STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, January 6, 2014

Msondo kumsindikiza Gurumo kuaga mashabiki jijini Tanga


Mzee Gurumo (kati) akiwa na waimbaji wa Msondo Ngoma, Tx Moshi Jr na Juma Katundu 'JK' enzi akiwajibika jukwaani
BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini Msondo Ngoma inatarajiwa kumsindikiza muimbaji wao za zamani na mwanamuziki mstaafu, Muhidini Gurumo katika onyesho maalum la kuwaaga mashabiki wake wa jijini Tanga.
Onyesho hilo ambalo ni muendelezo wa maonyesho maalum ya mkongwe huyo ya kuwaaga mashabiki wake nchini baada ya kuitumikiafani ya muziki kwa miaka zaidi ya 50, litafanyika Mkesha wa Siku ya Mapinduzi.
Msemaji wa Maseneta wa Msondo, Waziri Dewa aliiambia MICHARAZO kuwa, onyesho hilo la Tanga litafanyika Januari 11 kwenye ukumbi wa Tanga Hotel.
Dewa alisema katika onyesho hilo mashabiki watazawadiwa vitu mbalimbali kwa watakaowahi kuingia ukumbini na wale watakaoweza kuimba vyema nyimbo za muuimbaji huyo mstaafu maarufu kama 'Mjomba' na za bendi ya Msondo.
"Katika muendelezo wa kuwaaga mashabiki, Msondo itamsindikiza Gurumo jijini Tanga ambapo ataaga mashabiki siku ya Mkesha wa Siku ya Mapinduzi ambapo tutatoa zawadi kwa watakaoimba vyema nyimbo za Gurumo," alisema.
Dewa alisema miongoni mwa zawadi watakaopewa mashabiki hao ni pamoja na tisheti na CD za bendi hiyo hasa zenye nyimbo za zamani wa Msondo na zile zilizowahi kutungwa au kuimbwa na Gurumo mwenyewe.
Muhidini Mwalimu Gurumo alitangaza kustaafu muziki mwishoni mwa mwaka jana kutokana na matatizo ya afya na umri kumtupa mkono na aliagwa rasmi jijini Dar es Salaam Desemba 14 katika onyesho lililofanyika viwanja vya Sigara.
Mkongwe huyo ndiye aliyeiasisi bendi ya NUTA Jazz iliyokuja kufahamika kwa majina ya Juwata, OTTU na sasa Msondo, Mlimani Park iliyokuja kufahamika pia kama DDC Mlimani Park na Orchestra Safari Sound '(OSS) 'wana Ndekule'.

Ngoma bado! Hukumuya Zitto Kabwe kesho



Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeahirisha kutoa au kutotoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya Chadema kutojadili uanachama wa Zitto Kabwe mpaka kesho saa nane mchana!
GPL

TPBO yajivua gamba sakata la Cheka

Cheka (kushoto) alipokuwa akichapana na Phil Williams wa Marekani na kutwaa taji la WBF kabla ya kwenda kulipoteza nchini Russia hivi karibuni
OGANAIZESHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited) imejivua lawama juu ya kitendo cha bondia Francis Cheka kusafiri kwenda Russia bila maandalizi na kuvuliwa taji lake la dunia la WBF.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na oganaizesheni hiyo kupitia Rais wake, Yasin Abdallah 'Ustaadh', TPBO ilihusika kumsaidia Cheka aliyewafuata kulia ukata kupata nafasi ya kwenda kucheza nje kwa malipo yatakayomnufaisha kw akushirikiaa na PST iliyomsaidia kupata kibali cha safari yake nje ya nchi.
TPBO inasema siyo wao au PST ambao walipaswa kujua maandalizi ya bondia huyo ambaye alidai alikuwa katika hali mbaya kiuchumi zilizoathiri biashara zake kwani jukumu hilo ni la bondia mwenyewe na kocha wake.
Taarifa hiyo inasema baada ya Cheka kuwaomba wamsaidie kwa kushirikiana na PST, walimfanyia mipango ya kwenda Russia kupigana kwa makubaliano ya dau la Dola za Kimarekani 10,000 (sawa na Mil. 16) ikizingatiwa hali yake kifedha haikuwa nzuri pia kuwa na mkata bila fedha hakukuwa na faida kwake.
"Cheka alituarifu mimi na rais wa PST, Emmanuel Mlundwa kwamba anakabiliwa na matatizo makubwa sana ambayo yameathiri kwa kiasi kikubwa biashara zake, hivyo tumsaidie apate pambano ambapo bahati alijitokeza promota toka Kenya, Franklyne Imbenzi kabla ya kuzungumza moja kwa moja na promota wa nchini Russia waliyeafikiana baada ya awali Cheka kumgomea Mkenya," taarifa hiyo inasemeka hivyo.
"Naomba muelewe yote yaliyofanyika kuhusu Francis Cheka tulikuwa tunayajadili kwa pamoja kati ya PST, TPBO na bondia mwenyewe, pia katia ngumi za kulipwa bondia ni kama mfanyabiashara uangalia faida hivyo tusibebeshwe lawama kwa kulipoteza taji lake la Dunia," taarifa hiyo iliongeza.
Tarifa hiyo ilimalizia kwa kusema safari nzima ya kwenda Russia kuanzia kusaini mkataba kupewa visa na kupanda ndege hadi nchini humo na kupanda ulingoni, Cheka alikuwa akifanya kwa hiari yake bila kulazimisha hivyo wadau wa ngumi wasitafute mchawi wakati mhusika amefanya mambo kwa utashi wake.

