 na 71, huku wachezaji waliokuwa majeruhi nahodha Steven Gerrard na Daniel Sturridge wakifunga bao moja moja, Gerrard akifunga kwa mkwaju wa penati, huku bao la kuongoza la Liverpool likifungwa na beki wa Stoke City, Ryan Shawcross dakika ya 5 tu ya mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Britannia.
Sturridge alifunga bao la tano dakika tatu kabla ya kumalizika kwa pambano hilo akitokea benchi, huku wenyeji wakipata mabao yao ya kufutia machozi kupitia kwa  Peter Crouch, Charlie Adam na Jonathan Walters.
Kwa ushindi huo Liverpool imefikisha jumla ya pointi 42 na kurejea kwenye nafasi ya nne ikiishusha Everton na Tottenham ambazo jana zilitakata na ushindi wa mabao mawili kila moja.

Zimbabwe yaibana Morocco CHAN 2014

http://upload.wikimedia.org/wikipedia/en/8/8d/2014_African_Nations_Championship.png
TIMU ya soka ya taifa ya Zimbabwe imefanikiwa kuvuna pointi moja mbele ya Morocco baada ya kutoka nayo suluhu ya kutofungana katika pambano la kundi B la Michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani iliyoanza jana nchini Afrika Kusini.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Athlone, mjini Cape Town lilikuwa la vuta nikuvute kwa muda wote wa dakika 90 na kushuhudiwa timu hizo zikikosa mabao ya wazi na kufanya matokeo kuwa 0-0.
Mechi nyingine ya kundi hilo inatarajiwa kuanza hivi punde kati ya Uganda The Cranes itakayoumana na Burkina Faso kwenye uwanja huo huo wa Athlone.
Kesho katika mfululizo wa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2008,  Ghana itaumana mapema na Congo kabla ya Libya kuvaana na Ethiopia katika mechi za Kundi C na mechi za raundi ya kwanza zitamalizika Jumanne kwa mechi za kundi D kati ya DR Congo dhidi ya Mauritania na Gabon kuumana na Burundi.

Juventus haikamatiki Seria A, Roma, Napoli nazo zaua Italia

TIMU ya Juventus imeendelea kujikita kileleni baada ya kupata ushindi ugenini dhidi ya Cagliari, huku Roma na Napoli nazo zikipata ushindi wa kishindo katika mechi zao za Seria A jioni ya leo.
Juventus kwa ushindi huo wa mabao 4-1 dhidi ya wenyeji wao imeifanya ifikishe pointi 52 na kufuatiwa na Roma  yenye 44 baada ya kushinda nyumbani mabao 4-0 dhidi ya Genoa na Napoli kushinda mabao 3-0 na kujikita nafasi ya tatu ikiwa na pointi 42.
Mechi nyingine za leo katika Seria A imeshuhudia Fiorentina ikipata sare ya 0-0 ugenini dhidi ya Torino na  Atalanta ikishinda nyumbani 2-1 dhidi ya Catania.

Manchester City yaiua Newcastle kwao, na kuing'oa Chelsea kileleni

Edin Dzeko akishangilia bao lake dhidi ya NewcastleBAO la mapema lililofungwa na Edin Dzeko katika dakika ya nane na jingine la dakika za lala salama kupitia kwa Alvaro Negredo yametosha kuipaisha Manchester City hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiiporomosha Chelsea iliyokwea nafasi hiyo jana.
City wakiwa ugenini kuifuata Newcastle United iliweza kupata mabao hayo na kuifanya ifikishe pointi 47, moja zaidi ya ilizonazo Chelsea iliyoibamiza Hull City nyumbani kwao kwa mabao 2-0.
Dzeko alifunga bao la kwanza akimalizia kazi nzuri ya beki wa pembeni wa City, Aleksandar Kalarov kabla ya Negredo kuwaduwaza wenyeji dakika za nyongeza kwa kufunga bao la pili na kuifanya City imalize mechi hiyo ikiwa vidume, ikiwa ni mechi yao ya sita mfululizo kushinda katika Ligi.
Hata hivyo vijana hao na Manuel Pelligrini wanaweza kusalia kwa muda tu kileleni hapo kama Arsena ambayo kesho itashuka dimbani itapata ushindi ugenini dhidi ya Aston Villa katika mechi pekee ya ligi hiyo.
Hivi punde pambano la Stoke City dhidi ya Liverpool litaanza kuchezwa katika mfululizo wa ligi hiyo.

