STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 13, 2014

Nyota wa zamani Simba kutimkia Afrika Kusini

David Naftari
BEKI wa zamani wa AFC Arusha na Simba, David Naftar anajiandaa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya majaribio baada ya mkataba wake na Bandari Kenya ukielekea ukingoni.
Mchezaji kiraka huyo anayemudu nafasi nyingi uwanjani, alisema ataenda kwenye majaribio hayo mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza la Ligi Kuu ya Kenya iliyosaliwa raundi tatu kabla ya kuisha.
Akizungumza na MICHARAZO kutoka Kenya anakocheza soka la kulipwa katika klabu ya Bandari, Naftari alisema mipango hiyo ya kwenda Afrika Kusini inafanywa na wakala wake.
"Japo sijaambiwa nitaenda kujaribiwa katika klabu gani, lakini nitaondoka baada ya ligi kusimama, kwa sasa tumebakisha mechi tatu kabla ya duru hilo kumalizika," alisema.
Kuhusu mktaba wake na Bandari, Naftari alisema unafikia tamati Agosti mwaka huu na tayari viongozi wake wameonyesha nia ya kutaka kumuongezea, lakini mwenyewe hajafanya maamuzi bado.
"Uongozi wa Bandari unaonyesha bado unanihitaji, lakini nataka kwanza niende majaribuni nikirudi nitajua la kufanya kwani mkataba unaisha mwezi wa nane," alisema.
Mchezaji huyo alisema kwa kuwa soka ni maisha yake, daima huwa anapigana kuzidi kusonga mbele zaidi na alipo ndiyo maana hataki kurejea Tanzania kucheza baada ya kuchoshwa na mizengwe.
Naftari alikuwa miongoni mwa wachezaji walioibeba Bandari baada ya kipa Ivo Mapunda, Mohammed Banka na Thomas Mourice waliorejea nchini na Meshack Abel wanaendelea kuichezea mpaka sasa.

Rodgers wa Liverpool, Tony Pullis watwaa tuzo England

RODGERS AKIKABIDHIWA TUZO YAKE
KOCHA wa Liverpool, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Engalnd, Brendan Rodgers ameshinda tuzo ya kocha bora kuliko wote nchini England.
Tuzo hiyo maarufu kama LMA hutolewa baada ya makocha katika madaraja yote nchini humo kupiga kura kumchagua nani ni bora zaidi.
PULLS AKIPEWA TUZO
Pamoja na Liverpool kushika nafasi ya pili lakini Rodgers amekuwa kocha wa Liverpool kushinda tuzo hiyo.
Wakati kocha huyo wa Liverpool akibeba tuzo hiyo ya juu zaidi, Tony Pulls wa Crystal Palace amekuwa kocha bora wa Ligi Kuu England.
Hii maana yake, Rodgers ni bora kwa England kwa kujumuisha na ligi zote ikiwemo Ligi Kuu England wakati Pulls ni kocha wa ligi hiyo moja tu.

Machaku asema hana mkataba JKT Ruvu zinazomtaka zimfuate

MSHAMBULIAJI nyota wa JKT Ruvu, Salum Machaku 'Balotelli' amesema hana mkataba wowote na timu hiyo na hivyo kuiacha milango wazi kwa klabu yoyote inayomhitaji kuzungumza naye.
Machaku aliyewahi kutamba na timu za Simba, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro, alisema yupo tayari kutua katika klabu yoyote itakayokuwa ikimhitaji mradi waridhiane katika suala la masilahi.
Mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu huu akiwa na mabao manne alisema kwa sasa amekaa tayari kupokea maombi kutoka kwa timu yoyote ili kuweza kujiunga nayo au ikiwezekana kubaki JKT.
Alipoulizwa kama timu yake ya zamani ya Polisi Moro iliyorejea Ligi Kuu ikimfuata ili kumrejesha kikosini, alisema angefurahia kwa sababu hakuondoka kwa ugomvi katika timu hiyo iliposhuka daraja.
"Nipo tayari kurudi Polisi Moro, ni timu ninayoiheshimu, pia maisha yangu yanategemea soka sina cha kuchagua wala kubagua ila nimefurahi kuona wamerejea tena ligi kuu," alisema.
Machaku, mmoja wa watoto wa nyota wa zamani wa muziki wa dansi aliyewahi kutamba na bendi za Dar International na DDC Mlimani Park, Salum Machaku, alisema anaamini ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu kuliko ya msimu huu ambayo haikutabirika kirahisi.
"Ligi ya msimu huu ilikuwa ni noma, siyo kwa timu za juu wala mkiani. Hapakuwa na iliyokuwa na uhakika wa itakachovuna hadi dakika za mwisho," alisema.

