STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, October 20, 2013

Juve yafa 4-2 kwa Fiorentina, Tevez atupia moja

Fiorentina striker Giuseppe Rossi
'Muuaji' Giuseppe Rossi akishangilia moja ya mabao yake matatu yaliyoiangamiza Juventus

KIBIBI cha Turin, Juventus leo imekiona cha mtema kuni baada ya kusasambuliwa mabao 4-2 ugenini na Fiorentina, licha ya kutangulia kujipatia mabao katika pambano la Ligi Kuu ya Italia Seria A.
Bao la penati la Muargentina, Carlos Tevez katika dakika ya kabla ya Paul Pogba kuongeza jingine dakika tatu baadaye yaliipa uongozi Juventus hadi wakati wa mapumziko.
Hata hivyo wenyeji waliingia kipindi cha pili na moto mkali na kurudisha bao moja ya jingine na kuongeza mengine mawili ya ushindi na kuibuka na ushindi huo mnono.
Giuseppe Rossi alipiga hat trick katika pambano hilo akianza kwa bao la penati dakika  66 kabla ya kuongeza jingine dakika 10 baadaye na kumalizia kazi dakika ya 81, ambapo kabla ya hapo Joaquim aliifunga bao la tatu dakika ya 78 na kupeleka msiba kwa Kibibi kizee.
Katika mechi nyingine genoa ikiwa nyumbani imeikwanyua Chievo mabao 2-1, Hellas Verona ilitakata kwao kwa kuilaza Parma mabao 3-2, Sampdoria iliizamisha Livorno mabao 2-1 na Sassuolo ikaizamisha Bolgna kwa magoli 2-1. Pambano jingine linalotarajiwa kucheza baadaye ni kati ya Torino na Inter Milan.



























Tottenham yainyoa Aston Villa kwao EPL

Andros Townsend (right) sends in the cross from which he scored for Tottenham at Aston Villa
Andros Townsend akiifungia Spurs bao la kwanza katika mechi ya leo

MABAO mawili ya kila kipindi yaliiwezesha Tottenham Hotspurs kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 Aston Villa ikiwa nyumbani kwao katika Ligi Kuu ya England.
Andros Townsend aliianza kuifungia Spurs bao dakika ya 31 na kudumu hadi kipindi cha kwanza kilipoisha na Saldado aliiongezea vijana wa Andre Villas Boaz bao dakika ya 69 na kuifanya timu hiyo ichupe kutoka nafasi ya saba hadi nafasi ya tano ikifikisha pointi 16.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa pambano moja baina ya Crystal Palace itakayoialika Fulham.


