STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 15, 2013

Ikulu yamruka Prof. Lipumba kuhusu dai la Rais kujiongezea muda

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEidjNQBQqdZjtF5y5t9bESgSR8GHNRCBCUo0Rc8JHOw8AYPLCnnadkzUTivDnhn6-DxK8Lw5KPFoJ1UF9ZfiKVu-tno_bmcxvUvZ8X7fSnHOcm6QH4UtyIQz1-PgmeCajNNKNZQdvwLQP0/s640/lipumba.jpg
Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI  wa Chama cha CUF, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba amekaririwa na Gazeti la Mwananchi la leo, Jumatano, Mei 15, 2013 akisema kuwa “amenasa taarifa za siri za kuwepo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa madarakani”.

Katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Lipumba: Kuna njama za kumwongezea JK muda” Mheshimiwa Lipumba anadai kuwa Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete “ itakaa madarakani hadi mwaka 2017” kwa sababu kuna“wasiwasi kuwa mchakato wa sasa wa kupata Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014.”

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa taarifa hiyo ya Mheshimiwa Prof. Lipumba ni uzushi mtupu na ni upotoshaji usiokuwa na msingi. Rais Kikwete hafahamu kuwepo mipango hiyo.

Taarifa hiyo imedokeza kuwa itakuwa ni vyema kwa Mheshimiwa Lipumba kuisaidia jamii kusema nani anafanya mpango huo ili ukweli ujulikane.

Aidha, Mheshimiwa Rais anawasihi wanasiasa na Watanzania kwa ujumla kuacha tabia za uongo na uzushi na kuwapotezea muda Watanzania kufikiria mambo yasiyokuwepo.

Ukweli ni kwamba, kama ambavyo amesema mara nyingi, ni matarajio ya Rais Kikwete kuwa mchakato wa Katiba utakamilika mwaka 2014 na kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika chini ya Katiba Mpya kama inavyotarajiwa na kumpa nafasi ya kustaafu mwisho wa kipindi chake cha uongozi wa taifa letu.

Uongozi Yanga waishangaa Simba, wadai mchecheto unawasumbua

http://www.dullonet.com/sports/wp-content/uploads/2012/10/MWALUSAKO.jpg
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgSYmDLnie7hnVtrTGWYgRUFOpByrp157IOWYff81C3-BlBy3o9za2uTvhzv0o7KASc4-YKnTHPCapXXeqXludPGFhAz2fNsPF8yRHO0phXlHZAtawSSt5HRuGjR7Jx60KRzr7N0kNs_iFH/s400/yanga+mazoezi+pemba.jpg
Kikosi cha Yanga kikijifua visiwani Pemba

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhIcjvF_KtRuH7_RhsHmo6e35OvbZSy6TqFvBRrRQdfSxMs6muAQRtP3WyUo8ECwiHfHHtjETZKjgmlY_vnPp37UfdQrXTLq79G1sugF0cyUbaD6wk7bM1XxwwkKnJJx_PJ8zUEiqlPIsc/s1600/MAZOEZI.jpg
Simba wakijifua mjini Unguja, Zanzibar

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema hauna tatizo la badiliko la mwamuzi lililotangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ukidai kuwa jukumu la klabu yao ni kucheza soka na siyo kupendekeza waamuzi na kuwashangaa watani zao Simba walionukuliwa jana wakidai wanaweza kutopeleka timu uwanjani Jumamosi.

