STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 28, 2011

Timu ya Ngumi kuondoka leo mchana




TIMU ya taifa ya mchezo wa ngumi itakayoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Michezo ya Afrika (All African Games) inatarajiwa kuondoka mchana huu kuelekea nchini Msumbiji, ikiwa na mabondia wanne pamoja na viongozi wawili.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania, BFT, Makore Mashaga, aliiambia MICHARAZO kuwa, timu hiyo imelazimika kuwahia mapema kwenda Maputo, kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya kuanza kwa michuano hiyo kutoka Septemba 3 hadi Septemba 1.
Mashaga, alisema kikosi hicho kilitarajiwa kuondoka jana kwa ndege kikiwa na mabondia wanne na makocha wao wawili tayari kwenda kuwahi zoezi la upimaji afya litakalofanyika kesho (Agosti 30).
"Hapa ninapozungumza nawe nipo katika harakati za kukamilisha kuiwahisha timu uwanja wa ndege ili kuondoka kwenda Msumbiji, ambapo timu yetu itawakilisha na mabondia wanne na makocha wao wawili," alisema Mashaga.
Katibu huyo aliwataja mabondia hao kuwa ni Emilian Patrick atakayepigana uzani wa Feather, Martin Joseph (Middle) na Seleman Kidunda na Macmillian Patrick ambao watapigana uzito wa juu (kilo 91).
"Hao ndio mabondia watakaiwakilisha Tanzania baada ya kufanyika mchujo chini ya makocha, Hurtado Pimenter na msaidizi wake, ambao nao wapo kwenye msafara huo wa kwenda Msumbiji," alisema.
Mashaga alisema BFT ina imani kubwa kwa timu hiyo kufanya vema kama mabondia na makocha wao walivyowaahidi Watanzania kwamba wanaenda kushindana na sio kushiriki au kuwa wasindikizaji.
Mara ya mwisho Tanzania kufanya vema kwenye mashindano hayo kwa upande wa ngumi ilikuwa michuano ya mwaka 2007, yaliyofanyika nchini Algeria ambapo bondia Emilian Patrick aliambulia medali ya fedha.
Wakati huohuo timu ya taifa ya michezo ya Walemavu (Paralimpiki) yenye wachezaji watano inatarajiwa kuondoka Jumatano kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo ya All African Games.
Timu zingine zitakazowakilisha Tanzania katika michezo hiyo ya 10 ya Afrika itakayofanyikia kwenye dimba la Zimpeto, mjini Maputo ni zile za Riadha, Netiboli na Soka ambazo zitaondoka pia Jumatano.

Mwisho

Villa yaapa kufa na Simba, yadai ushamba umeshawatoka




KLABU ya soka ya Villa Squad umedai 'ushamba' waliokuwa nao katika Ligi Kuu Tanzania Bara umeshawatoka na kuionya Simba isitarajie mteremko kwenye pambano lao lijalo.
Simba waliopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo nyuma ya Toto Afrika, itaikaribisha Villa katika pambano litakalochezwa Septemba 8, uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga.
Licha ya uongozi huo wa Villa, kukiri kuwa Simba ni timu nzuri, bado wanaionya kwamba isitarajie wepesi kutokana na kikosi chao kujipanga kuwakabili ili kushinda mchezo huo.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi, alisema mapema leo asubuhi kuwa, kipigo cha mabao 3-0 walichopewa na Toto Afrika katika mechi yao ya awali iliwatoa ushamba na kwa sasa kikosi chao kimeanza kuizoea ligi hiyo na kuonyesha ushindani wa kweli.
Uledi, alisema kuthibitisha hilo waliweza kuibana Kagera Sugar nyumbani kwao na kutoka sare ya bao 1-1 , hali inayowafanya kujiamini wanaweza kuikabili timu yoyote ikiwemo Simba na Yanga.
"Aisee tunaendelea kujiandaa kwa ajili ya pambano letu na Simba, kifupi ni kwamba tumeshaanza kuizoea ligi na kwamba wapinzani wetu wasitarajie mteremko Mkwakwani, hiyo Septmba 8," alisema.
Aliongeza, benchi lao la ufundi linatumia mapumziko ya wiki moja ya ligi kuu kurekebisha matatizo yaliyotokea katika mechi za awali ili kuweza kuingia dimbani kuikabili Simba wakiwa fiti.
"Timu inaendelea kujifua na tuna imani mapumziko yaliyopo yatawapa nafasi makocha na wachezaji kuweka mambo sawa," alisema.
Uledi alisema wachezaji wao wawili waliokuwa majeruhi wameanza kupaata nafuu na kwamba hadi siku ya pambano hilo hali yao itakuwa imetengemaa na kurejea dimbani kuisaidia timu yao.
Klabu hiyo ya Villa Squad inayoshikilia mkia kwa sasa katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi moja, ni miongoni mwa timu nne zilizopanda ligi kuu msimu huu, nyimngine zikiwa ni Coastal Union, JKT Oljoro na Moro United.

