STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 29, 2013

Yathibitika M2P hajafa, ila bado yu mahututi

ASUBUHI zilizagaa taarifa nchini kwamba msanii aliyekuwa na marehemu Albert Mangwea 'Ngweair', M to the P aliyekutwa amezimia kwamba naye alikuwa amefariki dunia, ukweli ni kwamba msanii huyo bado yu hai ingawa hali yake inaelezwa kuwa bado si nzuri kwani anaendelea kupumulia gesi.
Kwa mujibu wa Mtangazaji wa kituo cha radio cha Clouds Fm, Millard Ayo, aliyekuwa akizungumza moja kwa moja kutoka Afrika Kusini alipoenda, alisema kuwa M2P bado yu hai, ingawa bado amelazwa na anapumua kwa kutumia mashine maalum.
Ayo alisema M2P aliyekuwa sambamba na Ngweair katika chumba kimoja, alionekana na baadhi ya marafiki zake akiwamo msanii Bushoke akinyanyuka mara aalipowaona wameenda kumjulia hali na kuthibitisha kuwa yu hai tofauti na taarifa za mapema asubuhi kwamba msanii huyo naye aliaga dunia.
Aidha mtangazaji huyo anayeendesha kipindi cha Amplifaya, alisema mwili wa marehemu Ngweair ulihamishw atoka hospitali ya Helen Joseph na kupelekwa hospitali ya serikali ukisubiri taratibu za kuusafirisha kuurejesha Tanzania kwa ajili ya mazishi.

Jide, aungana na MwanaFA, Kalapina kufuta onyesho


 
Judith Wambura Mbibo 'Jide' a.k.a Anaconda
MWANADADA mkali wa miondoko ya muziki wa kizazi kipya nchini, Lady Jaydee ameamua kufuta onyesho lake la miaka 13 tangu awe katika fani hiyo lililokuwa lifanyike Ijumaa kupisha msiba wa Albert Mwangwea 'Ngwair'.
Hatua ya Jide imekuja huku wakali wengine wa muziki huo nchini MwanaFA na Karama Masoud 'Kalapina' ambao nao walikuwa wafanye maonyesho yao Mei 31 jijini dar katika kundi tofauyti.
Jide, ambaye hivi karibuni aliingia kwenye mzozo na kituo cha radio cha Clouds, kiasi cha kufikishwa mahakamani, alinukuliwa akisema kuwa onyesho hilo halitafanyika tena kesho mpaka msiba wa Ngwair utakapomalizika.
Akihojiwa na kipindi cha Super Mix kinachorushwa na kituo cha EA Radio, Jide maarufu kama Komandoo a.k.a Binti Machozi au ukipenda Anaconda, mkongwe alikuwa na wakati mgumu alipoulizwa unamuelezeaje msanii Mangwear.
Jide aliyekuwa mwenye huzuni akijibu huku akilia kuwa, Tanzania imempoteza nyota. Juu ya shoo yake Jide alisema imebidi aisogeze mbele kidogo mpaka msiba huu upite kwanza ndipo atasema tarehe rasmi.
Ngwair alifariki jana nchini Afrika Kusini kwa kile kilichoelezwa kuwa kala kitu chenye sumu, taarifa nyingine zikidai alijidunga dawa na kuzimika yeye na rafikie M to the P aliyeripotiwa kulazwa hospitalini akiwa hoi mjini  Johannesburg.

Familia ya Ngwair watoa taarifa ya mazishi na jinsi mwili utakavyoletwa Bongo

http://3.bp.blogspot.com/-WhLAsO1Z0Cg/TftKo0GeYeI/AAAAAAAAAkY/Z6SKc0_7gz0/s1600/NgweaWEB.jpg
Ngwair enzi za uhai wake
BABA Mdogo wa 'Membaz' wa kundi la Chember Squad, Albert Mangwea 'Ngwair', Mzee Mangweha ambaye yuko Mbinga Songea kikazi, amesema kuwa wamekubaliana na kaka yake mkubwa yaani baba mkubwa wa Ngwair, David Mangweha ambaye naye yuko Songea kuwa watu watakutanika Mbezi kwa msiba na pia mapokezi yatafanyika hapa Dar es salaam Mbezi Beach. 
  

Baba huyo mdogo alisema kuwa kesho ndo watarudi Dar es Salaam pamoja na kaka yake yaani baba mkubwa wa marehemu. 
 
Kuhusu mwili kuletwa hapa Tanzania kutoka Afrika Kusini baba mdogo amesema kuwa mpaka sasa hawajajua jinsi gani mwili huo utafika hapa lakini kuna ndugu zao ambao tayari washaanza kufanya taratibu za kuwasiliana na ubalozi wa Afrika Kusini ili kujua ni jinsi gani mwili huo utafika hapa.

Kama kutakuwa na mabadiliko yeyote watakapowasili kesho baba mdogo na baba mkubwa baada ya kikao cha familia watatoa taarifa.
Lakini asuibuhi mmoja wa ndugu wa marehemu kutoka mkoa wa Mara alisema kuwa mwili wa msanii huyo aliyekuwa mkali wa Hip hop utakapowasili nchini utazikwa mjini Morogoro ambapo tayari kuna msiba umewekwa na mama yake.
Ndugu huyo alikuwa akihojiwa moja kwa moja na kituo kimoja cha redio na kusema wana ndugu wamekubaliana Ngwair akazikwe Morogoro alipohifadhiwa baba yake.
Ngwair, aliyefahamika baada ya kutoa kibao cha Ghetto Langu mwaka 2003 kabla ya kupakua albamu ya Mimi na kisha kufuatiwa na Nge, alifariki jana nchini Afrika Kusini kwa kile kilichoelezwa kujidunga dawa za kulevya, ingawa bado haijathibitishwa kidaktari alipoenda kufanya shoo na msanii mwenzake M2P. 

WASIFU WA MAREHEMU NGWAIR


 MAREHEMU Albert Kenneth Mangwea alizaliwa Novemba 16, 1982 mjini Mbeya akiwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto 10 wa baba yake na wa sita kwa mama.
Kiasili Ngwair alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Ruvuma kabila la Kingoni, ingawa amekuwa mjini Morogoro na mkoa wa Dodoma.
Shule ya Msingi aliisoma Shule ya Bungo mjini Morogoro alikohamia akiwa na miaka mitano kabla ya kuhamia Dodoma kulamizia darasa la saba toka la tano alilohama nalo Shule ya Mlimwa.
Sekondari aliisoma Mazengo Sec kabla ya kuendelea Chuo cha Ufundi cha Mazengo pia mjini Dodoma alipoanza kujihusisha na muziki kabla ya kutua kundi la Chamber Squad lililoundwa na Jafarah, Jay Mo, Noorah, Mez B, Mchizi Mox na Dark Master.
Amewahi kunyakua tuzo ya Kili Music Award kupitia kipengele cha muziki bora wa Hiphop, huku nyimbo kadhaa zilimtambulisha vyema kwa mashabiki baadhi ikiwa ni  Ghetto Langu, Mikasi na nyingine za kushirikishwa na wasanii mbalimbali.
Katika maisha yake ya muziki aliwahi kutoa albamu mbili za Mimi ya mwaka 2005 na Nge ya mwaka juzi ambayo hata hivyo haikufanya vyema sokoni kama ile ya awali.