STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, August 2, 2012

Baada ya kuiapa Yanga taji la Kagame, Saintfiet 'aibukia' Harambee Stars

MAKOCHA wa timu mbalimbali barani Afrika na waliowahi kufundisha soka barani humu, wametuma maombi ya kupata kazi ya kuifundisha timu ya taifa ya Kenya - Harambee Stars. Kwa mujibu wa kituo cha Supersport, ukiachana na makocha Otto Pfister, Adel Amrouche, Giuseppe Dossena, Ratomir Dujovic, Goran Stevanovic na Milovan Rojavic, kocha mkuu wa klabu ya Yanga kutoka Ubelgiji Tom Saintfeit nae ametuma maombi ya kutaka kuinoa Harambee Stars.
Tom Saintfiet ambaye bado hajatimiza hata mwezi mmoja tangu aje kujiunga na Yanga anapambana kocha wa zamani Ghana ambaye aliongoza Black Stars katika michuano ya African Cup of Nations 2012 na akatimuliwa baada ya timu kuondolewa kwenye michuano hatua ya nusu fainali. Japokuwa makocha ni wengi waliotuma maombi lakini Otto Pfitster anaonekana kuwa na nafasi kubwa kutokana na CV yake, akiwa tayari ameshazifundisha timu za Burkina Faso, DR Congo, Cameroon na Ghana. Pia tayari ameshachukua kombe la dunia la vijana chini ya miaka 17 na kikosi cha Ghana. Siku ya leo ndio shirikisho la soka la Kenya (FKF) kupitia kamati kuu watawatangaza makocha waliongia kwenye kinyang'anyiro cha mwisho katika kueleka kumteua kocha mkuu wa Harambee Stars. CHANZO:SHAFII DAUDA BLOGSPOT

Kocha wa Atletico ya Burundi kumrithi Stewart Azam?

KUSITISHWA mkataba kwa kocha wa Azam FC Stewart Hall kunamuweka kocha wa Atletico ya Burundi
katika nafasi nzuri ya kuifundisha timu hiyo. Baadhi ya vyombo vya habari nchini vimemkariri Stewart akikiri kusitishiwa mkataba wake huku akiweka bayana anafurahia kutimiza malengo makuu matatu katika klabu hiyo ikiwemo ujenzi wa Complex ya Chamazi, kuinua soka la vijana na kuiweka Azam katika chati ya juu katika soka la Tanzania. Uongozi wa Azam nao umekiri kuachana na kocha huyo ukidai kuwa walipofikishwa na kocha huyo kunahitaji mtu mwingine wa kuwaendeleza na kuzipuuza taarifa kwamba walimtimua Stewart kwa sababu ya kumpanga Ngassa katika mechi yao na Yanga kinyume na agizo lao. Hata hivyo uomgozi huo umesema kuwa wakati wakiendelea kumsaka kocha mpya timu itakuwa chini ya kocha wa vijana , Vivek Nagul na Kally Ongalla, ingawa taarifa ambazo bado hazijadhibitishwa ni kwamba Azam inamneyemelea kocha wa Atletico, Kaze Cedri aliyeufutia uongozi huo. Habari zilidai kuwa viongozi wa Azam walionyeshwa kuvutiwa na kocha huyo baada ya timu yake kuonyesha kandanda la kuvutia kwenye michuano hiyo. Ni siku ambayo ilicheza kandanda la kuvutia kwenye michuano ya Kagame Cup na kuichapa Yanga mabao 2-0, kabla ya kuoka sare na APR huku pia ikisakata kabumbu la uhakika. Aidha inaelezwa kuwa kutua kwa Cedri Azam itaisaidia klabu hiyo kupunguza gharama kubwa walizokuwa wakimlipa kocha huyo Muingereza ambaye aliwahi kuinoa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kabla ya kunyakuliwa na Azam. Habari za ndani katika klabu hiyo zinasema kuwa Stewart alikuwa akipokea 'mkwanja' mnene kuliko hata unaodaiwa kulipwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars na kutokea sakata la Ngassa limekuwa nafuu kwa uongozi huo kumpa mkono wa kwaheri. Juhudi zinafanywa na MICHARAZO kupata uthibitisho wa Cedri kutakiwa Azam na tukifanikiwa mtazipata kupitia hapa hapa.

