STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, August 27, 2013

Mpinzani wa Cheka kutua leo, Mashali bado 'amgomea' Maugo

http://www.minnesotaboxing.com/Interviews/phil_codrington.jpg
Bondia Phil 'The Drill'  Williams
Phil "The Drill" Williams/ SnapLocally.com
Phil 'The Drill' Williams
WAKATI bondia Phil 'The Drill' Williams kutoka Marekani pamoja na kocha na daktari wake wanatarajia kutua nchini usiku wa leo ili kumkabili Francis Cheka, Thomas Mashali ameendelea kusisitiza kuwa hatapigana na Mada Maugo siku ya Ijumaa.
Cheka na Williams wanatarajiwa kupigana kuwania ubingwa wa kimataifa wa WBF katika pambano la uzani wa Super Middle raundi 12 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam siku ya Agosti 30.
Rais wa TPBO-Limired wanaosimamia pambano hilo na mingine itakayochezwa siku hiyo, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema usiku wa jana wametuma tiketi ya bondia huyo na wasaidizi wake na watatua nchini leo saa nne kasorobo usiku.
Ustaadh alisema Mmarekani kutua kwa bondia huyo ni kuonyesha maandalizi ya pambano hilo yamepamba moto huku akiwaonya mashabiki na mabondia wasio na nidhamu kujihadhari mapema siku ya pambano kwa ulinzi utakaokuwepo.
"Bondia wa Marekani Phil Williams atatua nchini Saa 3:50 usiku wa kesho (leo) akiwa na kocha wake, Filbert Songola na Dk aitwaye Charles na TPBO-Limited tunawaonya mashabiki kujiepusha na uhuni siku ya pambano," alisema.
Alisema onyo hilo wanalitoa mapema kutokana na ukweli mapambano hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na mabalozi, mawaziri na viongozi wenye heshima zao na kwamba ulinzi utakuwa mkali hiyo asingependa wachache kuwavurugia.
Katika hatua nyingine bondia Thomas Mashali ameendelea kusisitiza kuwa hatapanda ulingoni Ijumaa kuzipiga na Mada Maugo akisema halitambui pambano hilo.
"Msimamo wangu ni ule ule kwa sasa akili yangu ipo kwenye pambano la kimataifa dhidi ya Mmalawi Chiotcha Chimwemwe nitakayepigana naye mjini Blantire nchini Malawi," alisema Mashali maarufu kama Simba  Asiyefugika.
Mashali alisema wameingia mkataba wa kupigana na Chimwemwe katika pambano la uzito wa kati litakalochezwa Oktoba 29 na kudai kwa kutambua ukali wa mpinzani wake ameanza mapema kujifua ili aweze kufanya vyema.

Kanali Msechu mgeni rasmi tamasha la Home Gym, Victoria kuwasha moto

Baadhi ya wanamuziki wa Victoria Sound, Mwinjuma Muumin na Waziri Sonyo wakiwajibika
WAKATI wadhamini wakianza kujitokeza kudhamini Tamasha maalum la kuadhimisha miaka 15 ya kituo cha mazoezi cha Home Gym, waratibu wamemtaja mgeni rasmi wa tamasha hilo kuw ani Kanali H.A Msechu wa 501.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Jumamosi hii kwenye uwanja wa Mwenge, jijini Dar es Salaam ukishirikisha michezo na wanamichezo mbalimbali wa soka, kutunisha misuli, kunyanyua vitu vizito na burudani ya muziki.
Mkurugenzi wa Home Gym, Andrew Mwangomango aliiambia MICHARAZO kuwa tayarui wadhamini wameanza kujitokeza kuwapiga tafu na kwamba tayari wamepata uthibitisho kuwa Kanali Msechu ndiye atakayekuwa mgeni rasmi.
"Kanali Msechu wa Kikosi cha 501 ndiye atakayekuwa mgeni rasmi wa tamasha letu ambalo linaendelea kuandikisha wanamichezo wanaopenda kushinda siku hiyo katika michezo wa kunyanyua vitu vizito na kutunisha misuli," alisema.
Mwangomango, aliongeza kuwa baadhi ya wadhamini wameanza kujitokeza  kuwapiga tafu na kuwaomba wengine wajitokeze wakati siku zikikaribia kwa ajili ya tamasha hilo litakalopambwa na bendi ya Victoria Sound.
"Bado tunahitaji wadhamini hivyo wenye kupenda kutusaidia wajitokeze kwani ni tamasha la aina yake likiwa na michezo ya kukikimbiza na kukamata kuku, kanga na sungura na soka litakalohusisha klabu za matevetani zaidi ya 20," alisema.
Kituo hicho cha Home Gym kilichopo Mwenge-Kijijini, kilianzishwa mwaka 1998 kikitoa mafunzo wa mazoezi ya viungo na michezo ya kunyanyua vitu vizito na utunishaji wa misuli.

