STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 13, 2017

Sanchez, Lukaku, Zlatan kuonyeshana kazi tuzo za PFA 2017

Lukaku

NYOTA wa Arsenal, Alexix Sanchez na yule wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic, watachuana kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Chama cha Soka cha Wachezaji wa Kulipwa nchini England, (PFA)
Mbali na wakali hao wanaochuana kwa kufumania nyavu katika Ligi Kuu ya England (EPL), pia watakula sahani moja na nyota wengine akiwamo kinara wa mabao wa sasa wa ligi hiyo, Romelu Lukaku wa Everton.
Orodha kamili ya wawania tuzo hiyo ipo hivi;

Mchezaji Bora
Eden Hazard - Chelsea Zlatan Ibrahimovic - Manchester United
Harry Kane - Tottenham Hotspur
N'Golo Kante - Chelsea
Romelu Lukaku - Everton
Alexis Sanchez - Arsenal

Wachezaji Chipukizi

Dele Alli - Tottenham Hotspur
Harry Kane - Tottenham Hotspur
Michael Keane - Burnley
Romelu Lukaku - Everton
Jordan Pickford - Sunderland
Leroy Sane - Manchester City

Mchezaji Bora Wanawake

Lucy Bronze - Manchester City
Karen Carney - Chelsea
Jane Ross - Manchester City
Jill Scott - Manchester City
Caroline Weir - Liverpool
Ellen White - Birmingham City

Mchezaji Bora Chipukizi wa KikeMillie Bright - Chelsea
Jess Carter - Birmingham City
Nikita Parris - Manchester City
Georgia Stanway - Manchester City
Keira Walsh - Manchester City
Caroline Weir - Liverpool

Viongozi DRFA warejea tena DRFA

Almas Kasongo aliyetetea kiti cha Uenyekiti wa DRFA
Na Rahim Junior
SEHEMU kubwa ya uongozi uliokuwepo kwenye Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), akiwamo Mwenyekiti Almas Kasongo na Katibu Mkuu wake, Msanifu Kondo wamerejea madarakani baada ya kushinda kwenye uchaguzi uliofanyika leo.
Uchaguzi huo uliofanyika Hoteli ya Lamada, Ilala ilishuhudia Kasongo akitetea kiti chake mbele ya Peter Mhinzi na Emmanuel Kazimoto kwa kupata kura 12 dhidi ya 9 za Mhinzi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Temeke (TEFA).
Kondo akitetea kiti cha ukatibu Mkuu  akimbwaga Frank Mchaki na Ramadhani Nassib, huku Mhazini aliyeongoza kiti hicho kwa muda mrefu, Ally Hassan akibwaga na Ally Masoud, huku Mtanganzaji na mchambuzi mahiri wa soka nchini, Shafii Dauda akitwaa Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
Wengine waliochaguliwa ni Salum Mwaking'inda aliyeshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti, huku Michale Lupiana akishinda Uwakilishi wa Klabu na Amour Amour na Chichi Mwidege wakitwaa Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho.

Yanga wawafuata Waalgeria kwa mafungu

MABINGWA wa Soka nchini, Yanga wameondoka nchini kwa mafungu kundi la kwanza likitimka jioni hii na jingine linatarajiwa kuondoka usiku huu ili kuwahi pambano lao la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria.
Kundi la kwanza lilitimka saa 10 likitumia ndege ya Shirika la Emirates Air likiwa na wakuu wa benchi la ufundi chini ya Kocha George Lwandamina sambamba na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na straika Amissi Tambwe ambao watapitia Dubai.
Mbali na Lwandamina wengine wa benchi la ufundi waliopo kwenye kundi hilo ni Wasaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila kutoka zambia na kocha wa makipa, Juma Pondamali.
Pia kundi hilo lina Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.
Kundi la pili litafuatia muda mchache ujao litaondoka kwa Ndege ya Shirika la Uturuki likiwa na wachezaji 13 na baadhi ya Maofisa wa timu hiyo likipitia Istanbul ambao ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul,  Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kevin Yondan.
Pia wamo viungo ni Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Emmanuel Martin wakati mshambuliaji ni Donald ngoma. 
Wawakilishi hao walishinda mchezo wa awali jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kwa bao 1-0 hivyo inahitaji sare ama kutofungwa zaidi ya mabao 2-1 ili kutinga makundi na kuwang;oa wenyeji wao MC Alger.
Yanga haijawahi kuitoa timu yoyote ya Afrika Kaskazini wala kupata ushindi ugenini katika nchi hizo, zaidi ya sare mbili ilizopata mwaka 1992 dhidi ya Ismailia ya Misri waliotoka nao 1-1 sawa na ile ya 2008 dhidi ya Al Alkhdar ya Libya.
Kama Yanga itapenya hapo itafuzu makundi ya michuano hiyo na kuweka rekodi kwa mara ya pili mfululizo kwani mwaka jana ilipenya, ikiwa chini ya Kocha Hans Pluijm ambaye alitimuliwa na kutua Singida United iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao.