Simba yafanya maajabu Taifa, Ngassa aokoa nyumba zake


Mrisho Ngassa akishangilia bao lake leo uwanja wa Taifa

MRISHO Ngassa ameziokoa nyumba zake zisichomwe moto, lakini Yanga wameshindwa kulinda ushindi wao wa mabao matatu kama walivyoahidi baada ya Simba kuchomoa mabao na kulazimisha sare ya mabao 3-3.
Wapinzani hao wa jadi waligawana utawala wa vipindi, Yanga ikitawala kipindi cha kwanza na kujipatia mabao yake matatu kupitia kwa Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza 'Diego' kabla ya Simba kung'ara kipindi cha pili.
Mabao ya Betram Mombeki na mabeki wa kimataifa Joseph Owino na Gilbert Kazze yalizima ndoto za Yanga kuwanyuka watani zao kwa mara ya pili mfululizo.
Pambano hilo lililosisimua wengi lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam limeisaidia tu Yanga kupanda nafasi moja toka ya tano hadi ya nne ikiishusha Mtibwa Sugar, huku Simba ikishindwa kurejea kileleni.
Sare hiyo imeifanya Simba ifikishe pointi 19, moja dhidi ya vinara Azam na Mbeya City ambazo jana zilitakata kwa ushindi wa bao 1-0 kila mmoja dhidi ya timu za maafande wa JKT Ruvu na Oljoro JKT.
Kwa ujumla Yanga itawabidi wajilaumu kwa matokeo hayo kwani ilikuwa na kila dalili za kuweza kulipa kisasi cha mabao 5-0 iliyopewa na Simba Mei mwaka jana na hata kurudisha bao 6-0 iliyofungwa miaka 36 iliyopita.
Kipindi cha kwanza iliwashika Simba na kucheza watakavyo hasa baada ya kiungo cha Simba 'kufa', lakini walionyesha kuridhika huku Simba kutumia muda wa mapumziko kurekebishana makosa na kujirekebisha.
Kuingia dimbani kwa Said Ndemla na William Lucian 'Gallas' walifanya Simba ipate uhai na kutawala kipindi cha pili na kuwafunika Yanga ambao walionekana kuridhika na kudhani wameshashinda mchezo huo.
Baadhi ya mashabiki wa soka wameonyesha kushangazwa na matokeo ya leo Yanga wakilaumiana na wachezaji wao, huku Simba wakishangilia, japo makocha wote wametoa lawama kwa wachezaji kwa jinsi walivyocheza.
King Kibadeni ameweka wazi kwamba katika kikosi chao kuna tatizo kubwa japo hakupenda kuweka bayana, huku Ernie Brandts akidiriki 'kuwatusi' wachezaji wake kwa kuruhusu mabao matatu kurudi.

Lakini kubwa ni kitendo cha Ngassa kufunga bao na kutimiza ahadi yake aliyotoa kwamba kama asingefunga au kutoa pasi ya bao basi angechoma moto nyumba zake tano.

Al Ahly yaifuata Orlando Pirates fainali za mabingwa Afrika

Al Ahly-caf-cl-final-2013
Al Ahly
NATIONAL Al Ahly ya Misri imefanikiwa kupenya katika Fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuing'oa Cotton Sports ya Cameroon kwa mikwaju ya penati 7-6 katika pambano la nusu fainali ya pili iliyosiha muda mfupi uliopita.
Al Ahly ikiwa nyumbani imelazimishwa sare ya bao 1-1 na kufanya matokeo kuwa 2-2 na kulazimisha kupigiana penati ambapo wenyeji walipata 7 dhidi ya 6 za Wacameroon ambao Mohammewd Abo Trika alikosa mkwaju wake wakati akifungua hatua hiyo ya kupigianja penati.
Wenyeji walianza kupata bao dakika ya tatu tu kupitia kwa Abdallah El Said kabla ya wageni kusawaxzisha kipindi cha pili.

Monaco washindwa kurejea kileleni Ligue 1 yabanwa na Sochaux



LICHA ya kutangulia kupata mabao mawili ya haraka na kuongoza kwa muda mrefu, Monaco imeshindwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Ufaransa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Sochaux muda mfupi uliopita.
Monaco walienguliwa kileleni na PSG, ilianza makeke kwa kutangulia kufunga mabao mawili ya haraka kupitia kwa Ferreira Carrasco aliyefunga katika dakika ya 5 na 10 na kudumu hadi mapumziko.
Hata hivyo wenyeji walicharuka na kurejesha mabao hayo katika kipindi cha pili kupitia Cedric Bakambu dakika ya 57 na Joseph Lopy dakika ya 69 na kufanya matokeo yaishe kwa sare ya 2-2 na kuifanya Monaco kusalia nafasi ya pili ikiwa na pointi 22, mbili nyuma ya PSG.
Michezo mingine inaendelea muda huu katika viwanja kadhaa katika ligi hiyo ya Ufaransa