Timu za Ruvu zachekelea kuanza vyema, yapania wapinzani wao wa Mbeya

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhaF1tsqvUmrtMICozA4dHcA_DetF8axYj97O_uDj0kkxxGOF6_BpM4UZbrAuxFzz8p04g6_20F6Y4D6lFqVkIPGh9tQ3Ad3NlFKR5UQCPex36z5AyqjybyV9U-_8S_GqOtYG6DPFj3-2QH/s640/JKT+RUVU+KIKOSI.jpg
JKT Ruvu
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhXtdUgJUQpoqJDsDusQZKcGKBjAz5VsgkU1d7LoYMp8k9R4EJMliB6GKtLSqbJpXRRbSWfurfjs0QQYhasY-3DPyM87v27C4nM5jOY7vrLhH7s7iM01OrbSAtJ0p-IIcVEFh_2tSEaTI4E/s640/RUVU+SHOOTING.jpg
Ruvu Shooting
UONGOZI wa timu za Ruvu Shooting na JKT Ruvu za Pwani umefurahishwa na kuwapongeza makocha na wachezaji wao kwa kuanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kupata ushindi wakidai huo ni mwanzo tu.
Ruvu Shooting ilianza kwa kishindo ligi hiyo kwa kuinyuka Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-0,  wakati maafande wenzake wa JKT walipata ushindi wa 2-0 jijini Tanga walipoumana na Mgambo JKT.
Ushindi huo umeziweka timu hizo kileleni sambamba na Yanga walioishindilia Ashanti United kwa mabao 5-1 katika mechi za ufunguzi wa ligi hiyo mwishoni mwa wiki na kuufanya uongozi wa klabu hizo kuwapongeza kwa kazi nzuri.
Afisa Habari wa timu hizo za JKT, Masau Bwire alisema uongozi unawapongeza makocha Charles Boniface na Mbwana Makatta na wasaidizi wao pamoja na wachezaji wa kuanza vyema pazia la ligi kuu kwa kupata ushindi.
"Tumefurahishwa na mwanzo nzuri uliofanywa na timu zetu na tunawapongeza makocha na wachezaji kwa kazi nzuri waliyofanya tukiamini wataendelea kugawa dozi hata katika mechi zijazo. Hii ni tahadhari kwa wapinzani wetu msimu huu," alisema Bwire.
Bwire alisema kwa sasa timu zao zinaelekeza nguvu kwa mechi zao za kesho ambapo Ruvu Shooting itakuwa ugenini mjini Mbeya kuumana na Mbeya City, wakati 'ndugu' zao JKT Ruvu watakuwa Mabatini, Mlandizi kuvaana na Prisons.

Tchico Tchikaya: Mkali aliyewakimbiza akina Kanda Bongoman

* Kibao cha Soukous Machine kilimtambulisha dunia nzima
* Kwa sasa yupo Australia na bendi mpya ya Warako Musica



