Bendi ya FM Academia itakayopamba shindano la Redd's Miss Kigamboni |
MREMBO atakayefanikiwa kutwaa taji la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" katika shindano litakalofanyika leo usiku kwenye ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni atajinyakuliwa zawadi ya Sh.500,000, imeelezwa.
Maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na warembo 12 kutoka sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam watapanda jukwaani kuwania taji hilo.
Akizungumza jana, mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa mrembo atakayeshika nafasi ya pili katika shindano hilo atapata zawadi ya Sh.300,000, mshindi wa tatu Sh.250,000 huku wawili watakaotangazwa kushika nafasi ya nne na ya tano kila mmoja ataondoka na Sh.200,000.
Somoe alisema kuwa warembo wengine saba waliobaki kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh.100,000.
Alisema bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma itatumbuiza katika shindano hilo ambalo kiingilio cha viti maalum ni Sh.10,000 na viti vya kawaida ni Sh. 5,000.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu.
Taji la Redd’s Miss Kigamboni linashikiliwa na Edda Sylivester ambaye pia ndiye mshindi wa kanda ya Temeke na alishika nafasi ya tatu katika shindano la Redd’s Miss Tanzania mwaka jana.
Aidha, shindano la Redds Miss Sinza pia litafanyika leo ambapo warembo 12 wanaowania taji la hilo watakapopanda jukwaani kwenye ukumbi wa Meeda Club kushindania taji hilo.
Mashindano hayo ambayo yamepangwa kuanza saa 1.00 usiku, yatashuhudia Redds Miss Tanzania, Brigitte Alfred akivua taji lake la kwanza katika usiku huo ambao utakuwa na burudani za kila aina. Mbali ya kuwa Miss Sinza, Brigitte pia anashikilia taji la Redds Miss Tanzania.
Mratibu wa mashindano hayo, Majuto Omary alisema jana kuwa maandalizi yameshakamilika na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' itatumbuiza siku kwa mara ya kwanza na kutoa zawadi kwa wakazi wa Sinza na vitongoji vyake.
Wakati huo huo, Furaha Eliab anaripoti kutoka Mbeya kuwa warembo 12 kutoka katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Mbeya watachuana kuwania taji la Redd’s Miss Mbeya yatakayofayika kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari, muandaaji wa mashindano hayo, Gabriel Mbwile, alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika kesho kwenye viwanja vya City Pub vya jijini Mbeya na yatapambwa na msanii wa kizazi kipya, Bob Junior, maarufu kama Rais wa Masharobaro.
Alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia zawadi ya Sh. milioni 1, mshindi wa pili Sh.750,000 na wa tatu Sh.500,000.
No comments:
Post a Comment