STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 13, 2014

Bao la TP Mazembe dhidi ya As Vita laua mashabiki 15 DR Congo


BAO pekee la dakika ya 35 lililofungwa na Gladson Awako wa TP Mazembe, klabu wanayochezea Watanzania  wawili Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu dhidi ya AS Vita katika mchezo wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limesababisha vifo vya watu 15.
Ushindi huo kwenye Uwanja wa Tata Raphael, unaifanya TP Mazembe iendeleze ubabe wake kwa Vita baada kuifumua 4-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza mjini Lubumbashi.
Timu hizo mbili zenye upinzani mkali pia zimepangwa kundi moja la Ligi ya Mabingwa Afrika na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou amehuzunishwa na vifo vya mashabiki zaidi ya 15 katika mechi hiyo huku 20 wakijeruhiwa baada ya Shirikisho la Soka DRC (Fecofa) kuipa CAF ripoti kamili ya kilichotokea.
Katika taarifa yake jana, Hayatou alisema bodi hiyo ya soka Afrika imesikitishwa na tukio hilo na kwamba wataweka mikakati ya kudhibiti vurugu viwanjani wakati wa mechi.
Hayatou raia wa Mcameroon ametoa pole kwa niaba ya CAF kwa familia za waliofiwa kutokana na vurugu hizo, Fecofa na kusema anatumai walioripotiwa kujeruhiwa wanapatiwa matibabu.
Juu ya hatua ambazo CAF itachukua kupambana na vurugu viwanjani, Hayatou alisema jana kuwa: "Aina yoyote ya vurugu haina nafasi kwenye uwanja wa soka. Lazima kuwe na sheria kali na ninawaagiza Fecofa na mamlaka husika DRC kufanya uchunguzi wa kina juu ya tatizo hili na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa ili isijirudie aina yoyote ya tukio kama hili."
Vurugu hizo zilianza baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo, Mazembe yenye washambuliaji wawili Watanzania, Samatta na Ulimwengu ikishinda 1-0 na Polisi walijaribu kutuliza vurugu hizo kwa kulipua mabomu ya machozi.
Gavana wa Kinshasa, Andre Kimbuta mara moja aliagiza uchunguzi ufanyike juu ya tukio hilo.
Vurugu hizo zinatokea wakati Mazembe na AS Vita zimepangwa kundi moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika na zitamenyana tena Mei 25, mwaka huu mjini Lubumbashi katika michuano hiyo ya Afrika. Mazembe iliifunga 4-1 Vita katika mchezo wa kwanza wa ligi ya DRC msimu huu Lubumbashi na inahofiwa mashabiki wa timu ya kina Samatta watalipa kisasi kwa mashabiki wa Vita Mei 25.
Rais wa Fifa, Sepp Blatter alieleza kupitia mtandao wa Twitter:  "Anasubiri habari zaidi kutoka DR Congo baada ya kuripotiwa tukio hilo. Huzuni yangu ni kwa wale waliopenda sana soka, ambao hawatarudi."

No comments:

Post a Comment