STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 25, 2015

Mkutano wa TFF sasa kufanyika Morogoro

Rais wa TFF, Jamal Malinzi
MKUTANO mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF uliokuwa ufanyike mjini Singida umehamishiwa Morogoro.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana jumapili Februari 22 mwaka huu, imefanya mabadiliko ya mahali utakaofanyika Mkutano Mkuu wa mwaka kutoka Mkoa wa Sinigida na kuhamishia mkoa wa Morogoro.
Hatua hiyo imefikiwa na Kamati ya Utendaji kutokana na sababu za kutokukamilika kwa miundombinu ya mkutano mkuu na kuwepo ka shughuli nyingine za kijamii mkoani humo.
Kamati ya Utendaji inamshukuru Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Singida (SIREFA), na uongozi mzima kwa kujitolea kuandaa mkutano huo na huko nyuma waliweza kuandaa mkutano wa makatibu wa vyama vya soka vya mikoa.
TFF itaandaa vikao na matukio mengine mkoani Singida itakapotokea hapo baadae, tarehe ya mkutano mkuu itaendelea kubakia ile ile ya Machi 14, 15 mwaka huu.

Simba, Yanga zavuna zaidi ya Sh. Mil. 100 viwanja vya ugenini


Kikosi cha Simba
Kikosi cha Yanga
KLABU za Simba na Yanga zimeingiza jumla ya Sh. Mil. 100 katika mechi zao za mwishoni mwa wiki viwanja vya ugenini.
Pambano lililowakutanisha wenyeji timu ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga dhidi ya timu ya Simba umeingiza jumla ya Sh. Mil.31.
Jumla la watazamaji 5,439 waliingia uwanjani kushuhudia mchezo huo, ambao timu ya Stand imepata mgao wa Sh. 6,564,268.22 na Simba wakipata mgao wa 4,661,581.78.
VAT (18%) tshs. 4,763,135.59 huku FA  mkoa wakipata tsh.665,940.25, FDF tsh. 1,141,611.86, Bodi ya Ligi tsh. 1,522,149.15, Gharama za mchezo tsh. 1,617,283.47, Uwanja tsh. 2,854,029.66, Gharama ya tiketi tsh. 1,593,000,00, FDF tsh. 2,921,000.00, TFF tsh.2,921,000.00
Wakati kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, jumla ya Sh. 74, 600,000.00, zilipatikana kutokana na watazamaji 14,920 waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo, lililozihusisha wenyeji Mbeya City na Yanga.
Kwa mujibu wa mgao VAT(18%) tsh.11,379,661.02, CDRB (5%) tsh.3,730.000.00, FDF tsh. 5,222,000,00, TFF tsh. 2,238,000.00, Uwanja tsh. 7,804,550,85, Gharama za mchezo tsh 4,442,578.81, Bodi ya Ligi tsh. 4,162,427,12.
Chama cha soka mkoa (FA) Mbeya kimepata tsh. 1,821,061.86, FDF(TFF) tsh. 3,121,820.34, wenyeji timu ya Mbeya city wakipata tsh. 17,950,466.95 na klabu ya Yanga tsh. 12,747,438.98.

Mtanzania ajiunga chuo cha soka Senegal

Mtanzania Nasry Daud Aziz atakayejiunga na kituo hiki cha Senegal
MWANASOKA chipukizi Nasry Daudi Aziz aliyezaliwa Agosti 21, 2001 amechaguliwa kujiunga na kituo cha kukuza vipaji cha Aspire Football Dream kilichopo katika mji wa Dakar nchini Senegal.
Mradi wa  Aspire nchini ulianza mchakato wa kusaka vijana mwezi Machi - Mei, 2014 ambapo vijana wengi walijitokeza na kuchaguliwa vijana 14 ambao walikwenda katika mchujo mwingine uliofanyika nchini Uganda uliowashirikisha vijana zaidi ya 50.
Kijana huyo ni miongoni mwa wachezaji 17 waliochaguliwa kati ya vijana 34 walikuwepo nchini Senegal kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo kulikuwa na vijana wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Amerika ya Kusini.
Kituo cha Aspire kilichopo Dakar nchini Senegal ni miongoni mwa vituo viwili vinavyoongozwa na mtoto wa mfalme wa Qatar na timu ya Barcelona, kituo kingine kipo mjini Doha.
Nasry Daud Aziz anatarajiwa kuondoka nchini Februari 28 mwaka huu kuelekea Dakar ambapo atakua kwenye kituo hicho kwa mkataba wa miaka miatano.
 Kutoka nchini Tanzania Nasry anakua ni kijana wa tatu kujiunga na kituo hicho, wengine ni Matine Taganzi na Orgenes Morrel ambaye aliitwa kwenye timu ya Taifa Stars maboresho na kocha Mart Nooj.