Mwanahawa Chipolopolo atua T Moto

ALIYEKUWA muimbaji nyota wa kundi la King's Modern Taarab 'Wana Kijoka Kazima Taa', Mwanahawa Ally 'Chipolopolo' amelihama kundi hilo na kutua T-Moto Modern Taarab. Akizungumza na MICHARAZO
, Chipolopolo alisema ametua T-Moto wiki iliyopita baada ya kuvutiwa na masilahi aliyoahidiwa na kundi hilo na kwa sasa anajifua nao kwa ajili ya maonyesho ya sikukuu ya Eid el Fitri ambapo ndipo atakapotambulishwa rasmi. Chipolopolo, alisema ameondoka King's kundi lililomtangaza vema kwa baraka zote bila ya ugomvi wala chuki kwa lengo la kusaka ujuzi na kusaka masilahi. "Yaani ni wiki tu iliyopita ndio nimetua hapa T-Moto nikitokea King's kwa nia ya kuongeza ujuzi na kutafuta masilahi zaidi, ila sijaondoka katika kundi langu la awali kwa chuki au ugonvi," alisema. Muimbaji huyo ambaye ni mtoto wa mpuliza saksafone wa zamani wa bendi za Urafiki Jazz, Bima Lee, Shikamoo Jazz na Msondo Ngoma, Ally Rashid 'Mwana Zanzibar' alisema anaamini kuwepo kwake T-Moto kutamsaidia kumpaisha zaidi kutokana na aina ya wasanii atakaokuwa nao. Alisema pamoja na kuondoka, King's, lakini hatalisahau kundi hilo kwa kusaidia kumnyanyua baada ya kusota katika makundi ya awali aliyoyapitia katika safari yake kimuziki. "Nimeondoka King's lakini silisahau asilan kwa namna lilivyonisaidia kufika hapa nilipo hata T-Moto wakakiona kipaji changu," alisema. Mwisho

Kim Poulsen awaita Bahanunzi, Chuji kikosi cha Stars

MFUMANIA nyavu aliyefunika kwenye michauno ya Kombe la Kagame, Said Bahanunzi wa Yanga na viungo 'watukutu' Athuman Idd Chuji na Ramadhani Chombo 'Redondo' ni kati ya wachezaji 21 waliotangazwa kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa Taifa Stars. Kocha mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen amekitangaza kikosi hicho jana kwa ajili ya kujiandaa na pambano la kirafiki la kimataifa linalotarajiwa kuchezwa katikati ya mwezi huu nje ya nchi. Poulsen alisema kikosi hicho kinatarajiwa kuingia kambini wiki ijayo tayari kujiwinda na mechi hiyo ya kirafiki ambayo hata hivyo mpaka sasa haifahamiki itakuwa dhidi ya nchi gani. Kocha huyo alisema amewaita wachezaji hao watatu na wengine kutokana na kuonyesha uwezo mzuri wakati wa michuano ya Kagame, ambapo bahanunzi aliibuka mfungaji bora huku Chuji na Redondo waking'ara katika nafasi ya kiungo mwanzo mwisho. Kim alisema ameomba mechi hiyo ya kirafiki ambayo iko kwenye kalenda ya FIFA ichezwe ugenini kwa lengo la kuwapa uzoefu wachezaji wake. Wachezaji waliotajwa na kocha huyo ni pamoja na makipa watatu, Nahodha Juma Kaseja (Simba), Deogratias Munishi 'Dida'na Mwadini Ally (wote Azam). Mabeki ni nahodha msaidizi, Aggrey Morris na Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba). Viungo walioteuliwa katika timu hiyo ni Chuji na Frank Domayo (Yanga), Haruna Moshi 'Boban', Ramadhani Singano 'Messi' na Mwinyi Kazimito (Simba), Mrisho Ngassa,Redondo na Salum Abubakar 'Sure Boy' (Azam) na Shabani Nditi kutoka Mtibwa Sugar. Wengine ni washambuliaji John Bocco (Azam), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu(TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo), Bahanunzi na Simon Msuva. Kocha huyo alisema ameshindwa kuwaita Amri Maftah wa Simba na Nurdin Bakari wa Yanga kwa sasa kutokana na kwamba wachezaji hao bado ni majeruhi.

