STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 7, 2013

Mbunge wa CCM ahukumiwa kifungo cha miezi 10 jela

MBUNGE wa Mbarali, Modestus Kilufi (CCM) amehukumiwa kifungo cha miezi 10 baada ya kupatikana na hatia ya kutishia kuua, Mbunge huyo (51) alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 10 akidaiwa kutishia kumuua Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa, Mbarali, Jordan Masweve.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo leo Mbunge aliomba Mahakama impunguzie adhabu, kwani ana watoto watano kati yao wawili wanasoma Chuo Kikuu na wananchi wanamtegemea kuwasilisha matatizo yao bungeni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Michael Mteite, alisema ameridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Epimack Mabrouk na Griffin Mwakapeje, pia mawakili wa upande wa mashitaka walimwomba Hakimu Mteite kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

"Kutokana na maelezo hayo na ushahidi ulioletwa mahakamani, ninakuhukumu kifungo cha miezi 10" alisema Hakimu Mteite.

Mbunge akihojiwa katika chumba cha mahakama alisema unajuwa siku hizi haki inatendeka pale tu iwapo mwanaCCM ametiwa hatiani, lakini kama ni mpinzani ametiwa hatiani utasikia ooh kaonewa au hii ni hukumu kutoka ikulu, hata hivyo alisema atakata rufaa katika hukumu hiyo.
Chanzo  http://networkedblogs.com

Mwili wa mume wa Khadija Kopa azikwa kwao Bagamoyo jioni hii

MWILI ya mume wa Malkia wa Mipasho nchini,Khadija Kopa, Jaffar Ally umezikwa jioni hii wilayani Bagamoyo baada ya kufariki jana jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa watu waliousindikiza mwili wa marehemu Jaffar ambaye anayetajwa kuwa alikuwa pia ni Diwani wa CCM Kata ya Magomeni mazishi hayo yamefanyika muda mfupi uliopita.
Pichani juu ni baadhi ya wakazi wa mtaa wa Magomeni wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na waombolezaji wengine wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mume huyo wa muimbaji huyo wa kundi laTOT Taarab kuelekea kwenye makaburi kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Picha: Said Swala Iddy.

TFF yawashukuru wadhamini Stars kujitosheleza

Viongozi wa TFF, Rais Leodger Tenga na Katibu Mkuu, Angetile Osiah
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye vizuri katika mechi yake ya kesho (Juni 8 mwaka huu) dhidi ya Morocco mjini Marrakech.

Stars, ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake la mashindano ya awali ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast kwa tofauti ya pointi moja, inacheza na Morocco katika mechi ya nne itakayofanyika Marrakech baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Machi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.

“Katika kipindi chote hiki hatujawahi kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF.

“Lakini katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri; kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata kuzilipia ada ya kucheza mechi (appearance fee).

“Posho za wachezaji zimepanda kwa karibu mara mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”

Tenga alisema kuwa udhamini huo ndio sasa umeanza kuzaa matunda na timu inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na maandalizi ya muda mrefu.

“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee timu na tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia kwa kuwa vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.

Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.

Katika mkutano huo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda Morocco kuishangilia timu.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine zilitarajiwa kusafirishwa jana.

Tenga aitega serikali ushiriki timu za Tz Kagame Cup Darfur

Rais wa TFF, Leodger Tenga
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.

Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.

“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.

“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.

“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”

Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.

Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.

“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.

“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.

Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.

“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.

“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”

Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.

“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.

“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”

Kaseba atamba kumnyuka Mmalawi kesho

http://2.bp.blogspot.com/-BqJYPtcUVOo/UNGU6CtcSXI/AAAAAAAABH4/vAtCOs_aM_M/s640/Japhet+Kaseba.jpg
Japhet Kaseba
 
 
Baadhi ya Mabondia watakaomsindikiza Kaseba atakapovaana na Mmalawi kesho
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchinim, Japhet Kaseba kesho anatarajiwa kupanda ulingoni kuzichapa na mpinzani wake kutoka Malawi, Rasco Chimwanza akiahidi kupata ushindi katika pambano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, Dar es Salaam.
Mabondia hao wawili walipimwa uzito na afya zao leo zoezi lililosimamiwa na Anthony Ruta, Ibrahim Kamwe, Pendo Njau na Dk John Lugambila na kugundulika kuwa wote wapo fiti tayari kuonyeshana kazi kesho.
Katika upimaji huo, Kaseba amejinadi atamsambaratisha mpinzani wake katika raundi za mapema za mchezo huo.
Kaseba na Mmalwi huyo watasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi ambapo Juma Fundi atapigana na Hassani Kiwale maarufu kama Moro Best,Joseph Onyanyo wa Kenya ataonyeshana kazi na Seba Temba wa Morogoro, huku Issa Omar 'Peche Boy'atavaana na Juma Seleman na michjezo mingine kadhaa.

