STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 5, 2013

Njemba yanusurika kufa kisa ujambazi

Jambazi likiwa hoi baada ya kichapo kutoka kwa wanachi.
Jambazi hilo likihojiwa.
Mmoja wa wanausalama (mwenye tisheti yenye mistari) akiwa na bastola aliyokutwa nayo jambazi huyo.
Wananchi wakiwa eneo hilo la tukio.
Wanausalama wakishauriana jambo kabla ya kulipiga pingu jambazi na kulipeleka hospitali.
Baada ya kichapo kikali jambazi lilipelekwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.

GPL

Chimwemwe atua Dara na kutamba kumnyuka Cheka

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Best Man Promotion, Zumo Makame (katikati) akiwatambulisha mabondia wawili kutoka Malawi,  Chiotcha Chimwemwe (kulia) na Bgright Mdoka (kushoto) kwa waandishi wa habari tayari kwa mapambano yao ya Agosti 10. Cimwemwe  atapambana na Cheka wakati Mdoka atazipiga na Jitu Samia. Mwingine katika picha ni promota wa Chimwemwe, Steven Msiska. (Na Mpiga Picha Wetu)

Na Mwandishi Wetu
BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa wa Malawi, Chimwemwe Chiotcha amewasili nchini na kutamba atamtwanga bondia alisyekuwa na mpinzani Tanzania, Francis “SMG” Cheka katika pambano lao la uzito wa super-middle lililopangwa kufanyika Jumamosi kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Chimwemwe ambaye hajawahi kupoteza pambano nchini Malawi zaidi ya kupigwa kwa pointi na Cheka Desemba 27 mwaka jana, alisema kuwa amekuja kulipiza kisasi huku akiponda matokeo ya awali kuwa Cheka alibebwa sana.
Alisema kuwa hajui ni ushindi wa aina gani atakaoupata kwa bondia huyo, kwani Knock Out (KO) au Technical Knock Out (TKO) utokea ulingoni tu na wala si ushindi wa kupangilia. “Nimekuja hapa kushinda na wala si vinginevyo, nakuja Cheka amejiandaa sana, sikuridhika na matokeo ya awali na ndiyo maana nimeamua kuja kurudiana naye, najua nitaibuka na ushindi,” alisema Chimwemwe.
Alifafanua kuwa si kweli kuwa kila bondia aliyepigana na Cheka na kushindwa kuwa hajui ngumi za kulipwa zaidi ya hofu tu kutoka kwa mabondia hao. Mimi nimedhamilia kufanya kweli na ninajua nitashinda, hii ni fursa yangu,” alisema Chimwemwe ambaye ni mwanajeshi wa Jeshi la Malawi.
Mkurugenzi wa kampuni ya Best Man Promotion inayoaandaa pambano hilo, Zumo Makame alisema kuwa maandalizi ya pambano yamekamilika na siku hiyo kutakuwa na mapambano makali nay a kusisimua.
Makame aliyataja mapambano hayo kuwa, Deo Njiku atawania ubingwa wa Taifa wa Shirikisho la Masumbwi la PST dhidi ya Cosmas Cheka, Rashid “Snake Man” Matumla atazichana na Maneno “Mtambo wa gongo “ Oswald na bondia mwingine kutoka Malawi, Bright Mdoka atazipiga na Jitu Samia.
Mapambano mwngine kwa mujibu wa Makame ni Nasibu Mkude atapigana na Juma Kihiyo katika uzito wa super welter bout, Juma Afande v Epson (featherweight) na  Karim Mandonga dhidi ya Ramadhan Agogo katika uzito wa superwelter.

