STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 6, 2012

Oswald, Njiku, Palasa kuwasindikiza akina Cheka

MABONDIA wanaotamba kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Maneno Oswald, Chaurembo Palasa na Deo Njiku wa Moogoro wanatarajiwa kupanda ulingoni kuzichapa kusindikiza pambano la Francis Cheka dhidi ya Karama Nyalawila.
Cheka na Nyalawila wanatarajiwa kupigana Januari 28 kwenye pambano lisilo la ubingwa litakalofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro ambapo mratibu wa pambano hilo, Philemon Kyando 'Don King' ametangaza michezo ya utangulizi.
Kyando, ambaye ni Mkurugenzi wa Don King Kyando Promotion, alisema kabla ya Cheka na Nyalawila kupanda ulingoni kupigana, mabondia 10 tofauti watawasindikiza ambapo Chaurembo Palasa anatarajiwa kuzichapa na Deo Njiku.
Mabondia wengine watakaopigana katika pambano hilo la akina Cheka litakalokuwa na raundi 10 uzani wa Super Middle ni mkongwe Maneno Oswald aliyeambulia sare hivi karibuni mbele ya mkongwe mwenzake, Rashid Matumla atakayepigana na Hamis Ally wa Morogoro.
"Mapambano mengine ya utangulizi yatawahusisha, JUma Idd wa Dar dhidi ya JUma Afande wa Morogoro, pia kutakuwa na pambano jingine litakalowakutanisha mabondia wa kike watakaoonyeshana kazi siku hiyo," alisema Kyando.
Promota huyo aliyekuwa kimya kwa muda mrefu, alisema michezo hiyo ya Januari 28 itakuwa maalum kwa uzinduzi wa kampuni yake sambamba na kumpongeza Mbunge wake wa Jimbo la Morogoro, Aziz Abood kwa kusaidia maendeleo ya jimbo hilo.
"Unajua mie natokea eneo la Kihonda na nimekuwa nikivutiwa na kasi anayofanya mbunge huyo katika kuleta maendeleo ndio maana nimeandaa pambano hili la Cheka na Nyalawila lifanyike Morogoro kama kuunga mkono juhudi zake," alisema Kyando.
Kyando, aliyetamba miaka ya 1980 na 2000 kabla ya kuzimika, alisema ujio wake mpya utaenda sambamba na kuwainua mabondia chipukizi waliopo kila kona ya nchi badala ya kufuata mkumbo wa mapromota wengine kung'ang'ania mabondia wa mijini tu.
Cheka anayefahamika kama SMG na Nyalawila maarufu kama 'Captain' watapigana likiwa pambano lao la pili kwani walishawahi kukutana na kushindwa kutambiana kwa kutoa sare, ingawa kila mmoja kwa sasa anashikilia mataji makubwa duniani.
Nyalawila ni bingwa wa dunia wa WBF, huku mpinzani wake akishikia mataji ya UBO, ICB na Kamisheni ya Ngumi ya WBC.

Mwisho

BFT yateua 25 kushiriki kozi ya kimataifa ya ukocha

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania, BFT, limetangaza majina ya makocha 25 walioteuliwa kushiriki kozi ya kimataifa ya mchezoitakayofanyika kati ya Januari 16-24.
Awali kozi hiyo ilipangwa kufanyika Novemba mwaka jana ikishirikisha makocha 30, lakini ilikwama kutokana na mkufunzi wa kimataifa toka Algeria aliyekuwa aiendeshe kushindwa kuwasili na kufanya BFT kuwapunguza washiriki watano safari hii.
Taarifa ya BFT inasema imewapunguza makocha hao watano kutokana na agizo la TOC linalosimamia kozi hiyo kufuatia hasara iliyopata awali wakati wa maandalizi ya awali ambayo hata hivyo haikufanyika.
Katibu wa BFT, Makore Mashaga, alisema idadi hiyo ya makocha hata hivyo inaweza kupunguzwa kulingana na bajeti iliyopo ambayo itawagharamia washiriki mwanzo mwisho katika kozi hiyo.
Mashaga aliwataja washiriki hao kuwa ni Rajabu Mhamila 'Super D', Anord Ngumbi,
Moses Lema, Anthon Mwang'onda na Edward Emmanuel kutoka Dar es Salaam, Yahya Mvuvi (Tabora), Joseph Mayanga na Zakaria Mwaseba wote wa Morogoro.
Wengine ni Omari Saady na Mussa Bakari (Mwanza), Ally Ndee (JKT-Mbeya), Emilio Moyo na Gaudence Uyaga (Pwani) Juma Lisso (Magereza-Kigoma), Lyinda Kalinga (Dodoma) na Abdallah Bakar (Tanga).
Washiriki wengine ni Mohammed Hashim (Polisi Dar es Salaam), Haji Abdallah, Said Omar na David Yombayomba (JWTZ), Mazimbo Ally, Rogated Damian na Fatuma Milanzi (JKT), Musa Maisori na Hamisi Shaaban (Magereza Dar es Salaam).
Katibu huyo alisema kozi hiyo itakayofanyika kwenye majengo ya Shule ya Sekondari Filbert Bayi, Kibaha-Pwani itaendeshwa na mkufunzi wa kimataifa Josef Diouf kutoka Shirikisho la Dunia la mchezo huo, AIBA atakayeshirikiana na Makamu wa Rais wa BFT, Michael Changarawe.

