STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 30, 2013

Rais Kikwete akabidhiwa Rasimu ya Katibu Mpya

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete leo amepokea rasmi Rasimu ya Katiba Mpya ambayo itajadiliwa hapo baade na Bunge maalum la Katiba. 
Rais Kiwete aliipokea Rasimu hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika makabidhiano yaliyofanyika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. Kuisoma zaidi rasimu hiyo Bofya hapa RASIMU YA KATIBA

Miyeyusho abadilishiwa mpinzani toka Kenya

Bondia Joshua Amukulu (kushoto) kutoka Kenya akitunishiana misuli na Francis Miyeyusho wakati wa upimaji uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika kesho Desemba 31. Awali ilitangazwa Miyeyusho angepigana na David Chalanga.

Bondia Kalama Nyilawila kushoto akitunishiana misuli na Ibrahimu Maokola  baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika Desemba 31 siku ya jumanne katika ukumbi wa New Msasani Club.
Bondia Francis Miyeyusho akipima uzito kwa ajili ya mpambano wake  Joshua Amukulu kutoka Kenya utakaofanyika kesho jumanne katika ukumbi wa Msasani Club.
BONDIA FRANSIC MIYEYUSHO AKIHOJIWA NA WAANDISHI WA HABARI BAADA YA KUPIMA UZITO KWA AJILI YA MPAMBANO WAKE NA MKENYA JOSHUA AMUKULU UTAKAOFANYIKA DESEMBA 31 KATIKA UKUMBI WA MSASANI CLBU (PICHA ZOTE NA SUPER D)
Bondia Ibrahimu Class 'king Class Mawe'  kushoto akitunishiana misuli na Mustafa Dotto  baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika kesho jumanne katika ukumbi wa Msasani Club.
IBRAHIMU CLASS 'KING CLASS MAWE AKIPIMWA AFYA
 IDDY MNYEKE AKIPIMWA AFYA

TBF yapata viongozi wapya, Maluwe, Phares chali Dodoma

Michael Maluwe (kushoto) na Magessa waliangushwa jana Dodoma
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limefanikiwa kupata safu mpya ya uongozi baada ya John Bandie kuchaguliwa kuwa Rais Mpya wa shirikisho hilo.
Uchaguzi huo ulifanyika jana mjini Dodoma na kutangazwa na Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Jamal Rwambow.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma na kuthibitishwa na mmoja wa makocha maarufu wa mchezo huo aliyechaguliwa kuwa Kamishna wa Ufundi na Mashindano Manase Zablon kupitia akaunti yake ya facebook, Rais huyo mpya alipata ushindi huo akimgaragara Phares Magessa.
Magessa alikuwa Makamu wa Rais katika uongozi uliomaliza muda wake ambaye alijikuta akipata kura 19 dhidi ya kura 24 za mpinzani wake aliyeibuka mshindi.
Katika nafasi ya Makamu wa Rais ilienda kwa Hamis Jafar aliyepata kura 39 za Ndiyo huku nne zikimkataa kwani alikuwa mwenyewe katika nafasi hiyo.
Kiongozi maarufu wa zamani wa mchezo huo, Saleh Zonga aliibuka kidedea kwenye nafasi ya Katibu Mkuu, akimshinda aliyekuwa Katibu Mkuu Msaidizi, Michael Maluwe kwa kupata kura 24 dhidi ya 13 za mpinzani wake.
Amina Ahmed alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mhazini wa shirikisho hilo kwa kupigiwa kura za ndito 43, huku Manase Zablon akichaguliwa kuwa Kamishna wa Ufundi na Mashindano kwa kupata kura 37 za ndiyo na mbili kumkataa.
Wengine walishinda katika uchaguzi huo ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba 10 mjini Mbeya na kukwama kabla ya kuhamishiwa Dodoma ni Michael Mwita aliyechaguliwa Kamishna wa Mipango kwa kura 39, huku Kamishna wa Watoto na Shule ikienda kwa Patrick Matete, Angela Bondo akichaguliwa Kamishna ya Wanawake na upande wa Walemavu nafasi ilienda kwa Aziz Mtogole.