Mjumbe CCM, awapasha wajumbe Tume ya Katiba

Mjumbe wa CCM, Evod Mmanda
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (MNEC) Evod Mmanda amewataka Wajumbe wa Tume ya Katiba kuacha kufanya kazi ya kujibu mapungufu yaliyopo katika rasimu hiyo kwani huu ni wakati wa Mabaraza kufanya kazi ya kurekebisha na kupendekeza.
Mmanda alitoa kauli hii wakati akiongea na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam ambapo alisema ameshuhudia baadhi ya wajumbe wa Tume wakitoa maelekezo kwa wajumbe wa mabaraza jinsi ya kutoa maoni.
Alisema ni vema Tume hiyo ikatambua kuwa wakati wao wa kuandaa rasimu umepita na sasa ni wakati wa kuyapa fursa mabaraza kutokana sheria inavyotaka jambo ambalo ni muhimu kuheshimiwa.
Mjumbe huyo wa Mkuatano Mkuu alisema CCM wanaamini kuwa fursa zikipatikana upo uwezekano wa kupatikana na kwa katiba ambayo itakuwa na maslahi na Taifa hivyo kuingilia maoni ya watu ni kinyume na katiba inavyotaka.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa wajumbe wa Tume ya Katiba kuwa wakati huu ni wakuwaachia wajumbe wa mabaraza kutoa maoni na mapendekezo yao hivyo kukaa na kujibu hoja hizo wakati wanatakiwa kusubiri ni kwenda kinyume na sheria inayowaongoza,: “ alisema.
Mmanda alisema iwapo wajumbe watatumia nafasi elekezi kuwashawishi wajumbe wa mabaraza kukubaliana na mapendekezo yao ni dhahiri kuwa kutakuwepo na katiba ambayo ina mitazamo ya watu wachache.
Alisema kuna mapungufu mengi ambayo yameonekana katika rasimu hiyo hivyo ni wakati muafaka kwa jamii na vijana kwa ujumla kutumi nafasi zao kutoa maoni ambayo yataweza kusaidia kizazi cha leo na kijacho.
Mjumbe huyo ambaye alionyesha dhahiri kutokuunga mkono wa uwepo wa Serikali tatu aliishutumu tume kwa kuweka maoni hayo kwa kile alichodai kuwa haikuwa sehemu ya muuongozo wao kufanya.
Aliweka bayana kuwa yeye ni muumini mkuwa wa serikali mbili hivyo hakuona sababu ya kuwepo mapendekezo juu ya aina ya muungano na kuwataka wachangiaji kupitia nafasi mbalimbali kuwa makini kwa maslahi ya Taifa.
Mmanda alitoa rai kwa vijana wa CCM kuwa watumie nafasi yao kuhakikisha kuwa katiba ijayo inakuwa na maboresho yesnye tija na kuacha tabia ya kuwa katika mitazamo ya watu amabao wanaweza kuwa na maslahi yakiuongozi.

Umeme Majanga! Mabwawa yote ya kuzalisha umeme yakauka

Prof.  Muhongo
Na Suleiman Msuya
WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema takwimu zinonyesha kuwa kwa sasa hamna bwawa lolote la maji ya kuzalisha umeme ambalo lenye maji ya kutosha ya kuzalisha umeme wa kutosha hapa nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akijibu swali la mwandishi habari hii aliyetaka kujua ni kwanini Serikali haikutaka kutumia Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) ili kuzalisha umeme pamoja na kwamba tafiti zinaonyesha kuwa lingeweza kuzalisha umeme wa zaidi ya megawati 3500 iwapo kungekuwepo na uwekezaji.
Profesa Muhongo alisema upo uwezekano wa tafiti kuonyesha hivyo ila kwa sasa serikali ipo katika harakati za kuleta umeme ambao utaweza kumfikia kila Mtanzania kwa gharama ndogo bila tatizo lolote.
Alisema serikali iliwataka RUBADA kutoa taarifa za uhakika kuhusu uwepo wa maji ya uhakika ambayo hayataweza kupungu jambo ambalo halijafanyika hadi sasa hivyo wao kama wasimamia sera mikakati yao ni kuhakikisha kuwa wanatatua matatizo makubwa ya umeme yaliyopo.
“Mimi kila siku napokea taarifa kutoka kwa wasaidizi wangu na wanasema hakuna bwawa hata moja ambalo lina maji ya kutosha ya kuzalisha umeme hivyo kwa sasa ni vema jamii ikajua kuwa sisi tunajikita katika vyanzo ambavyo havina changamoto,” alisema.
Waziri huyo alisema wao kama serikali wamejikita katika uwekezaji wa uzalishaji wa umeme wa gesi, jua, makaa ya mawe na vyanzo vingine ambavyo ni vizuri na rahisi katika uzalishaji wa umeme.
Alisema iwapo mvua zitanyesha wanaweza kufikiria vyanzo hivyo kama njia ya kutatua tatizo ila kwa sasa macho na nguvu zao zipo katika vyanzo hivyo ambavyo amevitaja kwani havina gharama kubwa ya uzalishaji.
Profesa Muhongo alisema mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 kunakuwepo zaidi ya uniti 2000 za umeme ambazo zinazalishwa hapa nchini hali ambayo itachangia kukuza uchumi.
Aidha akizungumzia maamuzi ya kuleta gesi mkoani Dar es Salaam kutoka mtwara alisema hilo ni jambo ambalo halina mjadala kwani Dar es Salaam ndipo mahali penye chanagamoto nyingi za umeme pamoja na uzalishaji mkubwa wa bidhaa mbalimbali.
Muhongo alisema suala la kwanini usambazaji usianze katika mikoa ambayo bado haijapata huduma ya umeme wa uhakika alibainisha kuwa lengo la Serikali ni kufikisha huduma hiyo kwa jamii yote bila ubaguzi ila kwa sasa watafikisha Dar es Salaam na maeneo mengine yatafuata.