Lazio yanyukwa 2-1 na Atalanta, Milan yajitutumua Seria A

 
WAKATI Lazio muda mfupi uliopita imekubali kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Atalanta, AC Milan jana iliendelea kujikongoja baada ya kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 ikiwa nyumbani San Siro dhidi ya Udinese.
Bao pekee la Milan lilifungwa na Valter Birsa akimalizia kazi nzuri ya Mbrazil Robinho na kuifanya ifikishe poingti 11 na kuiengua Udinese katika nafasi ya nane na kuishika wenyewe na Udinese ikiporomoka hadi ya tisa.
Mchezo mwingine uliochezwa pia jana, Cagliari iliizima Catania kwa mabao 2-1 kwa mabao ya Ibarbo na Pinilla huku la kufutia machozi la Catania lilifungwa na Bergessio.
Hivi punde tu pambano kati ya Atalanta dhidi ya Lazio limemalizika kwa Lazio ikiwa ugenini kucherzea kichapo cha mabao 2-1.
Cigarini alitangulia kuifungia wenyeji bao katika kipindi cha kwanza bao lilidumu hadi mapumziko kabla ya Brayan Perea kuisawazishia Lazio dakika ya 53, lakini bao la kwenye dakika ya 84 lililofungwa na Dennis liliwapa ushindi wenyeji.
Jioni hii kuna mechi nyingine za ligi hiyo, Juventus ikialikwa na Fiorentina, Inter Milan kupepetana na Torino, huku Genoa kuonyeshana kazi na Chievo.
Mechi nyingine zitakuwa ni kati ya Hellas Verona itakayoialika Parma na Livorno ikiikaribisha Sampodoria.

Polisi Dar wanasa wamwagia tindikali

 
Kamanda Kova
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kumwagia watu kemikali aina ya tindikali.
Watuhumiwa hao ambao hata hivyo hawakutajwa majina, walikamatwa Oktoba 10, mwaka huu saa 2:00 asubuhi katika maeneo ya Lumumba, Kariakoo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamishna wa Polisi, Kamanda wa Kanda hiyo Suleiman Kova alisema, watuhumiwa hao walikiri kuhusika na tukio moja la kummwagia mfanyabiashara Ally Farhat (33) ambaye ni raia wa Lebanon, tukio ambalo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi.
"Taarifa za kiintelejensia zinaonesha mbinu zilizotumika katika tukio hilo zinawiana na tukio la kumwagiwa sumu aina ya tindikali mfanyabiashara aitwaye Said Mohamed maarufu kama Saad (42) ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Home Shopping Center (HSC), tukio ambalo lilifanyika maeneo ya Msasani katika jengo la Msasani City Mall mwezi Julai, mwaka huu," alisema Kamanda Kova.
Hata hivyo Kamanda Kova hakutaka kuwataja majina yao kutokana na kile alichosema bado wanaendelea kuwahoji hivyo wanahofia kupoteza ushahidi endapo majina hayo yatawekwa wazi.
Aidha alisema pia wanaendelea kuwahoji ili kubaini ushiriki wao katika tukio hilo, pia wanashirikiana na mikoa ya Zanzibar na mikoa mingine ili kubaini kama walishiriki katika matukio ya aina hiyo.
Aidha katika tukio jingine Kamanda Kova alisema, wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja Raia wa Somali aitwaye Jamal Ibrahim (42) akiwa na nyaraka za Serikali zikiwemo stakabadhi za malipo ya vibali vya makazi.
Kamanda Kova alitaja vitu alivyokutwa navyo mtu huyo kuwa ni pamoja na fomu namba 130 za maombi ya makazi, stakabadhi 21 za malipo ya vibali vya makazi, nakala nane za hati za kusafiria zenye picha za waombaji ambao ni raia wa Somalia na bahasha moja yenye picha mbalimbali za waombaji ambao ni raia wa Somalia.

Orlando Pirates yatangulia fainali za Mabingwa Afrika

ORLANDO Pirates ya Afrika Kusini imetangulia Fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya jana kupata sare ya bao 1-1 ikiwa ugenini dhidi ya Esperance ya Tunisia.
Pirates imefuzu fainali hizo kwa faida ya bao la ugenini kwani katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Afrika Kusini timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana na sare ya jana ina maanisha imefuzu kwa faida ya bao la ugenini linalohesabiwa kama mawili.
Wageni hawakuwa na kazi rahisi kwani walimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa 0-0 na kuingia kipindi cha pili kwa kishindo kwa kuwashtua wenyeji baada ya kupata bao la kuongoza lililofungwa katika dakika ya 51 na Rooi Petros Muhamutsa.
Hata hivyo wenyeji walichomoa bao hilo dakika chache baadaye kupuitia kwa Mohammed Iheb Msakni na matokeo kusalia hivyo hadi dakika ya mwisho na kuifanya Pirates kusubiri mshindi wa pambano la leo kati ya wenyeji Al Ahly ya Misri dhidi ya Cotton Sports ya Cameroon, ambazo katika mechi ya awali Wamisiri walilazimisha sare ugenini ya bao 1-1, hivyo kuwa na kazi ya kulazimisha suluhu ili kuungana na Wasauzi.

