STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 9, 2015

KICHOMI NI JASHO NA DAMU-BETHA SHAIBU

MSANII na mtayarishaji chipukizi wa filamu nchini, Betha Shaibu amesema 'limemtoka' jasho na damu katika kufanikisha kuitengeneza filamu yake ya kwanza iitwayo 'Kichomi' ambayo inatarajiwa kuachiwa mwezi huu.
Akizungumza na MICHARAZO, Betha alisema filamu hiyo iliyoshirikisha mastaa kadhaa nchini ni moja ya filamu ya kimapenzi yenye mafunzo makubwa kwa jamii na hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Betha alisema anaomba Mungu filamu hiyo iingie sokoni ili mashabiki waone tofauti iliyopo kati ya kazi hiyo na nyingine kwa namna msuko wa filamu hiyo ulivyo.
"Kwa kweli sijapumua mpaka kazi iingie sokoni, najua mwanzo ni mgumu lakini nimekubali kupambana ili kusimama kwa kutambua nina kipaji kikubwa cha utunzi na uigizaji," alisema Betha.
Ndani ya filamu hiyo ya 'Kichomi', Betha ameshirikiana na wakali kama Hemed Suleiman, Sabrina Omari, Mzee wa Majanga na wengine na imetengenezwa kupitia kampuni ya Red Leaf Entertainment.

Safari ya Inspekta Haroun Japan sasa April

MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rashid Kahena 'Inspekta Haroun' a.k.a Babu anatarajiwa kwenda nchini Japan baadaye mwaka huu baada ya awali kushindwa kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka jana.
Inspekta Haroun aliliambia gazeti hili kuwa, ziara yake kwenda kutengeneza kazi mpya chini ya kampuni ya Hyper Production chini ya Deejay Kay Dee Beatz ilipangwa kufanyika Desemba mwaka jana, lakini ilishindikana baada ya kukosa visa.
Alisema hivyo wamekubaliana na 'mabosi' wake safari hiyo sasa iwe mwezi April akimini kuwa kila kitu kitaenda sawa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi chini ya lebo hiyo.
"Safari yangu ya kwenda Japan kuingia mkataba wa kufanya kazi chini ya lebo ya Hyper Production imekwama kwa kukosa visa na sasa itafanyika Aprili kwa kuamini kila kitu kitakuwa kimekamilika, ingawa tayari kampuni hiyo imetengeneza video za nyimbo zangu mbili ambazo nitaziachia hivi karibuni mashabiki wapate burudani," alisema.
Babu alisema video hizo ni za nyimbo za 'Mungu Ndiye Anayepanga alioimba na Sir Juma Nature na ule wa 'Bado Hujachelewa' alioimba pekee yake ambapo kampuni hiyo ilifanya kazi ya kuzichanganya picha na kuongeza vionjo baada ya kuvutiwa na nyimbo hizo.

K-One Suma Lee wana ngoma mpya kwa Baucha

BAADA ya kutamba na nyimbo za 'Yule' aliyoimba na Maunda Zorro na 'Jimama Zamiela', msanii K-One anajiandaa kufyatua 'ngoma' mpya aliyomshirikisha mkali wa zamani wa Parklane, Suma Lee.
Akizungumza na MICHARAZO, Mkurugenzi wa Baucha Records inayommilikia msanii K-One, Ali Baucha alisema wimbo huo upo hatua ya mwisho kabla ya kuachia rasmi mwezi ujao ukiwa umetengenezwa katika studio zake.
Baucha alisema wimbo huo ambao bado haujapewa jina ni kati ya kazi tatu mpya za studio hizo zinazotarajiwa kuachiwa karibuni, wimbo mwingine ukiwa ni wa Fizzo aliyemshirikisha Mshindi wa BSS 2013, Walter Chilambo.
"Baucha Records kwa sasa tupo katika maandalizi ya kutoa kazi mpya baada ya kuhamisha studio mahali tulipokuwapo awali pale Magomeni Mapipa, na kati ya kazi hizo moja ni wa K-One akiimba na Suma Lee na mdogo wangu anayeishi Ujerumani pamoja na ule wa Fizzo anaoimba na Walter Chilambo," alisema Baucha mmoja wa watayarishaji mahiri wa muziki wakongwe nchini.

Michuano ya Taifa ya Soka kwa wanawake kuanza kesho

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhcLvLEgI1HLK7c-HmKa5lTL3-7Sz3hW-nNnR1ogOhAVkhVKc6ERg0HahgcfqOkBf4_82s6MMwonfDQO7d_g2raIBEMLzyQP0shox0pazxJwKSHQDgzmt-H2s4PIlBvwSC8RTQiBheP3ss/s1600/IMG_8106.JPGMICHUANO ya soka ya Kombe la taifa kwa timu za Wanawake inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi ambapo mechi ya kwanza za raundi ya kwanza zitachezwa kesho kwenye miji 11 tofauti nchini.
Katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin, Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera (Uwanja wa Geita), Tabora itacheza na Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simiyu na Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha na Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro na Tanga (Uwanja wa Ushirika).
Mechi nyingine ni Lindi itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma na Njombe (Uwanja wa Majimaji), Mbeya na Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi na Rukwa (Uwanja wa Katavi), Dodoma na Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.
Timu hizo zitarudiana Januari 13 mwaka huu, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwaka huu.
Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Wazee wa 4 waaga Mapinduzi Cup, wapigwa kidude na JKU