Simba yaifuata Azam Robo fainali Mapinduzi, Kiemba aaah


BAO pekee la mapema la Amri Kiemba liliisaidia Simba kufuzu robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kuungana na Azam ambayo leo itakamilisha ratiba kwa kuvaana na Ashanti United katika mechi za kundi C.
Kiemba alifunga bao hilo akimalizia kwa kichwa pasi ya Ally Badru na kuwa bao lake la pili katika michuano hiyo na mawili kwa Simba ambayo imemaliza mechi za makundi usiku wa jana kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mabingwa wa visiwani, KMKM ikifikisha pointi 7.
Azam ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo wenyewe walikuwa wa kwanza kufuzu hatua hiyo baada ya kuongoza kwenye kundi lake la kupata ushindi mara mbili mfululizo na leo itaumana na Ashanti walioingizwa dakika za jioni baada ya Yanga kuchomoa kushiriki mashindano hayo.
Ashanti yenyewe ina pointi moja kutokana na mechi mbili.
Nyingine zilizofuzu hatua hiyo ni KCC ya Uganda, iliyoongoza kundi B lenye timu ya Simba, KMKM na AFC Leopards ya Kenya iliyoaga mashindano.
.

Babi ajitabiria makubwa UiTM

Babi (kati)nakiwa na wachezaji wenzake wa UiTM
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Kassim 'Babi' amesema ameyazoea kwa haraka mazingira ya nchi ya Malaysia alikoenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya UiTM na kudai ana imani atafanya vyema Ligi Kuu ya nchi hiyo ikianza.
Nyota huyo wa zamani wa klabu ya Mlandege, Mtibwa Sugar, Yanga, Azam na KMKM, aliliambia gazeti hili kwamba anashukuru kwa kipindi kifupi tangu atue katika nchi iliyopo Mashariki ya Mbali, ameweza kuzoea mazingira na kuzoeana na wachezaji wenzake wanaojiandaa na msimu mpya wa ligi.
Babi anayefahamika pia kama 'Ballack wa Unguja' alituma picha yake ikimuonyesha akiwa na wachezaji wenzake wa klabu hiyo wakiwa wamepozi baada ya kutokana kufanya mazoezi na kusema tofauti na fikira zake Malaysia kunaonekana kutakuwa kwepesi kwake kuliko ilivyokuwa Vietnam alipocheza soka la kulipwa.
Mchezaji huyo aliwahi kuichezea DT Long ya Vietnam kwa muda wa miezi nane baada ya kujiunga nayo mwaka 2010 akitokea klabu ya Yanga na kurejea nyumbani kujiunga na Azam kwa mkataba wa miaka miwili.
"Kwa hali hii nadhani nitafanya vyema kwa sababu nimeyazoea mazingira kwa kipindi kifupi mno tofauti na nilivyodhani. Bahati nzuri asilimia kubwa ya watu wa hapa ni waislam hivyo hata chakula ni kile nilichozea kula. Kwa sasa tunajifua kwa ajili ya msimu mpya wa ligi utakaoanza Januari 18," alisema Babi.
Babi alijiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea KMKM waliomsajili baada ya kuachana na Azam aliyoichezea msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Gwiji Eusebio afariki, aliliwa na wengi

