STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 26, 2011

MCHANGANYIKO WA HABARI

Kipigo chamchanganya kocha Toto


KIPIGO cha mabao 2-1 ilichopewa Toto Afrika na timu ya Mtibwa Sugar, kimemchanganya kocha wa timu hiyo ya Mwanza, Choke Abeid, aliyedai hakutegemea kama wangelala ila ameapa kupigana kufa na kupona kushinda mechi yao ijayo ya ugenini dhidi ya Kagera Sugar.
Toto ambayo kabla ya mechi hiyo iliidindia Simba na kisha kuilaza AFC Arusha, ilikumbana na kipigo hicho na kuiacha timu yao kwenye nafasi ya saba ikiwa na pointi 20, huku Choke akisema mipira ya faulo ya Mtibwa ndio iliyowamaliza.
Choke, mchezaji wa zamani wa Yanga, alisema Mtibwa walikuwa wazuri kwa mipira hiyo na kuwakwamisha kusogea nafasi waliopo, ingawa amesema wanajipanga vema kwa mechi ijayo ya Kagera itakayochezwa Machi 9.
"Kipigo kimetuchanganya, kwa vile tulijiamini tungeshinda, ila lazima nikiri mipira iliyokufa (faulo) ndio iliyotuumiza, ingawa tumekubali matokeo na kujipanga kwa mechi ijayo," alisema.
Choke, alisema licha ya mechi hiyo ijayo ni ngumu kutokana na Kagera kucheza nyumbani kwao, ila bado wanaamini wataenda kushinda ili kulipiza kisasi cha mabao 2-0 ilichopewa na wapinzani wao hao kwenye pambano lililochezwa jijini Mwanza, Oktoba 21, mwaka jana.
Kocha huyo alisema kuwepo kwa muda mrefu kabla ya pambano hilo, kutawapa fursa nzuri ya kurekebisha makosa yaliyowagharimu katika mchezo wao na Mtibwa Sugar ambao kwa ushindi huo imeweza kufikisha pointi 30 na kung'ang'ania nafasi yake ya nne waliopo.

***
Prisons yazifunda zilizopanda


TIMU ya Prisons ya Mbeya, imezitaka timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kukomaa na kutokubali kushuka daraja kirahisi kwa sababu, huko chini ni kugumu mno.
Prisons imetahadharisha kuwa bora hata hiyo Ligi Kuu yenyewe kuliko ligi daraja la kwanza Tanzania Bara ambapo kila timu inakuwa inatafuta nafasi ya kupanda daraja.
Katibu wa timu hiyo Antony Hau amesema tangu timu yao ishuke daraja miaka miwili iliyopita imekuwa ikijitahidi kupanda bila mafanikio kutokana na ugumu uliokuwepo.
"Yaani naziambia timu zinazoshiriki Ligi Kuu zikomae zisishuke daraja huku ni hatari, kubaya, ni kugumu sana, huko juu unakutana na timu zilizogawanyika, zingine zinataka ubingwa, zingine kubaki daraja, huku kila mmoja anataka kupanda kwa hiyo ligi inakuwa ngumu sana, " alisema.
Pamoja na hayo, Hau amesema kuwa utaratibu wa kutafuta timu za kupanda Ligi Kuu wa kuweka kituo kimoja kama michuano fulani haufai.
"Maana ya ligi ni timu zizungukane, zicheze nyumbani na ugenini, sasa ligi ya kituo kimoja, si ligi kwa maana ya ligi ni michuano fulani tu au kombe," alisema.
Alishauri kuwa ligi daraja la kwanza iwe inachezwa nyumbani na ugenini kama Ligi Kuu ili timu ziwe na nafasi pana ya kucheza mechi nyingi na pia kuondoa uwezekano au hisia ya mwenyeji kubebwa na kupanda daraja.
Ligi daraja la kwanza Tanzania Bara imemalizika na tayari timu za Coastal Union, Villa Squad, JKT Oljoro, na Moro United zimefanikiwa kuingia Ligi Kuu.
***