Cheki video mpya ya Belle 9 ft Joh Makini - Vitamin Music

Mwili wa Christopher Alex hatimaye wapumzishwa Dodoma

IMG-20150224-WA0007
Makazi ya milele ya Christopher Alex
Na Rahma Junior, Dodoma
MWILI wa kiungo nyota wa zamani wa timu ya Simba, Christopher Alex, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma, umezikwa jana kwenye makaburi ya Nkuhungu.
Mwili wa Alex ulifanyiwa ibada ya maziko nyumbani kwa mama yake Massawe, Martha Matonya chini ya  Mchungaji wa Kanisa la Anglikan, Parishi ya Chamwino, Mch. David Matonya na ilihudhuriwa wa mamia ya waombelezaji, wakiwamo waliokuwa wachezaji wenzake kwa nyakati tofauti.
Baadhi ya wachezaji walioshiriki kumsindikiza marehemu Alex ni Ulimboka Mwakingwe, Boniface Pawasa, Kelvin Mhagama, Amani Mbarouk, Juma Kaseja na Juma Ikaba aliyecheza naye kwenye timu ya CDA-Dodoma, ambaye sasa ni kocha wa timu hiyo.
Klabu ya Simba iliwakilishwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa timu hiyo, Ally Sulu, ambaye pia alizungumzia malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya waombolezaji kwamba klabu zimekuwa na kawaida ya kuwatelekeza wachezaji pindi wanapokuwa wamemaliza kuzitumikia.
Naye Pawasa, alisema siyo tu klabu vya mpira wa miguu bali Watanzania wengi wanafurahia mtu akiwa mchezaji, anapomaliza muda wa kucheza na ikatokea ameugua au kupatwa majanga, wanamtelekeza.
“Wasanii wengine mathalani wa filamu wanashuhudiwa wakisaidiwa hata wanapokuwa kwenye matatizo ya kujitakia. (Tulipaswa kumjali) Alex alifunga penalti ya mwisho katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya timu ngumu ya Zamalek ya Misri mwaka 2003,” alisema Pawasa.
Marehemu Christopher Alex atakumbukwa kwa kufunga penati ya mwisho iliyowavua ubingwa wa Ligi ya mabingwa Afrika Zamalek mwaka 2003 na kuvunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Yanga katika michuano hiyo tangu 1998 walipotinga hatua ya makundi kwa timu za Tanzania.
Simba ilishinda nyumbani bao 1-0 kabla ya kufungwa idadi kama hiyo katika mechi ya marudiano nchini Misri na kufikia hatua ya kupigiana penati na Sinmba kufuzu.

