STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 6, 2013

Mgombea Ubunge CHADEMA 'awapaka' Wabunge waliojimilikisha majimbo, aiomba NEC

Nagy Kaboyoka
ALIYEKUWA Mgombea wa Ubunge Jimbo la Same Mashariki kupitia CHADEMA, Naghenjwa 'Nagy' Kaboyoka amewataka wabunge kutojimilikisha majimbo na kuyafanya kama mali zao binafsi na kuchukia wengine kuchangia maendeleo wakidhani itawafanya wang'oke uongozini.
Aidha ameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inadhibiti vitendo vya wizi wa kura katika chaguzi zijazo ili kuliepusha taifa kuingia matatizoni iwapo wapiga kura watakapoamua waliyemchagua apewe ushindi.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum, Nagy, alisema imekuwa ni tatizo kubwa kwa wabunge waliopo madarakani kukerwa wanapoona wanasiasa wengine wakijitolea kwenye shughuli za kimaendeleo katika maeneo yao kana kwamba majimbo yake ni mali binafsi.
Alisema kwa vile maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini yakiwamo majimbo huletwa na wananchi wote hivyo wanaoshikilia uongozi wasichukie wanapoona watu wengine wakijitolea kwa hisia kuwa wataporwa nafasi zao.
"Imekuwa ni tatizo baadhi ya wabunge wanapoona watu wengine hasa wanasiasa wakipeleka miradi ya maendeleo kuchukia kwa kuhisi ni mbinu za kuwang'oa madarakani, bila ushirikiano maendeleo yatatoka wapi," alihoji.
Alisema kwa mfano yeye kupitia asasi yake ya WOYEGE ilipeleka mradi wa mnada wa Ng'ombe katika kijiji cha Muheza , Kata ya Maore uliokamilika hivi karibuni, lakini alipata vikwazo vikubwa kama sio busara za Mkuu wa Wilaya, Herman Kapufi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same,Joseph Mkude.
"Lazima nikiri DC na DED ni watu waliokomaa kisiasa na uongozi kwa namna walivyotusaidia kufanikisha lengo la kuwasaidia wafungaji kuwa na eneo la mnada na kuwapelekea maji, la sivyo nilishakwamishwa," alisema.
Alisema ni lazima wabunge na viongozi wengine watanguliza utaifa mbele kwanza badala ya itikidi za vyama na hisia kwamba nafasi walizonazo ni za kudumu au waliozaliwa nazo kiasi cha kujiona kama masultani.
Pia akaitaka NEC kuhakikisha chaguzi zijazo zinafanyika kwa uhuru na haki ili kuondoa uchakachuaji kama ulivyojitokeza katika baadhi ya maeneo kwenye uchaguzi uliopita akidai kuachwa kwake kunaweza kulata machafuko.
Nagy alisema wapiga kura watakapochoka kuona haki yao ya kutaka kuongozwa na nani ikipuuzwa inaweza kuleta maafa yasiyo na sababu hivyo kutaka NEC iwe makini licha ya kusubiri mabadiliko ya katiba mpya aliyodai inaweza kuondoa tatizo hilo la wizi wa kura unaolalamikiwa kila mara.
Nagy aliwania ubunge katika jimbo hilo na kuangushwa na mpinzani wake, Anne Kilango, huku ikielezwa kulikuwa na dosari kadhaa katika baadhi ya kata nakumfanya aamini 'alichakachuliwa' matokeo yake.

No comments:

Post a Comment