Mwisho

Saturday, August 27, 2011

Mnanda wamtoa Ferouz wa Daz Nundaz


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Feruzi Mrisho 'Ferouz' aliye mbioni kuachia kazi yake mpya iitwayo 'Ndege Mtini', amedai kibao hicho alichokiimba katika miondoko ya Mchiriku utamrejesha kwenye chati yake ya zamani.
Ferouz aliyekuwa kimya karibu miaka mitatu iliyopita, alisema aliamua kuimba kibao hicho kipya alichomshirikisha chipukizi wa THT, Shoz Dia, miondoko ya 'mnanda' ili kurudi upya.
"Nimeamua kutoa upya na mnanda kwa nia ya kurejesha makali yangu, pia kuonyesha utoauti wa Ferouz wa Das Nundaz au wa 'Starehe' na huyu wa sasa," alisema.
Mkali huyo aliyetamba na vibao kadhaa kikiwemo hicho cha Starehe alichoimba na Profesa Jay, alisema kibao hicho cha Niwqe Nawe anachojiandaa kukifyatulia video yake, ni utangulizi wa ujio wa albamu yake mpya itakayofahamika kwa jina la 'Reserve'.
Aliongeza ndani ya albamu hiyo atakayowashirikisha wasanii kadhaa nyota akiwemo mshindi wa Tuzo Tano za Kili Music Awards-2011, 20 Percent itakuwa na nyimbo nane.
Feropuz alizitaja nyimbo hizo kuwa ni pamoja na Ndege Mtini, Nimemfukuza, 'Reserve' na Tusifuatane.
Hiyo itakuwa ni albamu ya tatu kwa mkali huyo kwani baada ya kutoa albamu ya 'Safari' mwaka 2004 iliyokuwa na wimbo wa Starehe, alifyatua nyingine ya pili iitwayo Sauti Nyimbo na Vyombo iliyokuwa na wimbo wa 'Mr Policeman, kabla ya kutoweka hadi alipobuka juzi.

Mwisho.

