STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 15, 2017

Manchester City aibu tupu, wapigwa 4-0

Picha zote kwa hisani ya Mirror
AIBU tupu. MANCHESTER City jioni hii imekumbana na aibu kubwa baada ya kutandikwa mabao 4-0 na Everton kwenye uwanja wa Goodson Park, mjini Liverpool.
City inayonolewa na Kocha Pep Guardioala kwa kipigo hicho imesalia nafasi ya tano ya msimamo na ikiwa katika hati hati ya kuzidiwa maarifa na watani zao wa Jiji la Manchester, Man United iwapo itafanikiwa kuifunga Liverpool kwa idadi kubwa ya mabao, kwani zinaweza kulingana na kuzidiana uwiano wa mabao.
United ina pointi 39 na mabao 31 ya kufunga na kufungwa 19 wakati City kwa kipigo cha jioni hii imesaliwa na pointi 42 na mabao 41 ya kufunga na kufungwa 26, ikiwa na maana wana uwiano tofauti na mabao matatu tu mpaka sasa.
Mabao yaliyoiangamiza City leo ikiwa kiigo chao cha tano msimu huu yalitumbukizwa na Romelu Lukaku dakika ya 34, Kevin Mirallas dakika 47', Tom Davies dakia ya 79 na chipukizi Ademola Lookman aliyefunga dakika za nyingeza za mpambano huo mkali ambao umemfanya Guardiola kujikuta kwenye simanzi kubwa.
Muda mchache ujao Man United itakuwa wenyeji wa Liverpool kwenye Uwanja wa Old Trafford, kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kutofungana. Mechi ilichezwa Oktoba 17, 2016.

Mbao, Lyon zashindwa kutambiana kesho zamu ya Toto v Prisons

Mbao FC
Lyon
Na Mwandishi Wetu
KLABU za Mbao FC na wageni wao African Lyon zimeshindwa kutambia kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara baada ya kutoka suluhu.
Timu hizo zimeshindwa kufunga kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kuzifanya zigawane pointi moja moja.
Kwa matokeo hayo zimezifanya timu hizo kuendelea kusalia katika nafasi zao walizokuwa kabla ya mchezo huo uliomalizika hivi punde.
Lyon imefikisha pointi 21 na Mbao imekusanya alama 20, lakini zimeshindwa kusogea katika maeneo waliyokuwapo.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumatatu kwa mchezo mmoja kati ya Toto African na Prisons jijini Mwanza na Jumanne Yanga itakuwa wageni wa Majimaji Songea na Jumatano Simba na Azam zitashuka viwanja tofauti vya mjini Morogoro na Dar es Salaam.
Simba itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati usiku wa saa 1 jioni, Azam itakuwa wenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.
Simba ndio vinara wa Ligi Kuu mpaka sasa ikiwa na pointi 44 baada ya kushuka uwanjani mara 18, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 40 na Kagera Sugar kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31 ikiiengua Azam iliyoshuka nafasi ya nne na pointi zao 30.

Msimamo wa Ligi Kuu Bara

                                P  W   D  L   F   A  Pts
1. Simba                   18 14  2   2  30  6  44
2. Yanga                   18  12  4   2  39  9  40
3. Kagera Sugar        19  9   4   6   21 18 31
4. Azam                    18  8   6   4  23  15 30
5. Mtibwa Sugar        18  8   6   4  22  19 30
6. Stand Utd             19  6   7   6  18  16  25
7. Mbeya City            18  6   6   6  16  16  24
8. Ruvu                    19   5   9   5  18  20  24
9. Prisons                 18   5   7   6  10  13  22
10.Mwadui                19   6   4   9  16  24  22
11.African Lyon         19   4   9   6  11  16  21
12.Mbao                   19   5   5   9  17  24  20
13.Ndanda                19  5   4  10  15  26  19
14.Majimaji               18  5   2  11  13  26  17
15.Toto Africans         18  4   4  10  11  20  16
16.JKT Ruvu              19  3   9   7   7   17   15

Wafungaji:   