Mtangazaji aliyepigwa risasi aanza kufunguka juu ya mkasa wake, inatisha



Ufoo Saro akiwa na Rais Kikwete
MWANDISHI  wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye hivi karibuni alikumbwa na madhila ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na mzazi mwenzie, ameanza kufunguka kidogo kidogo na kueleza kwa kina jinsi tukio zima lilivyotokea.  Akizungumza kwa sauti ndogo na taratibu na gazeti hili kando ya kitanda alicholazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwanahabari huyo alieleza kushangazwa na ujasiri na nguvu za aina yake ambazo zilimwezesha kutambaa na kujiburuza hadi eneo la karibu ya barabara ili kuomba msaada wa kukimbizwa hospitali.

Ufoo ambaye alionyesha dhahiri kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazozingira tukio lake, alisema tayari alikuwa amewahakikishia polisi waliofika kumjulia hali hospitalini hapo kwamba alikuwa akisubiri afya yake iimarike kabla hajaeleza kwa kina kila anachokijua kuhusiana na tukio hilo.

“Alifika hapa kunijulia hali na kuangalia maendeleo yangu afande Msangi na nikasema nitakuwa tayari kueleza kila ninachokijua baada ya afya yangu kuimarika. Nasikitika kuna watu wanasema mambo wakifikia hatua ya kutaka kuonekana wananifahamu vizuri kuliko hata ninavyojifahamu mwenyewe,” alisema akionyesha kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazoripotiwa kuhusu sakata lake.


Ufoo ambaye alifikishwa hospitalini hapo Jumapili ya wiki iliyopita kutokana na kujeruhiwa kwa risasi na mwanaume aliyezaa naye mtoto mmoja alisema anamshukuru sana Mungu kwa uzima alionao sambamba na kuelezwa kupata faraja kubwa na kutiwa moyo na mwajiri wake, ndugu, jamaa na marafiki.


Ufoo Saro kushoto akiwajibika
Mwanahabari huyo ambaye bado yuko chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi mwilini mwake siku chache zilizopita, amelazwa katika chumba cha peke yake ambacho ingawa kina seti ya televisheni alisema alikuwa haruhusiwi kuiangalia kwa ushauri na maelekezo ya madaktari.

Huku akionekana wa chini ya uangalizi mwingine wa karibu na wa kudumu wa muuguzi ambaye muda wote wa mazungumzo haya alionekana kuwapo katika chumba hicho, Ufoo alisema alikuwa ana mapenzi makubwa kwa mzazi mwenzake huyo ambaye alipoteza maisha katika tukio hilo.

“Nilimpenda sana Antheri. Alikuwa kijana mtaratibu na mpole sana. Najua kile kilichotokea ni shetani tu na binafsi nilishasamehe alfajiri ile ile baada ya tukio lile,” alieleza Ufoo ambaye pia alimpoteza mama yake mzazi katika mkasa huo.

TUKIO ZIMA LILIVYOTOKEA

Ufoo ambaye mara kadhaa katika mazungumzo na gazeti hili alionekana kukunja uso akiashiria kupata maumivu, alionyesha eneo la chini ya bega katika mkono wake wa kulia lililofungwa na bandeji ambalo alisema ndipo alipopigwa risasi ya kwanza wakati akigeuka na kujaribu kuepuka mauti muda mfupi baada ya Antheri kumfyatulia risasi zilizomkuta mama yake mzazi.