Mwisho

Bella awang'onga wasanii Bongo



RAIS wa bendi ya Akudo Impact, Christian Bella, amewataka wasanii wa Kitanzania kujenga mazoea ya kuwashirikisha wasanii wenye majina makubwa wa kimataifa na wanaoimba miondoko tofauti na yao kwa lengo la kuteka soko la kimataifa.
Pia, amesema bila bendi za Tanzania kubadilika na kuachana na kuiga kazi za wasanii wa nje hasa wakongo, ni vigumu kuweza kutamba katika soko la kimataifa kwa vile watu wanaowaiga tayari wameshajiwekea mizizi ya kutosha karibu kila kona ya dunia.
Bella, alisema mtindo anaoutumia AY kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa kigeni unapanua wigo wa kazi za msanii huyo kufahamika kimataifa na kumtangaza vema.
Alisema jambo hilo linapaswa kuigwa na wengine, ambao wamezoea kufanya kazi na wasanii wenzao wa nyumbani au wanaoimba miondoko inayofanana.
"Unaona nimemshirikisha Isha Mashauzi katika kazi yangu 'Kilio cha Maskini' kwa lengo la kuteka mashabiki wa taarab, ila kwa kujitangaza kimataifa, lazima tuwashirikishe wasanii wa kigeni wenye majina makubwa tujitangaze," alisema.
Alisema wasanii wa Bongo wajiulize inakuwaje, Fally Ipupa aimbe na nyota wa Nigeria na miondoko yao haifanani, kisha wamwangalia AY na jitihada zake kisha wafuate nyayo hizo kwani zitawatangaza kimataifa tofauti na sasa.
Aliongeza, bendi za muziki wa dansi nchini ziache tabia ya kuiga kazi za wasanii wa nje hasa wakongo badala yake wabuni kazi zao wenyewe ili waweze kuteka soko la kimataifa.
Bella alisema bendi za Kibongo haziwezi kutamba soko la kimataifa kwa kupiga kama Koffi au JB Mpiana wakati kazi za wasanii hao zinatambulika karibu kila kona ya dunia.

Mwisho

Hassanal ajitosa Bongo Movie




MBUNIFU maarufu wa mitindo na mavazi nchini, Mustafa Hassanali, amejitosa kwenye fani ya uigizaji wa filamu za Kibongo baada ya kushirikishwa ndani ya filamu mpya iitwayo 'Glamour' inayotarajiwa kuachiwa hivi karibuni.
Hassanal amecheza filamu hiyo inayohusiana na masuala ya mapenzi na kijamii, pamoja na wakali wa fani hiyo kama Tecla Mjata.
Mbali na Mjata wengine waliopo ndani ya kazi hiyo ambayo ni miongoni mwa kazi mpya zinazotarajiwa kufungulia mwaka mpya wa 2012 kwa filamu za Kibongo ni' Eva Isaac, Edward Chogula, Amitabh Aurora na wengineo.
Wasambazaji wa filamu za Kibongo, wametoa taarifa kwamba tofauti na watu wanavyomchukulia Hassanal kwamba ni mkali wa ubunifu wa mavazi na mitindo, katika filamu hiyo ya Glamour ameonyesha uwezo wa hali juu kuthibitisha kuwa ana vipaji vingi.
"Huwezi amini kama aliyecheza ndani ya filamu hiyo ni Hassanal aliyezoeleka kwenye masuala ya ubunifu wa mitindo na mavazi, ni kazi inayotarajiwa kuachiwa hivi karibuni na kampuni yetu kwa ajili ya kuunza mwaka mpya wa 2012," alisema taarifa hizo inasomeka hivyo.
Mbali na filamu hiyo nyingine zinazotarajiwa kuachiwa mwezi huu ni 'My Son', 'I Hate My Birthday', 'DNA' na nyinginezo.

