STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 18, 2013

Miss Universe Tz 2013 akabidhiwa bendera

MREMBO wa Miss Universe Tanzania 2013 Betty Boniface Omara amekabidhiwa bendera leo na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Khamis Kagasheki.

Zoezi hili limefanyika katika ukumbi wa mkutano wa wizara hiyo tayari kwa safari yake ya kwenda kwenye mashindano ya Miss Universe yatakayofanyika Moscow nchini Urusi mapema mwezi Novemba.

Akimkabidhi bendera huku akimpongeza waziri Kagasheki pia amemtakia mafanikio mema huko aendako.

Betty pia aliwaahidi watanzania kuwa mbali na kurudi na ushindi lakini pia ataenda kuitangazia dunia kuacha kutumia nakshi(Mapambo) yanayotumia pembe za ndovu ili kumaliza tatizo la ujangili nchini.

Zoezi la kukabidhiwa bendera lilifanyika likishuhudiwa na Mkurugenzi wa Kitaifa Miss Universe Tanzania Maria Sarungi Tsehai.

Mashindano ya Miss Universe Tanzania 2013 yamedhaminiwa na hifadhi ya Taifa Tanapa na Mrembo Betty Boniface ameshaanza kutangaza hifadhi hizi kwa njia mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
 Mrembo wa Miss Universe Tanzania 2013 Betty Boniface Omara akipokea bendera ya taifa leo kutoka Waziri Maliasili na Utalii, Hamisi Kagasheki.

Mbeya City, Azam kuing'oa Simba kileleni VPL?

Vijana wa Mbeya City
Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kutimua vumbo kesho (Oktoba 19 mwaka huu) kwa mechi tano huku Mbeya City ikiikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, ambapo ushindi wowote unaweza kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza.
 

Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu ina pointi 17 sawa na Azam ambayo nayo ina nafasi ya kuing'oa Simba kama itaifunga Oljoro JKT wanaoumana nao jijini Arusha.

Simba wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa sasa ikiwa na pointi 18 na yenyewe itashuka dimbani Jumapili kuwakaribisha watani zao Yanga katika uwanja wa Taifa.


Mbali na mechi ya Mbeya City na JKT Ruvu na ile ya Oljoro dhidi ya Azam mechi nyingine zitazkazochezwa kesho ni Mtibwa Sugar na Mgambo Shooting (Uwanja wa Manungu, Turiani), Ashanti United na Ruvu Shooting (Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam) na Kagera Sugar dhidi ya Coastal Union (Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba).

Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea katika viwanja nane kesho (Oktoba 19 mwaka huu) huku Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ukiwa mwenyeji wa mchezo kati ya African Lyon na Friends Rangers.

Nayo Villa Squad itacheza na Green Warriors katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Polisi Morogoro na Kimondo (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Lipuli na Kurugenzi (Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa) na Mkamba Rangers dhidi ya Majimaji (Uwanja wa CCM Mkamba, Morogoro).

Toto Africans na Mwadui (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Polisi Dodoma na Polisi Tabora (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), wakati Polisi Mara na pamba zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Magari Maalum tu, pambano la Simba na Yanga J2

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura
MAGARI yenye shughuli maalumu tu ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanja wakati wa mechi ya Simba na Yanga itakayochezwa keshokutwa (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi itaanza saa 10 kamili jioni, na kila timu inaruhusiwa kuingia na magari matatu tu; gari la timu na mengine mawili ya viongozi. Ukaguzi wa kuingia uwanjani ni kwa watu wote, kwani utaratibu huo si wa kumdhalilisha mtu bali lengo lake ni kuhakikisha usalama.
Vilevile watu hawataruhusiwa kuingia uwanjani na mifuko ya aina yoyote ikiwemo mabegi, isipokuwa kwa waandishi wa habari wanaotumia mabegi hayo kwa ajili ya kubebea kamera zao. Pia hakuna wafanyabishara watakaoruhusiwa kufanya biashara katika maeneo yanayozunguka uwanja.
Kwa washabiki watakaokuwa katika mazingira ya kuwa kero kwa wenzao wakiwemo walevi hawataruhusiwa kuingia uwanjani, pamoja na wale wenye silaha kama bastola ambapo wakikamatwa wafikishwa polisi na baadaye kufunguliwa mashtaka kortini.
Barabara ya Uwanja wa Taifa itafungwa kuanzia saa 2 asubuhi upande wa Chang’ombe, hivyo washabiki wanatakiwa kununua tiketi zao mapema kesho (Jumamosi) ambapo zitaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali kuanzia saa 4 asubuhi.
Vituo hivyo ni mgahawa wa City Sports Lounge, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, mgahawa wa Brake Point uliopo Kijitonyama na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.