9- Shiza Kichuya                             (Simba)
     Simon Msuva                             (Yanga)   
     Amissi Tambwe                         (Yanga)
8- Abdulrahman Mussa  (Ruvu Shooting)
    Mbaraka Yusuf              (Kagera Sugar)
7- Rashid Mandawa         (Mtibwa Sugar)
    Donald Ngoma                           (Yanga)
    John Bocco                               (Azam)
6- Mzamiru Yasin                           (Simba)
    Haruna Chanongo        (Mtibwa Sugar)
5- Omar Mponda                         (Ndanda)
    Obrey Chirwa                             (Yanga)
    Riffat Khamis                           (Ndanda)
    Victor Hangaya                        (Prisons)
    Rafael Daud                      (Mbeya City)
    Venance Joseph              (African Lyon)
4-Peter Mapunda                      (Majimaji)
    Kelvin Sabato                (Stand United) 
    Laudit Mavugo                          (Simba)
    Marcel Boniventure             (Majimaji)
    Boniface Maganga                     (Mbao)
    Deus Kaseke                              (Yanga)
    Shaaban Kisiga            (Ruvu Shooting)
    Mohammed Ibrahim 'MO'        (Simba)   
    Tito Okello                       (Mbeya City)
3- Hood Mayanja                (African Lyon)
    Ibrahim Ajib                               (Simba)
    Abdalla Mfuko                        (Mwadui)
    Subianka Lambert                   (Prisons)
    Ditram Nchimbi                (Mbeya City)
    Wazir Junior                    (Toto African)
    Issa Kanduru               (Ruvu Shooting)
    Ally Nassor 'Ufudu'       (Kagera Sugar)
    Kelvin Friday                 (Mtibwa Sugar)
    Mfanyeje                                 (Majimaji)
    Francisco Zukumbawira             (Azam)
    Shaaban Idd                                 (Azam)
    Jamal Mnyate                             (Simba)
   Jamal Soud                  (Toto Africans)
    Adeyum Saleh               (Stand United)
    Jacob Massawe             (Stand United)
2- Adam Kingwande          (Stand United)
    Samuel Kamuntu                  (JKT Ruvu)
    Vincent Philipo                            (Mbao)
    Mcha Khamis                               (Azam)
    Danny Mrwanda            (Kagera Sugar)
    Pastory Athanas           (Stand United)
    Paul Nonga                             (Mwadui)
    Fully Maganga           (Ruvu Shooting)        
    Themi Felix                  (Kagera Sugar)
    Mudathir Yahya                        (Azam)
    Atupele Green                    (JKT Ruvu)
    Jerry Tegete                          (Mwadui)
    Jamal  Mwambeleko               (Mbao)
    Vincent Barnabas     (Mtibwa Sugar)
    Adam Salamba            (Stand United)
    Jaffar Salum             (Mtibwa Sugar)

Mbaraka Yusuf aibeba Kagera Sugar kwa Ndanda FC

Kagera Sugar wakishangilia moja ya mabao yao ya Ligi Kuu Bara
Na Rahim Junior
MABAO mawili moja kila kipindi yamemfanya Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar kuwasogelea vinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara, Simon Msuva, Amissi Tambwe wote wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba.
Yusuf aliyeisaidia Kagera kupata ushindi muhimu nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda katika mechi iliyopigwa jana, amefikisha jumla ya mabao nane, moja pungufu na waliyonayo kina Msuva.
Straika huyo wa zamani wa Simba, amelingana sasa kwa ufungaji mabao nane na mkali mwingine wa Ruvu Shooting, Abdulrahman Mussa aliyeisawazishia timu yake juzi isiadhiriwe na JKT Ruvu katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1.
Katika mechi nyingine ya jana Mwadui ikiwa ugenini Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga ilikumbana na kipigo cha kushtukiza cha mabao 2-0 toka kwa Chama la Wana, Stand United.
Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kwa Mwadui mbele ya wapinzani wao hao wa jadi wa mkoa huo na kuwafanya isalie na pointi zao 22 katika nafasi ya 10, huku Stand ikichupa toka nafasi ya saba hadi ya sita kwa kufikisha pointi 25.
Mabao ya beki Adeyum Saleh dakika ya 16 na lingine la penalti la Nahodha Jacob Massawe dakika nne baadaye yaliyotosha kuipa Stand ushindi wake wa kwanza tangu ilipokimbiwa na kocha wake, Mfaransa Patrick Liewig.
Kabla ya ushindi huo Chama la Wana ilikuwa imecheza mechi 11 bila kupata ushindi wowote, huku mitatu kati ya hiyo ikiwa chini ya Kocha Mkuu mpya, Hemed Morocco, ambaye ni Kocha Msaidizi wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Ligi hiyo jioni hii kuna mchezo mmoja unaoelekea ukingoni kati ya Mbao FC ya Mwanza dhidi ya African Lyon ya Dar es Salaam na kesho Toto Africans itaikaribisha Prisons Mbeya kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Carzola majanga matupu Arsenal, nje wiki 10 zaidi

MAJANGA. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anahofu kiungo wake nyota Santi Cazorla anaweza kukaa nje ya uwanja kwa wiki 10 zaidi kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu yanayomsumbua.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania amekuwa nje ya uwanja toka Oktoba baada ya kucheza mechi 11 katika mashindano yote msimu huu. Lakini Cazorla mwenye umri wa miaka 32 sasa anategemewa kuendelea kukaa nje zaidi kutokana na majeruhi kupona taratibu kuliko ilivyotegemewa awali.
Wenger alisema Cazorla bado hajaanza hata kukimbia hivyo hadhani kama atarejea uwanjani hivi karibuni.