Andy Murray aanza vema michuano ya Dubai Open

MUINGEREZA Andy Murray ameanza vizuri kampeni zake za kutwaa ubingwa wa mashindano ya Dubai baada ya kuibuka na ushindi wa seti 6-4 7-5 dhidi ya Gilles Muller.
Mscotland huyo, mwenye umri wa miaka 27, alipata ushindi huo kwa kutumia saa moja na dakika 45, na sasa atacheza na Joao Sousa katika raundi ya pili, ikiwa ni wiki mbili baada ya kumshinda Mreno huyo katika mashindano ya Australian Open.
Bingwa anayeongoza kwa ubora Novak Djokovic naye alianza vizuri mashindano hayo baada ya ku
mchakaza Mcanada Vasek Pospisil 6-4 6-4 katika mchezo wa rundi ya kwanza.
James Ward ambaye ni Muingereza anayeshikilia nafasi ya pili kwa ubora, alijikuta akishindwa kufanya kweli baada ya kushindwa mara mbili katika hatua ya kufuzu na kupoteza kwa 6-4 6-4 dhidi ya Muhispania Feliciano Lopez, anayeshikilia nafasi ya 13 kwa ubora duniani.
Muingereza huyo sasa atakwenda Glasgow kujiunga na timu ya Uingereza itakayocheza mchezo wa Davis Cup dhidi Marekani, utakaofanyika kuanzia Machi 6-8 huko Emirates.
Murray anatarajia kukawia kujiunga na wenzake huko Scotland endapo ataendelea kufanya vizuri huko Dubai baada ya leo kuanza vibaya mchezo huo katika jaribio lake la kwanza, lakini alifanya vizuri na kuibuka na ushindi katika seti hiyo ya kwanza.
Djokovic anashiriki kwa mara ya kwanza tangu alipotwaa taji la Australian Open Februari mosi na anaangalia kuwa mtu pekee wa 12 kushinda taji la 50.

Luis Enrique kuendelea kumtumaini Messi katika penati

Joe Hart
Joe Hart akiojkoa mkwaju wa penati ya Messi usiku wa jana
Lionel Messi watches on as Hart does brilliantly to save his last-minute penalty  
Messi akiwa haamini kama mkwaju wake umezuiwa na kipa wa Man City
Hart celebrates saving the last-gasp penalty as Pedro holds his head in his hands and Messi lies on the floor
Messi akiwa amelala chini baada ya kukosa penati
MENEJA wa klabu ya Barcelona, Luis Enrique amesisitiza kuwa Lionel Messi ataendelea kuwa mpiga penati wa timu hiyo pamoja na kukosa penati yake ya nne msimu huu katika mchezo dhidi ya Manchester City juzi.
Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alikuwa na nafasi ya kuipa ushindi Barcelona wa mabao 3-1 katika dakika za majeruhi lakini Joe Hart alifanikiwa kuokoa mchomo wake.
Messi pia amekosa penati katika mchezo dhidi ya Levante, Septemba mwaka jana na Brazil wakati akiitumikia timu yake ya taifa Oktoba lakini Enrique anaamini kuwa nyota huyo bado ni mpigaji mzuri na anamuamini.
Kocha huyo amesema wale wote wanaokosa penati ni wale wenye uthubutu wa kufanya hivyo na Messi bado ataendelea kuwa mpigani wao.
Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Etihad, Barcelona ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1, ikiwa ni siku chache ikitoka kupokea kipigo cha bao 1-0 nyumbani Camp Nou dhidi ya Malaga katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Kukosa penati hiyo ya juzi imemfanya Messi kulingana na Cristiano Ronaldo, Luis Figo and Andy Shevchenko katika michuano hiyo ya Ulaya wakitanguliwa na Ruud Van Nistelrooy aliyekosa mabao manne na Thierry Henry anayeongoza kwa kukosa penati tano.
Pia ni penati ya 13 kwa mkali huyo wa mabao wa Cataluna kati ya mikwaju 59 aliyopiga akiwa na klabu ya Barcelona, huku kwa upande wa nchi yake ya Argentina Messi amekosa mbili kati ya 12 alizopiga