Gwiji Eusebio enzi za uhai wake

Akiwajibika uwanjani enzi za uhai wake

Eusebio akiwa na Ronaldo
LISBON, Ureno
GWIJI wa soka wa Ureno na Klabu ya Benfica, Eusebio amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 71.
Akiwa amezaliwa nchini Msumbiji mwaka 1942, Eusebio alipelekwa Ureno na Kocha Mkuu wa Benfica, Bela Guttman, ambaye alimsajili  mchezaji huyo mwaka 1961 baada ya kufunga safari yeye mwenyewe ya kwenda Afrika kumuona akicheza.
Mshambuliaji huyo, aliyepewa jina la 'Lulu Nyeusi', aliibuka kuwa mmoja wa magwiji wakubwa kwa klabu na Taifa la Ureno, akishinda makombe ya Ligi ya Kuu mara 11, makombe ya matano ya ndani na 1962 ubingwa wa Ulaya akiwa na Aguias, pamoja na kuiwezesha Ureno kumaliza washindi wa tatu wa Kombe la Dunia 1966.
Kutokana na kasi yake, nguvu na ufundi, Eusebio alikuwa hazuiliki katika Ligi Kuu ya Ureno na alikuwa na wastani wa kufunga zaidi ya bao moja kwa mechi, 'akitupia' mabao 319 katika mechi 313 za ligi, anabaki kuwa mfungaji bora wa zama zote wa Benfica kwa sasa.
Kipaji chake kilimwezesha kumaliza mfungaji bora nchi Ureno mara sita, kushinda mara mbili tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya (1968 na 1973) na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya 1965 wakati Benfica ikitisha katika soka la Ulaya.
Utawala wa Eusebio haukuishia katika ligi za ndani tu. Aliichezea timu yake ya taifa mechi 61 na kuifungia mabao 41 kwa timu ya Taifa ya Ureno, na inayokumbukwa zaidi ni kumaliza fainali za Kombe la Dunia 1966 akiwa mmoja wa nyota wakubwa wa fainali hizo. Alifunga mabao tisa na kutwaa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa Kombe la Dunia 1966 na pia alifunga bao wakati timu yake ilipowalaza Soviet Union 2-1 na kuwa washindi wa tatu.
Baada ya miaka 15 akiwa Benfica, Eusebio alicheza muda wote uliobaki wa soka lake Amerika Kaskazini, akiwakilisha klabu kadhaa za nchini Mexico na Marekani kabla ya kustaafu 1978.
Mshambuliaji huyo anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasoka bora zaidi waliopata kutokea duniani na aliwekwa Na.9 katika tuzo ya Fifa ya 'Mwanasoka Bora wa Karne'. Wapo pia wanaomini Eusebio ndiye alikuwa mwanasoka bora kuliko wote duniani -- zaidi ya Pele na Maradona.
Cristiano Ronaldo alikuwa miongoni mwa waliotuma salamu zao za rambirambi kwa gwiji huyo kupitia akaunti yake ya Twitter: "Daima milele, Eusebio, upumzike kwa amani."
Ripoti nchini Ureno zinadai kwamba alifariki baada ya kupatwa na tatizo la moyo kusimama (cardiac arrest) asubuhi ya jana.
Pamoja na Ronaldo, nyota wengine waliomlilia gwiji huyo kupitia kurasa zao za Twitter na hivi ndivyo walivyoandika:-

Xabi Alonso
RIP Eusebio (1942-2014). Mmoja wa magwiji.

Luís Figo
Mfalme!! Grande perda para todos nos! O mais grande!!

Michael Owen
Huzuni kusikia kwamba Eusebio amefariki dunia. Mabao 733 katika mechi 745 daima itabaki kumtambulisha kama gwiji wa kweli wa soka. R.I.P.

Vincent Kompany
Heshima kwa mtu ambaye ameufanyia makubwa mchezo huu ninaoupenda. Eusebio, mmoja wa magwiji bora wa zama zote, alazwe mahala pema.

Manchester United
Tumehuzunishwa kusikia gwiji wa Benfica, Eusebio amefariki dunia. Alikuwa ni bonge la mchezaji na rafiki wa klabu.