Simba kupitia Mwenyekiti wake wa Usajili, Zakaria Hanspope alinukuliwa kutokubaliana na maamuzi ya kubadilishwa kwa mwamuzi, Israel Nkongo na nafasi yake kupewa Martin Saanya wa Morogoro ili kuzihukumu Simba na Yanga katika pambano la kufungia msimu wa 2012-2013.
Hanspope ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, alisema wanahisi kuna mchezo mchafu ambao unaweza umetumika katika kubadilisha ghafla mwamuzi huyo na kwamba wangekutana mara moja ili kujadili na kuona kama wasusie mechi au la.
Hata hivyo wenzao Yanga kupitia Katibu Mkuu wake, Lawrance Mwalusako aliiambia MICHARAZO kwamba hawaoni tatizo la kubadilishwa mwamuzi kwa sababu jukumu lao wao ni kucheza soka na siyo kuamua mechi zao zichezeshwe na nani kama wanavyolilia Simba.
Mwalusako alisema huenda TFF imebaini tatizo dhidi ya mwamuzi wa awali na kufanya mabadiliko kitu alichodai huwa ni kawaida na klabu hazina mamlaka ya kuingilia kati kwa vile jukumu lao ni kucheza soka na masuala ya waamuzi ni jukumu la TFF na washirika wake katika kusimamia soka nchini.
Katibu huyo, beki wa kati wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema huenda wenzao Simba wameanza kutafuta visingizio mapema baada ya kubaini kwamba ni vigumu Jumamosi kuepuka kipigo katika pambano lao litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
"Sisi hatuoni tatizo la kubadilishwa kwa mwamuzi wa pambano letu la Jumamosi kwa sababu hayo siyo makujumu yetu, pia kwa timu iliyojiandaa vyema haiwezi kulalamikia mambo ambayo sio kazi yao, labda wenzetu walikuwa na mipango maalum na mwamuzi wa awali ndiyo maana wanalalamika," alisema.
Mwalusako aliongeza, pia inawezekana Simba wameshaanza kuingiwa mchecheto na kuamua kutafuta visingizio mapema kwa mashabiki wao pale watakapokumbana na kipigo kikali toka Jangwani.
"Wao wasihangaike kutafuta visingizio, kipigo cha Jumamosi kipo kwa vyovyote timu yetu imejiandaa vyema na ina kiu ya kulipa kisasi pamoja na kusherehesha sherehe za ubingwa wa taji la 24 katika soka ya Tanzania," alisema Mwalusako.
Juu ya kikosi chao alisema kinaendelea vyema kwenye kambi yao iliyopo Pemba visiwani Zanzibar na kwamba wanahakika ya kupata ushindi mnono kwa watani zao Jumamosi na kuwataka mashabiki na wanachama wao kujiandaa kuupokea ushindi huo kwani Simba hawachomi vyovyote ilivyo.
Yanga iliyotwaa ubingwa huo msimu huu kwa kuinyang'anya Simba ina deni kubwa la kulipa kisasi cha mabao 5-0 iliyopewa Mei mwaka jana katika mechi kama hiyo ya kufungia msimu uliopita, pia kwa miaka zaidi ya 30 imeshindwa kurudisha kipigo cha bao 6-0 walizopewa na watani zao Julai 1977.
Wakati Yanga wanajiwinda wakiwa visiwani Pemba, wenzao Simba wamejichimbia Unguja, pia Zanzibar.

Maproo Azam FC waanza likizo, kuikosa JKT Oljoro


Kikosi cha Azam Fc
BAADA ya kutwaa nafasi ya pili kwenye ligi kuu msimu wa 2012/2013 kocha wa Azam FC Stewart Hall amewapa likizo wachezaji wake wa kimataifa hivyo hawatacheza mechi ya mwisho ya kumaliza ligi dhidi ya JKT Oljoro itakayochezwa siku ya Jumamosi mkoani Arusha.

Wachezaji hao wamechangia kiasi kikubwa cha kuifikisha timu katika mafanikio hayo pamoja na kufanya vizuri kwenye mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hiyo ilimaliza ikiwa imecheza mechi sita katika hatua tatu za mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Akizungumza na www.azamfc.co.tz kocha Stewart aliwataja wachezaji hao kuwa ni Kipre Tchetche, Michael Bolou wa Ivory Coast, Humphrey Mieno na Jockins Atudo wa Kenya pamoja na mshambulia Brian Umony wa kutoka nchini Uganda.