Imeelezwa huenda Wenger akafanya mpango wa kusajili mbadala wake.
Klabu hiyo jana Jumamosi ilivaana na Swansea City na kupata ushindi wa mabao 4-0 ugenini katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England.

PSG yaingia vita ya kumnasa Depay wa Man United

Memphis Depay
PSG nayo imoooo! Klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, imedaiwa nayo kuingia kwenye mbio za kumwania winga wa Manchester United, Mholanzi Memphis Depay.
Meneja wa United Jose Mourinho tayari ameshamwambia winga huyo kutafuta timu nyingine, huku Everton na Olympique Lyon zote zikitajwa kumtaka.
PSG walikaribia kumsajili Depay kabla hajakwenda Old Trafford kwa kitita cha Pauni milioni 25 mwaka 2015, lakini sasa wanaonekana kumhitaji tena mchezaji huyo ambaye hajacheza katika kikosi cha United toka Novemba mwaka jana. United inataka kitita cha Paundi milioni 15 kwa Depay baada ya kukataa ofa ya Paundi milioni 10 iliyotolewa na Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Breaking News: Mwili wa Amina kuletwa, kuagwa Dar kesho

Na Mwandishi Wetu

HABARI zilizotufikia muda huu, zinasema kuwa mwili wa Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Uhuru Wikiendi, Burudani na Mzalendo, Amina Athuman unatarajiwa kurejeshwa Dar es Salaam kesho asubuhi kwa boti kutoka Zanzibar. Msemaji wa Familia ya Marehemu, Athumani Kazukamwe, amesema jioni hii kuwa, mwili wa Amina utasafirishwa kutoka Zanzibar saa moja asubuhi kwa boti na unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kati ya saa tatu na saa nne asubuhi.
Kazukamwe, ambaye ni baba mkubwa wa mume wa marehemu, amesema mazishi ya Amina yamepangwa kufanyika keshokutwa Jumanne katika makaburi ya Soni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Amesema awali, upande wa mume wa marehemu ulitaka mazishi hayo yafanyike kesho Dar es Salaam, lakini baada ya majadiliano na familia ya marehemu, waliafikiana mazishi yakafanyika Tanga.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa familia ya marehemu, taratibu za kuuaga mwili wa Amina zitafanyika papo hapo bandarini na mara baada ya kumalizika, utasafirishwa kwa basi maalumu la kukodi kupelekwa Tanga.
Kaimu Mhariri Mtendaji wa UPL, Ramadhani Mkoma, amethibitisha mazishi ya marehemu Amina kufanyika Tanga.
Ramadhani amesema amepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwa sababu hakutarajia iwapo Amina angetangulia kuondoka duniani katika umri mdogo.
Amesema Amina ameacha pengo kubwa kwa sababu alikuwa mmoja wa wanahabari wa UPL waliokuwa wakifanyakazi kwa kujituma, aliipenda kazi yake na ilikuwa mwiko kwake kusukumwa kutimiza wajibu wake.
Amesema kazi aliyoifanya wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo alitumwa kuandika habari zake, ni uthibitisha wa wazi wa utendaji mzuri aliokuwa nao.
Amesema hawana la kufanya isipokuwa kumshukuru Mungu kwa kuwa kila alipangalo, hakuna anayeweza kulipangua. Amewataka wafanyakazi wa UPL kumuenzi Amina kwa kuiga utendaji wake wa kazi.

Mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Simbu ang'ara India Marathon