Azam, Yanga zaenda ugenini zikiwa na matumaini

Azam Fc watakaokuwa ugenini nchini Sudan
Yanga wao watakuwa vitani nchini Botswana
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Azam na Yanga zimeondoka nchini zikiwa na matumaini makubwa ya kushinda mechi zao za wikiendi hii za ugenini katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Azam waliondoka jana kuelekea Sudan watakuwa na kibarua kizito mbele ya wenyeji wao El Merreikh waliowafumua kwenye uwanja wa Chamazi, mabao 2-0 wakati Yanga wenyewe waliondoka alfajiri ya leo wakiwa na morali mkubwa baada ya ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Maafande wa BDF XI ya Botswana watakaorudiana nao Jumamosi.
Yanga waliowaacha baadhi ya nyota wake akiwamo Mbrazil, Andrey Coutinho kutokana na kuwa majeruhi, imeenda Botswana wakiwa na amani kutokana na mwenendo mzuri wa timu yao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ikipata ushindi mfululizo na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi nne mbele zaidi ya watetezi Azam ambao mechi zao mbili za mwisho waliambulia sare tupu.
Uongozi wa Yanga kupitia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Jerry Muro amesema Yanga inaenda ugenini ikiwa imepania kusonga mbele licha ya kutambua pambano lao litakuwa gumu kwa vile BDF watakuwa nyumbani na wana hasira ya kufungwa mabao 2-0.
Muro alisema vijana wake wote 20 waliopo kwenye msafara wao wameapa kupambana kuhakikisha wanapata ushindi ugenini ili kusonga mbele ya kuvaana ama na Sofapaka ya Kenya au Platnum ya Zimbabwe ambao walishinda mabao 2-1 katika mchezo baina yao wiki mbili zilizopita mjini Nairobi.
Upande wa Azam kupitia Meneja wake, Jemedari Said, alisema kuwa wanaenda Sudan wakiwa na nia ya kukamilisha malengo yao ya kufuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jemedari, nyota wa zamani wa Majimaji-Songea na klabu nyingine alisema kuwa Azam wanaenda Sudan wakitambua kuwa watakabaliwa na mechi ngumu kwa vile El Merreikh siyo timu ya kubezwa hata kama waliwafunga mabao 2-0 katika mechi ya kwanza nyumbani.
Meneja huyo aliongeza kuwa Azam inayoiwakilisha Tanzania kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka miwili mfululizo kushiriki Kombe la Shirikisho, imepania kufika mbali kwenye michuano hiyo ili kufuta dhana kwamba timu za Tanzania ni wasindikizaji tu katika michuano ya kimataifa.
Mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, watashuka dimbani keshokutwa, watahitaji sare ya aina yoyote ili kujihakikisha kusonga mbele na kukutana na ama timu ya Lydia Ludic B.A ya Burundi au Kabuscorp do Palanca ya Angola ambazo zilishindwa kufunga katika mechi mechi yao ya mkondo wa kwanza iliyochezwa nchini Burundi.
Wawakilishi wengi wa Tanzania visiwani, KMKM waliofungwa mabao 2-0 na Al Hilal na POlisi Zanzibar walifumuliwa mabao 5-0 na Maunama ya Gabon watashuka dimbani mwishoni mwa wiki kukamilisha ratiba ya mechi zao za michuano hiyo ya kimataifa ya Afrika.
Mabingwa wa Zanzibar, KMKM watahitajika kuwafunga wa Sudan mabao 3-0 ili kufuzu, huku Polisi wakihitajika kushinda mabao 6-0 kitu kinachoonekana kuwa ndoto ikizingatiwa wawakilishi wa Zanzibar hawajawahi kuvuka raundi ya awali tangu nchi hiyo ilipotambuliwa rasmi na Shirikisho ya Soka Afrika (CAF) mnamo Desemba mwaka 2004.