Swagger sasa aja na Bongo Series Extra

Swagger katika pozi
MTAYARISHAJI wa filamu aliyewahi kutamba kwenye muziki wa kizazi kipya akiwa na kundi la Crime Busters, Hussein Ramadhani 'Swagger' anatarajiwa kuibuka na kipindi kipya cha burudani cha kwenye runinga kiitwacho 'Bongo Series Extra'.
Akizungumza na MICHARAZO, Swagger alisema kipindi hicho kitakachokuwa kikionyesha tukio kali la wiki, onyesho 'live' la burudani jukwaani, mahojiano ya msanii mkali wa wiki pamoja na kuangalia watoto wa mitaani waishivyo na pamojana mapitio ya filamu, kimeshakamilika ingawa bado hajajua kitarushwa kwenye kituo gani.
"Kila kitu kimekamilika na tayari nipo kwenye mazungumzo na baadhi ya vituo vya televisheni kwa ajili ya kuruhusu kurushwa hewani, hivyo wapenzi wa burudani wakae mkao wa kula kupata burudani ya aina yake kwani Bongo Series Extra imeshiba vya kutosha," alisema.
Swagger aliyeanza kuigiza michezo ya kwenye runinga kupitia kundi la Niger Theare akiwa na mmoja wa waasisi wa michezo ya kwenye televisheni kupitia kituo cha DTV, Qudrat Olomoda 'Chombeza', alisema aliamua kuja na kipindi hicho chenye mambo mseto ili kuwakamata mashabiki ambao walikuwa wanakosa kipindi cha namna hiyo.
Alisema ukiondoa masuala ya muziki na filamu pia kipindi hicho kitakuwa kinamulika maisha halisi ya watoto wa mitaani ili kusaidia kuizundua jamii na serikali kwa ujumla kujua tatizo hilo namna lilivyo na kuangalia jinsi ya kuwasaidia.
"Hakuna asiyejua tatizo la watoto wa mitaani au wanaoishi katika mazingira magumu, lakini nani anayejua ugumu wanaokutana nao mitaani, watasaidiwaje ili kuwafanya wafurahie maisha kama watoto wengine. Hivyo tumeona tuje namna hiyo," alisema Swagger.
Swagger ambaye kwa sasa yupo mbioni kukamilisha filamu yake mpya iitwayo 'Nyaraka' iliyowashirikisha wasanii mbalimbali wakiwemo Mzee Magari na wengine alisema anatarajia maombi yake ya kurusha kipindi hicho yakikamilika na kukubaliwa mashabiki wa burudani na jamii nzima itaburudika vya kutosha.

Kocha Logarusic 'afagiliwa' Simba

Ibrahim Twaha, katika mazoezi ya siku za nyuma
Kocha Logarusic aliyefagiliwa
KIUNGO Mshambiliaji wa klabu ya Simba, Ibrahim Twaha 'Neymar', amemwagia sifa kocha mpya wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic 'Loga' kwamba ni bonge na kocha na kuwa na imani ya kuipa Simba ubingwa katika Ligi Kuu msimu huu.
Aidha mchezaji huyo amesema anashukuru ameanza mazoezi mepesi baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, japo anajisikia vibaya kuikosa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza rasmi kesho visiwani Zanzibar.
Akizungumza na MICHARAZO, Twaha aliyesajiliwa na Simba kutoka Coastal Union akifahamika kwa jina la utani kama 'Messi' na kubadilishiwa jina kuwa 'Neymar', alisema japo hajaanza kufundishwa na kocha huyo lakini amekuwa akihudhuria mazoezi ya timu hiyo na kuvutiwa na ufundishaji wa Logarusic.
Twaha alisema Mcroatia huyo ni bonge la kocha na hataki mchezo na anayependa timu kucheza kwa kasi kitu ambacho kwa wachezaji waliopo Simba akiwemo yeye wataimudu na kuiletea klabu yao mafanikio.
"Siyo siri kocha wetu mpya ni kocha mzuri, anataka timu icheze kwa kasi na wachezaji kujituma na kujitambua bila kusubiri kusukwa kitu ambacho ni kizuri na nina imani ataisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huu," alisema Twaha.
Twaha, alisema kitu cha muhimu kwa wachezaji wenzake kuzingatia maelekezo ya mwalimu huyo aliyedai ni mmoja wa makocha wasiotaka masihara kazini kitu ambacho anaamini kitajenga nidhamu nzuri kwa timu yao.
Mchezaji huyo aliyekuwa majeruhi wakati duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara likielekea ukingoni, alisema anashukuru hali yake imeanza kutengemaa kwa kufanya mazoezi mepesi akisubiri ripoti kamili ya daktari wa timu yao ili kama aanze kujumuika na wenzake.
"Nashukuru nimeanza kufanya mazoezi mepesi, na leo jioni natarajia kuonana na daktari kunikagua, ila najisikia vibaya kuyakosa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, lakini kama hali itaimarika zaidi naamini nitaanza mechi za duru la pili la ligi kuu mwakani," alisema Twaha.
Simba ilimnyakua Logarusic aliyewahi kuinoa Gor Mahia-Kenya baada ya kumtimua Abdallah Kibadeni mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza.