Boti ya Kilimanjaro yaua 6,. miili yatambuliwa


WATU kumi wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti  katika Bahari ya Hindi.
Katika ajali ya kwanza, watu sita walifariki baada ya boti ya Kilimanjaro II ilipokumbwa na dhuruba kali katika mkondo wa Nungwi, Zanzibar wakati ikitokea Pemba kwenda kisiwani Unguja jana asubuhi.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Juma, alisema jana jioni kuwa maiti sita zilipatikana na kwamba abiria watatu waliokolewa wakiwa hai huku uokoaji ukiendelea.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yusuph Ilembo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa kazi ya kuwatafuta watu wanaohofiwa kupotea imeanza kufanywa na mabaharia kwa kushirikiana na wananchi.
Alisema boti hiyo ilipofika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa na wimbi moja kubwa na injini kuzimika na watu waliokuwa wamekaa juu wakiwamo watoto waliteleza na kuhofiwa kutumbukia ndani ya bahari.
Alisema kuwa boti hiyo baada ya injini zake kuzimika ilibakia ikielea baharini na kwamba Nahodha wake alifanikiwa kuziwasha tena na kuendelea na safari na abiria waliobakia walifika salama.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar Maalim, alisema wazamiaji waliondoka jana mchana kuungana na baadhi ya wananchi huko Nungwi kufanya kazi ya kutafuta watu wanaohofia kupotea baada ya ajali hiyo.
Hata hivyo, alisema ZMA itatoa taarifa baada ya kukamilika uhakiki wa majina ya abiria kwa meli zote zilizosafiri jana kutoka kisiwani Pemba pamoja na wazamiaji kufika katika eneo la tukio na kufanya kazi ya kutafuta watu hao.
Hata hivyo, wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khalfan Mohamed Mshangi, alisema baadaye kuwa zimepatikana maiti tano na tatu zimetambuliwa.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Akram Khamis issa (11), mkazi wa Mwanakwerekwe; Masoud Hamad Abdallah (30), mkazi wa Wete na Nashra Khamis (9), mkazi wa Mombasa, Zanzibar.
Aliongeza kuwa boti hiyo ilikuwa na abiria 396 wakiwamo watoto 60 na kwamba abiria ambao hawajapatikana ni 18.
Baadhi ya mashuhuda waliohojiwa  walisema mkasa huo ulitokea sasa 2:30 asubuhi wakati boti hiyo ilipofika eneo la Nungwi na kupigwa wimbi kali na kuelemea upande mmoja.
Suleiman Muhammed Said, abiria katika boti hiyo, alisema baada ya boti hiyo kuelemea upande mmoja, baadhi ya watu walidondoka baharini pamoja na mizigo na kwamba boti iliendelea na safari baada ya kukaa sawa.
Alisema boti hiyo iliondoka Pemba majira ya saa 2:00 asubuhi na kwa mujibu wa  ratiba, boti ilitarajiwa kufika Unguja saa 4:00 asubuhi, lakini kutokana na hitilafu hiyo, ilifika saa 6:00 mchana.
Alisema boti ilipoondoka Pemba, hali ya bahari haikuwa nzuri na ilipofika Nungwi hali ya bahari ilizidi kuchafuka na boti kuyumba.
Alisema hadi boti inafika bandarini, ndugu zake wawili hawakuonekana pamoja na mizigo waliyokuwa  nayo katika boti hiyo.
“Nilikuwa na ndugu zangu wawili na mizigo, baada ya meli kutaka kuzama mizigo na baadhi ya watu walidondokea baharini, lakini meli ilipoibuka iliendelea na safari bila ya kuwatafuta,” alisema Suleiman huku akitokwa machozi.
Baadhi ya watu walifika bandarini Malindi waliangua vilio na sura zao kujaa na huzuni kutokana na kutowaona ndugu na jamaa zao.
Abdallah Mohammed Abdallah, aliyefika bandarini kumtafuta mtoto wake ambaye bado hakuwa na taarifa zake, alisema alipokea simu ya mtoto wake aliyekuwamo katika boti saa 2:30 asubuhi kuwa boti inazama.
“Nilipokea simu ya mtoto wangu, alikuwa akilia na kuniambia baba baba tunakufa, meli huku inazama, baada ya hapo simu yake ikawa haipatikani” alisema Abdallah.
Aidha alisema alifika bandarini kupata taarifa sahihi, lakini hakupewa jibu linaloridhisha kutokana na boti kufika bila kumuona mtoto wake.