Suarez aiangamiza Manchester City, Juve yaiua Dortmund

Suarez akishangilia bao lake la pili
Suarez akishangilia bao la kwanza

Lionel Messi akipambana kabla ya kukosa penati dakika za lala salama
MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Liverpool, Luis Suarez amewadhihirishia Waingereza kuwa yeye bado ni moto wa kuotea mbali baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiangamiza Manchester City kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Etihad, mjini Manchester katika mechi ya mkondo wa kwanza ya mtoano wa 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Suarez aliyeibeba Liverpool msimu uliopitwa kabla ya kuuzwa kwa 'hasira' na klabu hiyo kwa Barcelona kutokana na tukio lake la utovu wa nidhamu alililolifanya katika Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, aliiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kujiweka nafasi nzuri ya kutinga Robo Fainali katika mechi yao ya marudiano baadaye mwezi ujao mjini Barcelona.
Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay, alianza kuwashtua wenyeji ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England baada ya kufunga bao la kwanza dakika 16 akiwa ndani ya  'boksi' la lango la Manchester City kabla ya kuongeza jingine katika ya 30 akimalizia kazi nzuri ya Lionel Messi na kuifanya Barcelona iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili Manchester City ambao baadhi ya wachezaji wake walinukuliwa wakitamba haiwahofii Barcelona, walijitutumia na kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Sergio 'kun' Aguero katika dakika ya 69 kabla ya beki wake Gael Clichy kutolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu katika dakika ya 74 baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kutokana na kumchezea rafu Dani Alves.
Lionel Messi aliinyima Barcelona kuondoka na ushindi mnono zaidi baada ya mkwaju wake wa penati kuokolewa na kipa Joe Hart dakika za lala salama. Hiyo ilikuwa ni penati ya nne kwa Messi kukosa kati ya saba alizopiga katika msimu huu.
Kipigo hicho kinaifanya Manchester City kuwa na kazi yaziada ya kuhakikisha inapata ushindi usiopungua mabao 2-0 iwapo inataka kusonga mbele katia michuano hiyo iliyopenya hatua ya 16 Bora kibahati, vinginevyo mechi ya Machi 18 itakayochezwa Camp Nou huenda ikawa ndiyo ya kuagia michuano hiyo.
Katika pambano jingine la hatua hiyo ya mtoano, Juventus wakiwa uwanja wa nyumbani mjini Turin, Italia waliizabua Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa mabao 2-1 na kuzidi kumpa wakati mgumu kocha Jurgen Klopp ambaye kikosi chake kimekuwa na matokeo mabaya msimu huu kwenye ligi ya nyumbani ya Bundesliga.
Carlos Tevez na Alvaro Morato ndiyo walioinusisha Juventus harufu ya kucheza robo fainali baada ya kila mmoja kufunga bao katika muda usiozidi nusu saa huku, wageni wakifuta machozi kwa bao la Marco Reus.
Tevez alitangulia kufunga katika dakika ya 13 kabla ya wageni wao kulisawazisha kupitia kwa Reus dakika tano baadaye na Morata kuongeza la pili dakika ya 42 akimaliza pasi nzuri ya Paul Pogba na kuifanya Juventus kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kabla ya mechi yao ya marudiano itakayochezwa nchini Ujerumani Machi 18.

Kocha Spurs awaonya nyota wake pambano la Fiorentina

KOCHA wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino amewaonya wachezaji wake akiwataka kuichukulia pambano lao la marudiano ya Ligi Ndogo ya Ulaya wakiwa ugenini dhidi ya Fiorentina ya Italia kama pambano la fainali.
Pochettino amewataka wachezaji wake wasiweke akili zao kwa pambano la Fainali za Kombe la Ligi (Capital One) dhidi ya Chelsea litakalochezwa Jumapili kwenye uwanja wa Wembley na kujisahau mbele ya Fiorentina iwapoa wanataka kutinga 16 Bora.
Spurs itavaana Chelsea kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Wembley tangu mwaka 2008 na kocha huyo amesisitiza wachezaji wake waelekeze nguvu kwa pambano hilo lakini wasisahau 'fainali' nyingine dhidi ya Fiorentina ambao walitoka nao sare ya 1-1 wiki iliyopita.
Pochettino alisema: Alhamisi (leo) litakuwa pambano gumu mno. Nafikiri itakuwa ni fainali ya kwanza kwetu kabla ya Jumapili, Fiorentina ni timu pekee ambayo itaweza kutuvusha hatua nyingine ya michuano ya Ligi Ndogo ya Ulaya."
"Tunajua tunahitajika kufunga baada ya sare ya 1-1 na tunajiamini. Tunajiamini na tunapaswa kuchukua tahadhari kwa mchezo hio wa Alhamisi. Tunapaswa kupambana ili tushinde na wachezaji wanapaswa kufanya hivyo," alisema kocha huyo kuyoka Argentina.
Kocha huyo aliongeza kuwa; "Hii ni fainali nyingine na tunahitaji kufanya maamuzi (ya nani acheze) kwa sababu tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Fiorentina na West Ham,".
Spurs ambao mwishoni mwa wiki walinusurika kipigo nyumbani kwa kutoka nyuma na kurudisha mabao mawili dhidi ya West Ham Utd na kutoka sare ya 1-1 watavaana na Fiorentina katika mjini ya Frolence wakihitajika kushinda au kupata sare ya mabao zaidi ya mawili ili kutinga 16 Bora ya michuano hiyo ambayo leo pi itashuhudiwa mechi kadhaa za marudiano kabla ya kujulikana timu 16 zitakazosonga mbele.
Mojha ya pambano linalosubiwa kwa hamu ni lile la Liverpool dhidi ya Besiktas ya Uturuki ambao katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanja wa Anfied, Liverpool ilishinda bao 1-0 la mkwaju wa penati ya 'kulazimisha' ya Mario Balotelli.