Kaseba, Oswald kuzipiga Okt Mosi




BINGWA wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini, Ernest Bujiku na Chaurembo Palasa ni kati ya mabondia watakaopanda ulingoni kusindikiza pambano la mkongwe Maneno Oswald na Japhet Kaseba litakalofanyika Oktoba Mosi.
Pambano hilo la raundi 10 lisilo la ubingwa la uzani wa kilo 72 la Kaseba na Oswald maarufu kama Mtambo wa Gombo litafanyikia kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine Magomeni likisimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini, PST, chini ya uratibu wa promota, Gervas Muganda wa kampuni ya Babyface ya jijini Dar.
Akizungumza na Micharazo jana, Kaseba, alisema kabla ya yeye kupigana na Oswald watasindikizwa na michezo kadhaa akiyataja baadhi likiwakutanisha Chaurembo Palasa dhidi ya Sweet Kalulu, Ernest Bujiku atakayepigana na Mbukile Chuwa.
Kaseba alisema pia siku hiyo Venance Mponji atapanda ulingoni kuzipiga na Jafar Majiha 'Mr Nice' na kutakuwa na michezo miwili ya kick boxing ambapo Ramadhani Mshana atapigana na Hamed Said na jingine la wapiganaji chipukizi.
Mkali huyo alisema amekuwa akiendelea kujifua vema ili kuweza kukkabili Oswald aliyekiri ni mmoja wa mabondia bora na wenye uwezo mkubwa katika mchezo huo.
"Naendelea kujifua kwa lengo la kutaka kumshinda Oswald ambaye namheshimu kwa umahiri wake katika mchezo wa ngumi, naamini nikizembea anaweza kunitoa nishai," alisema Kaseba.
Katika hatua nyingine, bondia Stan Kessy anatarajiwa kupanda ulingoni Septemba 25 kupigana katika pambano lisilo la ubingwa dhidi ya Seleman Habib, ambalo litasindikizwa na michezo mitano tofauti ya utangulizi.
Mratibu wa pambano hilo litakalofanyikia kwenye ukumbi wa Friend's Rangers jijini Dar es Salaam, Dk John Magambo, alisema Kessy na Habib watapigana kwenye uzani wa middle raundi 10 na kusindikizwa na mabondia wengine.
Dk Magambo aliwataja watakaowasindikiza wawili hao ni Salehe Mkalekwa atayaepigana na Jafari Majiha, Doto KIpacha dhidi ya Jones Godfrey, Yohana Thobias atayepigana na Huseni Mashaka na Omar Rajab dhidi ya Husseni Mandula.

Mwisho

UAE embassy used US$ 80,000 for Tanzania Moslems



The United Arab Emirate (UAE) embassy in the country through its charity organization Khalifa Bin Zaayid Al Nahyaan has set aside $80.000 to provide food and other necessities to Muslims in the country during this holly months of Ramadhan.
Disclosing this, Abdallah Ahmedna, who represented UAE ambassador to the country, Mallalla Mubarak Al –Ameri he said the money has been set aside to help people during this month of ramadhan, he said it’s the traditional of his embassy to help people especially this holly months.
He was speaking this at a futari provided by his embassy at Anwar mosque in Msasani.
“This is the fourth year for our embassy through Khalifa Bin Zaayid Al Nahyaan to provide food and money to people during this month of ramadhan” he said
Ahmedna also disclosed that from tomorrow his embassy will start giving out money to the elderly, the disabled and other less privileged people, he said the money will help them to buy food and other necessities at Eid El Fitry .
He disclosed that the exercise will begin at Al Rahman mosque in Kinondoni

Ubalozi watumia Dola 80,000 kufuturisha waislam Tz




UBALOZI wa Nchi ya Falme za Kiarabu, UAE nchini kupitia taasisi ya kutoa huduma za kijamii ya Khalifa Bin Zaayid Al Nahyaan, umekuwa ukitumia Dola za Kimarekani 80,000 kila mwaka kufutisha waumini wa kiislam waliopo jijini Dar na mikoa mingine.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Mhasibu wa Ubalozi huo, Abdallah Ahmedna, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Balozi wa UAE, Sheikh Mallalla Mubarak Al Ameri wakati wa kuwaturusiha waumini wa msikiti wa Anwar, Msasani.
Ahmedna, alisema fedha hizo zimekuwa zikitolewa karibu mwaka wa nne sasa na ubalozi wao kwa ajili ya kuwafuturisha na kuwasaidia waumini wa misikiti 10 iliyopo mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mwanza, Tanga, Pwani na Mtwara.
Alisema, msaada huo wa futari, daku na fedha kwa wasiojiweza hutolewa kwa muda wa mwezi mzima wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani kila mwaka, ambapo kwa Dar mbali na msikiti wa Anwar mwingine unaonufaika ni Al Rahman, uliopo Kinondoni.
"Kama waislam tumekuwa tukithamini waumini wa Tanzania kwa kuwafuturisha pamoja na kuwapa misaada, ambapo ubalozi umekuwa ukifadhili misaada hiyo kwa kiasi cha Dola za Kimarekani 80,000 kwa kila mwaka," alisema.
Baadhi ya waumini waliofuturishwa msikiti hapo waliushukuru ubalozi huo na kuomba watu wengine wenye uwezo kuiga mfano huo wakidai mwezi huu ndio wa waumini wa kweli kuonyesha upendo, ukarimu na kuhurumiana katika kutekeleza nguzo ya nne kati ya tano za Imani za Kiislam.