Hiki ndicho kikosi cha Black Stars, wamo Essien, Boateng

KIUNGO nyota wa AC Milan, Michael Essien na Kevin-Prince Boateng wamejumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 26 kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.
Kikosi hicho kitapunguzwa na kubaki wachezaji 23 baada ya mchezo wa kirafiki na Uholanzi Mei 31, ambacho ndiyo watakwenda Brazil.
Essien na Boateng wameitwa baada ya kurejea kwenye soka ya kimataifa mwaka jana, kufuatia awali kuomba kujipumzisha kuichezea timu hiyo.
Nchi ya Ghana imepangwa kundi moja na timu za  Marekani, Ujerumani na Ureno likitajwa kuwa ni moja ya makundi ya kifo katika fainali za mwaka huu zitakazoanza mwezi ujao nchini Brazili.

Kikosi kamili cha Black Stars ni kama kifuatavyo:
Makipa: Stephen Adams (Aduana Stars), Fatau Dauda (Orlando Pirates), Adam Kwarasey (Stromsgodset)
 
Mabeki: Harrison Afful (Esperance), Jerry Akaminko (Eskisehirspor), John Boye (Stade Rennes), Samuel Inkoom (Platanias), Jonathan Mensah (Evian Thonon Gaillard), Daniel Opare (Standard Liege), Jeffrey Schluup (Leicester City), Rashid Sumaila (Mamelodi Sundowns)
 
Viungo: David Accam (Helsingborg), Afriyie Acquah (Parma), Albert Adomah (Middlesbrough), Emmanuel Agyemang Badu (Udinese), Kwadwo Asamoah (Juventus), Christian Atsu (Vitesse Arnhem), Andre Ayew (Olympique Marseille), Michael Essien (AC Milan), Rabiu Mohammed (Kuban Krasnodar), Sulley Muntari (AC Milan), Mubarak Wakaso (Rubin Kazan)
 
Washambuliaji: Jordan Ayew (Sochaux), Kevin Prince Boateng (Schalke 04), Asamoah Gyan (Al Ain), Abdul Majeed Waris (Valenciennes).

Homa ya Dengue yampitia Pentangone wa Twanga

MUIMBAJI wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Ramadhani Mhoza 'Pentagone' ameongeza idadi ya wasanii waliokumbwa na ugonjwa mpya wa homa ya Dengue baada na kulazwa hospitalini kutokana na kuugua ugonjwa huo unaofanana na Malaria.
Pentagone alikumbwa na ugonjwa huo wiki iliyopita na kulazwa hospitalini kwa siku tatu kabla ya kupata nafuu na kuruhusiwa kwenda kujiuguzia nyumbani kwake, ambako kwa sasa anaendelea vyema.
Akizungumza na MICHARAZO akiwa mapumziko nyumbani kwake, Pentagone, alisema hakuwa anajua lolote kuhusu ugonjwa huo mpya hadi alipokimbizwa hospitalini baada ya kuumwa kichwa, kuhisi uchovu na kuumwa kwa viungo vya mwili na alipopimwa na madakatari aligundulika kuambukizwa homa hiyo mpya inayozidi kushika kasi kwa sasa nchini.
Pentagone alisema anashukuru kwa sasa anaendelea vyema japo bado hana nguvu na anaamini wakati wowote atarejea tena jukwaani kuungana na wanamuziki wenzake.
"Namshukuru Mungu naendelea vyema, nilikuwa hoi hospitalini kutokana na hii homa mpya iitwayo Dengue, kwa sasa sina nguvu tu mwilini, lakini naendelea vyema," alisema.
Kuugua kwa Pentagone kumefanya idadi ya wasanii waliokumbwa na homa hiyo kufikia watatu kwa sasa baada ya awali mwanadada Rehema Chalamila 'Ray C' kuthibitishwa kuugua ugonjwa huo na kulazwa hospitali sawa na ilivyomkuta pia, Mukhsen Awadh 'Dk Cheni na muigizaji mkongwe ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa Times Fm, Susan Lewis 'Natasha'.
Ugonjwa huo unaelezwa kuambukiwa na mbu aina ya Aedes unafanana kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Malaria kwa dalili zake na watu wanaohisi kuupata wanahimizwa kuwahi hospitalini kupata matibabu.

