STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 6, 2013

Wanafunzi 29 na mwalimu wao wauwawa katika shambulio la kigaidi

Potiskum, Nigeria (AP)
WANAFUNZI 29 pamoja na mwalimu wao wameuwawa alfajiri ya leo Kaskazini mwa Naigeria kwa kile kilichoelezwa shambulio la kigaidi lililofanya na kundi la waasi la Boko Haram
Baadhi ya waathirika ambao bado wanatibiwa majeraha ya risasi na kuchomwa moto wamesema baadhi ya wanafunzi walichomwa moto wakiwa hai katika shambulio hilo kabla ya alfajiri ya Jumamosi (leo) katika shule ya sekondari ya serikali iliyopo mjini Mamudo jimboni Yobe.
Huku akitokwa na machozi ya uchungu pembeni ya miili ya wavulana wake wawili, mkulima Malam Abdullahi aliapa kuwaondoa wanae watatu waliobaki katika shule ya jirani.
Alilalamika kwamba kulikuwa hakuna ulinzi kwa ajili ya wanafunzi licha ya kupelekwa kwa maelfu ya askari tangu serikali ilipotangaza hali ya dharura katikati ya Mei katika majimbo matatu ya Kaskazini-mashariki.
Shule nyingi zimechomwa moto na idadi kubwa ya wanafunzi kuuawa wakiwamo zaidi ya waathirika 1,600 waliouawa katika matukio hayo ya kigaidi tangu 2010.

Baada ya Khanga Moja sasa zamu ya Baikoko

BAADA ya kundi la Khanga Moja kuacha gumzo kubwa katika ziara yake ya Kanda ya Ziwa kwa kupigwa picha wakinengua utupu kama nchi haina serikali, safari hii imekuwa zamu ya kundi la Baikoko kutokea Tanga.

Kundi hilo ambalo linanengua muziki asilia wa chakacha na zile zenye asili ya mkoa wa Tanga, nalo limelipuka na picha za kudhalilisha kama zinavyoonekana hapo chini ambapo MICHARAZO inawaomba radhi kwa jinsi zilivyo, lakini lengo kutaka kuikumbusha serikali marufuku yao bado haifanyiwi kazi.

Dansa wa kundi hilo akimuonyesha manjonjo shabiki kwa mauno
Mnenguaji wa kundi hilo akionyesha staili ya kubana kalio
Huu ni uungwana?
Kwa unenguaji huu halafu tunapamba na ugonjwa wa UKIMWI, tutafika kweli?
 
Shuhudia mwenyewe, hii kama sio laana ni nini?

AJALI! SUMRY LAUA 9 WENGINE HOI

Basi la Sumri likiwa kwenye mto baada ya kutumbikia na kuua abiria 9


Basi hilo likiopolewa na 'kijiko' toka mtoni huku watu wakishuhudia
BASI la kampuni ya Sumry limetumbukia mtoni Iku na kuuwa watu tisa na kujeruhi wengine hamsini na tatu.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa sita usiku kuamkia Julai 5, 2013 basi hilo lilipokuwa likitokea mjini Sumbawanga kuelekea Mpanda mkoani Katavi likiwa na abiri waliokuwa wametoka Mbeya.

Ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele mkoani Katavi

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Katavi Emanuely Nnley alisema jana kuwa ajali hiyo ilihusisha basi aina ya Nissan Diesel lenye namba T909 AZT mali ya kampuni ya Sumry lililokuwa likiendesha na dereva aliyetajwa kwa jina na Stephano Chimane maarufu kwa  jina la Ntungu.

Alisema basi hilo lilipofika katika daraja hilo lenye kona kali na mteremko dereva wake alishindwa kulimudu na kulenga daraja hali iliyosababisha tairi za nyuma kupanda juu ya ukingo na kutumbukia mtoni ambapo dereva wa basi hilo aliweza kutoka na kukimbilia kusikojulikana Mkuu wa mkoa wa Katavi Dk Rajabu Rutengwe alitoa rambi rambi kwa wafiwa wote na kuwapa pole wahanga wa ajali hiyo mbaya kutokea tangu mkoa huo uanze.

Sylona ndiye Redd’s Miss Temeke 2013

Mshindi wa Redds Miss Temeke 2013, Sviona Nyameyo (katikati), akiwa na mshindi wa pili,  Narietha  Boniface na mshindi wa tatu,  Latifa Mohamed mara baada ya kutangazwa washindi katika shindano hilo lililofanyika jana TCC Chang'ombe.

KISURA Sylona Nyameyo jana usiku alifanikiwa kutwaa taji la Redd’s Miss Temeke lililofanyika katika Ukumbi wa TCC Changombe, jijini Dar es Salaam.
Sylona mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akisomea mambo ya sheria alifanikiwa kuwashinda warembo wengine na kufanikiwa kujitwalia taji hilo.
Katika shindano hilo lililokuwa na upinzani mkali, ulioambatana na burudani za kumwaga, ilishuhudiwa nafasi ya pili ikienda kwa Marietha Boniface, ambaye naye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUCHS).
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Latifa Mohammed ambaye amemaliza kidato cha sita mwaka huu, hivyo warembo hao kujihakikishia nafasi ya kuingia katika fainali za Redd’s Miss Tanzania.
Ushindani ulionekana dhahiri katika shindano hilo, ambapo warembo walikuwa wakichuana mno, huku mashabiki waliojitokeza hapo wakijikuta wakishangilia muda wote.
Akizungumza mara baada ya kuvikwa taji hilo, Sylona alisema amefurahishwa mno na matokeo hayo na atahakikisha hawaangushi wakazi wa Temeke katika shindano la Redd’s Miss Tanzania.
“Nilijua toka mwanzo lazima niwashinde, maana nilijiamini na niliona nina vigezo vyote, sasa ni wakati wa kwenda kupambana katika Redd’s Miss Tanzania ili kurudisha heshima ya Temeke,” alisema.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Polisi wadai kumnasa gaidi linalosakwa UK