Fainali za Qatar ni faida kwa Waingereza-Phil Neville

NYOTA wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, Phil Neville amesema kuandaliwa kwa michuano ya Kombe la Dunia kati ya Novemba na Desemba mwaka 2022 nchini Qatar ni jambo zuri kuwahi kutokea kwa nchi yake.
Kikosi kazi cha Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kilipendekeza michuano hiyo kuhamishwa wakati wa majira ya baridi kwasababu ya joto kali nchini Qatar.
Wakati wadau wengi wakikosoa uamuzi huo, Neville yeye anafikiri michuano hiyo itakuwa na faida kubwa kwa matumaini ya Uingereza kunyakuwa taji hilo.
Neville anaamini katika kipindi hicho wachezaji wanakuwa bado wako vyema na tayari kwa ajili ya kupambana na timu bora duniani. Mapendekezo hayo ambayo yanatarajiwa kufikishwa mbele ya kamati ya utendaji ya FIFA itakayokutana jijini Zurich, Machi mwaka huu, tayari inaungwa mkono na Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Michel Platini, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia (AFC).

John Riise athibitisha kumuaga Gerrard

http://sillyseason.com/sites/default/files/styles/article_top/public/article_images/riise_gerrard_reut960_1212152704.jpg?itok=zL9GLXlT
Riise akiwa na nahodha wake wa zamani, Gerrard
John Arne Riise enzi akiitumikia Liverpool
LONDON, England
BEKI wa kushoto wa zamani wa kimataifa wa Norway, John Arne Riise amethibitisha kushiriki pambano maalum la kumuaga Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard akiungana na nyota wengine wa klabu hiyo ya Anfield.
Mechi hiyo maalum inatarajiwa kuchezwa Machi 29 kwenye uwanja wa Anfield, ikiwarejesha nyota wa zamani wa Liverpool waliwahi kucheza na nahodha huyo ili kuaga kabla ya mwanasoka huyo wa kimataifa wa Uingereza ajahamia klabu yaLA Galaxy ya Marekani mwishoni mwa msimu huu.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Riise alithibitisha kuwa atakuwa miongoni mwa watakaokuwapo Anfield kumuaga Gerrard katia pambano hilo litakalohusisha kikosi cha sasa cha Liverpool na kikosi cha zamani cha mabingwa hao wa zamani wa England na Ulaya.
Nyota wengine watakaoshiriki pambano hilo ni Fernando Torres 'El Nino', Xabi Alonso, Pepe Reina, Javier Mascherano na Luis Suarez ambao wameshathibitisha kucheza pambano hilo, huku Riise akimtaja pia Luis Garcia naye atakuwapo.
"Najisikia fahari kubwa kwa kuwalikwa kwenye pambano la hisani la Steven Gerrard la Machi 29, sio la kusubiri kushuhudia magwiji waliocheza pamoja kushuka tena dimbani ," aliandika Riise.