Sheria bila Sera 'miyeyusho' mitupu kwa maendeleo ya jamii


Na Suleiman Msuya
KITENDO cha kuwepo kwa sheria bila sera kimetajwa kama moja ya chanzo cha kukwamisha na kudididimiza jitihada za kuleta maendeleo kwenye jamii hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Dk. Frateline Kashaga wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam.
Alisema kumekuwepo kwa utaratibu wa kuwepo kwa sheria bila sera jambo ambalo ukiliangalia kiundani ndicho chanzo kikubwa kinachokwamisha juhudi za kupigania maendeleo hapa nchini kwa utekelezaji haupo.
Dk. Kashaga ambaye pia ni Mwahadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu Cha  Dar es Salaam tawi la (DUCE) alisema ni vema amichakato hiyo ikaenda kwa pamoja ili iweze kuleta tija kwa Taifa.
“Nimekuwa nikifuatilia mara kwa mara sheria zetu ambazo zinaundwa nimegundua mapungufu mengi ambapo kubwa zaidi ni ukosefu wa sera kwa wakati huku sheria ikiwepo kwa muda mrefu jambo ambalo linanishangaza,” alisema.
Mwahadhiri huyo Mwandamizi alisema huu ni wakati muafaka kwa jamii ya wanataaluma kutafakari kwa kina juu ya changamoto hiyo na kuja na mapendekezo ambayo yatakuwa na manufaa kwa nchi.
Alisema ni muhimu kwa Taifa likahakikisha kuwa kunakuwepo kwa sera sahihi ambazo zitafaidisha jamii kwani kutokana na takwimu kunaonyesha nchi zilizoendfelea ndizo zinafaidika kwa rasilimali za nchi.
Dk. Alisema zaidi ya dola bilioni 150 zinapotea kutoka bara la Afrika takribani kila mwaka katika mazingira ambayo hayakubaliki hali ambayo inaonyesha dhahiri kuwa ni ukosefu wa sera sahihi za kusimamia rasilimali za nchi.
Kashaga alisema ni vema Tanzania na Afrika kwa ujumla wakatengeneza sera za kimkakati ambazo zitaweza kufanya mataifa yao kufaidika na rasilimali zilizopo kwa kipindi kirefu.
Aidha mmoja wa changiaji aliweka bayana kuwa uvutiaji wa wawekezaji katika bara la Afrika takwimu zinaonyesha kuwa bara la Afrika linaingiza dola bilioni 130 kwa mwaka kutoka nje ambapo lenyewe linapeleka zaidi ya dola trilioni mbili uwioano ambao sio sahihi.