Ufoo Saro alipokuwa akitolewa kwenye chumba cha upasuaji Muhimbili
Akijaribu kuvuta kumbukumbu ya tukio lilivyoanza, Ufoo alisema mzazi mwenzake huyo alifika nyumbani kwake akitokea Sudan alikokuwa akifanya kazi usiku huo huo wa tukio na akamtaka kwenda kwa mama yake (Ufoo) eneo la Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kabla ya kufika Kibamba na kwa sababu ambazo Ufoo hakuzieleza, alimkariri mzazi mwenzake huyo akisema alikuwa amefikia uamuzi wa kujiua yeye na mtoto wao.

“Hata sijui ni nini kilitokea. Wakati tukitoka nyumbani Antheri alianza kwa kuniambia kwamba alikuwa amepanga kujiua yeye na mtoto wetu,” alisema Ufoo kabla ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa na kuendelea na simulizi yake ya kusikitisha.

Akiwa na sura ya ujasiri, Ufoo anasema pamoja na kumwambia maneno hayo bado Mushi alimsisitiza kwamba waende kwa mama yake (Ufoo) baadae warudi kumchukua mtoto wao japo Ufoo hakusema walitaka kwenda wapi baada ya hapo.

Alisema walipofika nyumbani kwa mama yake walikwenda moja kwa moja sebuleni na wakiwa wamekaa kwenye makochi baada ya salamu za hapa na pale ghafla Mushi akasimama akamwambia mama yake Ufoo kwamba; “Mama nimeishafanya maamuzi”

Kwa mujibu wa maelezo ya Ufoo, baada ya Mushi kutamka maneno hayo ghafla akaingiza mkono nyuma ya suruali  alikokuwa ameweka bastola  yake na kisha akaichomoa.

Katika maelezo yake Ufoo alisema baada ya kuichomoa bastola hiyo mama yake naye alisimama na kwenda kujaribu kumpokonya, kitendo hicho kilimfanya amiminiwe risasi mfululizo.

Alisema kuona hivyo aliamua kukimbia kuelekea jikoni ambapo Mushi alimuona na kuanza kumiminia risasi ambayo moja ilimpata eneo la mkono wa kulia ambayo ilitokezea mbele na kuchana titi la kulia.

Kwa mujibu wa Ufoo jeraha hilo halikumfanya akate tamaa ya kunusuru maisha yake kwani alijaribu kukimbia ingawa Antheri alifyatua risasi nyingine kadhaa ambazo zilimpata juu kidogo ya mgongo na kutokea tumboni ambazo zilisababisha aanguke chini

Akiendelea kusimulia, anasema ingawa alikuwa akivuja damu nyingi, na huku akijiburuza ardhini, Ufoo alisema wakati akitambaa aligeuka nyuma na akamuona Antheri akijielekeza bastola eneo la kidevu na alipofyatua risasi alianguka chini.

“Nikiwa chini nilimuona Antheri akijipiga risasi kidevuni na akaanguka chini, sikujua kilichofuata baada ya hapo kwani niliendelea kujiburuza ili kuokoa maisha yangu,” alisema Ufoo

ALIVYOJIOKOA

“Nyumbani kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati nikikaribia kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku nikihisi tumbo langu limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye nilimuomba khanga ili nijifunge kuzuia damu zisitoke kwa wingi”.

Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke mmoja.

“Nilipoona kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada. Liliposimama nilimuona mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali ya Tumbi na kwamba akifika pale tu aniache mlangoni.

“Si rahisi kuamini, yule mama alikataa kunisaidia akisema alikuwa akiwahi sehemu kumchukua mzazi. Sina la kusema niliamua kumsamehe tu yule mama ingawa niliumia sana,” alisema Ufoo.

Alisema muda mfupi tu baadaye alitokea kijana aliyekuwa na pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda ambaye alimuomba msaada wa kumkimbiza hospitali ya Tumbi na akakubali.

“Yule kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia vizuri na niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda.