Oscar Joshua 'aigwaya' Al Ahly Ligi ya Mabingwa Afrika

Oscar Joshua
BEKI kisiki wa timu ya Yanga, Oscar Joshua ameibuka na kuitahadharisha klabu yake kwa kuitaka kuwa makini na kujiandaa vyema kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili ising'olewe mapema kwenye michuano hiyo.
Joshua, beki wa pembeni alisema mechi ambayo Yanga inapaswa kuwa makini nayo ni ile dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri watakaocheza nao iwapo watafanikiwa kuing'oa Komorozine ya Comoro.
Joshua alisema Al Ahly ndiyo timu pekee inayoonekana kuwa kikwazo kwa Yanga na kama itajipanga na kuitoa itajifungulia njia ya kufanya vyema kwenye michuano hiyo itakayoishiriki mwakani.
Akizungumza na MICHARAZO, Joshua alisema Al Ahly ni hatari sana kwa Yanga, lazima klabu yao ijiandae na kujipanga vyema.
"Al Ahly ni hatari sana wale, ni muhimu kwetu kujipanga vyema ili kuweza kuwatoa. Hii ndiyo timu tishio kwa Yanga michuano ya mwakani," alisema.
Beki huyo anayemudu nafasi nyingi uwanjani mbali na kucheza kama beki wa kushoto alisema, kwa kikosi kilichopo Yanga ikijipanga inaweza kufanya maajabu.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Al Ahly katika mechi ya raundi ya kwanza mapema mwezi Machi, na hii ni iwapo tu watafanikiwa kuindosha mashindanoni Komorozine ya Comoro wanaotarajiwa kuanza nao kwenye hatua ya awali kati ya Februari 7-9 na kuridiana nao wiki mbili baadaye.
Rekodi pekee ya Yanga ya kujivunia kwenye michuano hiyo ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi mwaka 1998 na kucheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo 1969 na 1970.

Miyeyusho, Mkenya kumaliza ubishi kesho Msasani


BINGWA wa Ngumi za Kulipwa wa Kimataifa anayetambuliwa na UBO, Francis Miyeyusho na Mkenya David Chalanga wanatarajiwa kupima uzito na afya zao asubuhi hii kabla ya kesho kupanda ulingoni kupigana jijini Dar es Salaam.
Mabondia hao watapigana kesho kwenye ukumbi wa New Msasani Club katika pambano lisilo la ubingwa la kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 ambalo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), Yasin Abdallah 'Ustaadh' mabondi wote watakaopanda kesho ulingoni watapimwa uzito wao leo kuanzia saa 3 asubuhi.
Ustaadh alisema zoezi hilo la upimaji wa afya na uzito litafanyika kwenye ukumbi huo wa New Msasani na kuwasisitizia mabondia hao kuwahi mapema.
Mkenya David Chalanga aliwasili nchini juzi usiku akitokea kwao Kenya tayari kwa ajili ya pambano hilo la uzani wa Bantam.
"Bondia David Chalanga ameshatua nchini kwa ajili ya kupigana na Miyeyusho na Jumatatu (leo) watapima uzito na afya zao kabla ya kupanda ulingoni Desemba 31," alisema Ustaadh.
Ustaadh alisema wengine watakaopima uzito na afya zao leo kabla ya kusindikiza pambano la Miyeyusho ni Kalama Nyilawila atakayecheza na  Ibrahimu Maokola,  Ibrahimu Class 'King Class Mawe' atakayevaana na Mohamed Kashinde.
Mabondia wengine watakaopigana hiyo kesho ni Cosmas Cheka dhidi ya Idd Mnyeke, Anthony Mathias atakayepimana ubavu na Fadhili Majiha na Nyota wa muziki wa Hiphop, Karama Masoud 'Kalapina' ataonyeshana kazi na Kimbunga Noma .
Kocha wa Ibrahim Class, Rajab Mhamila 'Super D' aliiambia NIPASHE bondia wake yupo tayari kumtoa nishai mpinzani wake kwa jinsi alivyomuandaa.
Super D, alisema anaamini bondia wake atamshinda Kashinde mapema ili kuendeleza rekodi yake na kuuaga vyema mwaka 2013.