Makamba awataka vijana kuwania nafasi za uongozi


Mhe. January Makamba

Na Suleiman Msuya
MLEZI wa Shirikisho la Vijana wa Vyuo Vikuu wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia January Makamba amewataka vijana nchini kujitokeza na kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi za mitaa hadi Taifa.
Makamba aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu katika kongamano la kujadili rasimu ya Katiba ambayo kwa sasa ipo kwenye mchakato wa mabaraza.
Alisema vijina wanapaswa kutambua kuwa ufumbuzi wa mahitaji yao yao ni pamoja na wao kushiriki moja kwa moja katika kugombea nafasi za uongozi ambazo zinapatikana na kuacha tabia ya kulalamika.
Naibu Waziri alisema ili Taifa liweze kupiga hatua ni dhahiri kuwa mchango wa vijana hasa wasomi unahitajika kwani ndio chachu ya kuleta maendeleo katika nchi na wananchi kwa ujumla.
“Kimsingi vijana wa Tanzania wamekuwa walalamikaji bila kuwajibika ila napenda kuwapa usia huu kuwa njia ya kukomboa Taifa ni sisi kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi na kiutumishi ili tuwe sehemu ya maendeleo,” alisema.
Mlezi huyo alitolea mfano wa Nabii Musa wakati alipoulizwa na Mungu mkononi ameshikilia nini ambapo alimjibu fimbo na kumtaka aiweke chini fimbo hiyo ambayo ilibadilika kuwa nyoka na baadae ilibadilika kuwa fimbo tenda hivyo taaluma zao ziwe ni fimbo kwa kusaidia maendeleo ya Taifa.
Alisema fursa zilizopo nchini zinahitaji vijana kushiriki kikamilifu ili ziweze kuwa na tija kwani kuendelea kusubiri kutachangia nchi kupoteza rasilimali nyingi ambazo zipo.
Naibu Waziri alisema iwapo vijana watakuwa washiriki katika uongozi ni dhahiri kuwa viongozi sahihi wenye uzalendo na uadilifu wanaweza kupatikana bila kuwepo kwa lawama za ufisadi na kashfa nyingine nyingi ambazo zimekuwa zikiibuliwa.
Akizungumzia juu ya kongamano hilo alisema CCM imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki katika majadiliano yoyote ambayo yanahusu Taifa kwa lengo kuu kwamba wao ndio wasimamizi wa rasilimali za nchi.
Makamba alisema vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo kuwasilisha hoja ambazo zitasaidia nchi na kuachana na tabia ya kulalamika mara kwa mara bila kuja na suluhisho

Azam yaanza vibaya Sauzi, yapigwa 3-0

Na Bin Zubeiry
AZAM FC imeanza vibaya ziara yake ya mechi za kujipima nguvu mjini hapa, baada ya kufungwa mabao 3-0 na wenyeji, Kaizer Chiefs katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa mazoezi wa wa timu hiyo, eneo la Nachurena.
Azam iliyoondoka nchini jana mchana kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini, kuja Johannesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya, katika mchezo wa leo iliathiriwa na uchofu wa safari na hali ya hewa ya baridi, hivyo kucheza chini ya kiwango.
Azam FC

Timu hiyo yenye maskani yake, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, iliyoondoka na kikosi chake kizima, kasoro wachezaji wawili tu majeruhi, kiungo Mkenya, Humphrey Mieno na mshambuliaji Mganda, Brian Umony, imefikia katika hoteli ya Randburg Towers.
Azam jana ilifanya mazoezi yake ya kwanza kwenye Uwanja wa Wits University asubuhi na jioni na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall amefurahishwa na mazingira ya kambi na Uwanja wa mazoezi.
Baada ya mchezo wa leo, Azam itashuka tena dimbani Agosti 7, kumenyana na Mamelodi Sundowns kabla ya kuivaa Orlando Pirates Agosti 9 na Agosti 12 itamaliza ziara yake kwa kumenyana na Moroka Swallows.
Azam inatarajiwa kurejea nchini Agosti 13 tayari kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Safari hii Azam, washindi wa pili mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu wamepania kutwaa Ngao mbele ya Yanga, baada ya mwaka jana kufungwa na Simba SC na kocha Muingereza Stewart Hall anajiandaa kikamilifu kwa ajili hiyo.   

Azam kuikabili Kaizer Chiefs 'Bondeni'

Wachezaji wa Azam wakiwa katika picha tofauti nchini Afrika Kusini, jioni hii wataumana na Kaizer Chiefs


MAKAMU bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Azam wanaanza rasmi ziara ya mechi za kirafiki nchini Afrika Kusini leo kwa kuikabili timu ya Kaiser Chiefs ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam, Jaffer Idd aliyefutana na timu hiyo, mechi hiyo inachezwa jijini Johannesburg, likiwa ni pambano la kwanza kati ya manne ambayo Azam itajipima nguvu nchini humo ilipoenda kuweka kambi ya muda kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu inayoanza Agosti 24.
Mechi nyingine ambazo Azam itacheza ni ya keshokutwa dhidi ya Orlando Pirates, Mamelodi Sondowns na Moroka Swallows.

Hatimaye Katiba ya TFF yapita kwa Msajili

Rais wa TFF, Leodger Tenga na katibu wake, Angetile Osiah
Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa kusajili Katiba ya TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Julai 13 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Agosti 5 mwaka huu), Rais Tenga ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Naibu wake Amos Makala na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ushirikiano ambao wametoa kwa TFF katika kufanikisha suala hilo.