“Wakati huo nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa. Nikiwa kwenye pikipiki kuna wakati nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na kuanguka katika barabara na kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha. Lakini nilipata ujasiri na kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini.


Alisema anakumbuka wakati walipofika eneo la Kibaha ilipo mizani ya kupima uzito wa magari makubwa walikuta barabara ikiwa imejaa magari na yeye alimuomba dereva huyo wa bodaboda kupita hata nje ya barabara eneo la nyasi ili kumwahisha hospitalini jambo ambalo kijana yule alilifanya.

“Nilipofika eneo la mapokezi pale Tumbi nilimueleza muuguzi niliyemkuta kwamba nilikuwa nimejeruhiwa kwa risasi na nikamuomba asaidie kuokoa maisha yangu. Yule nesi alisita akitaka kwanza kupata kibali cha polisi (PF3) lakini nikaumuomba apigiwe simu, Kaimu Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk. Dattan ambaye tunafahamiana”

“Baada ya muda mfupi Dk. Dattan alifika na nikamweleza yaliyonipata na mara moja nikaanza kuhudumiwa kwa kuniwekea dripu, na nikamsikia akiwaeleza wauguzi kwamba isingekuwa busara kwa hali niliyonayo kama wangeanza kuchukua picha za X-ray kwani hatua hizo zingeweza kusababisha kupoteza maisha,” alieleza akikumbuka yaliyojiri hapo Tumbi.

Kwa mujibu wa Ufoo, akiwa bado ana fahamu alimsikia daktari aliyekuwa akimhudumia akiomba msaada wa gari la kubeba wagonjwa ili limchukue na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wito ambao ulijibiwa kwa maelezo kwamba lilikuwa halina mafuta.

Majibu hayo kwa mujibu wa Ufoo, yalisababisha daktari huyo aombe kuletewa gari la wagonjwa la wagonjwa maarufu (VIP) ambalo lililitwa na muda mfupi baadaye akapakizwa tayari kwa safari ya kukimbizwa Muhimbili.

Alisema wakati akikimbizwa Muhimbili anakumbuka namna alivyokuwa akipatwa na maumivu makali wakati wote gari ile ya wagonjwa ilipokuwa ikipanda matuta ya barabarani na kuna nyakati alikuwa akihisi kupoteza pumzi na kuishiwa nguvu. 


RAI

PSG yaua Ufaransa, Ibrahimovic akipiga bao la mwaka

Zlatan Ibrahimovic
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Ufaransa, PSG jana ilitoa kipigo cha mbwa mwizi wakati walipoisulubu Bastia kwa mabao 4-0 na kuiengua Monaco kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa muda.
Mabao mawili ya kipindi cha kwanza kutoka kwa mshambuliaji 'mtukutu' kutoka Sweden Zlatan Abrahimovic moja likiwa la aina yake akiunganisha mpira kwa tiktak ya kisigino na kumtungia kipa wa Bastia.
Magoili mengine yalifungwa katika kipindi cha pili na Edinson Cavani na kuifanya PSG ikwee kileleni ikiwa na pointi 24.
Cavani aliifungia PSG bao la nne kwa mkwaju wa penati na kuzima matumaini ya wageni Bastia ambayo imeporomoka hadi nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hiyo.

Hata hivyo huenda mabingwa hao wakaa kwa muda tu katika kiti hicho cha uongozi kabla ya kuwapisha Monaco ambayo muda mchache ujao itashuka dimba la ugenini kupepetana na Sochaux. Monaco ikishinda itarejea kileleni kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo maarufu kama Ligue 1, juzi Ijumaa Nice iliinyoa Olimpique Marseille kwa bao 1-0, Reims ikilala nyumbani kwa mabao 2-1 mbele ya Toulouse, huku jana Ajaccio ikiwa nyumbani ilikubali kipigo cha bao 1-0 toka kwa Nantes, Evian TG nayo ikilala 2-1 nyumbani dhidi ya Guingamp, nayo Lille ikiicharaza Montpellier bao 1-0 na Rennes na Valenciennes zikitoka sare ya mabao 2-2.
Leo mbali na Monaco kuvaana na Sochaux ugenini, Saint Etienne itaialika Lorient na Olimpicque Lyon itapepetana na wageni wao Bordeaux.