Kim Poulsen aahidi ushindi ugenini kesho dhidi ya Morocco

Kocha Kim Poulsen

Kikosi cha Stars

Na Boniface Wambura, Morocco
TIMU ya taifa, Taifa Stars inatupa karata yake ya pili ugenini kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia kwa kesho (Juni 8 mwaka huu) kuikabili Morocco (Lions of the Atlas) kwenye Uwanja wa Grand Stade hapa Marrakech, Morocco.

Ilipoteza ya kwanza ugenini dhidi ya Ivory Coast mwaka jana, na kushinda mbili mfululizo nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco. Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Morocco ni ya pili kwa Stars katika uwanja huo ambapo mwaka juzi ilifungwa mabao 3-1.

Washabiki wa Morocco wanaonekana kuikatia tama timu yao yenye pointi mbili tu nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kundi hilo la C ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Tanzania yenye sita. Huo ni mtazamo wa washabiki, lakini kwa upande wa timu inaonekana imepania kujichomoa katika nafasi za chini.

Kwa upande wa Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema timu yake imepania mechi hiyo, lengo likiwa ni kuona inapata matokeo mazuri baada ya dakika 90 za mechi hiyo itakayokuwa chini ya refa Daniel Frazier Bennett wa Afrika Kusini.

Amesema timu yake itacheza kwa umakini na uangalifu kwa vile wanajua wapinzani wao wakicheza mbele ya washabiki wao watakuwa katika shinikizo za kushinda, jambo ambalo wamejiandaa kukabiliana nalo.

Kwa upande wa maandalizi, Kim amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadhamini wa timu hiyo Kilimanjaro Premium Lager wameiandaa vizuri kwani iko kambini kwa wiki tatu sasa na kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan iliyochezwa wiki iliyopita nchini Ethiopia.

Stars iliifunga Morocco mabao 3-1 zilipokutana Machi 24 mwaka huu jijini Dar es Salaa. Lakini zilipokutana hapa Marrakech mara ya mwisho mwaka 2011, Morocco iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kim amesisitiza kuwa kikosi chake kimepania kufanya vizuri katika michuano hii ya mchujo ya Kombe la Dunia, ha hiyo inathibitishwa na matokeo ya timu kadri inavyoendelea kucheza mechi za mashindano.

“Moja ya mipango yetu katika mechi hizi za Kombe la Dunia ni kushinda nyumbani, hilo hadi sasa tumelifanya kwa asilimia 100. Lakini ili tukae vizuri zaidi tumekuja hapa Morocco kwa lengo la kupata matokeo mazuri, ingawa tunajua mechi itakuwa ngumi,” amesema kocha huyo raia wa Denmark.

Kwa hapa Marrakech mechi hiyo imekuwa haizungumzwi mara kwa mara, na kubwa ni kuwa Wamorocco wengi wanaamini kuwa timu yao ambayo hadi sasa ina pointi mbili haina nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.


Arsenal yaridhia Wenger kumsajili Rooney


http://i.dailymail.co.uk/i/pix/2012/12/21/article-2251594-165E1B03000005DC-807_634x569.jpg
Wayne Rooney

http://static.guim.co.uk/sys-images/Football/Pix/pictures/2009/8/1/1249153548354/Arsene-Wenger-001.jpg
Kocha Arsene Wenger