Afrika Kusini, Mali waanza vyema CHAN 2014

Wachezaji wa Bafana Bafana wakishangilia ushindi wao jana dhidi ya Msumbiji

TIMU ya taifa ya Nigeria jana ilianza vibaya michuano ya CHAN baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Mali huku wenyeji wa michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika, ikipata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Msumbiji.
Katika mechi ya wenyeji iliyochezwa uwanja wa Cape Town, jijini Cape Town, Msumbiji iliwashtua wenyeji wao kwa kupata bao la kuongoza lililofungwa kwenye dakika ya 11 kupitia Diogo.
Bao hilo lilikuja kurejeshwa na Bernard Parker katika dakika ya 30 kwa mkwaju wa penati na kufanya hadi mapumziko timu hizo kuwa nguvu sawa  kwa bao 1-1.
Kipindi cha pili kilikuwa cha wenyeji baada ya kujipatia mabao mawili kupitia kwa Hlompho Kekana na Parker kwa mara nyingine tena na kufanya Afrika Kusini kuzoa pointi tatu na kuongoza kwenye kundi lake la A ikifuatiwa na Mali waliowazabua majirani zao Nigeria kwa mabao 2-1.
Mabao ya washindi yalifungwa na Abdoulaye Sissoko katika dakika ya 11 na Adama Troure la dakika ya 54 kabla ya Nigeria kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Fuad Salami.
Jioni hii kuna mechi nyingine mbili zinazoendelea ambako Zimbabwe na Morocco mpaka sasa hazijafunga zikikaribia kwenda mapumziko na mechi ya Uganda The Cranes na Burkina Faso itafanyika usiku na MICHARAZO itawaletea matokeo yake.

Tanzia! Nyota wa zamani wa Reli, Taifa Stars afariki


Boniface Njohole enzi za uhai wake (Picha: Mtanda Blogu)
MCHEZAJI wa zamani wa klabu ya Reli ya Morogoro na Taifa Stars, Boniface Njohole amefariki dunia katika kijiji cha Mngeta tarafa ya Ifakara wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkoani Morogoro Karibu Mtendaji wa chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) Hamis Semka alisema Njohole amefariki dunia katika kijiji cha Mngeta majira ya saa 5:30 asubuhi baada ya kuumwa kwa muda mrefu.
Hata hivyo taarifa zaidi zinasema kuwa Njohole aliyekuwa akifahamika kama Boni, alikuwa akisumbuliwa na matataizo ya Figo na alikuwa akitibiwa Moshi, kabla ya kurejeshwa nyumbani kwake Ifakara na kukutwa na mauti. 
Taarifa zaidi zinaendelea kufuatiliwa kujua mazishi na taratibu nyingine juu ya msiba wa mwanandinga huyo
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na wadau wote wa soka kwa msiba wa Boniface Njohole na kutakia moyo wa subira kwa kutambua kuwa Kila Nafsi Itaonja Mauti. Mungu Aiweke Roho ya Marehemu Mahali Pema. Ameen

TFF yamlilia Sultan Sikilo

Jeneza la Mwili wa Sultan Sikilo likiswaliwa kabla ya kwenda kuzikwa jana, jijini Dar es Salaam..
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mtangazaji wa michezo wa Radio Abood, Sultan Sikilo kilichotokea jana alfajiri (Januari 11) jijini Dar es Salaam.

Sikilo ambaye pia aliwahi kufanyia kazi Radio Times na Radio Kheri na hadi umauti unamkuta alikuwa Mweka Hazina Msaidizi wa Chama cha Waandishi wa habari za Michezo Tanzania (TASWA) amezikwa jana jioni katika makaburi ya Kibada, Kigamboni.

Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Sikilo alifanya kazi na TFF kwa kuripoti shughuli zetu nyingi za mpira wa miguu, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Sikilo, Radio Abood na TASWA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF imetoa ubani wa sh. 100,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Jamal Malinzi aanza vita dhidi ya dawa za kulevya katika soka

Rais wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza kwenye uzinduzi wa programu ya Ishi Huru
Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amezindua programu ya kutoa elimu ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana iitwayo Ishi Huru.
Programu hiyo iliyozimduliwa jana (Januari 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam iko chini ya taasisi ya Africa Inside Out inayoongozwa na Rebecca Young wakati washirika (partners) ni TFF na kampuni ya Rhino Resources ya Marekani.
Rais Malinzi amesema matumizi ya dawa za kulevya nchini yamekuwa yakiongezeka, hivyo kuwa kikwazo kwa maendeleo ya vijana ambapo ameipongeza Africa Inside Out kwa programu hiyo kwa vile itazuia vijana
wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo.
“Moja athari kubwa za matumizi ya dawa za kulevya ni kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na kuchangia sindano za kujidunga dawa hizo.
“TFF tutatoa ushirikiano wa kutosha katika programu hii. Lakini pia tutaingiza Ishi Huru katika programu zetu za mpira wa miguu kwa vijana. Tutahamasisha jamii katika kupambana na dawa za kulevya,” amesema.
Katika uzinduzi huo, pia Rais Malinzi alizundua semina ya waelimishaji na kuwaeleza kuwa wamepata fursa hiyo kwa vile ni vijana wanaojituma, hivyo watafikisha vizuri ujumbe wa Ishi Huru katika shule na vituo vya vijana.

Wanawake, viongozi wa kitaifa, waalikwa Maulid Dar

MWENYEKITI Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Maulid kwa wanawake wa    mkoa wa Dar es Salaam, kuadhimishwa kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W),  Aisha Sururu (wa kwanza kulia), akiwaongoza wanawake wengine kuomba dua, baada ya kumaliza kikao cha maandalizi ya sherehe hizo
zitakazofanyika kesho, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
***
WANAWAKE viongozi wa kitaifa na mkoa wa Dar es salaam, wameombwa
kujitokeza ili kuungana na wanawake wengine wa kiislam, katika
sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W).

Wito huo ulitolewa na Kamati ya Maandalizi ya sherehe hizo kwa upande
wa wanawake, na kubainisha kuwa hawataalika mgeni rasmi, badala yake ,
viongozi na wanawake wengine wawe kitu kimoja kuadhimisha siku hiyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aisha Sururu, alisema, sherehe itafanyika
Januari 14, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, na kwamba
itawakutanisha wanawake waislam wa mkoa wa Dar es Salaam na mkoa
jirani wa Pwani.

"Wanawake wa hali ya chini, wamefikiria kwanini sherehe za kidini
ambazo hazina harambee, michango wala kitu chochote, tualike mgeni
rasmi? Wakaona ni vyema kutangaza ili nao kama wananchi wajumuike na
wanawake wa hali ya chini, ambao watafarijika zaidi, kuona wamekaa
mkekani pamoja na viongozi wakubwa,"alisema
Aisha.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni diwani viti maalum Ilala, alisema, kwa
wale ambao hawatafikiwa kwa mualiko wa mmoja mmoja, wanaruhusiwa
kujumuika na wenzao siku hiyo ya maadhimisho.

Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), huadhimishwa duniani  kote kila ifikapo mfungo wa sita kwa kalenda ya kiislam. ikiwa ni

kumbukumbu tangu kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa wafuasi wa dini ya
kiislam.

Maandalizi ya sherehe hiyo kitaifa, mwaka huu yatafanyika mkoani
Kigoma, ambapo Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), limesema
mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.

Kesho, Keshokutwa Wabongo kula shushu!