Mwisho

Sekretarieti ya CCM yashtukiwa, ila Nape mmmh!



WASOMI wa Vyuo vya Elimu ya Juu wanaokiunga mkono chama tawala, CCM, wamemtaka Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye asitishwe na kauli za watu wachache katika kuendeleza moto aliouanza dhidi ya vigogo wanaoatakiwa kujivua gamba wakiapa kumuunga mkono kwa hali yoyote.
Kadhalika wanachama wa CCM hasa vijana wajipange na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi ndani ya Jumuiya ya chama hicho, ili kuleta mabadiliko yatakairejeshea heshima chama hicho mbele ya wananchi.
Katibu wa Shirikisho la Wana-CCM Vyuo vya Elimu ya Juu mkoa wa Dar es salaam, Asenga Abubakar, alitoa kauli hizo juzi kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari akizungumzia kufifia kwa moto ulioanzishwa na Sekratarieti ya chama chao.
Abubakar, alisema moto ulioanzishwa na sekretarieti ya chama hicho chini ya Katibu Mkuu, Wilson Mukama, ni kama imefifia na hasa zile kelele zilizokuwa zikitolewa na Nape Nnauye, wakidai huenda zimetokana na vitisho vinavyotolewa dhidi yao.
Hata hivyo shirikisho hilo lilimtaka Nnauye, kutohofia vitisho hivyo na badala yake aendeleze moto zaidi ili kuhakikisha chama cgao kinasimama imara dhidi ya wachache wanaoutolea macho nafasi ya Urais kwa Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
"Tunamuomba asitishwe na wanaoutolea macho uraisi wa 2015 na wafuasi wao, sisi tunamuonga mkono na tupo pamoja nae dhidi ya wachache hao wenye njaa," taarifa hiyo ya Abubakar inasomeka hivyo.
Taarifa hiyo ya Abubakar, licha ya kuihimiza sekretarieti hiyo kusimama imara, pia imewaomba na kuwataka wanachama wa CCM waliopo vyuoni na vijana kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuwania nafsi katika uchaguzi mkuu wa chama hjicho utakaofanyika mwakani, ili kuleta mabadiliko mbele ya umma wa Watanzania.
Kadhalika shirikisho hilo limesisitiza kwa kuwataka vijana wasiamini kwamba ndani ya CCM kuna ufisadi, bali wafuasi wachache wa chama hicho ndio wenye vitendo hivyo na hivyo wakijitokeza kushiriki uchaguzi watasaidia kurahisisha dhana ya kujivua gamba na kukifanya CCM kiwe makini nchini.
Kwa muda mrefu ndani ya CCM kumekuwa na msigano wa shinikizo la kuwataka baadhi ya wanachama wao wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ufisadi kujivua gamba, kitu kilichomlazimisha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga, Rostam Aziz kung'atuka.
Wengine wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo walipewa muda hadi mwezi ujao kuamua mwenyewe kufuata mkumbo wa Rostam au wang'olewe kwa nguvu.