Sunday, December 29, 2013

Zilizoboronga dirisha dogo zapewa muda hadi Jan.10 kurekebisha

 
Awadh Juma (kulia0 mmoja wachezaji sita wapya wa Simba.

KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.
Taarifa ya TFF, imesema baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.
Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.
Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.
Kuhusu mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyesajiliwa Yanga, TFF imesema inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa fedha za kumuuza klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.

Rage funika bovu...awagaragaraza akina Kinesi hivi hivi

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage amewagaragaza wapinzani wake baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kumtambua na kumtaka aitishe Mkutano Mkuu kwa klabu hiyo kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao.
Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.
Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.
Aidha, TFF imewataka wanachama wake kuheshimu uamuzi halali unaofanywa na vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni zake.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya klabu ya Stand United kukata rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuagiza mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Kanembwa JKT iliyovunjika kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini Tabora.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili itoe mwongozo kwa vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za ligi husika.
Kamati imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa ya mpira wa miguu ambapo uamuzi unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani, hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa katika mahakama za kawaida za kisheria.
Wakati huo huo: Wanachama wa klabu ya Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa Pan African baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulalamikia uongozi wao wakati wao si wanachama wa TFF.
Wanachama hao wanalalamikia uongozi wa klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi kabla ya ule wa kawaida ambao unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo kwa vile wanachama hao katika malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.
Pan African ni mwanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA. Hivyo, TFF imemtaka mwanachama wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.

Mohammed Matumla akabidhiwa Bodaboda lake

BONDIA Mohamed Matumla akiwa amepanda pikipiki yake baada ya kukabidhiwa.
Promota wa mpambano wa masumbwi Kaike Siraju katikati akimwinua mkono juu bondia Mohamed Matumla baada ya kumkabidhi pikipiki yake kwa kumshinda Nasibu Ramadhani wakati wa sikukuu ya krismas na kuibuka na bodaboda hiyo.
Promota wa mpambano wa masumbwi Kaike Siraju katikati akimpongeza bondia Mohamed Matumla baada ya kumkabidhi pikipiki yake kwa kumshinda Nasibu Ramadhani wakati wa sikukuu ya krismas na kuibuka na bodaboda hiyo. Kushoto ni Baba wa bondia huyo Rashidi Matumla na wa pili kulia ni Meneja Mkuu wa G S Group Limited wasambazaji wa pikipiki ya Haojue ambao wametoa pikipiki hiyo,Bruce Shi
Meneja Mkuu wa G S Group Limited wasambazaji wa pikipiki ya Haojue ambao wametoa pikipiki hiyo, Bruce Shi akimpongeza bondia Mohamed Matumla baada ya kumkabidhi bodaboda hiyo.

Friday, December 27, 2013

Jackie Cliff AKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA CHINA...


.
Mwanamke wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28 ambae ni video Queen wa nyimbo ya Linex -KIMUGINA amekamatwa na kilo 1.1 za dawa za kulevya aina ya heroin huko Macao. Dawa hizo zilikutwa tumboni mwake baada ya kushtukiwa na kufanyiwa X-ray ambapo alikutwa na jumla ya vidonge 66 vyenye thamani ya dola za Kimarekani 137,720.
Mwanamke huyo alikuwa akisafiri kutoka Thailand akielekea Macao Jumanne iliyopita. Aliwaambia polisi kuwa

alikuwa anaelekea Guangzhou ambao ni mji wa jimbo la Guangdong huko China.



Pichani ni mwanamke huyo wa Kitanzania (akiwa amefunikwa uso) aliyekamatwa na kilo 1.1 za heroin huko Macau. Hapo amepigwa picha na vidonge vyake kwenye press conference huko Macau, Disemba 19, 2013.