Amesema baada ya kupokea usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu wa TFF kumwandikia rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa TFF.

Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa marekebisho hayo yasingeweza kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya TFF, Rais Tenga amesema alikuwa ana haki ya kusema hivyo kwa sababu hakuwepo kwenye Mkutano huo, na kuongeza:

“Makala hakuwepo kwenye mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana haki ya kuuliza, nina hakika sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu ni msikivu. Kuhusu marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo lisingewefanyika kwa sababu hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.

Rais Tenga amesema marekebisho hayo yalipitishwa kwa kauli moja (unanimous) hivyo hakukuwa na sababu ya kuanza kunyoosha mikono kupiga kura, kwa maana hiyo mkutano ulipitisha marekebisho kwa asilimia 100 wakati Katiba ilikuwa ikihitaji theluthi mbili tu.

“Hakukuwa na dispute (mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa wajumbe walitumia muda mwingi kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu ambao wangeingia kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo Maalumu ni watu wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

“Labda itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia. Mtu yeyote wa mpira wa miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni lazima yatekelezwe, na Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.

Pia Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu wenye sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya Uchaguzi itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.

Huyu ndiye 'Tanzania One' Juma Kaseja

Kipa Juma Kaseja akiwa na Katibu wa kituo cha yatima cha New Life Orphans Home Hamad Kombo walipokitembelea kituo hicho jana ambapo watoto walipagawa naye wakionyesha wanaomfuatilia kupita maelezo.

Ebu niambie wewe msimu huu unaenda wapi? Ashanti au Fc Lupopo? Kaseja akiteta jambo na Mlezi wa klabu ya Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' huku wachezaji wenzake wakisikiliza kwa makini na watoto wakiwa bado wana hamu ya kufurahia naye kama wanvyoonekana kando yake kwa ndani..

Huyo hana lolote anaenda zake Mbeya City? Kaseja akiteta na beki wa zamani wa Yanga na Reli, Yahya Issa huku Ticotico na Faraji wakisikiliza.
Kaseja mkekani na watoto
Akimakinika na watoto ambao baadhi walikuwa wakimshangaa


Kwani hiyo simu inauzwa kiasi gani? Ni kama dogo huyo anamuuliza Kaseja
Watoto wakiwa sambamba na Kaseja

Kaseja akizungumza na watoto waliotaka kupiga naye picha jana kwenye kituo cha kulelea yatima cha New Life Orphans Home
Yaani kila mtoto alitaka kuwa karibu na Kaseja

Kaseja na mlezi wa Golden Bush, Onesmo 'Waziri Ticotico' aliyembeba mtoto katikapicha ya pamoja na watoto.
 
Sheikh huwezi kutoka bila kupiga picha na miye! Katibu wa kituo cha kulelea yatima, Hamad Kombo(kati) akiwa pichani na Kaseja (kushoto)
HUENDA kipa Juma Kaseja ndiye mchezaji anayetambuliwa na kufahamika kirahisi nchini iwe kwa watoto ama hata wanawake ambao mara nyingi huwa siyo wafuatiliaji wa soka.
Mara kadhaa katia mahojiano yangu na wasanii au wanamichezo hasa wa kike wanaoshabikia soka wengi humtaja Kaseja kama mchezaji wanayemjua kwa umahiri wake, wengine huwa ni Mrisho Ngassa, Ally Mustafa 'Barthez', Athuman Idd 'Chuji' na wakati mwingine Emmanuel Okwi japo kwa sasa hayupo nchini.
Kitu gani kinachomfanya Kaseja awe kivutio na gumzo midomoni mwa watu, kama ambavyo ilivyo sasa baada ya kutemwa na Simba? Sina shaka ni umahiri wake dimbani, nidhamu na kule kujiweka chini licha ya usupa staa alionao.
Jana wakati timu ya Golden Bush FC ilipowatembelea yatima wa kituo cha New Life Orphans Home, Kaseja ndiye aliyekuwa gumzo kwa watoto na hata uongozi wa kituo hicho na kuomba kupiga naye picha, huku kipa wa Mbeya City, Aman Simba akifananishwa na Chuji kwa mzuzu aliokuwa nao.
Hata wakati wenzake wakiwa wamekaa kwenye mabenchi na viti, Kaseja alijichanganya na watoto katika mkeka kabla ya baadaye wachezaji wenzake wakati wa kupiga picha ya pamoja na watoto kuungana naye kwenye mkeka.