Juma Luizio amchimbwa mkwara Tambwe

Juma Luizio (kushoto) alipokuwa katika mazoezi ya Taifa Stars nchini Uganda hiviu karibuni
MSHAMBULIAJI chipukizi anayekuja juu nchini anayeichezea Mtibwa Sugar, Juma Luizio 'Ndanda' amemchimba mkwara mkali wa mabao wa Simba Amissi Tambwe akimwabia asahau kuhusu kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora msimu huu kwani hicho ni mali yake.
Luizio amesema anataka kuwa mfungaji bora msimu huu na kumuapia Tambwe kuwa atakula naye sahani moja.
Akizungumza na MICHARAZO hivi punde, Luizio ambaye jana alifunga mabao mawili wakati Mtibwa Sugar ikizamisha Mgambo JKT kwa mabao 4-1 na kufikisha jumla ya mabao saba moja nyuma ya Tambwe mwenye mabao nane, alisema lengo lake ni kufunga jumla ya mabao 17.
Chipukizi huyo aliyeanza kuitumikia timu ya wakubwa ya Mtibwa Sugar mwaka jana baada ya kupandishwa kutoka kikosi cha vijana, alisema amekuwa akitupia mipira nyavuni kwa lengo la kuwa Mfungaji Bora na kunyakua kiatu cha dhahabu.
Luizio alisema kila Mtibwa inapokuwa dimbani akili zake uziweka katika kutikisa nyavu na ndiyo maana amekuwa akifunga karibu kila mechi na kudai lengo ni kuwa mfungaji bora na siyo kuwasindikiza wenzake.
"Nafunga kwa sababu nataka kuwa mfungaji bora, nimepanga msimu huu nitupie jumla ya mabao 17 ambayo naamini yatanibebesha kiatu hicho, yakizidi haitakuwa neno," alisema.
Kuhusu kinara wa mabao kwa sasa Mrundi Amissi Tambwe wa Simba, Luizio alisema hana hofu naye kwani atamkamata na kumpita kutokana na kasi yake kuongezeka siku hadi siku.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuzichezea timu za Docks na Polisi Morogoro kabla ya kutua Mtibwa baada ya kung'ara kwenye michuano ya Taifa Cup na kuwa Mfungaji Bora namba mbili wa Uhai Cup mwaka uliopita, alisema ligi ni ngumu lakini atapigana kutimiza lengo.
Luizio alifichua siri ya mafanikio yake ya kufumania nyavu ni kuaminiwa na makocha na kuiga kwake mbinu za Zlatan Ibrahimovic anayemzimia.

Msiba! Mtangazaji Julius Nyaisanga 'Uncle J' hatunaye


Julius Nyaisanga enzi za uhai wake
TAARIFA zilizotufikia kutokana Morogoro zinasema kuwa, Mtangazajai nguli aliyewahi kutamba na vituo mbalimbali vya Radio kuanzia RTD, Radio One/ITV, Julius Nyaisangah 'Uncle J' amefariki dunia kutokana na kuugua kwa muda mrefu akiwa hospitali ya Mazimbu mjini humo.
Marehemu Nyaisanga anayekumbukwa kwa umahiri wake wa kutangaza taarifa habari na kuendesha vipindi vya Misakato na Klabu Raha Leo Show wakati yupo RTD na kisha kutisha na Mambo Mseto na Watoto Show akifahamika kama Babu wa Kimazichana akiwa Radio One, mpaka mauti yanamkumba alikuwa Mhairir Mtendaji wa Abood Media inayomiliki vituo vya Radio Abood na Abood Televisheni za mjini Morogoro.
Haijafahamika chanzo halisi cha mauti ya mtangazaji huyo, japo inaelezwa alikuwa akiigua kwa muda mrefu kisukari na Shinikizo la damu.
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia ya marehemu pamoja na wadau wote wa tasnia ya habari na kuwatakia subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema  Ameen