Stewart amesema ameamua kuwapa mapumziko wachezaji hao ili wakae pamoja na familia zao kwa muda mrefu kutokana na mechi ya mwisho haitakuwa na umuhimu sana zaidi ya kumalizia ratiba kwa kuwa wameshapata nafasi ya pili na pia wametoa mfungaji bora.

“Kwangu kumpumzisha Kipre ni kutokana na mchezaji huyo kufunga magoli mengi ambayo hayatafikiwa na mchezaji yoyote, pia tumepata ushindi wa pili hivyo nimeona waende nyumbani kwa kuwa ni muda mrefu hawajakaa na familia zao” amesema Stewart.

Azam FC Jumamosi, Mei 18, itamaliza mechi zake za ligi kuu ikiwa ugenini dhidi ya JKT Oljoro kwenye mchezo utakaochezwa uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, Azam FC inacheza mechi hiyo ikiwa na pointi 51, mshambuliaji Kipre amefikisha jumla ya magoli 17 ya kufunga.

Akizungumzia mchezo huo kocha Stewart amesema kikosi cha mechi hiyo ya mwisho kitaundwa na wachezaji wa ndani ambao watashirikiana pamoja na wachezaji vijana waliopo katika timu yake.

Michael Bolou na Tchetche Kipre wanatarajiwa kuondoka siku ya Alhamisi kuelekea kwao nchini Ivory na wachezaji wa Tanzania wataanza mapumziko yao mara baada ya kumaliza mchezo wa ligi kuu siku ya Jumamosi.

Chelsea, Benfica vitani Europa League

Chelsea wakishangilia moja ya mabao yao

BENFICA wamejaaliwa zaidi kiufundi  kuliko Chelsea lakini wataingia katika mechi ya fainali ya Ligi ya Europa leo mjini Amsterdam wakiwa hawapewi nafasi, kwa mujibu wa kocha wa zamani wa England, Sven-Goran Eriksson.
Kocha huyo Msweden anawafahamu vyema Benfica baada ya kuwafundisha mabingwa hao mara mbili wa Ulaya.
"Hakika, Chelsea ndiyo inayopewa nafasi zaidi kutoka na kuwa na kikosi kilichokamilika kila idara lakini kwa mtazamo wangu wachezaji wa Benfica ni 'mafundi' zaidi," Eriksson aliliambia gazeti la kila siku la aBola.
"Kiufundi Benfica wana makali zaidi. Wanamiliki mpira vizuri sana na wachezaji soka zuri."
Mabingwa hao wa Ulaya wa kwaka 1961 na 1962 watawategemea viungo wao 'mafundi' Eduardo Salvio, Nicolas Gaitan, Pablo Aimar, Ola John na Nemanja Matic kumlisha mshambuliaji wao wa Paraguay anayelijua goli, Oscar Cardozo na patna zake wa mashambulizi na Lima na Rodrigo.
Cardozo, Lima na Rodrigo wamefunga magoli 71 katika mechi 118 za klabu hiyo msimu huu.
Eriksson, ambaye aliiongoza timu hiyo ya Ureno wakati ilipolala 1-0 dhidi ya AC Milan katika fainali ya Kombe la Ulaya mwaka 1990 mjini Vienna, anaamini Benfica watasahau haraka kipigo cha 2-1 kutoka kwa mahasimu wao wa jadi Porto Jumamosi.
Chelsea inaweza kuomba dondoo za wapinzani zao kutoka kwa wachezaji wao wa kimataifa wa Brazil, David Luiz na Ramires, ambao wote walisajiliwa kutoka timu hiyo ya Ureno.
Nahodha John Terry huenda akapata pigo jingine kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kukosa pia fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa mwaka jana waliyoshinda kwa 'matuta' dhidi ya Bayern Munich kutokana na kufungiwa. Beki huyo huenda ashindwe kuanza baada ya kutengua 'enka' katika mechi waliyoshinda 2-1 dhidi ya Aston Villa Jumamosi.
Vikosi vinavyotarajiwa:
Benfica: 1-Artur; 34-Andre Almeida, 4-Luisao, 24-Ezequiel Garay, 25-Melgarejo; 22-Nicolas Gaitan, 18-Eduardo Salvio, 21-Nemanja Matic, 35-Enzo Perez; 7-Oscar Cardozo, 11-Lima.
Chelsea: 1-Petr Cech, 28-Cesar Azpilicueta, 4-David Luiz, 2-Branislav Ivanovic, 3-Ashley Cole; 7-Ramires, 8-Frank Lampard, 13-Victor Moses, 10-Juan Mata, 11-Oscar, 9-Fernando Torres.