Wasomi CCM, wamlilia Kikwete avunje ukimya kwa yanayoendelea nchini



RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzaania, Dk Jakaya Kikwete ametakiwa kutekeleza kwa vitendo dhana ya uwajibikaji kwa kuwatimua kazi mawaziri ambao wizara zao zimekumbwa na kashfa ikiwemo wa Nishari na Madini na ile ya Maliasili na Utalii.
Aidha serikali imeombwa kuchukua hatua ya haraka katika kutatua matatizo yaliyopo katika sekta ya elimu ikiwemo suala la kutimuliwa kwa wahadhiri na kusimamishwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma, UDOM, taasisi ya IMTU na Chuo cha Ustawi wa Jamii.
Wito huo umetolewa na Shirikisho la Wana-CCM Vyuo vya Elimu ya Juu mkoa wa Dar es Salaam, katika mkutano wa viongozi wake na waandishi wa habari uliofanyika juzi jijini humo.
Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Lusekelo Mwandemange, alisema bila Rais Kikwete kufanya maamuzi magumu katika utekelezaji wa vitendo dhana ya uwajibikaji ni wazi serikali yake itaendelea kupoteza sifa mbele ya wananchi.
Mwandemange alisema kwa kuwa dhana ya uwajibikaji ipo ndani ya CCM tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa, Mwl Nyerere, katika kulinda maadili ya viongozi ni vema Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa akatekeleza kwa kuwawajibisha baadhi ya watendaji wake.
Mwenyekiti huyo alisema kwa kashfa zilizoikumba wizara za Nishati na Madini na ya Maliasili na Utalii za kusimamishwa baadhi ya watendaji wake haipaswi kuachwa kwa wahusika tu bila mawaziri wanaoziongoza wizara hizo kuwajibishwa kwa yaliyotokea.
Mwandemange alisema ni vigumu wananchi kuielewa serikali kama watu waliovurunda mambo serikalini wakapewa likizo za malipo na kurejeshwa kinyemela kwa bashasha kama mashujaa, wakati wanafunzi wanaosimama kutetea haki zao wakitimuliwa vyuoni bila huruma yoyote.
"Tunamuomba Mwenyekiti wetu wa CCM ambaye ndiye Rais wa Jamhuri, afumbe macho na kuwapiga chini (kuwaondoa) viongozi wote dhaifu serikalini, bila kufanya hivyo hatutaweza kurudisha taswira nzuri ya serikali na chama mbela ya wananchi," alisema Mwandemange.
Aliongeza pia kwa kulipongeza Bunge la Jamhuri kwa uamuzi wa kuunda Tume ya

kuchunguza upya sakata la katibu wa wizara ya Nishati na Madini, akiiomba Tume hiyo isiishie kwa David Jairo, bali iimulike wizara nzima pamoja na wizara nyingine za serikali zilivurunda.
"Tume hiyo ichunguze kashfa ya wizara ya Maliasili na Utalii ambayo waziri wake, Ezekiel Maige aliwasimamisha watendaji wake akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Wanyama Pori nchini, Obed Mbangwa bila mwenyewe kuwajibika kwa hilo," alisema.
"Kwa hili tunashangaa waziri anaendelea kukalia kiti kwa kuwasimamisha kazi watendaji wake kwa staili ile ile ya Jairo, alikuwa wapi siku zote hadi wabunge walipofichua, lazima naye awajibike, ndio maaana tunamkata Rais avunje ukimya kwa kuwajibisha wahusika," aliongeza.
Shirikisho hilo liligusia matatizo ya sekta ya elimu yaliyopo katika baadhi ya vyuo vikuu nchini kwa kuitaka serikali ichukue hatua za haraka kuyatatua, licha ya kuipongeza kwa uamuzi wa kuongeza posho za wanavyuo kutoka Sh 5,000 hadi kuwa Sh 7,000.
Uongozi wa shirikisho hilo kupiotia taarifa yao iliyosainiwa na Katibu Mkuu wao, Asenga Abubakar, umesema hawakubaliani na maamuzi ya fedha za mikopo kupelekwa moja kwa moja vyuoni badala ya Bodi ya Mikopo kama zamani wakidai itazidisha matatizo.
Pia waliiomba serikali kuwarejesha wanafunzi na wahadhiri walitimuliwa na kusimamishwa vyuo vya Chuo cha Ustawi wa Jamii, taasisi ya IMTU na UDOM, wakidai kinachofanywa dhidi yao ni uonevu aliodai kama shirikisho hawaridhiki nayo.