Bao la TP Mazembe dhidi ya As Vita laua mashabiki 15 DR Congo


BAO pekee la dakika ya 35 lililofungwa na Gladson Awako wa TP Mazembe, klabu wanayochezea Watanzania  wawili Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu dhidi ya AS Vita katika mchezo wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limesababisha vifo vya watu 15.
Ushindi huo kwenye Uwanja wa Tata Raphael, unaifanya TP Mazembe iendeleze ubabe wake kwa Vita baada kuifumua 4-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza mjini Lubumbashi.
Timu hizo mbili zenye upinzani mkali pia zimepangwa kundi moja la Ligi ya Mabingwa Afrika na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou amehuzunishwa na vifo vya mashabiki zaidi ya 15 katika mechi hiyo huku 20 wakijeruhiwa baada ya Shirikisho la Soka DRC (Fecofa) kuipa CAF ripoti kamili ya kilichotokea.
Katika taarifa yake jana, Hayatou alisema bodi hiyo ya soka Afrika imesikitishwa na tukio hilo na kwamba wataweka mikakati ya kudhibiti vurugu viwanjani wakati wa mechi.
Hayatou raia wa Mcameroon ametoa pole kwa niaba ya CAF kwa familia za waliofiwa kutokana na vurugu hizo, Fecofa na kusema anatumai walioripotiwa kujeruhiwa wanapatiwa matibabu.
Juu ya hatua ambazo CAF itachukua kupambana na vurugu viwanjani, Hayatou alisema jana kuwa: "Aina yoyote ya vurugu haina nafasi kwenye uwanja wa soka. Lazima kuwe na sheria kali na ninawaagiza Fecofa na mamlaka husika DRC kufanya uchunguzi wa kina juu ya tatizo hili na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa ili isijirudie aina yoyote ya tukio kama hili."
Vurugu hizo zilianza baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo, Mazembe yenye washambuliaji wawili Watanzania, Samatta na Ulimwengu ikishinda 1-0 na Polisi walijaribu kutuliza vurugu hizo kwa kulipua mabomu ya machozi.
Gavana wa Kinshasa, Andre Kimbuta mara moja aliagiza uchunguzi ufanyike juu ya tukio hilo.
Vurugu hizo zinatokea wakati Mazembe na AS Vita zimepangwa kundi moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika na zitamenyana tena Mei 25, mwaka huu mjini Lubumbashi katika michuano hiyo ya Afrika. Mazembe iliifunga 4-1 Vita katika mchezo wa kwanza wa ligi ya DRC msimu huu Lubumbashi na inahofiwa mashabiki wa timu ya kina Samatta watalipa kisasi kwa mashabiki wa Vita Mei 25.
Rais wa Fifa, Sepp Blatter alieleza kupitia mtandao wa Twitter:  "Anasubiri habari zaidi kutoka DR Congo baada ya kuripotiwa tukio hilo. Huzuni yangu ni kwa wale waliopenda sana soka, ambao hawatarudi."