KLABU ya Arsenal ya England imempa ruksa Meneja wake Arsene Wenger kumnunua mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney  endapo atahisi kuwa mchezaji huyo anahitajika kwenye klabu hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis amenukuliwa na gazeti la The Sun akisema kuwa klabu yake ina uwezo wa kumnunua, Wayne Rooney kwa paundi milioni 25 na kumlipa mshahara wa paundi 200,000 kwa wiki sawa na anaolipwa kwenye klabu ya Manchester United kwa sasa .
Gazidis aliongeza kuwa, iwapo kocha wao (Wenger) atapeleka maombi ya kutaka kumnunua mchezaji huyo  bodi ya wakurugenzi haitakuwa na sababu ya kuyakataa kwa vile wanao uwezo wa kumnunua na kumlipa  mshahara huo mnono.
Rooney amekuwa kwenye wakati mgumu ndani ya klabu ya Manchester siku za karibuni juu ya hatma yakee Old Trafford baada ya kupeleka maombi ya kutaka kuuzwa mwishoni mwa msimu ulioisha hivi karibuni, huku klabu yake ikinyakua taji kwa kuwapokonya mahasimu wao Manchester City.
Hata hivyo duru za kimichezo zinasema kuwa, Rooney anajiandaa kubadilisha uamuzi wake wa kutaka kuondoka Old Trafford kwa kusalia baada ya kocha Sir Alex Ferguson kustaafu akitajwa hakuwa na uhusiano mzuri naye kwa siku za karibuni.
Tangu ilipotangazwa nia yake ya kuondoka United, klabu kadhaa zimekuwa zikipigana vikumbo kumnyemelea mshambuliaji huyo tegemeo wa timu ya taifa ya England zikijiandaa kumnunua zikiwemo Arsenal na PSG , lakini wakisubiri kupata maafikiano na klabu yake ya sasa ya United.

Miss Kigamboni, Sinza, Mbeya kupatikana leo


http://1.bp.blogspot.com/_PnI9d8LAaQQ/TIqmm7PZ5GI/AAAAAAAARos/mGUNpwjh1Po/s1600/fm8.jpg
Bendi ya FM Academia itakayopamba shindano la Redd's Miss Kigamboni

MREMBO atakayefanikiwa kutwaa taji la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" katika shindano litakalofanyika leo usiku kwenye ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni atajinyakuliwa zawadi ya Sh.500,000, imeelezwa.
Maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na warembo 12 kutoka sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam watapanda jukwaani kuwania taji hilo.
Akizungumza jana, mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa mrembo atakayeshika nafasi ya pili katika shindano hilo atapata zawadi ya Sh.300,000, mshindi wa tatu Sh.250,000 huku wawili watakaotangazwa kushika nafasi ya nne na ya tano kila mmoja ataondoka na Sh.200,000.
Somoe alisema kuwa warembo wengine saba waliobaki kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh.100,000.
Alisema bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma itatumbuiza katika shindano hilo ambalo kiingilio cha viti maalum ni Sh.10,000 na viti vya kawaida ni Sh. 5,000.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu.
Taji la Redd’s Miss Kigamboni linashikiliwa na Edda Sylivester ambaye pia ndiye mshindi wa kanda ya Temeke na alishika nafasi ya tatu katika shindano la Redd’s Miss Tanzania mwaka jana.
Aidha, shindano la Redds Miss Sinza pia litafanyika leo ambapo warembo 12 wanaowania taji la hilo watakapopanda jukwaani kwenye ukumbi wa Meeda Club kushindania taji hilo.
Mashindano hayo ambayo yamepangwa kuanza saa 1.00 usiku, yatashuhudia Redds Miss Tanzania, Brigitte Alfred akivua taji lake la kwanza katika usiku huo ambao utakuwa na burudani za kila aina. Mbali ya kuwa Miss Sinza, Brigitte  pia anashikilia taji la Redds Miss Tanzania.
Mratibu wa mashindano hayo, Majuto Omary alisema jana kuwa maandalizi yameshakamilika na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' itatumbuiza siku kwa mara ya kwanza na kutoa zawadi kwa wakazi wa Sinza na vitongoji vyake.
Wakati huo huo, Furaha Eliab anaripoti kutoka Mbeya kuwa warembo 12 kutoka katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Mbeya watachuana kuwania taji la Redd’s Miss Mbeya yatakayofayika kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari, muandaaji wa mashindano hayo, Gabriel Mbwile, alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika kesho kwenye viwanja vya City Pub vya jijini Mbeya na yatapambwa na msanii wa kizazi kipya, Bob Junior, maarufu kama Rais wa Masharobaro.
Alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia zawadi ya Sh. milioni 1, mshindi wa pili Sh.750,000 na wa tatu Sh.500,000.