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com press@ikulu.go.tz              

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
       P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
                                         
TAARIFA KWA  UMMA.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa kesho, Jumatatu, Januari 13, 2014, itakuwa ni Siku ya Mapumziko (Public Holiday) kwa Watanzania wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Rais Kikwete ameutangaza uamuzi huo mjini Zanzibar ambako leo ameungana na Watanzania na Wazanzibari wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.

Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na mwasisi wa Zanzibar na Taifa la Tanzania, Hayati Abeid Amaan Karume yalifanikiwa kuung’oa madarakani utawala dhalimu wa Sultan na kuwawezesha kwa mara ya kwanza katika historia Waafrika walio wengine kujitawala ndani ya nchi yao wenyewe.

Yalikuwa ni Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofungua njia ya kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – miezi mitatu baada ya Mapinduzi hayo – Aprili 26, 1964.               
Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Ali Mohamed Shein ametangaza kuwa kesho itakuwa Siku ya Mapumziko Tanzania Visiwani kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Rais Shein alitangaza mapumziko hayo wakati alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Amaan mjini Zanzibar katika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi.

Rais Shein alitangaza mapumziko hayo wakati alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Amaan mjini Zanzibar katika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi.

Mwisho.
Imetolewa na;
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS
Ikulu,
es Salaam.
12 January, 2014

Manchester City kuiengua Chelsea kileleni itaivaa Newcastle Utd

KLABU tishio kwa sasa nchini England, Manchester City chini ya kocha Manuel Pellegrini leo ina nafasi ya kukalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu ya Engalnd iwapo itaishinda ugenini dhidi ya Newcastle United na kuinegua Chelsea iliyoing'oa Arsenal jana kwa kuicharaza Hull City.
City itakuwa ugenini kuvaana na Newcastle ina pointi 44 na iwapo itashinda mechi hiyo ya jioni ya leo itafikisha pointi 47, moja zaidi ya zile ilizonazo Chelsea iliyokaa kileleni na pointi 46, moja zaidi ya waliokuwa vinara Arsenal ambayo yenyewe itashuka dimbani kesho kuvaana na Aston Villa ugenini.
Kikosi cha Pellegrini ambayo kimecheza mechi 12 kuanzia Desemba Mosi na kufunga mabao 36 katika michuano yote inayoshiriki msimu huu, huku ikiwa na rekodi ya kushinda nyumbani hata hivyo hawatakuwa na kazi nyepesi kwa Newcastle watakaokuwa uwanja wao wa nyumbani wa St James Park kutokana na timu kupoteza mechi mbili mfululizo kutoka kwenye lindi la ushindi wiki chache zilizopita.
Manchester City wanapewa nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo kutokana na kuwa na safu kali ya ushambuliaji ikiongozwa na Alvaro Negredo, Edin Dzeko na kiungo Yaya Toure Mchezaji Bora wa Afrika kwa mara ya tatu mfululizo.
Mbali na mechi hiyo inayofuatiliwa kwa ukaribu na mashabiki wa kandanda pia leo kuna mechi nyingine nzuri ya Stoke City itakayopikaribisha Liverpool kabla ya kesho kuhsuhudiwa Aston Villa kuialika Arsenal katika pambano ambalo kama The Gunners watashinda itadhihirisha dhamira yake ya kunyakua taji la Ligi msimu huu baada ya miaka mingi ya kulikisikia kwenye bomba tu.

RATIBA
Jumapili Januari 12 
17:05 Newcastle V Man City
19:10 Stoke V Liverpool
Jumatatu Januari 13 