Monday, August 8, 2011

RITA yaingilia kati mgogoro wa Answar Sunna

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini, RITA, umewataka waumini wa Jumuiya ya Answar Sunna Tanzania wanaoshinikiza uongozi wa juu ya jumuiya hiyo ung'oke madarakani kutulia hadi watapotoa maamuzi yao mwishoni mwa mwezi huu.
Waumini hao wa Answar Sunna wanataka uongozi wao ung'oke kwa kukiuka katiba na kushindwa kuiendesha kwa mafanikio jumuiya yao inayotajwa ni taasisi kubwa ya pili nchini baada ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania, BAKWATA.
Meneja wa Ufilisi na Udhamini wa RITA, Linna Msanga Katema, aliiambia MICHARAZO kuwa, ofisi yao inatambua kuwepo kwa mgogoro ndani ya jumuiya hiyo baina ya waumini na uongozi wao na wanaendelea kuufanyia kazi.
Linna, alisema hatua waliyofikia katika kuutatua mgogoro huo ni vema waumini kupitia kamati yao maalum wakavuta subira ili waweze kutoa maamuzi mwishoni mwa mwezi huu baada ya kukutana na kupitia vielelezo vya pande hizo mbili.
Meneja huyo, alisema tofauti na hapo awali walipokuwa wakikosa ushirikiano toka kwa viongozi wanaolalamikiwa wakiwemo Baraza la Wadhamini na Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Juma Poli, sasa mambo ni shwari na ndio maana wanataka waumini watulie.
"Tumeshawaandikia barua kuomba watupe muda wa mwezi mmoja toka Julai 26 hadi Agosti 26, ili RITA tutoe maamuzi juu ya kinachoendelea baina ya pande hizo mbili, hivyo tunaomba waumini watulie haki itatendeka," alisema Linna.
Nao waumini hao waliofanya mkutano wao Jumapili iliyopita walitoa maamuzi ya kuvuta subiri ili kuona RITA itaamua nini, lakini wakisisitiza wanataka haki itendeke kwa manufaa ya jumuiya yao waliyodai inazidi kudumaa kutokana na uongozi uliopo.
Wakizungumza kwenye mkutano huo waumini hao waliutaka uongozi wa kamati yao inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Hamis Buguza na Katibu, Abdulhafidh Nahoda, kuendelea kufuatilia kujua RITA itaamua kitu gani na wao wameamua kuvumilia.
Mzozo wa waumini na uongozi wa jumuiya hiyo ulianza tangu mwaka juzi kutokana na madai ya ukiukwaji katiba ikiwemo kutoitishwa kwa mikutano kwa muda wa miaka 10, pamoja na kubinafsishwa mali za jumuiya hiyo bila waumini hao kushirikishwa.
Katibu wa Baraza la Wadhamini wa Jumuiya, Abdalla Lihumbi, alinukuliwa na gazeti hili wiki iliyopita akikiri uongozi wao kwenda kinyume akidai wanafanya mipango ya kupata suluhu kwa manufaa ya jumuiya yao iliyotambuliwa kitaifa mwaka 1992.