TFF bado ina kinyongo na Shafii Dauda yamchinja, ikitangaza majina wagombea uchaguzi mkuu, mwenyewe adai hakubali

Shafii Dauda 'Tishio' akiwa kwenye shughuli zake za habari
 KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza orodha ya mwisho ya wagombea wa uchaguzi wa TFF na wa Bodi ya Ligi (TPL Board) utakaofanyika baadaye mwezi huu, 'ikimchinja' tena Shafii Dauda katika kinyang'anyiro hicho.
Uchaguzi wa Bodi ya TPL utafanyika Oktoba 25 mwaka huu wakati ule wa TFF utafanyika Oktoba 27 mwaka huu. Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa TPL Board na ule wa TFF zimeanza leo (Oktoba 18 mwaka huu)  zitamalizika siku moja kabla ya uchaguzi saa 10 kamili alasiri. Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni amewataja wagombea kwa upande wa TPL Board kugombea uenyekiti ni Hamad Yahya Juma (Mtibwa Sugar), Makamu Mwenyekiti ni Said Muhammad Said Abeid (Azam). Wanaowania ujumbe wa Bodi ya Uendeshaji ni Kazimoto Miraji Muzo (Pamba) na Omary Khatibu Mwindadi (Mwadui).
Wagombea kwenye uchaguzi wa TFF ni Athuman Jumanne Nyamlani na Jamal Emily Malinzi (Rais), Imani Omari Madega, Ramadhan Omar Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais).
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera), Jumbe Odessa Magati, Mugisha Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Lufano (Kanda namba 2- Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu).
Ali Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omar Walii Ali (Kanda namba 4- Arusha na Manyara), Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamis Kitumbo (Kanda namba 5- Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo (Kanda namba 6- Katavi na Rukwa), Ayoub Shaibu Nyenzi, David Samson Lugenge, John Exavery Kiteve, Lusekelo Elias Mwanjala (Kanda namba 7- Iringa na Mbeya).
James Patrick Mhagama na Stanley William Lugenge (Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma), Athuman Kingombe Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder (Kanda namba 9- Lindi na Mtwara), Hussein Zuberi Mwamba, Stewart Ernest Masima, Charles Komba (Kanda namba 10- Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala) na Twahil Twaha Njoki (Kanda namba 11- Morogoro na Pwani).
Davis Elisa Mosha, Khalid Abdallah Mohamed (Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani), Alex Crispine Kamuzelya, Kidao Wilfred Mzigama, Muhsin Said Balhabou na Omary Isack Abdulkadir (Kanda namba 13- Dar es Salaam).
Mbwezeleni amewataka wagombea kufanya kampeni bila kukashfu wenzao, kwani Kanuni ya Uchaguzi za TFF toleo la 2013 inatoa fursa kwa Kamati ya Uchaguzi kuwaondoa wagombea wa aina hiyo kwenye uchaguzi.
Aliyekuwa mgombea wa Ujumbe wa Kanda ya 13, Shafii Dauda ametoswa licha ya kulipa faini aliyotakiwa kulipa ndani ya siku tatu na Kamati ya Maadili ya Rufaa.
Akihojiwa muda mfupi uliopita na kituo cha Uhuru Fm, Shafii amesema hakubali hata kidogo na ameshaanza mchakato wa kupeleka malalamiko yake FIFA kwa madai kuna mchezo mchafu amefanyiwa na kamati hiyo ya uchaguzi ya TFF.
Shafii alisema tangu awali kulikuwa na zengwe kwa lengo la kuwabeba wagombea fulani kutetea nafasi zao na dai kwamba hana uzoefu ni sababu tu, lakini alisema hakubali haki yake ipotee bure na Jumapili atakwea pipa kwenda Zurich makao makuu ya FIFA kupeleka mashtaka yake.
Baadhi ya wadau wa soka waliozungumza na MICHARAZO wamedai kushtushwa na maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF wakidai ni kama kutaka kuleta malumbano yasiyokuwa na sababu yoyote.