23:00 Aston Villa V Arsenal

Ni Bobby Williamson au Adel Amrouche kuinoa Yanga

Bobby Williamson
Adel Amrouche


Na Sanula Athanas, Zanzibar
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga ameweka wazi kuwa pamoja na kupokea majina ya makocha 60 walioomba kazi ya kuifundisha timu hiyo, ni makocha wawili tu ambapo Yanga wameona wanauwezo wa kuifundisha timu hiyo.
Akizungumza mjini Zanzibar juzi usiku, Sanga alisema Kocha wa Gor Mahia, Bobby Williams raia wa Scotland na Kocha wa timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars), Mbelgiji Adel Amrouche, ndiyo makocha pekee wenye sifa za kuinoa timu yao inayokabiliwa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mapema mwezi ujao.
Sanga, aliyekuwa kisiwani hapa tangu juzi kwa ajili ya kuiomba radhi serikali ya Zanzibar kwa kutoleta timu yao kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi, alisema baada ya kufanya mchujo wa majina zaidi ya 60  waliyokuwa nayo makocha hao ndio wawili ndiyo wamekidhi vigezo vinavyotakiwa na klabu hiyo ya Jangwani.
 “Unajua yanazungumzwa mengi kuhusu kocha wetu ajaye, lakini ukweli ni kwamba mpaka sasa hatujapata kocha mkuu na timu itaendelea kuwa chini ya Mkwasa (Boniface) hadi pale tutakapopata,” alisema kiongozi huyo.
“Tulipata zaidi ya maombi ya makocha 60, wanaotufaa ni Bobby na kocha wa Harambee Stars (Amrouche). Tumefanya mazungumzo nao lakini kuna masharti magumu yanayotuchelewesha kwa sababu wana mikataba na timu zao,” aliongeza Sanga.
Alisema kuwa bado wapo kwenye mazungumzo kuona ni kwa namna gani wanaweza kumpata kocha mmoja wapo kati ya hao kwa ajili ya kuchukua nafasi ya kocha aliyetimuliwa, Ernest Brandts raia wa Uholanzi.
Kocha huyo alitimuliwa siku mbili baada ya kufungwa na Simba magoli 3-1 kwenye mchezo maalum wa kirafiki wa 'Nani Mtani Jembe' uliochezwa Desemba 21 mwaka jana.
Kikosi cha Yanga kwa sisi kipo chini ya Kocha Charles Mkwasa ambaye amchukuliwa pamojana Juma Pondamali kuchukua nafasi za Fred Felix 'Minziro' na Mkenya Razaq siwa ambao pia walitupiwa virago pamoja na Brandts.

Yanga ipo nchini Uturuki ilipokwenda kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu pamoja na ligi ya klabu bingwa Afrika.NIPASHE JUMAPILI

Waziri Miuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon afariki

BDEA70B3-44DF-4D1E-BDDB-A5DCEBA4F87F_w640_r1_sWaziri mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, amefariki dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 85.
Alikuwa waziri mkuu wa Israel mwaka 2001.
Amekuwa mahututi tangu mwaka 2006 kufuatia mfululizo wa matatizo ya kiharusi. 
Ariel Sharon alikuwa askari wa vita na baadae kuwa kiongozi wa nchi.
Alipokuwa mwanajeshi, alijulikana kwa ushujaa wake katika uwanja wa mapambano kwa miongo kadhaa kufuatia kuundwa kwa taifa la Israel, akijulikana hasa wakati wa vita vya jom kippur vya mwaka 1973. Katika mbinu za hali ya juu alizozionyesha, aliwaongoza wanajeshi wa Israel kuvuka mfereji wa suez, na kulikabili jeshi la misri.
Pia alijulikana na wengi kwa kuwa jabari na mbabe. Mwaka 1982, aliongoza uvamizi wa Lebanon ambao ulipelekea mauaji yaliyofanywa na wanamgambo wa Lebanon kwa mamia ya wapalestina katika kambi za wakimbizi za sabra na shatilla huko Beirut.
Kama mwanasiasa, Ariel Sharon pia alikuwa na utatanishi. Akiwa waziri, alihamasisha kuundwa kwa makazi ya walowezi wa kiyahudi kote katika maeneo ya wapalestina.
Serikali yake ilizikandamiza vurugu katika muda wa miaka michache, na kuanza kazi ya kuweka vizuizi vya usalama ambavyo hivi sasa vinawatenga waisraeli na wapalestina.
Mwaka 2006, bwana Sharon alipata mfululizo wa matatizo ya kiharusi na kuingia katika hali ya kupoteza fahamu. Nafasi yake ya waziri mkuu ilichukuliwa na Ehud Olmert.
Chanzo:VOASWAHILI.COM