Mwisho

Simba Day ni leo Arusha, uhondo wapungua




KUHAMISHWA kwa tamasha la klabu ya Simba, 'Simba Day' kupelekwa jijini Arusha kumevuruga baadhi ya ratiba zilizokuwa zimepangwa, ingawa uongozi umesema kila kitu kipo sawa na kwamba leo watatambulisha rasmi kikosi chao kipya cha msimu huu jijini humo.
Tamasha hilo linalofanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo, awali lilipangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, lakini limekwama baada ya kukosekana muafaka wa malipo baina ya uongozi wa klabu hiyo na ule unaosimamia uwanja wa Taifa, na kulazimika kupelekwa Sheikh Amri Abeid.
Kutokana na kuhamishwa huko mkoani Arusha, baadhi ya mambo yaliyotarajiwa kufanyika leo kama pambano la timu za vijana za Simba na Azam U20 limefutwa na badala yake itachezwa mechi ya timu ya veterani ya Arusha dhidi ya viongozi wa Simba.
Kadhalika, bendi na vikundi vilivyokuwa vitumbuize katika tamasha hilo, pia vimeshindikana sawa na tukio la utoaji wa tuzo za wadau walioisaidia Simba kwa hali na mali, ambapo kesho watapewa wachache watakaobahatika kwenda jijini Arusha na wengine watatangazwa tu.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliiambia MICHARAZO, kuwa pamoja na hali iliyotokea iliyowatatiza kidogo, kila kitu kinatarajiwa kufanyika kwa ufanisi leo ambapo timu yao itakitambulisha rasmi kikosi chao kipya chenye wachezaji wapya wa kimataifa.
"Ni kweli kuhamishwa kwa tamasha hili toka Dar hadi Arusha kumevuruga baadhi ya mambo, lakini kila kitu kipo sawa na wakazi wa Arusha watarajie burudani ya kutosha kwani mambo yamerekebishwa, ili kufanikisha tamasha hilo," alisema Kamwaga.
Kamwaga, alisema kikosi chao tayari kipo jijini humo tangu Ijumaa kikijifua kabla ya leo kuvaana na Simba ya Uganda iliyotarajiwa kutua jana na kusafiri kwenda Arusha kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa.
Alisema kikosi chao kipo kamili ukiondoa Mwinyi Kazimoto anayeendelea kujiuguza majeraha yake aliyopata siku ya mechi ya fainali ya Kombe la Kagame kati ya Simba na Yanga, huku wachezaji wengine wawili, Ulimboka Mwakingwe na Amri Kiemba wakirejea toka majeruhi.
Kamwaga alisema watatumia tamasha hilo na hasa mechi yao na Simba ya Uganda kupima kikosi chao kabla ya kuvaana na Yanga wiki ijayo katika pambano la Ngao ya Jamii ikiwa ni uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Agosti 17 katika pambano litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, ikiwa ni wiki kadhaa tangu timu hizo kukutana kwenye fainali hizo za kombe la Kagame na Yanga kuibuka mshindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mghana Kenneth Asamoah.

Mwisho

Villa Squad yahaha kusaka Mil 7.2 kuianza Ligi Kuu

UONGOZI wa klabu ya soka ya Villa Squad inahaha kusaka kiasi cha Sh. Milioni 7 kwa ajili ya kuiwezesha timu yao kwenda kuianda Ligi Kuu Tanzania Bara 2011-2012 ugenini Kanda ya Ziwa, huku aliyekuwa mlezi wao, Abdalla Bulembo akisisitiza kujiweka kando katika uongozi.
Villa iliyorejea kwenye ligi hiyo baada ya kushuka daraja mwaka 2008, imepangwa kuanza mechi zake kwa kucheza na Toto Afrika siku ya uzinduzi wa ligi hiyo Agosti 20 kabla ya kuivaa Kagera Sugar ndipo irejee Dar es Salaam kucheza mechi za nyumbani.
Habari za ndani za klabu hiyo zilizothibitishwa na uongozi wake zinasema kuwa, kwa bajeti ya haraka inayotakiwa kwa timu hiyo kwenda kucheza mechi hizo mbili za awali za Ligi Kuu inahitajika kiasi cha Sh. Milioni 7.2 ambazo klabu haijui itazipata wapi kwa sasa.
Katibu wa Villa, Masoud Yasin, alisema kinachowachanganya zaidi ni kuchelewa kutolewa kwa fedha toka kwa wadhamini ambazo kwa kawaida hupitia Shirikisho la Soka Tanzania, TFF na kutoa wito kwa wadau wa soka wa Dar es Salaam hasa wakazi wa Kinondoni kuwasaidia.
"Tunaomba wadau wa soka watusaidie ili Villa tuweze kuianza ligi kwa umakini kwani tuna hali mbaya ya kiuchumi, na hasa kuzisaka fedha hizo kwa ajili ya mechi hizo mbili za kanda ya Ziwa ambapo bajeti yake ni zaidi ya Sh. milioni saba," alisema katibu huyo.
Yasin, alisema hali yao kiuchumi ni mbaya na hawajui watafanyaje katika ushiriki wao hasa baada ya mlezi wao, Abdalla Bulembo kujiweka kando akikataa hata kuzishika nafasi ambazo zipo nje ya katiba yao kama pendekezo lililotolewa na Rais wa TFF, Leodger Tenga.
Tenga alitoa pendekezo hilo wakati akitatua sakata la kuenguliwa kwa Bulembo kuwania Uenyekiti wa Villa na kuibua mtafaruku kabla ya kutulizwa kwa uchaguzi huo kufanyika kwa kuachwa wazi nafasi zilizokosa wagombea wake ikiwemo hiyo ya Mwenyekiti.
Bulembo mwenyewe alipotafutwa na gazeti hili, alikiri ni kweli hana haja ya uongozi baada ya TFF kumwekea kauzibe, ingawa alisema anasikitika na hali inayoendelea na viongozi wa soka nchini kushindwa kuonyesha dhamira ya kweli ya kuinua mchezo huo kupitia klabu ndogo.
"Sitaki hata kusikia habari za kuongoza tena, maadam TFF iliamua kunikwamisha basi mie naendelea na shughuli zangu, ila sidhani kama viongozi wa soka nchini wanania ya kuinua mchezo huu," alisema Bulembo.
Villa ni miongoni mwa timu nne zilizopanda ligi kuu toka daraja la kwanza nyingine zikiwa ni JKT Oljoro Arusha, Coastal Union ya Tanga na Moro United ya Dar es Salaam na tayari TFF imeshatangaza ratiba ya kuanza kwa ligi hiyo Agosti 20 ikishirikisha jumla ya timu 14.