Kazimoto aomba radhi Watz, Simba kuvuna Mil. 62

Mwinyi Kazimoto

KLABU ya Al-Makhia ya nchini Qatar, imekubali kutoa kiasi cha Dola la Kimarekani 40,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 62 za Tanzania ili kukamilisha usajili wa kiungo Mwinyi Kazimoto, aliyetokea Simba ya Dar es Salaam.


Balozi wa klabu hiyo kwa Tanzania, Boniface Pawasa, alisema kuwa klabu yake imekubali kutoa kiasi hicho cha fedha ili kukamilisha usajili wa Kazimoto ambapo katika mkataba wa makubaliano baina ya Simba na klabu hiyo, Wekundu wa Msimbazi watakuwa wakipata asilmia 20 ya mapato kila mchezaji huyo atakapokuwa anauzwa.

“Tumefanikiwa kukamilisha baadhi ya mambo ya msingi ambayo yanamhusu mchezaji mwenyewe, lakini pia klabu ya Simba ambayo ndiyo wanaommiliki.
“Tunaelewa kuwa aliondoka katika mazingira yasiyokuwa bora kwa sababu kulikuwa  na majukumu ya kitaifa, lakini klabu yake haikuwa imeridhia lakini amewaomba radhi wadau wote waliokwazwa na  hali hiyo,” alisema Pawasa, nyota wa zamani wa Simba ambaye pia alishaitumikia Al-Makhia  inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza nchini humo.

Mbali na kitita hicho, lakini kwa upande wa maslahi atakuwa akipokea mshahara wa Sh milioni 15 kwa mwezi pamoja na marupurupu mengine ya msingi ambayo yataendelea kuinua kipato chake.
Kwa upande wake, Kazimoto aliliambia Dimba kwamba kitendo alichofanya si kizuri na anakiri kosa, hivyo anawaomba radhi Watanzania wamsamehe na kwamba atakuwa balozi mzuri kwa nchi yake.

“Ni kweli nilifanya makosa, lakini naomba Watanzania wanisamehe kwa kile kilichotokea, ila ilikuwa kwenye harakati za kutafuta maisha tu,” alisema Kazimoto kupitia mtadao wa kijamii wa Facebook.

Mwinyi Kazimoto alisajiliwa na Simba katika usajili wa mwaka 2011 akitokea JKT Ruvu Stars ya mkoani Pwani, ambapo sasa kazi iliyobakia ni Simba kutoa ruhusa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hufanya uhamisho wa kimatifa ambao utaombwa na chama cha soka cha Qatar (QFA).

Lenzi ya Michezo

Jaji Mutungi ndiye Msajili wa Vyama vya Siasa, amrithi Tendwa


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgTYy1tXHsu-VoVz-W0VGnrZjYG-Y5qEX-6aQrlO10GYaiMhcTSpZ30Oe6u4ZyMpbbDQgI8NMkE1GvZUTDWZDzL25fWf8J5rtoRZZFvxl45rBygkFyi4BKfKnt4iiunig1ffG3qZcidwxa2/s640/P+1.jpg
Jaji Francis Mutungi (kulia) alipokuwa akiapishwa na Rais JK mara alipoteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu Juni mwaka jana.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemteua Jaji Francis S.K. Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo Jumatatu (Agosti 5, 2013 na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Ijumaa iliyopita (Agosti 2, 2013).
Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama na Siasa, Mhe. John Tendwa ambaye amestaafu utumizi wa umaa kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.

Rashid Gumbo awatabiria 'Mapro' kutamba tena Ligi Kuu

Rashid Gumbo 'Chid' (kushoto) akimchuana na Shomar Kapombe katika mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita

KIUNGO nyota wa timu ya Mtibwa Sugar, Rashid Gumbo 'Chid Boy', amesema kama ilivyokuwa msimu uliopita hata msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, 'mapro' wataendelea kung'ara kuliko wazawa.
Aidha amesema kikosi chao kimejipanga kuhakikisha hakirudii makosa yaliyoigharimu msimu uliopita kiasi cha kumaliza ligi katika nafasi ya tano badala ya nafasi za juu walizokuwa wamezikusudia awali.
Akizungumza na MICHARAZO, Gumbo aliyewahi kutamba na timu za Simba na Yanga, alisema anahisi wachezaji wa kigeni wataendelea kufunika msimu huu unaotarajiwa kuanza Agosti 24, kwa sababu wageni hupewa nafasi kubwa na kutobalika kwa wazawa hasa wa klabu kubwa.
Gumbo, alisema kuridhika kwa wachezaji wazawa kunafanya wageni wazidi kuwavutia makocha na kupewa nafasi kwa vile baadhi yao wanatambua wamekuwa nchini kufanya nini.
"Kama ilivyokuwa msimu uliopita, hata msimu huu nahisi wageni wanaocheza baadhi ya klabu watang'ara kwa sababu wachezaji wazawa wanaridhika na kutobadilika," alisema.
Juu ya msimu ujao, alisema anatarajia utakuwa mgumu japo alidai kwa kikosi chao cha Mtibwa kimejifunza makosa yaliyowagharimu msimu ujao na safari hii watakuwa makini zaidi.
"Tumejifunza makosa na unajua Mtibwa ni timu ya ushindani, hivyo tunaamini tutafanya vyema tofauti na msimu mpya japo ligi itakuwa yenye ushindani kutokana na maandalizi na timu zitakazoshiriki hasa zilizopanda daraja." alisema.
Timu mpya katika ligi hiyo kwa msimu huu unaoanza wiki tatu zijazo ni Mbeya City, Ashanti United na Rhino Rangers.
Mtibwa iliyonyukwa mabao 3-1 na Yanga jana kwenye pambano la kirafiki itafungua pazia la ligi hiyo Agosti 24 kwa kuvaana na Azam nyumbani uwanja wa Manungu, katika pambano la msimu uliopita uliochezwa Manungu  wakata miwa hao walilala kwa magoli 4-1.
Kipigo hicho kilikuwa kama marejeo ya msimu wa 2010-2011 ambapo Azam waliitoa nishai Mtibwa kwenye uwanja huo kwa kipigo cha mabao 4-0.

Mauaji tena! Mume anyonga mkewe, naye auwawa


MWANAMUME mmoja amemnyonga hadi kufa mkewe na yeye akauawa na wananchi wenye hasira, katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara. 
Tukio hilo lililothibitishwa na polisi wilayani hapa, lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Kisangwa Kata ya Mcharo, kwenye sherehe ya ufunguzi wa nyumba ya ndugu yao.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mcharo, Waziri Kingi, alimtaja mwanamke aliyeuawa kwa kunyongwa na mume wake kuwa ni Paulina Samson Misinzo. 

Kingi alimtaja mwanamume huyo ambaye pia aliuawa na wananchi wenye hasira, baada ya kukimbilia mlimani kuwa ni Batule Masanja, mkazi wa kijiji hicho.

Imeelezwa kuwa siku ya tukio mwanamume huyo aliyekuwa amekwishatengana na mke wake kwa zaidi ya miezi miwili baada ya kutokea ugomvi wa kifamilia, alimfuata mke wake kwenye sherehe hiyo usiku.

Imedaiwa kuwa baada ya kufika nyumbani hapo huku akiwa na watoto wao wawili, alimuita mke wake aliyekuwa anacheza muziki na kumpeleka nyuma ya nyumba, ambapo alimnyonga kwa kutumia mikono yake hadi kufa.

Taarifa hizo zilieleza kuwa baada ya kumaliza unyama huo, mwanamume huyo alibeba mwili wa marehemu mkewe na kuutupa pembezoni mwa nyumba ya jirani.

“Alifika na watoto wao wawili na baada ya kufika alimuita na kumtoa pembeni….sasa sisi tukadhani kuwa labda anaongea naye tu huko nyuma, kumbe huko ndiko alikomnyongea,” alisema mwanafamilia mmoja.

Mashuhuda walisema kuwa baadaye mwanamume huyo alikimbilia mlimani na kwamba, wananchi wenye hasira kesho yake asubuhi walipiga yowe na kuanza kumsaka na baada ya kumpata walimshushia kipigo kikali kilichoondoa uhai wake.

Walisema kuwa mwanamume huyo aliachana na mke wake, kutokana na kumpiga kila siku alipokuwa akirejea nyumbani akiwa amelewa na ndipo mwanamke huyo alipoamua kwenda kwao.