Mwanamke wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28 amekamatwa na kilo 1.1 za dawa za kulevya aina ya heroin huko Macao. Dawa hizo zilikutwa tumboni mwake baada ya kushtukiwa na kufanyiwa X-ray ambapo alikutwa na jumla ya vidonge 66 vyenye thamani ya dola za Kimarekani 137,720.

Mwanamke huyo alikuwa akisafiri kutoka Thailand akielekea Macao Jumanne iliyopita. Aliwaambia polisi kuwa alikuwa anaelekea Guangzhou ambao ni mji wa jimbo la Guangdong huko China.


Polisi wakichunguza vidonge ambavyo huyu mrembo alikuwa amevimeza.


Ok kwa wale walokuwa wakilalamika 'habari nusu nusu' huyo binti anaitwa Jackie Cliff. ..appeared in Diamondz Nataka Kulewa. Was a runners up or something kwenye Miss Tz huko nyuma.






Waandishi wa habari wakipiga picha vidonge vya heroin alivyokamatwa navyo mremboi huyu wa Kitanzania

Chanzo cha habari: jamiiforum.
You might also like
- See more at: http://onelovetz.blogspot.com/2013/12/jackie-cliff-akamatwa-na-madawa-ya.html?utm_source=feedburner&utm_medium=feed&utm_campaign=Feed%3A+blogspot%2FhgdRs+%28Onelove+Tz%29#sthash.zSUH9Hcq.dpuf

Thursday, December 26, 2013

Ismail Rage awashangaa wanaombeza Simba

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage, amesema hakuwatuma askari Polisi kwenda kuwatimua Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wanachama wa klabu hiyo waliokuwa wanakutana klabuni kuipanga mikakati ya kuishinda Yanga.
Bali alifanya hivyo ili kwenda kuhakikisha usalama kwao na mali ya klabu na ndiyo maana aliposikia wanaipangia mikakati Yanga aliwataka askari hao awaache waendelee na mkutano..
Pia alidai kushangazwa akidaiwa hakushiriki kufanikisha ushindi wa Simba dhidi ya Yanga katika mechi ya Nani Mkali Jembe, wakati yeye aliyewasajili wachezaji Ally Badru na Awadh Juma aliyefunga bao la tatu, na kudai Kamati ya Utendaji haikamiliki bila ya Mwenyekiti.
Akizungumza MICHARAZO, Rage alisema siyo kweli kama aliwatumia viongozi na wanachama wenzake askari ili kuwatimua klabu wakipanga mikakati ya kuifunga Yanga, bali alifanya hivyo ili kulinda usalama klabuni.
"Siyo kweli kama mimi niliwatumia Polisi ili kuwatimua, bali kulinda usalama kwa kuhisi labda mkutano wao ulikuwa na ajenga mbaya na hivyo kuzua tafran na kuharibu mali za klabu, lakini nilipoelezwa lengo lao nini niliagiza askari hao awaache wafanye mkutano wao ili kufanikisha ushindi wa Simba," alisema.
Pia alisema madai kwamba hakushiriki kwa namna yoyote kufanikisha ushindi wa Simba wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, hayana mashiko kwa vile alikutana na matawi siku moja kabla ya wenzake kukutana, na kamati haikamiliki bila ya Mwenyekiti ambaye ni yeye (Rage).
"Mimi ndiye mwenyekiti, ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, sijachangia vipi wakati katika usajili wa dirisha dogo nimesajili wachezaji wawili Ally Badru na Awadh Juma aliyefunga bao moja na kusababisha jingine, watu watambue hizi ni blabla za kutaka kunitia ubaya tu," alisema Rage.
Aliongeza anafahamu ni watu watatu tu ndiyo wakorofi wanaomsakama kila uchao, bahati nzuri wanachama wa Simba wanafahamu yeye ni mmoja wa viongozi shupavu na makini wasiyoyumbishwa ataendelea kusimama mpaka dakika ya mwisho kuona Simba inakuwa ya amani na utulivu.
Rage alisimamishwa na Kamati ya Utendaji ya Simba kabla ya TFF kumrejesha na kumtaka aitishe mkutano wa dharura aliougomea na sakata lake limepelekwa katika Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji kwa maamuzi.