Simba wamalizana na Azam kuhusu Ngassa, mwenyewe adai haendi kokote kwa vile hajashirikishwa

MABINGWA wa soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba wametangaza kumsajili mshambuliaji nyota wa Azam na timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngassa kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja. Hata hivyo Ngassa mwenyewe amesisitiza kuwa hajashirikishwa katika 'dili' hilo na kudai kama uongozi wa Azam haumtaki katika klabu yao imvunjie mkataba na kumlipa chake kuliko kumpeleka kwenye klabu ambayo hajawahi kuitoa kuichezea. Uongozi wa Simba na Azam jana ulinukuliwa kwamba umefanikisha mpango wa Ngassa kutua Msimbazi baada ya kuwazidi kete Yanga waliokuwa tayari kulipa Sh Milioni 20, milioni tano pungufu na zile walizotoa Simba. Awali, uongozi wa Azam ulishatangaza kuwa uko tayari kumuuza winga huyo kwa klabu yoyote itakayotoa dau la dola 50,000 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 80), jambo ambalo limeonekana kuwa gumu kabla ya Simba kumpata mchezaji huyo kwa ofa ya mkopo ya Sh. milioni 25. Ngassa ambaye alitakiwa sana na kocha wa Simba, Milovan Circkovic, anatarajiwa kuichangamsha safu ya ushambuliaji ya timu yake mpya katika ligi kuu ya Bara na pia katika michuano itakayoanza mapema mwakani ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika. Akizungumza jana jijini Dar, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa wamemsajili Ngassa kwa mkopo na tayari wamefikia makubaliano na Azam, hivyo mchezaji huyo ataichezea timu yao katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo inatarajiwa kuanza Septemba Mosi. Kaburu alisema kuwa wamemsajili mshambuliaji huyo kutokana na maelezo ambayo walipewa na Cirkovic ili kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi ambaye sasa anaelekeza nguvu zake katika kusaka timu atakayoichezea soka la kulipwa barani Ulaya. "Usajili wa Ngassa umeshakamilika, ni mali yetu kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kukamilisha usajili wake wa kuichezea Simba kwa mkopo," alisema Kaburu. Naye Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alinukuliwa akisema wameamua kumpeleka Ngassa Simba kutokana na maelezo ya Cirkovic kumuhitaji ambapo wanaamini ataendeleza kipaji chake na kuendelea kuisaidia Taifa Stars. Kahemele alisema kuwa Azam ilifikia maamuzi ya kumuuza mshambuliaji huyo baada ya kuonyesha hadharani mapenzi aliyonayo na mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga, lakini alidai Yanga imekwama kumpata kwa vile iligoma kuongeza dau katika fedha ilizotaka kutoa. Azam ilitangaza kwamba iko tayari kumuuza Ngassa kwa gharama ya Dola za Marekani 50,000 baada ya nyoya huyo kuonyesha mapenzi yake kwa Yanga kwa kuvaa na kuibusu nembo ya klabu hiyo wakati akishangilia goli aliloifungia Azam katika mechi yao ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ngassa aliyeihama Yanga mwaka juzi aliisaidia Azam kumaliza kwenye nafasi ya pili katika msimu wa ligi uliopita ambapo mwakani itashiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Kombe la Shirikisho yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa alisema hana taarifa za kupelekwa Simba na kudai kwa tararibu anazopfahamu alipaswa kushirikishwa katika mazungumzo ya klabu hizo mbili kabla ya kufikiwa maamuzi. "Kama ni kweli wamefanya hivyo hawajanitendea haki, nilipaswa kushirikishwa na kama klabu ya Azma hainitaki basi inilipe changu nijue wapi pa kwenda na sio kunipeleka sehemu kama mzigo usio na maamuzi," alisema Ngassa mtoto wa kiungo wa zamani wa Pamba na Simba, Khalfan Ngassa. Ngassa alisema yeye anauheshimu mkataba wake na Azam ambao umesaliwa muda wa mwaka mmoja, lakini ni vigumu kwake kukubali kirahisi kupelekwa Simba, ingawa hakuweka bayana atachukua hatua gani katika sakata hilo ambalo kwa kiasi fulani linataka kufanana na lile la wachezaji Mohammed Banka aliyekuwa Simba na Ramadhani Chombo wa 'Redondo' wa Azam ambao walitolewa kwa mkopo na klabu zao kwa klabu za Villa Squad na Moro United lakini wakagoma kwa vile hawakushirikishwa katika uhamisho huo.