Algeria yamteua Kocha Mkuu Mpya

CHAMA cha Soka cha Algeria, kimemteua Lucas Alcaraz kuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Mbweha wa Jangwani, ikiwa ni mara ya nne kufanya hivyo katika kipindi cha miezi 13 iliyopita.
Alcaraz raia wa Hispania alitimuliwa Jumatatu iliyopita kama kocha wa Granada kufuatia klabu hiyo kusuasua kwenye La Liga ikiwa mkiani kwenye msimamo. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 anachukua nafasi ya Georges Leekens wa Ubelgiji ambaye alijiuzulu baada ya Algeria kuenguliwa katika hatua ya makundi ya michuano ya Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu.
Mechi ya kwanza ya mashindano kwa Alcaraz itakuwa dhidi ya Togo wakati Algeria watakapoanza kampeni zao za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2019.

Mbeya City ikiibana Lyon, Pazi kama kawa

BAO la kipindi cha pili lililofungwa na Thomas Morris limeisaidia African Lyon kuepuka kipigo mbele ya Wakali wa Green Town, Mbeya City baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye pambano la Ligi Kuu Bara lililochezwa jioni ya leo Alhamisi.
Katika pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Mbeya City itabidi ijilaumu kwa kushindwa kuibuka na ushindio baada ya kupoteza mkwaju wa penalti dakika ya 37 kabla ya zahoro Pazi kusahihisha makosa dakika tano baadaye kwa kuifungia timu hiyo bao la kuongoza.
Bao hilo lilikuwa la tano kwa winga huyo teleza ndani ya timu hiyo iliyomrejesha uwanjani baada ya kuwa nje ya karibu misimu miwili kwa tatizo la ITC iliyokuwa imenasa FC Lupopo ya DR Congo.
Uzembe uliofanywa na mabeki wa Mbeya City ulisaidia mkongwe Thomas Morris aliyewahi kutamba na Yanga na Moro United kufunga bao la kusawazisha na kuifanya Lyon kufikisha pointi 31 baada ya mechi 27.
City kwa sare hiyo imeifanya ifikishe pointi 32 sawa na Mwadui ila imebebwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikishika nafasi ya saba ikiwatoa wachimba madini hao wa Shinyanga ambao wanarudi nafasi ya 8.
Ligi hiyo itaendelea tena wikiendi hii kwa mechi sita ambapo nne zitachezwa Jumamosi ikiwamo ile inayosubiwa kwa hamu kubwa kati ya Toto Africans itakayoikaribisha Simba wanaoongoza msimamo wa ligi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na Jumapili zitapigwa mechi mbili tu.

Messi aichanganya Argentina adhabu ya FIFA


WAMEPAGAWA. Kitendo cha nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi kufungiwa mechi nne na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limewatia wazimu Waargentina kiasi Chama cha Soka nchini humo (AFA) kuamua kujitosa kumtetea.
Rais wa AFA, Claudio Tapia amefunga safari mpaka Hispania ili kujadili kesi inayuomkabili Messi, ambaye ndiye tegemeo na tumaini la nchini hiyo katika mbio zake za kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2018.
Tapia alisisitiza safari ya kwenda nchini Hispania ni mahsusi kwa ajili ya kwenda kujadili kesi ya Lionel Messi ya kufungiwa mechi nne na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na sio kwenda kuzungumza na Jorge Sampaoli au Diego Simeone kuhusiana na kibarua cha kuinoa nchi hiyo.
Messi alilimwa adhabu hiyo na FIFA baada ya kumtolea kauli chafu mwamuzi wakati wa ushindi wa bao 1-0 Argentina iliyopata dhidi ya Chile mwezi uliopita na kumfanya kukosa mchezo waliofungwa na Bolivia mabao 2-0 na nyingine tatu zijazo za kufuzu Kombe la Dunia.
Nyota huyo wa Barcelona anayo nafasi ya kukata rufani ya kutaka kupunguzwa kwa adhabu hiyo mwezi ujao kitu ambacho Tapia alitaka kwenda kujadili naye ana kwa ana.
Tapia alisema FIFA imemtaka Messi kupeleka shauri lake hilo la kufungiwa mechi nne baada ya mchezo wao dhidi ya Chile Alhamisi Mei 4 mwaka huu hivyo ilikuwa muhimu kwenda kujadiliana naye kuhusiana na hilo.
Mchezo ujao wa Argentina utakuwa ni ule wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Brazil utakaofanyika nchini Australia Juni mwaka huu huku mechi za kufuzu Kombe la Dunia zikitarajiwa kuendelea Agosti.

Mabao ya Barcelona yampa ulaji Dyabala Juventus

SAA chache baada ya kuitia aibu Barcelona katika mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Straika wa Juventus, Paulo Dybala amesaini mkataba mpya na mabingwa hao wa Italia ambao utamalizika mwaka 2022.
Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 23 ameifungia Juventus mabao 16 msimu huu na kulikuwa na tetesi zikimuhusisha na kuondoka. Dybala alijiunga Juventus kwa kitita cha Pauni 23 milioni kutoka Palermo na kupewa mkataba wa miaka mitano Juni 2015 na kufanikiwa kushinda mataji mawili mwaka jana.
Dybala alisema siku zote amekuwa akitaka kufanikiwa kwenye kila kitu na anafahamu Juventus ndio mahali sahihi kuwepo kama anataka kushinda mataji. Dybala amefunga mabao 39 na kusaidia mengine 16 kwenye mechi 82 toka ajiunge na Juventus, ikiwa ni dadi kubwa zaidi ya mchezaji yeyote katika klabu kwa muda aliojiunga.