Robert Manumba akionyesha picha za mtu anayehisiwa kuwa gaidi anayesakwa pia na Uingereza

JESHI  la Polisi nchini limemtia mbaroni mtu mmoja mjini Mbeya anayedaiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi akiwa na hati mbili za kusafiria, na mwingine Mtanzania adakwa akidaiwa kusaidiana naye.
Mtu huyo aliyekamatwa wilayani Kyela, pia anatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi nchini Uingereza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia majina mawili tofauti kwenye hati za kusafiria na alikuwa akijaribu kuvuka mpaka wa Tanzania kuelekea Malawi.

Alisema mtuhumiwa huyo alitumia hati ya Tanzania yenye namba AB 651926 yenye jina la Adil Ally Patel na hati ya Uingereza yenye namba NO 51555382 yenye jina la Iqbal Hassan Ally.

Manumba alisema hati ya Tanzania aliyokamatwa nayo ni kati ya hati 26 zilizoibiwa kwenye Ofisi za Uhamiaji mwaka mmoja uliopita.

Alisema mshukiwa wa ugaidi alikuwa akisaidiwa na Mtanzania mmoja ambaye hakumtaja jina na baada ya kukaguliwa kompyuta mpakato (laptop) yake ilikuwa na maneno ya uchochezi ya kidini kuhusu imani tofauti.

Manumba alisema aliwasiliana na Serikali ya Uingereza kuhusu hati ya mtuhumiwa huyo na kuelezwa kuwa ni halali na kufahamishwa kuwa mtu huyo wanamtafuta kwa tukio la ugaidi nchini Uingereza.

Alisema kuna Mtanzania mwingine ambaye hakumtaja jina, alikamatwa kwa kuhisiwa kujihusisha na mtuhumiwa huyo wa ugaidi ambaye baada ya kukaguliwa pia alikutwa na kompyuta yenye maneno ya uchochezi dhidi ya dini isiyomhusu.

Alisema mtuhumiwa huyo alijitambulisa kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kimoja kilichopo nchini Sudan.

Manumba aliwataka wazazi kuwa waangalifu na vijana wao wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa kuwa baadhi yao hurubuniwa na kujiingiza katika mambo yanayohusiana na ugaidi.

Aliongeza kuwa polisi wana uhakika kwamba kuna baadhi ya vikundi vya kigaidi ndani ya nchi ambavyo vina mipango ya siri ya kutekeleza ugadi nchini.

Aliwataka Watanzania kuwa waangalifu wakati polisi ikifanya kazi yake ya uchunguzi na kuonyesha kuwa hali ya usalama si nzuri nchini kutokana na matukio ya kihalifu yanayoendelea.

Aidha, alisema polisi inaendelea na uchunguzi dhidi ya matukio ya mlipuko miwili ya mabomu iliyotokea mkoani Arusha na lile la kuuawa kwa Padri Evarist Mushi, Zanzibar.

Alisema matukio hayo yameonyesha sura mbaya kwa Tanzania ya kuwepo kwa tishio la ugaidi.
Alisema uchunguzi utakapokamilika washitakiwa watafikishwa kwemnye mikono ya sheria kuhukumiwa kwa makosa ya jinai.

Aliongeza kuwa taarifa zitakazokuwa zikitolewa na raia wema zitasaidia polisi kurahisisha uchunguzi na kuwakamata wahusika kwa wakati.

Manumba ametahadharisha kuwa ongezeko la uhalifu nchini limekuwa likihusisha baadhi ya wananchi kutumika vibaya na wavunjifu wa amani.

Alisema kufuatia matukio hayo, baadhi ya watuhumiwa wanashikiliwa na baada ya uchunguzi kukamilika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Hii ni sifa mbaya Watanzania wanapaswa kujiepusha na vishawishi vya aina yoyote vitakavyopelekea kuvunjika kwa amani iliyopo tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania,” alisema.

Katika matukio ya kigaidi yaliyotokea siku za hivi karibuni watu watatu walikufa na zaidi ya 70 kujeruhiwa baada ya kurushwa bomu kanisani na mtu asiyefahamika katika kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Arusha wakiwa wamejumuika katika uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti.

Katika tukio jingine jijini humo, bomu lilipuka kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) eneo la Soweto kata ya Kaloleni mkoani Arusha.

Katika tukio hilo watu watatu walifariki dunia kutokana na mlipuko wa bomu wakati chama hicho kikiwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani.
Wakati huo huo Manumba alisema polisi jijini Dar es Salaam limekamata meno ya tembo 347 katika eneo la Kimara ambayo yanaamika yamepatikana kwa njia za kijangili katika mbuga za Tanzania.

Alisema mbali na nyara hizo, kuna meno mengine ya tembo 788 yalikamatwa nchini Malawi katika mji wa Mzuzu na kwamba inaamika kuwa yalisafirishwa kutoka Tanzania kama mzigo wa saruji kutoka katika kiwanda cha Saruji Mbeya.

Manumba alisema polisi nchini wanafanyakazi kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa kuhakikisha kuwa ukweli wa matukio yanakuwa wazi na uchunguzi ukikamilika wahusika watafikishwa katika vyombo vya sheria. 

CHANZO: NIPASHE