_MG_8474
Na Suleiman Msuya
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ipo katika mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma zake zinapatikana kwa njia ya mtandao kieletroniki (online registration) ambapo kwa kuanzia imekwisha weka baadhi ya nyaraka za mafaili kwenye mfumo huo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Huduma, Utawala na Fedha Bosco Gadi wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na kujipanga kuingia katika mkakati huo wa kieletroniki pia wapo mbioni kurahisisha njia za malipo kwa kutumia mabenki ambapo kwa sasa wamekubaliana na CRDB na NMB na mpango huo utaanza Julai 15 mwaka huu katika benki ya CRDB.
Gadi alisema mpango huo utasaidia wadau kulipa ada za usajili kwa njia ya benki popote walipo, pia mfumo huo utasaidia kuwahakikisha kuwa wadau kupata huduma zote ambazo zinasimamiwa na BRELA.
“Tupo kwenye mchakato wa kutoa huduma katika njia ya kieletroniki pamoja na wadau kulipia kupitia benki ambapo kwa sasa tumeanza na CRDB kuanzia Julai 15 mwaka huu,” alisema.
Aidha Kaimu Meneja huyo wa Huduma, Utawala na Fedha alisema BRELA katika kuhakikisha kuwa dhana ya ushirikiano na Sekta Binafsi yaani PPP inafanikiwa imeingia mkatapa wa ushirikiano na Chama Cha Wafanyabiashara na wenye Viwanga na Kilimo Tanzania (TCCIA) ili waweze  kutoa huduma saidizi za awali za kusajili makampuni na leseni za biashara katika ngazi ya Mikoa na Wilaya Tanzania Bara.
Gadi alisema kuchaguliwa na TCCIA kunatona na taasisi hiyo kuwa na mtandao mpana wa kieletroniki unaounganisha ofisi zao za Wilaya takribani nchi nzima kwa upande wa Bara.
Alisema wateja wa BRELA waliopo Wilayani na Mikoani wanaombwa kutumia ofisi za TCCIA kwani maombi yao yatawafikia makao makuu bila tataizo lolote.
Kaimu Meneja alisema mfumo huo ambao ulianza Desemba mwaka 2012  umeonyesha mafanikio makubwa ambapo hadi sasa maombi 500 yamefanikiwa kusajiliwa kupitia TCCIA.
Aidha alisema kupitia utaratibu huo unagharimu shilingi 6,000 za uasajili wa jina la biashara ambazo zinalipwa BRELA na shilingi 2,000 ambazo zinalipwa kwa ajili ya masuala ya utawala na kutumwa kwa maombi.
Pia aliweka bayana kuwa kwa upande wa makampuni ada ya usajili inayotakiwa kulipwa itategemea na kiasi cha mtaji cha mteja anachokiandika kwenye katiba ya kampuni anayotarajia kuisajili.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa BRELA Andrew Mkapa alisema ofisi yao haitosita kuichukulia kampuni au biashara ambayo inaenda kinyume na sheria zinazoiongoza BRELA.
Alisema ni vyema watu na kampuni ambazo zinasajiliwa kufuata taratibu ziliopo katika katiba zao pamoja na zile za BRELA.
Mkapa alisema iwapo kampuni au leseni ya biashara itaonekana kuvunja sheria kuna taratibu za kumtaarifu muhusi ambapo itakuwa ni ya muda wa miezi mitata na iwapo hakutakuwa na majibu sahihi uamuzi wa kuifuta utafanyika.