STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 29, 2010

Mtakuwa wa kwanza kutupongeza kwa ubingwa-Adebayor

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Azam, John Bocco 'Adebayor' amesema pamoja na kwamba hajaonyesha makeke yake kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, bado anatumaini ya kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora.
Aidha nyota huyo amekiri kufanya vibaya kwa timu yao katika baadhi ya mechi zake kumewaweka mahali pabaya, lakini anaamini mwisho wa siku wanaoiponda Azam watakuwa wa kwanza kuwapongeza kwa taji la ubingwa.
Akizungumza na Micharazo, Bocco, alisema ingawa amechwa na washambuliaji Jerry Tegete na Mussa Mgosi wenye mabao zaidi yake, bado anaamini ataibuka kinara wa mabao.
Bocco alisema mabao mawili aliyoyapata kupitia mechi mbili ni dalili za wazi kasi yake haijapungua, ila kilichotokea ni hali ya kawaida ya soka lenye ushindani kama ilivyo msimu huu nchini.
"Sina hofu ya kiatu cha dhahabu, kwani najiona nipo vema kutokana na ukweli nimecheza mechi mbili na nina mabao mawili, wakati wenzangu wamecheza mechi kibao wamenipita mabao mawili tu," alisema Bocco.
Kuhusu kuboronga kwa timu yake nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa, alisema ni wameyumba, lakini hiyo haina maana ndoto yao ya kutwaa ubingwa ndio imeyeyuka kwa sababu mechi za ligi hiyo bado zipo nyingi.
"Wanaotucheka sasa ndio watakaokuwa wa kwanza kutupongeza, naamini tutakaa vema na kufanya vizuri katika mechi zetu zijazo kwa vile tuna kikosi kizuri kinachocheza kitimu haswa," alisema Bocco.
Timu hiyo iliyoshika nafasi ya tatu msimu uliopita hivi karibuni iliyumba katika mechi zake tatu baada ya kufungwa na Simba, Kagera Sugara na Toto Afrika kabla ya kuzinduka mwishoni mwa wiki kwa kuilaza African Lyon.
Kikosi cha timu hiyo kimesheheni nyota kama Mrisho Ngassa, Bocco, Kally Ongala, Patrick Mafisango, Peter Ssenyonjo, Jabir Aziz na wengineo.

Mwisho

Mgossi hana hofu ya kiatu cha dhahabu

NYOYA wa Simba na mpachika mabao bora msimu uliopita, Mussa Mgosi amesema kasi ndogo ya ufungaji mabao aliyoanza nayo kwenye Ligi Kuu msimu huu, haina maana kwamba makali yake ya kuzifuma nyavu yamekwisha.
Msimu uliopita, Mgosi alitwaa kiatu cha dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora na kumshinda aliyekuwa akichuana naye kwa karibu Mrisho Ngassa aliyekuwa akiichezea Yanga kabla ya msimu huu kujiunga na Azam FC.
Mgosi aliyeifunga Yanga mara mbili msimu uliopita, amesema hana sababu ya kuwa na hofu katika kupachika mabao kwani ndio kwanza ligi iko hatua ya awali.
Mgosi ameongeza pamoja na Jerry Tegete kurejesha mbio zake za ufungaji kama ilivyokuwa msimu, hana huwezo wa kuifikia kasi yake itakayoibuka tena msimu huu.
"Ligi ndio kwanza imeanza, sioni sababu ya wapenzi na mashabiki wa Simba kuwa na hofu kiatu cha dhahabu nitakitwaa tena na taji la ubingwa litaenda Msimbazi mwishoni mwa msimu huu," alisema.
Kuhusu pambano lao lijalo dhidi ya Yanga, Mgosi alisema kama ilivyokuwa msimu uliopita pia safari hii kajiandaa kuwazamisha watani zao ili kulinda heshima yao ambayo ilitibuliwa kwenye mechi ya ngao ya hisani ambapo Simba walilazwa mikwaju ya penati 3-1.
"Sitaki kuanza kusema sana, tusubiri Oktoba 16 itafika na utaona kitu gani nitakachoifanyia timu yangu dhidi ya Yanga," alisema.
Wakati ligi ikiingia mapumzikoni kupisha pambano la kuwania kufuzu fainali za Afrika za mwaka 2012, kati ya Tanzania na Morocco, Jerry Tegete ndiye aliyekuwa kiongoza kwa ufungaji magoli akipachika mabao manne dhidi ya matatu ya Mgosi.
Hata hivyo Mgosi alikuwa na nafasi ya kumpita Tegete kwani timu yao ilikuwa ikiumana na Mtibwa Sugar dimba la Jamhuri Morogoro, wakati tukiingia mitamboni.