Pondamali:Haya yataibeba Villa Ligi Kuu


BAADA ya kuirejesha Villa Squad katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha wa timu hiyo, Juma Pondamali 'Mensah' ameupa uongozi wa klabu hiyo mambo manne ya kuyatekeleza iwapo wanataka Villa isishuke tena daraja.
Villa ambayo ilishuka daraja msimu wa 2008-2009, ilirejea tena kwenye ligi hiyo baada ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Daraja la Kwanza ikiungana na timu za JKT Oljoro, Coastal Union na Moro United.
Kutokana na kutambua ugumu wa Ligi Kuu ulivyo kocha, Pondamali alisema ni vema uongozi wa klabu ya Villa ukajipanga mapema kuhakikisha timu yao hairejei ilikotoka kwa kufanya mambo manne muhimu ambayo anaamini yakaibeba klabu hiyo.
Pondamali, kipa wa zamani wa kimataifa aliyewahi kung'ara na klabu za Pan Afrika, Yanga na AFc Leopard, alisema jambo la kwanza ambalo uongozi wa Villa unapaswa kutekeleza ni kuongeza wachezaji wapya 12 katika kikosi chao ili kukiimarisha.
"Kikosi kinahitaji wachezaji wapta 12 kwa ajili ya kukiimarisha, hivyo ni vema uongozi ukalitekeleza hilo, Ligi Kuu Tanzania Bara ni ngumu na ina ushindani hivyo inahitaji wachezaji mahiri na wenye uwezo wa kuibeba timu," alisema.
Aliongeza kuwa jingine ni viongozi kuzungukia na kuhudhuria kwenye michuano yote ya ya mchangani kwa nia ya kusaka wachezaji wapya, akidai mbinu hizo ndizo zilizoisaidia na kuipa sifa Ashanti United iliwahi kutamba kwenye ligi kuu msimu kadhaa iliyopita.
"Mambo hayo yakifanywa naamini Villa tutadumu kwenye ligi, vinginevyo hata mie sintoweza kuendelee kukaa na klabu hiyo, hilo naliweka wazi," alisema Pondamali ambaye pia ni kocha wa makipa wa timu ya taifa, Taifa Stars akisaidiana na Mdemark Jan Poulsen.
Pondamali alitoa mapendekezo hayo katika mahojiano na kituo cha Radio One, akizungumzia mafanikio ya timu yake kurejea ligi kuu na mikakati ya kuzuia isishuke tena kama awali.
***

Mao, ahofia ratiba ya Ligi Kuu


KIUNGO mahiri wa timu ya soka ya Azam, Himid Mao, amedai ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara bado inaonyesha hali ya upendeleo kwa baadhi ya timu kitu ambacho amesema sio haki.
Mao, mtoto wa kwanza wa nyota za zamani wa kimataifa nchini, Mao Mkami aliyewahi kung'ara na timu za Pamba na Simba, alisema ni vema TFF ikaangalia upta ratiba ya ligi hiyo.
Kiungo huyo aliyeteuliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana U23 kinachojiandaa kwenye Cameroon, alisema kwa ratiba iliyopo ni wazi ni vigumu kwa timu yao ya Azam kuendelea kukaa kileleni na kutwaa ubingwa.
"Ratiba ya sasa haitendi haki kwa baadhi ya timu, angalia Simba na Yanga zimecheza mechi chache, lakini bado wanapewa mapumziko marefu, hali ambayo haifanyi ligi iwe tamu, leo Azam tupo kileleni, lakini nafasi yetu sio ya kudumu kwa kuwa wenzetu wana mechi chache," alisema.
Alisema ni kweli vigogo hivyo vilikuwa vikiiwakilisha nchi kimataifa, ila kwa vile zilisharejea zingepaswa kucheza viporo vyao ili uwiano wa mechi uwe sawa na kuifanya ligi ichangamke zaidi.
Mao, alisema sio kama ana hofu ya timu yao kutwaa ubingwa, ila anaona kuwepo kwa tofauti na mechi kunaweza kutumiwa vibaya na timu zingine kuwavurugia mipango yao.
"Unajua kila mchezaji Azam akili yake kwa sasa ni kuona tunakuwa mabingwa, hivyo tunataka tufukuzane na wenzetu kama inavyotakiwa na sio kuachana kwa mechi katika ratiba kwani ni mbaya kwa upangaji wa matokeo," alisema.
Mkali huyo anayechekelea kuifungia timu yake kwa mara ya kwanza kwenye mechi za Ligi Kuu walipocheza na African Lyon na kuwalaza mabao 3-0, alisema anaamini pamoja na dosari ya ratiba bao Azam wataweka rekodi Tanzania Bara msimu huu.
Azam ambayo iliyokuwa ikiongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo kabla ya mechi ya jana kati ya Simba na Mtibwa Sugar, ndio inayoongoza kwa kufunga mabao mengi hadi sasa ikiwa na mabao 32, yenyewe ikiruhusu mabao 11 tu.
***

