STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 15, 2017

Mbaraka Yusuf aibeba Kagera Sugar kwa Ndanda FC

Kagera Sugar wakishangilia moja ya mabao yao ya Ligi Kuu Bara
Na Rahim Junior
MABAO mawili moja kila kipindi yamemfanya Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar kuwasogelea vinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara, Simon Msuva, Amissi Tambwe wote wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba.
Yusuf aliyeisaidia Kagera kupata ushindi muhimu nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda katika mechi iliyopigwa jana, amefikisha jumla ya mabao nane, moja pungufu na waliyonayo kina Msuva.
Straika huyo wa zamani wa Simba, amelingana sasa kwa ufungaji mabao nane na mkali mwingine wa Ruvu Shooting, Abdulrahman Mussa aliyeisawazishia timu yake juzi isiadhiriwe na JKT Ruvu katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1.
Katika mechi nyingine ya jana Mwadui ikiwa ugenini Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga ilikumbana na kipigo cha kushtukiza cha mabao 2-0 toka kwa Chama la Wana, Stand United.
Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kwa Mwadui mbele ya wapinzani wao hao wa jadi wa mkoa huo na kuwafanya isalie na pointi zao 22 katika nafasi ya 10, huku Stand ikichupa toka nafasi ya saba hadi ya sita kwa kufikisha pointi 25.
Mabao ya beki Adeyum Saleh dakika ya 16 na lingine la penalti la Nahodha Jacob Massawe dakika nne baadaye yaliyotosha kuipa Stand ushindi wake wa kwanza tangu ilipokimbiwa na kocha wake, Mfaransa Patrick Liewig.
Kabla ya ushindi huo Chama la Wana ilikuwa imecheza mechi 11 bila kupata ushindi wowote, huku mitatu kati ya hiyo ikiwa chini ya Kocha Mkuu mpya, Hemed Morocco, ambaye ni Kocha Msaidizi wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Ligi hiyo jioni hii kuna mchezo mmoja unaoelekea ukingoni kati ya Mbao FC ya Mwanza dhidi ya African Lyon ya Dar es Salaam na kesho Toto Africans itaikaribisha Prisons Mbeya kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

No comments:

Post a Comment