* Nusu fainali ni Simba v POlisi, Mtibwa v JKU

BAADA ya kutamba kwa kugawa 'dozi' nono ya mabao manne manne kwa wapinzani wao katika mechi ya makundi kabla ya kupunguzwa na Shaba kwa kuishinda bao 1-0, Yanga imeaga michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kufungwa bao 1-0 na JKU.
Yanga waliosheheni wachezaji 'ghali' na mastaa wanaotamba Afrika Mashariki walishindwa kufurukuta kwa maafande hao wa Jeshi la Kujenga Uchumi visiwani Zanzibar kunakofanyikia michuano hiyo itakayofikia tamati Jumanne.
Bao lililowazima Yanga na kuhitimisha tambo zake liliwekwa kimiani na Amour Omary 'Janja' aliyemfikia Andrey Coutinho aliye na mabao matatu katika orodha ya wafungaji.
Janja alifunga bao hilo lililokuwa la tatu kwake katika dakika ya 72 na kuwaacha vijana wa Hans van der Pluijm wakijilaumu kutokana na kukosa mabao mengi ya wazi katika muda wote wa pambano hilo lililochezwa uwanja wa Amaan.
Ushindi huo kwa JKU imeifanya timu hiyo kutinga Nusu Fainali na kupata nafasi ya kuvaana na Mtibwa Sugar waliowang'oa Azam kwa mikwaju ya penati baada ya kumaliza pambano lao kwa kufungana bao 1-1, Azam wakilazimika kusawazisha dakika za jioni kupitia Kipre Tchetche baada ya Shomar Ally kutangulia kufunga.
JKU imekuwa timu ya tatu kutoka kundi C ambazo zote zimepenya robo fainali na kutinga pia Nusu Fainali.
Nyingine ni Simba ambayo itaumana kesho na Polisi Zanzibar waliowavua taji la michuano hiyo KCCA ya Uganda kwa mikwaju ya penati baada ya kutoka suluhu ndani ya muda wa kawaida na Mtibwa Sugar ambao ni Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sabrina Omar, PHD 'wauza sura' katika KICHOMI

SALOME
PHD
WAIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Sabrina Omar 'Salome' na Hemed Suleiman 'PHD' wanatarajiwa kuonekana kwenye filamu mpya iitwayo 'Kichomi' ambayo imewashirikisha wakali wengine.
Mtayarishaji wa filamu hiyo, Betha Shaibu aliiambia MICHARAZO jana kuwa, filamu hiyo inayotarajiwa kuachiwa sokoni hivi karibuni, ni kazi yake ya kwanza kupitia kampuni ya Red Leaf Entertainment na kuongozwa na Joseph Jembe na Daudi.
Betha alisema filamu hiyo ya kijamii imewashirikisha nyota wakali kadhaa wenye majina nchini akiwamo Salome, Hemed Suleiman 'PHD', Raheem David 'Kibeberu' na Mzee wa Majanga.
"Ni filamu yangu ya kwanza ambayo nimeigiza kwa jina la Jameth nikishirikiana na wakali kama PHD, Sabrina Omar, Kibeberu na Mzee wa Majanga na inatarajiwa kuwa sokoni ndani ya mwezi huu," alisema Betha.
Betha alisema washiriki wa filamu hiyo wameitendea haki na kuwaomba mashabiki wasikose kuiona mara itakatoka hadharani kwani ina mafunzo makubwa kwa jamii mbali na kuburudisha.