Bakule ajiuengua TOT-Plus

MWANAMUZIKI Badi Bakule 'Jogoo la Mjini', amejivua uongozi wa bendi ya TOT-Plus 'Achinengule' ili kutoa nafasi kwa wengine kuongoza jahazi hilo.
Bakule, alimeiongoza TOT tangu mwaka 2005 alipowapokea Mwinjuma Muumin na Ally Choki waliowahi kuiongoza bendi hiyo kwa nyakati tofauti.
Akizungumza na Micharazo, Bakule alisema amelazimika kuachia ngazi kwa sababu chini ya uongozi wake haoni maendeleo yanayopigwa na bendi.
"Kila mwaka tumekuwa na mipango ya maendeleo isiyotekelezeka, hivyo bora niachie ngazi ili nipishe wenzangu kuongoza bendi," alisema.
Alisema amemuandikia 'bosi' wake, Kapteni Mstaafu John Komba kumjulisha rasmi dhamira yake na kwamba hatarajii kiongozi huyo kupinga uamuzi wake.
Alisema katika kipindi chote cha miaka mitano aliyokuwa kiongozi, hakuwahi kuamini kwamba Muumin na Choki waliondoka kwa sababu uongozi hautekelezi ahadi zake kwa vitendo, sasa ameamini.
"Naomba nieleweke kuwa sijaondoka TOT, nilichofanya ni kuachia ngazi nafasi ya uongozi baada ya kuona kwa muda wote huo bendi haipigia hatua za maendeleo na badala yake inazidi kuanguka," alisema Badi.
Alipoulizwa kuwa hatua hiyo inawezekana ni moja kati ya kuondoka kundini, Badi alisema kila jambo linawezekana na kwamba wakati wa kuamua vinginevyo ukifika anaweka wazi.
Micharazo ilipowasiliana na Komba kwa simu haikupokelewa ingawa taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema baada ya barua hiyo kumfikia mkurugenzi, alilazimika kuitisha kikao cha dharura na wanamuziki makao makuu ya bendi.
***
Extra Bongo kutoka mafichoni

BENDI ya Extra Bongo, iliyokuwa kambini karibu wiki tatu sasa, inatarajia kuvunja kambi hiyo na kuanza maonyesho yake kama kawaida.
Extra ilijichimbia kambini eneo la Mbezi Louis, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya albamu yao mpya ya pili siku moja baada ya kuibomoa Africana Stars 'Twanga Pepeta' kwa kuwanyakua wanamuziki wake sita.
Ikiwa kambini, bendi hiyo pia imefanikiwa kurekodi video mbili za nyimbo zao za Neema na Under 18.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki Extra Bongo inatarajia kuingia mitaani kuanzia Ijumaa wiki hii itakapofanya onyesho maalum la kuwatambulisha wanamuziki wapya iliowachukua toka Twanga Pepeta.
Choki alisema onyesho hilo litafanyika katika ukumbi wa New Msasani Club na kufuatiwa na lingine la Jumamosi litakalofanyika katika ukumbi wa TCC-Chang'ombe.
"Jumapili tutarudi rasmi katika ukumbi wetu wa nyumbani wa Mango Garden ili kuendelea kutoa burudani sambamba na kuwatambulisha wanamuziki wapya," alisema.
Wanamuziki hao wapya ni Super Nyamwela, Super Danger, Otilia Boniface (wanenguaji) Hoseah Mgohachi (besi), Saulo John 'Ferguson' na Rogert Hegga (waimbaji).
Aliongeza kuwa kwa sasa bendi hiyo imekuwa ikifanyia mazoezi nyimbo nyingine mpya za 'Fisadi wa Mapenzi' na Chuki ambazo ni miongoni mwa zile zitakazokuwa kwenye albamu hiyo ya pili, huku wakiwa wanatambia mtindo na rapu mpya kutoka kwa wakali hao wapya.

