STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 8, 2012

Zuri Chuchu: Muimbaji wa zamani Double M anayeishi na VVU

HUENDA mashabiki wa muziki wa dansi na ule wa kizazi kipya, bado wanalikumbuka jina Zuri Chuchu, mmoja wa waimbaji mahiri wa kike waliowahi kutamba nchini na bendi mbalimbali pamoja na kazi zake binafsi. Moja ya kazi binafsi zilizomtambulisha muimbaji huyo wa zamani wa Bambino Sound na Double M Sound ni kibao kilichokimbiza kwenye vituo vya runinga kiitwacho 'Channel ya Mapenzi' alichokitoa mwaka 2005 kuelekea 2006 kikiwa katika miondoko ya zouk. Ila wakati mashabiki walipokuwa wakisubiri vitu zaidi kutoka kwake, ghafla alitoweka kitambo kirefu na kuja kuibuka akijitangaza kwamba ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Wapo baadhi ya wanamuziki wenzake, mashabiki wa muziki na hata ndugu, jamaa na rafiki zake walishindwa kumuamini wakidhani labda 'amedata' au alikuwa akitafuta mbinu za kurejea upya kwenye game kwa njia hiyo. Hata hivyo, mwenyewe alikuwa akisisitiza hajitangazi kutafuta sifa au 'promo' bali ni kweli yeye anaishi na VVU kabla ya kuanza kuendesha kampeni za kuelimisha watu wengi kujikinga na maambukizo ya VVU na Ukimwi. Baada ya kuendelea na msimamo wake, jamii ilikubali ukweli hasa alipomuona akiendesha kampeni zake shuleni na ndani ya jamii bila ya hofu yoyote, huku mwenyewe akitoa ushuhuda jinsi anavyoendelea kutumia vidonge vya ARV. Msanii huyo anayejishughulisha kwa sasa na muziki wa Injili akijiandaa kutoa albamu yake ya kwanza iitwayo 'Napenda Kuishi' yenye nyimbo 12, alisema hata yeye awali alipopewa taarifa kuwa ameathirika hakuamini kirahisi. "Hata mimi jambo hili awali lilinitesa kabla ya kukubali ukweli na kujitangaza hadharani nikibeba jukumu la kuwaelimisha wengine juu ya ugonjwa huo." Zuri Chuchu ambaye majina yake kamili ni Esther Charles Mugabo, alisema kumtumainia Mungu na ushauri aliopewa na wataalamu wa afya umemfanya leo ajione mtu wa kawaida akiendelea na shughuli zake kuelimisha wengine. ALIPOTOKEA Zuri Chuchu alizaliwa Septemba 8, 1974 mkoani Mara akiwa mtoto wa tano kati ya saba wa familia yao na alisoma Shule ya Msingi Nyamboto na kuishia kidato cha pili kwa masomo katika Shule ya Sekondari Tarime. Alisema tatizo la kifedha la kifamilia ndilo yaliyomkwaza na kukimbilia kusaka maisha katika machimbo ya Dhahabu ya Nyamongo kabla ya mwaka 1994 kwenda Kenya kufanya shughuli zake binafsi na kutamani kuingia kwenye muziki. Zuri alisema ingawa kipaji cha sanaa hasa uimbaji alizaliwa nacho na kuimba shuleni na kanisani, kupenda uimbaji wa Ally Choki aliyekutana nae Kenya akiwa bendi ya Extra Kimwa, ndiko kulikomfanya atamani nae kuingia katika fani hiyo. Ndipo alipoanza kujifunza taratibu fani hiyo na aliporejea nchini mwaka 2000 alienda kunolewa na Nyoshi El Saadat kabla ya baadae kutua Bambino Sound. Baadae alitoka Bambino kwenda Stono Musica alioenda nao umangani mwaka 2004 na aliporejea alitua Tango Stars na kusafiri na Patcheko kwenda Oman chini ya kundi la Kampiosa Sonare. Alirejea nchini na kujiunga Double M Sound akiwa miongoni mwa walioshiriki kupika albamu ya 'Titanic' kabla ya kujiunga African Beats na kusafiri nao 2006 kwenda Arabuni ambapo alirejeshwa nchini kwa madai hati yake ina tatizo. "Sikujua chochote niliporudishwa, ila nikiwa nchini nilitumiwa ujumbe wa simu na mwanamuziki mwenzangu mmoja aliyenieleza kwamba nijiandae kufa kwani nimerudishwa kwa vile nilikuwa muathirika, nilistuka mno," alisema. Katika wiki kadhaa za mateso ya moyo akijifungia ndani, Zuri alisema alijiwa na nguvu za kiroho na kwenda kupima Muhimbili