Afande Sele arudi na roho yake



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Seleman Msindi 'Afande Sele', amefyatua wimbo mpya uitwao NItarudi na Roho Yangu wakati akijiandaa kuiachia mtaani albamu yake ya tano.
Akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu toka mjini Morogoro, Afande Sele, alisema kibao hicho kipya amefyatua kwa kushirikiana na Abbas Hamis '20 Percent' ikiwa ni miezi kadhaa tangu atangulize kibao cha 'Maskini Hafulii'
Afande, alisema kibao hicho kama ilivyo nyimbo zake zote kipo katika miondoko ya hip hop na ni utambulisho wa albamu yake mpya ambayo alipanga kuitoa mwaka jana, lakini alisita na kuamua kuitoa mwaka huu.
"Wakati najiandaa kuitoa hadharani albamu yangu ya tano tangu nijitose kwenye fani hii iitwayo 'Kingdom' ambayo itakuwa na jumla ya nyimbo 14 badala ya 10 nilizopanga kutoa awali," alisema.
Alizitaja nyimbo za albamu hiyo iliyowashirikisha wasanii mbalimbali nyota nchini ni; 'Kingdom', 'Maskini Hafulii', 'Soma Ule', 'Machozi ya Suzy', 'Nguvu' na Akili', 'Dume' na 'Nikupendeje'.
Albamu nne za mwanzo za mkali huyo ambaye pia ni Mfalme wa Rhymes ni 'Mkuki Moyoni' ya mwaka 2001, 'Darubini Kali' (2004), 'Nafsi ya Mtu' (2006) na 'Karata Dume' ya mwaka 2008.

Mwisho

Margareth Somy afyatua mpya za Injili



BAADA ya kimya kirefu tangu alipoachia albamu yake iliyofanya vema sokoni ya 'Tenda Wema', muimbaji wa muziki wa Injili ambaye pia ni muigizaji wa filamu, Margareth Somy, ameanza maandalizi ya kupakua albamu yake ya pili.
Akizungumza na MICHARAZO, Somy, alisema albamu hiyo ya pili mpya itafahamika kwa jina la Yesu Ndiye Maarufu na itakuwa na jumla ya nyimbo nane.
Somy alizitaja nyimbo ambazo zimeshaanza kurekodiwa kwa ajili ya albamu hiyo ni 'Yesu Ndiye Maarufu', 'Jerusalem', 'Nitainua Macho Yangu' na 'Yatima'.
"Nimeanza kurekodi nyimbo za albamu yangu mpya itakayokuwa ya pili, ambayo nimepanga kuitoa ndani ya mwaka huu," alisema Somy.
Somy alisema nyimbo nyingine za kujazia albamu hiyo ameshaziandikia mashairi yake ingawa hajazipa majina, hadi atakapozirekodi," alisema.
Muimbaji huyo, ambaye kitaaluma ni muuguzi akifanya kazi katika hospitali moja iliyopo Ilala-Bungoni, jijini Dar es Salaam, alisema anadhani kabla ya Juni albamu hiyo itakuwa sokoni, ingawa anatarajia kusambaza baadhi ya nyimbo ili zianze kusikika mapema.
Alisema wakati akianza kusambaza nyimbo hizo ataingia mzigoni kufyatua video zake ili mashabiki wake wapate uhondo kupitia kwenye vituo vya runinga.

Msondo kugawa zawadi Zenji




MASHABIKI wa bendi ya Msondo Ngoma wa visiwani Zanzibar wanatarajiwa kushindanishwa kuimba na kucheza nyimbo na miondoko ya bendi hiyo katika kuwania zawadi mbalimbali kama shamrashamra za kusherehekea miaka 48 ya Mapinduzi.
Zawadi hizo ikiwemo fulana, kanda za kaseti na cd za albamu za bendi hiyo kongwe, zitatolewa kwa mashabiki watakaomudu kuimba na kucheza vema nyimbo za Msondo katika onyesho maalum litakalofanyika wiki ijayo visiwani humo.
Shindano la mashabiki hao wa Msondo litafanyika kwenye ukumbi wa Gym Khan, wakati bendi hiyo itakapotumbuiza kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ambayo yatafikia kilele chake Alhamis ijayo.
Makamu Mwenyekiti wa Maseneta wa Msondo, ambaye ndiye mratibu wa onyesho hilo, Wazir Dewa, aliiambia MICHARAZO kwamba wameamua kuwaandalia mashabiki wao zawadi hizo kama njia ya kuwashukuru kwa ushirikiano wanaipa bendi yao.
Dewa alisema, pia wanawapelekea zawadi hizo mashabiki hao katika kuungana nao kusherehekea Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.
"Tumewaandalia zawadi mbalimbali mashabiki wetu wa Msondo watakashiriki kwenye onyesho letu ambapo tutawashindanisha kucheza na kuimba nyimbo za bendi hiyo na watakaofanya vema watatunukiwa fulani, cd na kanda za kaseti," alisema.
Aliongeza, kwamba licha ya kupambanishwa, pia mashabiki hao watapata fursa ya kupigiwa nyimbo za zamani zilizoifanya bendi hiyo kuwa 'Baba ya Muziki' nchini.
***