Refa: Bjorn Kuipers (Uholanzi)

Mradi wa usafiri wa Boti Dar umefikia pazuri




MCHAKATO wa kuanzishwa kwa usafiri wa kutumia Boti kwa wakazi waliopo kando ya Bahari ya Hindi ili kuwapunguzia kero na msongamano kwenye usafiri wa barabarani upo katika hatua nzuri, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam umedokeza mapema leo.
Aidha uongozi huo wa jiji hilo umewapongeza wabunge kwa kupitisha bajeti wa Wizara ya Ujenzi ambayo imeipa kipaumbele uboreshaji wa miundo mbinu ya jiji hilo, licha ya kukiri kwa hali halisi fedha zilizotengwa kutatua kero ya msongamano Dar es Salaam ni ndogo, ila wanashukuru kufikiriwa.
Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Abdallah Chaurembo alisema mpango wa jiji kusaidia kero ya msongamano kwa kutaka kuanzisha mradi wa boti zitakazokuwa zikiwahudumia wakati wa maeneo ya Kunduchi na Mbweni kutokea katikati ya jijini (Bandarini) upo katika hatua nzuri.
Meya Chaurembo alisema hivi karibuni uongozi wao ulikutana na wahisani kutokana China ambao waliwaelezea juu ya mipango hiyo na kuahidiwa kusaidiwa na hivyo kuwataka wakazi wa jijini kuondoa hofu kwani wakati wowote mradi huo utaanza kufanyiwa kazi ili kuwatatulia kero ya usafiri.
"Suala la mradi wa usafiri wa bori kutoka bandari kuelekea maeneo ya Kunduchi, Mbweni na Bagamoyo mchakato wake upo katika hatua nzuri sawea na ule wa ujenzi wa barabara nyingine za kupunguza kwero ya msongamano hasa baada ya kukutana na wahisani wetu wa China," alisema.
Chaurembo alitoa ufafanuzi huo katika mahojiano yake na kipindi cha Kumepambazuka cha Radio One kilichosika asubuhi, ambapo alieleza pia furaha yao ya kupitiwa kwa bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambayo safari hii imetengeza fedha nyingine kwa ajili ya kutatua  kero ya usafiri jijini Dar.
Hata hivyo Naibu Meya huyo alisema pamoja na fedha zilizotengwa kwa jiji lao katika bajeti ya mwaka huu kuwa nyingi, bado hazitoshi kulinganisha na hali halisi ya tatizo lililopo Dar es Salaam hasa kartika suala la kuwawezesha kulipa fidia kwa waathiriwa na upitishwaji wa miradi ya ujenzi wa barabara.
Alisema hata hivyo pamoja na kwamba fungu la fedha lililotengwa halijitoshelezi kulinganisha na hali halisi iliyo jijini humo, lakini wanashukuru na kufurahi kuona kilio chao cha muda mrefu kimesikilizwa na wabunge hao.
Juu ya miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea jijini humo ikiwamo ule wa mabasi ya kwenda kasi, alisema wanashukuru inaendelea vyema na kuwaahidi wananchi kwamba itakamilika kulingana na mikataba iliyoingiwa baina ya wakandarasi na serikali hivyo wananchi watulie na kuvumilia kwa sasa.