Mwisho

Ubalozi wa UAE wafuturisha waislam Dar

UBALOZI wa Nchi ya Falme za Kiarabu, UAE nchini kupitia taasisi ya kutoa huduma za kijamii ya Khalifa Bin Zaayid Al Nahyaan, umeamua kuwafuturisha waumini wa dini ya kiislam wa Msikiti wa Al Rahman wa Dar es Salaam kwa mwezi mzima wa mfungo wa Ramadhani.
Msaada huo wa futari unaoambatana na tende, ulianzwa kutolewa juzi jioni ambao mamia ya waumini wa msikiti huo walipata fursa ya kufuru chakula hicho kabla ya usiku kugawiwa tende zilizotolewa na ubalozi huo wa UAE.
Imamu wa Msikiti huo wa Al Rahman uliopo eneo la Kinondoni, Sheikh Abdullah Salim Bahssany, akiwahutubia waumini wake wakati wakigawiwa futari hiyo, alisema huo ni msaada toka ubalozi wa UAE na utakuwa ukitolewa hapo kila siku hadi mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapomalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Imamu huyo aliwaambia waumini hao kuwa wale waliokuwa na shaka na kupata futari katika funga zao, waondoe hofu kwani sasa watakuwa wakipata chakula hicho, huku akiushukuru ubalozi huo kwa ukarimu iliyouonyesha kwa waumini hao.
"Jamani futari mnayokula leo imetolewa na ubalozi wa nchi za Falme za Kiarabu na msaada huu utakuwa ukitolewa kwa mwezi mzima katika mfungo huu wa Ramadhani hivyo msiwe na hofu katika funga zenu,"alisema Sheikh Bahssany.
Baadhi ya waumini waliofuturishwa msikiti hapo waliushukuru ubalozi huo na kuomba watu wengine wenye uwezo kuiga mfano huo wakidai mwezi huu ndio wa waumini wa kweli kuonyesha upendo, ukarimu na kuhurumiana katika kutekeleza nguzo ya nne kati ya tano za Imani za Kiislam.

Mwisho

Kondoo mwenye maandishi ya kiarabu azaliwa Kilimanjaro


KONDOO MWENYE MAANDISHI WA KIARABU YANAYOTAFSIRIKA 'YASIN' AKIWA KANDO YA MAMA YAKE PICHA KWA HISANI WA BLOG YA BURUDAN