Kicheko Hawezi Kulala videoni


Picha:Kicheko


MCHEKESHAJI maarufu nchini anayetamba katika kipindi cha Ze Comedy Show, Rogers Richard 'Massawe Mtata' ameuweka wimbo wake mpya wa 'Kulala Siwezi' kwenye video huku akijiandaa kupakua albamu yake binafsi ya tatu itakayokuwa na nyimbo nane.
Akizungumza na MICHARAZO, msanii huyo ambaye hufahamika kama Kicheko, alisema video ya kibao hicho kilichoanza kurushwa hewani wiki hii, imerekodiwa na kampuni yake ya Kausha Production yenye makao yake eneo la Magomeni, Dar es Salaam.
Kicheko, alisema kwa sasa video hiyo inafanya uhariri kabla ya kuanza kusambazwa kwenye vituo vya runinga ili kuanza kurushwa hewani, wakati akiendelea kumalizia nyimbo nyingine za albamu yake mpya ya tatu aliyopanga kuitoa mwaka huu.
"Baada ya kusambaza kibao changu cha Kulala Siwezi, nimekamilisha kufyatua video yake ambayo inahaririwa kwa sasa, nadhani hadi wiki ijayo nitaanza kuisambaza ili irushwe hewani wakati nikiendelea kurekodi nyimbo nyingine," alisema.
Kicheko alisema albamu yake hiyo mpya itakuwa na nyimbo nane na atashirikiana na wasanii kadhaa nyota nchini, na itakuwa katika miondoko aliyoibuni iitwayo 'Bongo Tecno'.
Hiyo itakuwa ni albamu ya tatu kwa msanii huyo, aliyewahi kutamba na kundi la Kidedea lililorushwa michezo yake hewani kupitia kiyuo cha ITV baada ya awali kufyatua 'Say Ye' au 'Unanipenda Mimi' na 'Mirinda Nyeusi' iliyofahamika pia kama 'Kicheko.com'.
Kicheko alisema amepania ndani ya mwaka huu wa 2012 kuweza kufanya mambo matatu kwa mkupuo, kuchekesha, kufanya muziki na filamu kudhihirisha vipaji alivyojaliwa.
***

Idd Azan ajitosa kuisaidia Villa Squad




MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azan naye amejitosa kuiokoa timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Villa Squad ambayo ipo katika hali mbaya kiuchumi kwa lengo la kuona inafanya vema katika duru lijalo la ligi hiyo litakaloanza wiki mbili zijazo.
Azan, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka wilayani humo, KIFA na kile cha mkoa wa Dar es Salaam, DRFA, amejitolea kuigharamia timu hiyo posho za wachezaji wanaojifua ufukweni pamoja na kulipoa gym ya kuwajengea stamina.
Kaimu Katibu Mkuu wa Villa, Frank Mchaki alisema licha ya kwamba Mbunge huyo amekuwa akijitolea mara kwa mara kuipiga tafu timu yao, lakini safari hii ameonyesha dhamira yake ya kutaka kuona Villa haishuki daraja kwa kuigharamia mazoezi.
Mchaki alisema uongozi wao umefarijika na itikio la viongozi na wadau wa soka wilaya ya Kinondoni wanavyojitolea kuisaidia timu yao, akiahudi kwamba misaada wanayotoa haitapotea bure kwani watahakikisha timu hiyo haishuki daraja msimu huu.
"Bada ya DC wa Kinondoni, Jordan Rugimbana kuahidi kutuingiza kambini wiki ijayo, naye Mbunge wa Jimbo hilo, Idd Azan amejitolea kuigharamia timu yetu mazoezi ya kuwapa stamina wachezaji na tunawashukuru mno kwa misaada yao," alisema Mchaki.
Aliongeza kutoa wito kwa wadau wengine wajitokeze zaidi kuisaidia timu hiyo akidai kuporomoka kwa Villa Squad kutaifanya wilaya yao ya Kinondoni kukosa timu za Ligi Kuu kama ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita baada ya kutowekwa kwa Twiga Sports na kushuka daraja kwa Villa ilipopanda daraja msimu wa 2008-2009.
Mchaki alisema, kujitokeza kwa viongozi hao wakuu wa Kinondoni na wadau wengine kunawapa moyo wachezaji wao ambao walikuwa katika hali ngumu kutokana na Villa kukabiliwa na hali mbaya ya ukata.

Mwisho