AIBU! Ulimboka anaswa akihonga MtibwaWINGA wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya soka, Ulimboka Mwakingwe, alikamatwa na polisi na kulazwa korokoroni juzi kwa tuhuma za kumhonga fedha kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado ili aachie magoli wakati Mtibwa itakapocheza dhidi ya Simba katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo jioni.
Ulimboka alinaswa na kisha kutupwa mbaroni katika kituo cha polisi Mtibwa, ikiwa ni muda mfupi baada ya kunaswa kwenye eneo la kambi ya Mtibwa iliyopo Manungu, Turiani Morogoro, akidaiwa kumhonga Kado kiasi cha fedha kinachotajwa kuwa ni Sh. 400,000 ili aiachie Simba katika mechi yao.
Habari zilizoifikia Micharazo jana, zilisema kuwa Ulimboka, winga aliyeng’ara Simba kwa misimu kadhaa kabla ya kuomba apumzike msimu huu, alinaswa kirahisi kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ni mtego uliowekwa mapema dhidi yake.
Chanzo kingine kilidai kwamba alikamatwa majira ya saa 2:30 usiku na kupata kashkash za kupewa kipigo baada ya kukutwa na Kado kwenye kota za Mtibwa, na kudaiwa vilevile kwamba alikutwa na fedha zote zinazodaiwa kuwa za hongo.
Alipoulizwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alithibitisha juu ya kukamatwa kwa Ulimboka kambini kwa timu ya Mtibwa na kwamba kilichomkamatisha ni hizo tuhuma za kumhonga Kado.
Alisema kuwa polisi walimshikilia katika kituo chao cha Mtibwa hadi jana asubuhi kabla ya kumuachia kwa dhamana.
"Ni kweli… taarifa za kukamatwa kwa mchezaji huyo (Ulimboka) ninazo, ila sina uhakika kama alipigwa. Nilichoambiwa ni kwamba alinaswa na fedha na kufikishwa kituoni na watu wa Mtibwa Sugar ambapo alihojiwa, akafunguliwa kesi na kisha kuachiwa asubuhi hii (jana)," alisema Kamanda Andengenye.
Kamanda huyo alisema kuwa pamoja na kuachiwa kwake (Ulimboka), bado jeshi lao linaendelea na upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Awali, kocha msaidizi wa Mtibwa, kipa wa zamani wa Simba, Patrick Mwangata, alikiri pia kutokea kwa tukio hilo kambini kwao, lakini hakutaka kuzungumza zaidi kwavile yeye si msemaji rasmi na kwamba, suala hilo liko mikononi mwa polisi.
Micharazo haikumpata Ulimboka ili aelezee sakata hilo na sababu za kuhusishwa na Simba wakati akiwa ameshaachana nao na kubaki kuwa mchezaji mstaafu wa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Baadhi ya viongozi wa Simba hawakupatikana pia kupitia simu zao za mikononi, ingawa Afisa Habari wa klabu hiyo, Clifford Ndimbo, alipatikana awali na kuomba apigiwe baada ya dakika kumi, jambo ambalo halikufanikiwa kwani alipopigiwa tena baada ya muda huo kwa zaidi ya mara mbili, simu yake haikuwa ikipatikana.
Wakati Simba na Mtibwa zikishuka dimbani leo, Idda Mushi anaripoti kutoka Morogoro kuwa African Lyon walilazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya ligi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Kagera walipata goli la utangulizi katika dakika ya 43 kupitia kwa Gaudence Mwaikimba na Lyon wakasawazisha katika dakika ya 54 kwa penati iliyopigwa na Adam Kingwande kufuatia kipa Amani Simba kumdaka miguu Idrisa Rashid na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Huku wakiwa 10 uwanjani, Kagera walipata goli la pili katika dakika ya 66 kupitia kwa Sunday Hinju kabla Kingwande tena kuisawazishia Lyon kwa goli la dakika ya 88.