Kitabu cha Steven Kanumba kuzinduliwa leo Landmark Hotel

Steven Kanumba enzi za uhai wake
Mwanamuziki Christian Bella na Mama yake Kanumba, Flora Mtogoha wakikinadi kitabu cha maisha ya marehemu Steven Kanumba kitakachozinduliwa leo pale Ubungo
Mtunzi wa kitabu hicho akikitambuliosha kwa wanahabari huku mratibu wa onyesho la uzinduzi, Frank akifuatilia kwa makini
MWANDISHI wa kitabu kinachohusu maisha ya nyota wa zamani wa filamu, Steven Kanumba kinachoitwa 'The Great Fallen Tree', Emmanuel Zirimwabagabo, amesema mauzo ya kitabu hicho  yataingizwa kwenye mradi wa Kanumba Foundation.
Taasisi hiyo ya inahusika na masuala ya kusaidia wajane na yatima ilianzishwa ikiwa ni njia ya kumuenzi marehemu Kanumba aliyefariki takriban miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza na wanahabari, mtunzi huyo raia wa Canada mwenye asili ya DR Congo, alisema amefikia hatua hiyo baada ya kuongea na Mama Kanumba kuhusu ndoto za marehemu Kanumba aliyekuwa akipenda kuwasaidia yatima na alipanga kuwa na taasisi ya kusaidia wajane, lakini alifariki kabla ya kukamilisha ndoto zake.
“Mimi nilikuwa mpenzi wa kazi za Steven Kanumba baada ya kufariki niliumia sana, lakini nikafikiria ni jambo gani ambalo naweza kulifanya ili Kanumba aendelee kuishi japo hatupo naye kimwili lakini kiroho tupo naye,” alisema
“Nilifikiria kuandika kitabu kama sehemu ya heshima yangu kwake shujaa huyu kwetu sisi watu tunaopenda kazi zake, kwani Kanumba kanisaidia kujua kuongea Kiswahili kupitia filamu zake, hivyo napenda kuwe na kitu cha kumkumbuka," alisema Zirimwabagabo aliyetoa kitabu hicho kwa lugha mbili, cha Kiswahili na Kiingereza.
Naye Mama Kanumba, alitoa shukrani zake na akisema hakuwahi kufikiria kama mwanaye alikuwa na thamani kubwa kama hiyo hadi watu wa mataifa mengine kuja kuona kama ni mtu ambaye anatakiwa kuwekewa kumbukumbu kwa kuwekewa kitu au taasisi.
Kitabu hicho cha maisha ya kanumba kitazinduliwa kesho kwenye ukumbi wa Landmark Hotel, Ubungo ambako sherehe hizo zitaenda sambamba na uzinduzi wa taasisi hiyo ya Kanumba Foundation chini ya uratibu wa muigizaji Mohammed Mwikongi 'Frank' na burudani itakayosindikiza uzinduzi huo itatolewa na muimbaji Christian Bella.

2014 ni Yaya Toure tena, aweke rekodi akiifikia ile ya Samuel Eto'o

Yaya  Toure aliyenyakua tuzo ya Mwanasoka Bora akiweka rekodi ya aina yake Afrika
Samuel Eto'o aliyekuwa akishikilia rekodi ilivyofikiwa na Toure
KIUNGO wa kimataifa wa Ivory Coast anayeichezea klabu ya Manchester City, Yaya Toure ameibuka tena kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mara ya nne na kufikia rekodi ya Samuel Eto'o wa Cameroon.
Toure alishinda tuzo hiyo ikiwa ni rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza kutwaa mara nne mfululizo katika hafila iliyofanyika usiku wa kuamkia leo mjini Lagos Nigeria.
Toure, 31, aliibuka kidedea kwa kupata pointi nyingi mbele ya mshambuliaji wa Borussia Dortimund raia wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang na kipa wa Nigeria Vincent Enyeama.
Mchezaji huyo aliyeipa City taji la Ligi Kuu msimu uliopita na kuipeleka Tembo ya Ivory Coast kwenye Fainali za Afrika zitakazoanza wiki ijayo, alishatwaa tuzo miaka mitatu iliyopita 2011, 2012 na 2013.

Ni Eto'o pekee aliyekuwa na rekodi ya kutwaa tuzo hiyo mara nne baada ya kufanya hivyo mwaka 2003, 2004, 2005 na 2010.
Katika tuzo nyingine Mwanasoka Bora anayecheza barani Afrika imeenda kwa Firmin Mubele Ndombe (DR Congo), huku Mwanasoka Bora wa Kike tuzo akiwa ni Asisat Oshoala wa Nigeria ambaye pia alinyakua tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike anayechipukia.
Mwanasoka Chipukizi kwa wanaume ilienda kwa Yacine Brahimi (Algeria) wakati tuzo ya Kocha Bora ni; Kheireddine Madoui wa ES Setif.
Timu Bora kwa 2014 ni Algeria kwa wanaume na Nigeria kwa wanawake ilihali Klabu Bora ni ES Setif (Algeria) na Kiongozi Bora ni Rais wa TT Mazembe Moise Katumbi Chapwe.
Orodha ya Mwanasoka Bora Afrika tangu 1995:
1995- George Weah (Liberia)
1996- Nwankwo Kanu(Nigeria)
 1997-    Victor Ikpeba (Nigeria)
1998-    Mustapha Hadji (Morocco)
1999-     Nwankwo Kanu (Nigeria)
2000-    Patrick Mboma (Cameroon)
2001-     El Hadji Diouf (Senegal)
2002-     El Hadji Diouf (Senegal)
2003-     Samuel Eto'o (Cameroon)
2004-    Samuel Eto'o (Cameroon)
2005-     Samuel Eto'o (Cameroon)
2006-    Didier Drogba (Ivory Coast)
2007-     Frederic Kanoute (Mali)
2008-    Emmanuel Adebayor (Togo)
2009- Didier Drogba (Ivory Coast)
2010-     Samuel Eto'o (Cameroon)
2011-     Yaya Toure     (Ivory Coast)
2012-     Yaya Toure (Ivory Coast)
2013-     Yaya Toure (Ivory Coast)
2014-     Yaya Toure (Ivory Coast)