http://img.youtube.com/vi/U6ojiWpk6tk/0.jpg
UNAPOLITAJA jina la Tchico Tchicaya kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa Soukous, akili zao zitaenda hadi miaka zaidi ya 20 iliyopita wakikumbukia kibao cha  Soukous Machine kilichomtambulisha mno mwanamuziki huyo.
Kibao hicho kilichofyatuliwa mwaka 1987, kilimtambulisha vema Tchico kama mmoja wanamuziki wabunifu na aliyekuwa akipenda na kuuenzi utamaduni wa nchi yake ya Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville).
Wakati kibao hicho kinatamba wanamuziki wakali wa Congo-Kishansa kama akina Pepe Kalle, Nyboma Mwandido, Kanda Bongoman na wengine ndio kwanza walikuwa wameanza kuiteka dunia kwa muziki wao na kumfanya Tchico kuenda nao sambamba na nguli hao ambao baadhi wameshafariki.
Nguli huyo ambaye kwa sasa ameweka maskani yake nchini Australia akiwa na bendi mpya iitwayo Warako Musica akishirikiana na Passi Jo, katika kibao hicho aliweka madoido ya ngoma asilia na milio ya ndege iliyovutia.
Katika kibao hicho mwanamuziki huyo, alikuwa akiisifia Afrika na kutaja majina ya baadhi ya miji ya nchi za bara hilo, huku akiufagilia muziki huo wa Soukous, ambao unaendelea kubamba mpaka leo katika medani ya muziki.
Tchico aliyeanza muziki zaidi ya miaka 30 iliyopita, majina yake kamili ni  Pambou-Tchicaya Tchico, lakini majina yake ya mwisho ndiyo yakifahamika zaidi kwa wapenzi wa muziki wa Soukous aliokuwa akiupiga.
Ukali wa Tchico ulianza kuonekana mwaka 1970 alipoanza muziki kama muimbaji katika bendi iliyofahamika kwa jina la Monta Lokoka iliyokuwa na maskani yake katika mji mkuu wa Congo, Brazzaville.
Akiwa na bendi hiyo alifanikiwa kupakua na kutamba na albamu kali mbili zilizofahamika kwa majina ya Rina ya mwaka 1970 na Loemarthe iliyotoka mwaka 1971.
Miaka miwili baada ya kujiona kaiva vema, mkali huyo alijitosa katika bendi ya Les Bantous de la Capitale akiwa mmoja wa waimbaji nyota wa bendi hiyo iliyokuwa maarufu mwa makundi yaliyotamba enzi hizo jijini Brazzaville.
Ndani ya Les Bantous de la Capitale, Tchico alitoka na albamu za Isabelle ya 1972, Celia-Shantina (1973) na Santana ya mwaka 1974, ambapo baadaye alifyatua albamu nyingine za Shanta Maguy (1974), Sambela Sambela (1975) na Ah Ponton la Belle mwaka 1976 akiwa na kundi la African Kings.
Mwaka 1977 na 1979 Tchico alipeleka 'maujuzi' yake nchini Nigeria alipoishi na kufanikiwa kupakua albamu nne tofauti ambazo zilimpa mafanikio makubwa kiasi cha kubatizwa jina la utani la  Voix d'or.
Katika kipindi hicho cha mafanikio ndipo alipokuwa akiimba na mkali Lolo Lolita ambapo walifyatua albamu iliyotamba ya Jeannot.
Mwaka 1983, Tchico aliamua kwenda Paris Ufaransa, kabla ya kufuatwa baadaye na utiriri mkubwa wa wanamuziki wa Kicongo kwenda nchini humo.
Akiwa katika jiji hilo la maraha, Tchico, aliweza kurekodi nyimbo mbalimbali katika studio tofauti tofauti, kulikoenda sambamba na kubadilika kwa jina la bendi yake toka Afro Festival hadi Les Evades de Ponton la Belle na kisha baadaye Les Officiers de la Musique Africaine.
Nyota yake ilizidi kung'ara zaidi katikati ya mwaka 1980 na mwanzoni mwa 1990 baada ya kubadili jina la kundi lake toka Orchestre Kilimandjaro hadi kuwa La Voix d' Or au Soukous Machine akitumia moja ya vibao vilivyompaisha kama jina la kundi, ambapo alifyatua vibao mbalimbali vikali vilivyotambulisha karibu bara zima la  Afrika na dunia kwa ujumla.
Baadhi ya nyimbo alizotoa kipindi hicho ni pamoja na Lucie Matanga, Paris-Tropical, Les larmes de Les Iles, Kembo Na Nzambi, Guyguy wa Mapendo, Adios Luluna, Jambo Afrika, Deliverance na A'Argent Ange ou Demon.
Kutokana na kutambulika huko dunia nzima, mwanzoni mwa karne mpya yaani miaka ya 2000, aliamua kuhamia na kuweka makazi yake nchini Australia akiendelea na kazi yake ya muziki akiwa na Passi Joo katika bendi yake mpya iitwayo Warako Musica aliyotoa nao albamu ya 'Ya Banganga'.
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kutoa kibao cha Soukous Machine cha mwaka 1987 na ambacho pengine ndicho maarufu kwa Watanzania ni pamoja na yeye Tchico Tchicaya aliyeongoza katika uimbaji, Jacqueline Brouta na Samba Kadhy Bell waliokuwa waimbaji waitikiaji.
Katika gitaa la solo alikuwa Denis la Cloche, huku Casanova de Ketchel akicharaza gitaa la rhythms na katika gitaa zito la besi alisimama Remy Salomon, na 'mkaanga chips' (mpiga dramu) alikuwa ni Denis Hekimian.
Lolitta Babind alikuwa akipiga nyanga, wakati mpapasa kinanda alisimama mkali wa zamani aliyeitwa Tony na Jean Marie Kabongo na wajina wake, Jean Claude Leandre walikuwa wakipuliza ala za upepo Kabono akipuliza 'Domo la Bata' na mwenzie akipiga tarumbeta.
Mbali na kibao ca Soukous Machine, Tchico pia alitamba na vibao vingine kama Africa Dance Machine, Sonima, African Carnaval, Cocktail Tropical,
L'ambiance à Paris, Dynamic Afro-Soukous, L'argent domine le monde, Full Steam Ahead, Nostalgie d'Afrique, Amour maternel, Mon enfant na Giselle.
Nyingine ni pamoja na Amie Clara, Tania, Rosalie, Jeannot, Lucia, dans Tam Tam d'Afrique, Méditation, L'heure a sonné, Operation Soukous, Mamy Rosa, Josintha,  From Congo to Nigeria, Ah Ponton la Belle na nyinginezo.
Ingawa ni miaka mingi imepita bila ya nyimbo za mkali huyo kusikika hapa nchini, lakini bila shaka Tchico hatasahulika kirahisi kwa vile namna ya uvaaji wake na hata upigaji wake wa muziki katika bendi alizozifanyia kazi, umemfanya kuwa vichwani kwa wapenzi wa muziki hususani wa Soukous.