alikothibitishwa kuwa ni kweli alikuwa na VVU, jambo lililozidi kumchanganya na akakata tamaa. "Nilikuwa najifungia ndani tu nikiwakimbia watu kwa jinsi nilivyoshtushwa na hali hiyo, ila nikajiuliza rohoni nitaendelea kujifungia ndani hadi lini, ndipo nikajitokeza hadharani, ingawa nilipokewa tofauti," alisema. Zuri alikiri alipokuwa kwenye muziki wa kidunia alijirusha na kujiachia kwa raha zake, pia akiwahi kuishi na wanaume watatu bila ya ndoa, lakini hana hakika alivipatia wapi virusi hivyo na hataki kumnyooshea mtu kidole. "Siwezi kumlaumu mtu kwani sikuishi kwa utulivu enzi za nyuma, ila najua kila limpatalo mtu ni mipango ya Mungu, nimejikubali na nasonga mbele kuwasaidia wengine waweze kubadili maisha yao," alisema. MLOKOLE Zuri ambaye sasa ameolewa na Dennis Ignas Mhala ambaye naye ni muathirika, alisema kabla ya kujigundua ni muathirika na kuingia kwenye muziki wa injili, alishaokoka kitambo. Alisema aliokoka mwaka 2005 kutokana na kusumbuliwa na mizimu ya upande wa mama yao iliyomtaka awe Mganga wa Kienyeji. "Nilikuwa nalazimishwa kuwa mganga, sikutaka, nikasumbuliwa sana. Ndipo nilipopata uponyaji na kuokoka hata kabla ya kugundulika kwa tatizo langu," alisema. Alisema anashukuru tangu alipokabidhi maisha yake kwa Mungu na kujitolea kuendesha kampeni dhidi ya Ukimwi amefarijika akiishi kwa amani na utulivu kuliko ilivyokuwa zamani. Zuri anashukuru muziki kumsaidia kwa mengi ikiwemo kujenga nyumba kwao Mara, kuanzisha miradi yake ya biashara ya vyakula akitengeza na kuuza maandazi, kazi anayoifanya kwa sasa. "Sio siri muziki wa kidunia ulinisaidia mengi tofauti na muziki wa Injili kwa vile muziki ninaoufanya sasa siufanyi kibiashara zaidi ya kujitolea kueneza neno la Mungu ila nashukuru sapoti ninayopata kwa watu mbalimbali." Zuri anayependa kula ugali kwa mbogamboga na matunda na kunywa maji na juisi, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama kuvishinda VVU kwa kujikubali, amesema mambo yanayomsikitisha ni kusikia waathirika wenzake wanasambaza virusi kwa makusudi. Pia alisema tabia ya unyanyapaa ni tatizo kubwa linalofanya jamii kushindwa kuwa wazi katika ugonjwa huo na kufanya walioathirika kujificha na kuendelea kuwaumiza wengine. HARAKATI Msanii huyo anayewashukuru wakuu wa shule kwa namna wanavyomuunga mkono katika harakati zake, alikiri amekuwa na wakati mgumu kuendesha kampeni zake kwa kutokuwa na fedha na kutopigwa tafu na serikali. "Nilidhani kwa nilivyokuwa muwazi na kipaji cha sanaa nilichokuwa nacho ningetumiwa na serikali kuendesha kampeni za kutokomeza Ukimwi kwa ufanisi zaidi, lakini ukweli sina sapoti yoyote najitolea mwenyewe tu," alisema. Alisema anachoshukuru ni kwamba juhudi zake zimesaidia kuwaokoa wengi na wale walioathirika kujikubali akishirikiana nao kuendesha maisha yao kupitia mashamba ya kilimo cha mboga waliyoyaanzisha ili kujikimu. Alidai mashamba hayo yapo Gongolamboto na Kisarawe, ambayo yamekuwa wakiwawezesha waathirika kumudu maisha bila ya kuwa ombaomba. Zuri aliitaka jamii ibadilike na kukubali kuwa Ukimwi ni tatizo linalohitaji vita ya kila mmoja anakawataka wanandoa kuheshimu ndoa zao na wale wasio na ndoa kuwa waaminifu. "Wengi wameumizwa na Ukimwi, hivyo jukumu letu kila mmoja kuchukua jukumu la kuwa makini nao ili kuepusha au kupunguza maambukizo mapya, kubwa watu wawe waaminifu katika ndoa zao, tusirukeruke ovyo," alisema. Alisema yeyote anayetaka kumuunga mkono katika harakati zake awasiliane nae kwa 0656-756356 au kumtupia mchango wa kuendesha shughuli zake katika akaunti ya Benki ya Posta 01000294431 kwa jina la Esther A. Mugabo.