Coastal Union yamweka kiporo Mganda wao hadi mwakani

Baadhi ya wachezaji wapya wa Coastal Union wakisalimiana na wachezaji wa URA ( walioipa mgongo kamera)


KLABU ya soka ya Coastal Union imesitisha mipango wa kumsajili mshambuliaji chipukizi kutoka Uganda, Nelson Ssenkatuuka badala yake itafanya hivyo katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani ili wamchunguze kwanza kama atawafaa.
Aidha uongozi wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, imesema haitaenda nje ya nchi kujifua kama ilivyofanya msimu uliopita badala yake itajinoa nyumbani kw akucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kujiwinda na mechi yao ya ufunguzi wa ligi dhidi ya JKT Oljoro jijini Arusha.
Akizungumza na MICHARAZO, Afisa Habari wa Coastal Union, Edward 'Edo' Kumwembe, alisema wamesitisha mipango ya kumsajili Ssenkatuuka ili kumchunguza zaidi na kama wataridhika naye watafanya hivyo katika dirisha dogo.
Edo alisema wasingependa kukurupuka kusajili mchezaji hasa kwa nafasi hiyo ya ushambuliaji ambayo ndiyo iliyosalia kwa sasa kikosini mwao.
Hata hivyo alisema anaamini waliosajiliwa na timu hiyo wataibeba Coastal katika lipute chja Ligi kinachoanza Agosti 24.
Pia alisema tofauti na msimu uliopita walipoenda Kenya kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu safari suala hilo halitakuwepo na badala yake uongozi unajipanga kutafuta mechi mbili zaidi ya kirafiki hapa hapa nyumbani kabla ya kuanza kwa ligi.
"Uongozi unatarajiwa kukutana leo jioni kwa ajili ya kujadili namna ya kuoata mechi hizo mbili za kirafiki kabla ya kuanza kwa ligi," alisema Edo.
Coastal waliomaliza katika nafasi ya sita msimu uliopita imesajili wachezaji wapya nane ambao ni  viungo kutoka Simba, Haruna Moshi 'Boban' na Uhuru Seleman, beki Juma Nyosso, kipa Said Lubawa, Mkenya Crispian Odulla, Marcus Ndehele, Abdullah Othman Ali na Kenneth Masumbuko aliyeichezea Polisi Moro msimu uliopita.

Tumba Swedi 'Mdudu Kiwi' atua Ashanti United

Tumba Swedi 'MduduKiwi' (kulia) akiwa na Jackson Chove 'Mandanda' walipokuwa Moro United


BEKI wa zamani wa Azam na Moro United, Tumba Swedi aliyekuwa China akijaribu kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa nchini humo, amerejea na kutua Ashanti United kwa ajili ya kuichezea katika Ligi kuu Tanzania Bara inayoanza Agosti 24.
Akizungumza na MICHARAZO kutoka Kigoma ilipo kambi ya Ashanti, Swedi alisema kuwa mipango yake ya kucheza China imeshindikana na wiki mbili zilizopita amerejea nchini na kuingia mkataba wa miaka miwili na Ashanti iliyorejea tena katika Ligi Kuu.
Beki huyo wa kati mwenye uhusiano na nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Said Swedi 'Pannuci' na Salum Swedi 'Kussi' anayeichezea Mtibwa Sugar, alisema anachofurahia ni kwamba Ashanti imekubaliana naye aichezea na ikitokea nafasi ya kuondoka haitakuwa na kikwazo kwake.
"Ingawa nimerejea, lakini kuna mchakato naendelea kuufanya ambapo kama utakaa vyema huenda Septemba nikatimka tena nje ya nchi, ila Ashanti nimewafahamisha na kukubaliana nami ndiyo maana nimesaini mkataba huo wa kuitumikia wakati nikiwa bado nipo nipo Bongo," alisema.
Mchezaji huyo anayemudu pia kiungo namba sita na kucheza kama mshambuliaji wa kati, alisema hakuona sababu ya kukaa tu bila kujiunga na timu yoyote kama alivyofanya msimu uliopita tangu Moro United ilipoteremka daraja.
Swedi aliyeanzia soka lake katika klabu ya Friends Rangers inayocheza Ligi Daraja la Kwanza kabla ya kuwa miongoni mwa walioiwezesha Kinondoni kutwaa ubingwa wa Copa Coca Cola 2007 na kusajiliwa timu ya vijana na Azam kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa, alisema kiu yake kucheza soka la kulipwa barani Ulaya, lakini atatafuta uzoefu kwanza barani Asia.