Simba, Mtibwa ni kisasi kitupu kesho

SIMBA na Mtibwa Sugar kesho zinakutana katika mechi yenye sura na mvuto wa pekee kwa aina yake ligi kuu bara, huku wekundu hao wa Msimbazi wakipania kuiporomosha kileleni mwa msimamo Azam FC na wapinzani wao wakipania kulipa kisasi cha kupoteza mechi ya kwanza.
Hata hivyo ushindi kwa Simba utawapeleka kileleni kwa muda tu, kwani watani wao wa jadi--Yanga wanaoshika nafasi ya pili wanaweza kuwashusha juu iwapo wataifunga Ruvu Shooting keshokutwa uwanja wa Uhuru.
Azam ina pointi 35 sawa na Yanga, lakini vijana wa Jangwani wako nyuma kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga, na Simba inaweza kufikisha pointi 37 kama itashinda mchezo wa kesho.
Kwa upande wao Mtibwa wenye kumbukumbu nzuri ya kuwalaza Yanga, wamepania kuwazima vigogo Simba, na iwapo hilo litatimia watakuwa wamekaza mwendo wa kuelekea kileleni kwa kufikisha pointi 33.
Mtibwa imetangaza vita kwa Simba kutokana na kipigo cha bao 1-0 kwenye mechi ya kwanza iliyoghubikwa na mazingira ya tuhuma za rushwa kabla ya mechi kuchezwa.
Mtibwa itamkosa mlinda mlango wake namba moja, Shaaban Kato ambaye anatumikia adhabu ya kutocheza mechi kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Toto Afrika ya Mwanza.
Kocha msaidizi wa Mtibwa, Mecky Mexime na bosi wake Tom Olaba, kila mmoja kwa nyakati tofauti wamesema wamejiandaa kushinda mechi hiyo.
"Nia yetu si kulipa kisasi tu, tumepania kushinda mechi zote zilizosalia na kutwaa ubingwa," alisema Maxime.
Olaba alilalamikia kadi nyekundu ya Kado, lakini hata hivyo alisema kukosekana kwa mlinda mlango huyo si tatizo la kuwanyima ushindi.
"Kwetu sisi hakuna mechi rahisi, hivyo maandalizi tunayofanya ni kwa ajili ya mechi ngumu," alisema Mexime, nahodha wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars.
Simba wenyewe waliokutana jana kujadili mambo mbalimbali, wamesema wamepania ushindi kabla ya kwenda Zanzibar kuiwekea kambi Simba.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo.
"Tukimaliza mechi, Jumatatu asubuhi tunakwenda Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi kabla ya mechi inayofuata," alisema Mtawala.
Mtawala alisema Simba itaenda Zenji na kikosi chake chote isipokuwa Uhuru Seleman ambaye bado anauguza goti, huku Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Hillary Echessa wakirejea toka kwenye majeruhi.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana kwenye mechi ya marudiano itakayochezwa Machi 5 kwenye dimba la Taifa, Simba ikiwa na deni la kipigo cha bao 1-0 iliyopewa na Yanga kwenye mechi ya awali iliyochezwa jijini Mwanza kwa bao tamu la Jerry Tegete.
Mwisho

Simba wazidi kuikamia Mazembe

BAADHI ya nyota wa klabu ya Simba, wametamba kuwa hawana hofu yoyote juu ya pambano lao dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wachezaji hao wa Simba wamesema licha ya kutambua ugumu watakaopata kwa wapinzani wao ambao ni mabingwa watetezi, bado wana imani ya kurejea rekodi ya mwaka 2003 walipoing'oa waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Zamalek ya Misri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili katikati ya wiki iliyopita, wachezaji wa Simba walisema kama wawakilishi wa Tanzania wataendelea kupigana kiume kuona wanasonga mbele hata kama TP Mazembe wanatisha kwa sasa katika soka la kimataifa.
Beki wa kushoto wa Simba, Juma Jabu, alisema kama mabingwa wa Tanzania wataenda Congo kupigana kiume kuipeperusha bendera ya nchi kwa kushinda, ingawa wapo watu wanaoikatia tamaa.
Jabu, alisema hata mwaka 2003 Simba ilipuuzwa ilipopangwa na Zamalek, lakini walipigana kiume na kuing'oa mabingwa hao watetezi jambo linalowezekana kutokea msimu huu.
"Hakuna ubishi Mazembe ni wazuri na wanatisha Afrika na Dunia kwa ujumla, lakini kama wawakilishi hatutishwi nao, tutapigana kiume ili kusonga mbele, muhimu Watanzania watupe sapoti badala ya kutukatisha tamaa," alisema Jabu maarufu kama JJ.
Mchezaji mwingine aliyejinadi kutokuwa na hofu na Mazembe ni Rashid Gumbo, aliyekiri ni kweli Mazembe wanatisha, lakini bado wanaweza kufungika kama timu zingine muhimu mipango mizuri na kujituma kwao uwanjani.
"Tukijipanga na kucheza jihad uwanjani tunaweza kuweka maajabu, TP Mazembe ni timu kama timu zingine licha ya kuwa tishio, tutapigana kuhakikisha tunashinda," alisema Gumbo.
Kauli ya wachezaji hao zimekuja wakati wadau wengi wa soka wakiwemo wanaojiita wachambuzi wakiikatisha tamaa Simba kwa madai haiwezi kutoka kwa mabingwa hao watetezi katika mechi zao za raundi ya kwanza .
Simba ilipata fursa hiyo kwa kuing'oa Elan de Mitsodje ya Comoro kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo katika mechi ya awali ilitoka suluhu ugenini kabla ya kushinda mechi ya marudiano iliyochezwa uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Mwisho