Simbu (wa pili kushoto) akipozi na washindani wake baada ya kutwaa nafasi ya kwanza wa Mbio za kimataifa za India Marathon 2017
Na Lasteck Alfred
MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu, ameibuka mshindi kwenye mbio ndefu za Mumbai Marathon  2017, akifanikiwa kumpiku Mkenya Joshua Kipkorir na wakimbiaji wengine wazoefu kutoka mabara mbalimbali.
Mashindano hayo yajulikanayo kama Standard Chartered Mumbai Marathon huwa yanafanyika kila Jumapili ya tatu ya Januari katika jiji la Mumbai, India na yanaaminika kuwa ni mbio kubwa kabisa barani Asia kwa idadi ya washiriki.
Simbu, aliyedhaminiwa na kampuni ya Multichoice Tanzania, aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa dakika 2:09:28 muda ambao ni mzuri sana kwa mbio za aina hiyo.
Akizungumzia ushindi wake, Simbu alisema ushindi huo umesababishwa na maandalizi mazuri aliyoyafanya.
Alisema anauchukulia ushindi huo kama changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu. Amesisitiza kuwa ushindi huo sio wake pekee yake au Multichoice ambao ndio wathamini wake, bali ni ushindi wa Taifa zima.
Kwa upande wa Serikali,  Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimpongeza kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema: "Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania."
Kwa upande wake Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana alisema Multichoice imefurahishwa sana na matokeo hayo na kwamba wataendela kumdhamini Simbu kwa mujibu wa makubaliano yao, ili kuhakikisha anaendelea kufanya vyema na kuliletea taifa sifa kubwa.
“Tulichukua jukumu la kumdhamini simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote.
Alisema Mshana na kuongeza “Dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani”
Katika mbio hizo, waigizaji maarufu wa Bollywood John Abraham and Neha Dhupia walikuwepo kuleta amsha amsha kwa washiriki. Alphonce anatarajiwa kurejea nyumbani leo Jumatatu.

Beki Mholanzi akichonganisha Chelsea na Man United

Beki Stefan De Vrij
LAZIMA kieleweke. Klabu za Chelsea na Manchester United zimedaiwa kuingia vitani kwa ajili ya kusaka saini ya beki wa Lazio, Stefan De Vrij.
Duru za kisoka zinasema kuwa, Chelsea imejipanga kupambana na Man United katika kipindi cha kiangazi kwa ajili ya kumwania beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na Mashetani Wekundu.
Chelsea inadaiwa nao wako tayari kuingia katika kinyang’anyiro hicho, huku klabu yake ya Lazia imeondoa uwezekano wa kumuuza beki huyo katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Hatua hiyo imetoa mwanya kwa klabu hiyo kuweka kitita cha Euro milioni 40 kwa timu itakayomhitaji majira ya kiangazi, ambapo klabu yoyote kati ya Man United ama Chelsea wakituliza kichwa inaweza kueleweka kwao kwa beki huyo.

Simanzi! Mwandishi Amina Athuman hatunaye, Malinzi amlilia

Amina Athuman enzi za uhai wake
Na Alfred Lucas
SIMANZI. Mwandishi wa habari wa michezo wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Amina Athuman amefariki dunia asubuhi ya leo Jumapili na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi.
Malinzi ametuma salamu hizo kwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kutokana na kifo hicho cha Amina, aliyekuwa visiwani Zanzibar kuripoti michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika juzi Ijumaa.
Katika salamu hizo ambazo pia zimeenda kwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto; Rais Malinzi ameelezea kushtushwa kwake kwa taarifa za kifo cha ghafla cha Amina.
“Niseme tu wazi kuwa tangu kuanza kwa michuano ya Mapinduzi, nimekuwa nikifuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanahabari. Huwa pia sikosi magazeti ya Uhuru na Mzalendo na kuona byline (jina la mwandishi) ya Amina. Mpaka matokeo ya fainali zilizofanyika Januari 13, mwaka huu.
“Sasa asubuhi hii nimepata taarifa za kifo chake, ama kwa hakika zinasikitisha. Ni kifo cha ghafla, ninavyomfahamu binti huyo ni mchapakazi hodari na mfano uko wazi kwani katika hali ya ujauzito alikuwa hakosi kufuatilia habari,” amesema Rais Malinzi.
Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu hizo za rambirambi kwa familia ya marehemu Amina, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
“Binafsi naona ni kama askari aliyefia vitani. Naweza kumwita ni shujaa, lakini ndivyo hivyo tena, huwezi kupingana na mipango ya Mungu, nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, naomba wenzangu pia muwe na subira wakati huu mgumu ambao tasnia na Kampuni ya Uhuru Publications imepoteza mwanahabari mahiri.
Taarifa zinasema Amina alifariki dunia leo Jumapili Januari 15, 2017 akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mnazimmoja, iliyoko Zanzibar mara baada ya kujifungua jana kwa mtoto ambaye pia alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Hadi mauti yanamkuta alikuwa Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo pamoja na gazeti la Burudani linalochapisha mahsusi habari za michezo na sanaa kabla ya hapo aliwahi pia kufanya kazi kampuni na Business Times Limited. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Amina Athuman Mahala Pema Peponi. Inna Lillah wa Innaa Ilaihi Rajaajiuun.